Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,286
OOH RABI, NILIDHANI KARANGA, KUMBE MAVI YA MBUZI.
1. Nilidhani ni karanga, kumbe ni mavi ya mbuzi,
Sikudhani ni pakanga, katika wangu mchuzi,
Kuamini mtu janga, jiandae na mauzi.
Kuna mambo ya kuchunga, sifanye tu maamuzi.
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
2. Nilidhani ni maziwa, kumbe ni tui la nazi,
Ati nimependelewa, na mola wangu Azizi,
Kumbe janga nimepewa, wallahi si kumaizi,
Yale niliyotendewa, mlipaji ni mwenyezi.
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
3. Nilidhani ni malaika, kumbe adui shetani,
Mimi nilimchunuka, tena nilimuamini,
Kumbe vile anicheka, aniingize mjini,
Akapanga kuchomoka, na sanduku la thamani.
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
4. Nilidhani muumini, alo na sifa stahiki,
Kumbe najenga imani, kwa kiumbe mnafiki,
Akafanya ushetani, kanirushia mkuki,
Namshukuru Manani, yuko uchi mnafiki,
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
5. Nilidhani ni kitanda, kumbe tusi la maiti,
Kule kote kunikanda, ni mbinu zake afriti,
Ili apate niponda, aibe zangu tikiti,
Mja alivyonitenda, nusura niwe maiti.
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
6. Aheri shetani jini, kuliko shetani mtu,
Nani amtuma jini, si kama kiumbe mtu?
Hata ndugu wa ndani, kumwamini sithubutu,
Aweza kuwa shetani, anipige na mtutu.
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
7. Unapoweka imani, uweke na tahadhari,
Silaha za kibindoni, na dua kwa Qahari
Ujue wafanya nini, inapotokea shari,
Kilio chafaa nini, mtenda hana habari,
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
8. Yupo fanani bubusa? katika sanaa zake?
Yaani aso yagusa, mambo ya jamii yake?
Au ashindwe papasa, tako la moyo wake?
Kama yupo ni tutusa, ina shida rasi yake,
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
9. Niliuchonga ujiti, nichore yalo nisibu,
Nikafuata shuruti, pamoja na taratibu,
Wino wa chani kiwiti, ukakinakshi kitabu,
Mwisho ikawa kunuti, nipate chuma thawabu
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
10. Sijui niweke koma, ama niweke mkato,
Watendwa si hukoma, ama hukwepa kong'oto,
Sitarudia pogoma, kama ng'ombe aso kwato,
Kuwa boya nimekoma, sikiza msaka sato.
Usimwamini yeyote, amini kivuli chako.
Shairi hili lipo hapa kwa hisani ya watu wa Machame.
Njano5.
0784845394