Operation Barracuda

Operation Barracuda

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Joined
Jun 28, 2016
Posts
351
Reaction score
887
OPERATION BARRACUDA: "MISSION YA KIJASUSI" ILIYOKATISHA MAISHA YA PATRICE LUMUMBA, NA KUZIMA NDOTO YA UHURU NCHINI KONGO.

Na.Comred Mbwana Allyamtu
Thursday -17/1/2018
Marangu, Kilimanjaro -Tanzania.

Neno "Barracuda" ni neno lenye asili ya Latin America, lenye maana ya "Samaki wakubwa wa baharini walao Samaki wadogo". Hivyo misheni ya kutamatisha maisha ya Patrice Lumumba ilipewa jina "Operation Barracuda", ndio code name ya kijasusi iliyotumika kukamilisha unyama na mauaji ya Lumumba. Misheni hiyo iliratibiwa na mashirika ya kijasusi ya CIA ya Marekani, Ml6 ya Uingeraza na VSSE ya Uberigiji, na kutamatisha ndoto ya Uhuru ndani ya Kongo huku yakimwaga damu ya mwana Afrika, mwasisi, baba wa taifa na mkombozi wa Wakongomani Patrice Emery Élias Okit'Asombo Lumumba. Mauaji yake ya kusikitisha yalitekelezwa usiku wa saa 10:00 tarehe 17/1/1961, baada ya kumuua waliuyayusha mwili wake ndani ya pipa la tindikali. Mpango mzima wa kuuwawa kwake ilikuwa hivi.....

Jumatatu July 13, 1960 Washington D.C, wiki Ikiwa inaanza na pilikapilika zikiwa zinaanza ndani ya ikulu ya White House, kuliripotiwa kuwepo wageni waliotaka kumuona rais, "Put that away." Hiyo ndiyo ilikuwa sentesi ya kwanza Rais Dwight Eisenhower kuitamka mara baada ya kuingia ndani ya Oval Office katika makazi yake ya White house. Maneno hayo Dwight Eisenhower aliyatamka mara baada ya kumuona moja ya wageni wake waliokuja ofisini kwake anatoa makaratasi kutoka kwenye briefcase iliyokuwa imebebwa na mmoja wapo.

Huu ulikuwa mtindo wa Rais Eisenhower pale anapotaka kuongea na mtu mambo ya siri nzito na akiwa hana mpango wa kuwashirikisha Baraza la Mawaziri au Baraza la Ulinzi. Huyu Dwight Eisenhower ndie rais anayetajwa kutekeleza misheni nyingi zaidi za kijasusi na zenye mafanikio makubwa, baada ya utulivu kidogo rais na wageni wake wakaanza kikao. Kikao hiki kilikuwa ni kikao cha siri kubwa na kilihusisha washiriki watatu tu. Yani Rais Dwight Eisenhower mwenyewe na wageni wawili ambao walikuwa ni ndugu. Mtu na kaka yake, katika wageni hao mmoja aliitwa John Foster Dulles ambaye alikuwa ni Waziri wa mambo ya nje wa Marekani na Wapili aliitwa Allen Dulles ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Shirika ka kijasusi la Marekani, CIA.

Eisenhower alikuwa na utaratibu wa kufanya mambo yake kwa siri sana, tena hakupenda kushilikisha masuala yake ya misheni za kijasusi na timu kubwa ya Pentagon au baraza lake la mawaziri, hivyo mtindo huo wa yeye kutotaka kuwepo na aina yoyote ya nyaraka inaweza kuihusisha ofisi ya Rais pale ambapo akitaka kuamuru ifanyike jambo ambalo alihisi linaweza lisiungwe mkono na jamii ya kimataifa. Na hii ndio ilikuwa sababu ya kumuamuru Allen Dulles arudishe makaratasi yake kwenye briefcase.

Wiki nne zilizopita yani tarehe 1 July 1960, kilifanyika kikao kama hiki kati ya watatu hawa, kikao hicho kilifanyika baada ya kupokea, file lilo beba barua iliyotumwa kwa telegram kuja kwa Rais Dwight D. Eisenhower, barua hiyo ilitoka London Uingeraza, kwenye shirika la kijasusi la Uingeraza la M16 , ilisomeka "Tunaitaji kutaarifu kuwa ofisi ya Waziri mkuu No.10 Downing street, inaitaji usaidizi juu ya mpango wa kumwua Lumumba". Hivyo barua hiyo ilionesha kuwa baraka na mipango yote kutoka kwa Waziri mkuu wa Uingeraza wakati huo Winston Churchill ilikuwa Imekamilika, isipokuwa iliitaji msaada kutoka Marekani.

Katika kikao hicho ndani ya ofisi ya rais wa Marekani ilibidi wazungumzie kukubali kushiriki katika misheni hii au watupilie mbali mpango huu kama walivyo tupia mbali mpango wa kumg'oa madarakani rais wa Misri wakati huo Abdul Nasser Gamal, na juu ya changamoto kubwa ya kufanikisha jambo hilo, jambo yenyewe ilikuwa ni kumuondosha madarakani Patrice Emiery Lumumba, Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo huru.

Mwezi mmoja nyuma Kongo DRC, wakati huo ikiitwa Kongo Belgium ilikuwa imepata uhuru, ilikuwa ni tarehe 30 June 1960, pale Uberigiji walipoamua kuwapatia wakongo uhuru wao, katika siku ya kukabidhiwa uhuru, mfalme wa Ubergiji Baudoin alihudhuria na kutoa hotuba yake, katika hotuba ya mfalme huyo alisifia nchi yake ya Ubergiji kwa kuwapatia maendeleo Kongo, na kumwagia sifa babu yake, mfalme Leopard ll kwa kuwastarabisha wakongomani. Lakini sherehe hiyo iliingia dosari wakati wa Lumumba alipotoa hotuba iliyo wakadhibisha sana Wabelgiji na mapebari wote walio hudhuria sherehe ile.(Unawaze kuitazama hotuba hiyo ya Patrice Lumumba aliyoitoa kwa lugha ya kiswahili kupitia hapa [emoji116] )

Kwani Lumumba hakufurahishwa hata kidogo na uhuru elekezi na mashariti yaliyo kuwa yakitolewa na mfalme huyo wa Ubergiji. Pamoja na kwamba hakuwekwa kwenye ratiba ya wazungumzaji wa siku ile, Lumbumba alisimama na kuhutubia ukimbi ule wa "National de Palace" na kutoa hotuba kali iliyo tibua hali ya mambo kwa kusema *“…Tulizoea matusi, dhihaka na vipigo asubuhi, mchana na usiku, kwa sababu sisi ni watu weusi… Tumeona ardhi yetu ikinajisiwa kwa sheria zilizowapendelea wazungu na kuwabagua weusi. Hatujasahau kwamba sheria hazikuwa sawa kwa mweupe na mweusi, zilikuwa rafiki kwao na katili kwa wengine.”* Baada ya kutoa hotuba ile, Lumumba alikwenda kukaa kwenye kiti chake huku akipongezwa kwa makofi na wajumbe wake na marafiki zake wazalendo kutia ndani Anton Gizenga, na Pierre Mulele, rais kasavubu, mfalme Boudoin na wageni kutoka nje wakipigwa na butwa na kukadhibishwa na hotuba hiyo. Na Lumumba alipopita mbele ya mfalme wa Ubeligiji alimwangalia na kumwambia, '‘Sisi sio nyani wenu tena.’'

Kupitia hotuba hiyo serikali ya Uberigiji walianza kuamini kuwa Lumumba awafai kusalia Kongo kama kiongozi, hofu ya Wabelgiji juu ya siasa za mrengo wa kushoto za Patrice Lumumba na Chama chake cha “The Movement National Congolais” (MNC) kutumikia Congo, waliona ni tishio dhidi ya masrahi yao.Hofu hiyo iliongezeka baada ya MNC kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1960, na Lumumba kuunda serikali, lakini kwa upinzani mkubwa wa Wabelgiji waliotaka Joseph Kasavubu, kibaraka wao wa Chama cha kikabila cha ABAKO ambacho hakikushinda, kutia ndani hotuba ile na fununu za Lumumba kuwa na ushirika na siasa za kikominist uliwafanya Ubergiji kuanza mikakati ya kuidhofisha serikali halali ya Lumumba.

Serikali ya Ubergiji walituma ombi Uingeraza kuwaomba wawasaidie kuandaa mpango wa kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Lumumba, mkuu wa mikakati na misheni za kijasusi wa CIA James Angleton,(CIA Chief of Counterintelligence), alieleza mwaka 1974, kuwa "mpango wa Mauuaji ya Lumumba yalipangwa nchini Ubergiji, kupitia shirika lao la kijasusi la VSSE, na baadae Uingeraza kuishirikisha Marekani..." Wasiwasi mkubwa wa Ubergiji na Uingereza mpaka kuamua kuishirikisha Marekani katika mpango huu wa kuuliwa Lumumba, ulikiwa ni mwenendo wa Lumumba dhidi ya masrahi ya kimagharibi na hasa hasa namna ambavyo aliiandama Uberigiji na makampuni ya kibepari yaliyo kuwa nchini Kongo. Aliwatia sumu zaidi pale alipo onekana kuukaribisha Ukominist Kongo.

Tishio la Usovieti na kuingia kwa siasa za ukominist nchini Kongo, ikitegemea kipindi hicho dunia ilikuwa kwenye minyukano mikali dhidi ya Ubepari na Ukominist, kulifanya kuchochea hasira kwa mataifa ya magharibi dhidi ya Lumumba, Hali hii ikaamsha hasira za Uingereza na Uberigiji na wakaweka nia kwamba ni lazima Lumumba aondoke madarakani. Kikwazo kikubwa kilikuwa ni kwamba Lumumba alikuwa amechaguliwa kidemokrasia kwa kupigiwa kura na kushinda na alikuwa anakubalika mno na wananchi wa Kongo kipindi hicho. Ndipo hapa wakaona umuhimu wa kuwaomba wamarekani wawasaidie kutimiza amza yao.

Sasa turejee kwenye kikao White house, Washington DC, Wiki nne nyuma katika kikao chao cha kwanza Rais Eisenhower alikuwa amewapa ''Majukumu'' waziri wake wa kigeni na mkurugenzi wa CIA wakaandae mkakati wa kutekeleza kumuondosha Lumumba ambao watakuja kuuwasilisha kwenye kikao cha leo hii. Ndipo ambapo Mkurugenzi wa CIA Allan Dulles akaanza kumpa mkakati alioufikiria namna ya kufanikisha kumuondosha Lumumba, Kwanza akaanza kumpa tahadhari kadhaa za kuzingatia kuhusu mpango ambao watauweka. Moja ya tahadhari ya mpango huo ni vyema usijadiliwe kwenye Baraza la Mawaziri au Baraza la Usalama wa Taifa, kwasababu lazima utazua mtafaruku mkubwa kwasababu ni dhahiri baadhi ya watu wataupinga.

Pia Dulles alitaka mpango huo ubaki siri kwanza katika viongozi wa Marekani, alisema kama ni watu wachache wataufahamu hii ina maana uwezekano wa siri kuvuja utakuwa ni mdogo. Lakini pia Allan Dulles akashauri ni lazima oparesheni hii itekelezwa pasipo watu kujua kuna uhusika wa marekani ili kufanya dunia na washirika wa marekani kukubaliana na serikali mpya itakayo wekwa kama ikitokea oparesheni ikafanikiwa. Kufatia hatua hiyo, Kwa kuzingatia hayo basi, Allan Dulles akamshauri Rais Eisenhower atumie mamlaka yake aliyopewa na sheria ya usalama wa taifa ya mwaka 1947 (U.S. National Security Act, 1947), kuidhinisha operation ya usiri mkubwa zaidi (Covert operation) kutekeleza Operation hiyo kumpidua Waziri mkuu Patrice Lumumba. Nchini Marekani Sheria hii inampa mamlaka Rais wa Marekani kuamuru kufanyika kwa "covert operation" pasipo kumuweka Rais kutambuliwa uhusika wake kwenye hilo ikitokea siri ya operation hiyo imevuja. Kwa maneno mengine Sheria hii inampa uwezo Rais kukana kuhusika kuamuru oparesheni kufanyika au kufahamu chochote juu ya kufanyika kwa oparesheni hiyo ikitokea siri imevuja kuhusu oparesheni hiyo. Hii ndio inajulikana kama 'Plausible Denialbility'.

Kwahiyo baada ya kukubaliana wote kwa pamoja juu ya kutekeleza operation hiyo, Allan Dulles mkurugenzi wa CIA, pamoja na Rais Eisenhower na John Dulles ambae alikuwa waziri wa mambo ya nje, waliamua kuipa kazi hii idara ya CIA-SAD, hii ni moja ya idara katika vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya Marekani yenye weledi, uwezo, watu, ufanisi na ruhusa ya kisheria kutekeleza mkakati wa kuingilia (intervention) nchi nyingine kwa lengo la kutekeleza mapinduzi au, mauaji maalumu kwa masrahi ya Marekani. Idara hiyo ya SAD (Special activities division), ilundwa na Marekani kama kitengo maalumu ndani ya CIA, Kutokana na changamoto za kimataifa , ambazo nyingine zinatishia usalama au maslahi ya mrekani lakini marekani haiwezi kuchukua hatua zozote kutokana kujiepusha na lawama kutoka jamii ya kimataifa ndipo hapo ikaonekana kuna umuhimu wa kuwa na kitengo maalumu kwa ajili ya suala hili.

Kwa mantiki hiyo kitengo hiki kilikuwa kinafanya kazi kwa niaba ya serikali ya marekani lakini kulikuwa hakuna uwezekano wowote wa adui kuunganisha uhusika wa kikosi hiki na serkali ya marekani. Moja ya matukio ambayo kitengo hiki kimehusika sana na CIA wamekiri kwenye nyaraka zilizowekwa wazi mwaka 2013 ilikuwa ni kueneza propaganda ambayo ilichangia kupinduliwa kwa Rais wa Iran mwaka 1953, Pia kitengo hiki kilitumika kuzuia chama cha kikomunisti cha Italia kushinda uchaguzi mwaka 1960, kitengo hiki kimewahi kufanya oparesheni ya siri iliyoitwa "Operation Mockingbird" katika taifa la marekani. Oparesheni hii ilikuwa na lengo la ''kucontrol na kuremot" habari zinazoandikwa na Vyombo vya habari nchini humo.

Baada ya kuafikiana kwa pamoja na rais Dwight Eisenhower kusaini, Allan Dulles mkurugenzi wa CIA akaanda mkakati wa kuingia Kongo, mkakati huo wa kumshughulikia Lumumba ukapewa jina,(code name) *"Operation Barracuda"*, siku iliyofuata ndani ya Ofisi za CIA zilizopo kitongoji cha Langley jijini Virginia, Dulles akapanga askari wa SAD ndani ya CIA, watakao simamia mpango huu. Jasusi nguli wa CIA, Frank Carlucci, akapewa jukumu hilo la kumuangamiza Patrice Lumumba.

Huyu Carlucci Kabla ya kupelekwa Kongo kumshughurikia Lumumba, amewahi kufanya kazi Ureno alikopewa jina la “The Hangman of Portugal” ikimaanisha "Mnyonyaji watu wa Ureno" kwa ukatili wake dhidi ya wanaharakati wa kikomunisti. Na baadae ya kutekeleza mission hizo za kijasusi mwaka 1965, Carlucci alirejea Marekani na alipanda cheo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa CIA. Carlucci baada ya kupokea jukumu hilo, asubuhi ya July 18 akawasiliana na maafisa wa kijasusi wa M16 wa Uingeraza, aliwapatia mpango mzima wa operation ile ya Barracuda, na namna ya kumuangamiza Lumumba.

Maafisa ujasusi wa CIA, M16 na wale wa VSSE wa Uberigiji, wakiongozwa na Carlucci wakawasili Leopardville (sasa ikijulikana Kinshasa), August 19 1960, Leopardville walipokelewa na jasusi maalumu aliyeitwa Larry Devlin, huyu alitangulia mapema Kongo ili kuanza kazi, mpango wa kwanza ilikuwa ni kumuua Lumumba kwa sumu, hivyo jukumu hilo alipewa daktar wa kimarekani ambae pia alikuwa ni askari wa CIA, aliyeitwa Dr, Sidney Gottlieb (Senior CIA scientist), Dr Sidney Gottlieb akatengeneza sumu na kuituma Kongo, sumu hiyo ilitoka Virginia Marekani kupitia Accra Ghana, kupitia "diplomatic pouch" hizi diplomatic pouch ni 'Vifurushi' maalumu vya kidiplomasia ambavyo huwa havikaguliwi mahali popote pale.

Huyu jasusi wa CIA,Dr.Sidney Gottlieb alichagua kutumia njia ya sumu ya kumuangamiza Lumumba kwakua ndio njia nyepesi isiyo acha madhara kijasusi, sumu hiyo ilikuwa na madhara makubwa mno kwani madhara yake hayana tiba. Dr.Sidney alisafiri kwenda kongo baadae ili kumuelekeza afisa wa CIA aliyekuwa Leopardville Kongo, Larry Devlin jinsi ya kuitumia,mpango wa sumu hiyo ilikusudiwa waiweke kwenye chakula au dawa ya meno atakayotumia Lumumba. Lakini bahati mbaya CIA walishindwa kukamilisha mpango huo kwa wakati huo, kutokana na sumu ku-expire (kupitia muda wa kutumika), kutokana na kuchelewa kufika Leopardville. Hivyo ikatupwa mto Kongo na mpango huo wa plan "A" ukaferi.

Taarifa ikatumwa Washington DC kwa Waziri wa mashauri ya kigeni, John Dulles, juu ya kuferi mpango huo, Waziri huyo kwa kushirikiana na mkurugenzi wake wa CIA Allan Dulles, haraka wakawasiliana na maafisa wa London, M16 na wale wa VSSE, Brussels Uberigiji, na kuazimia kutumia njia ya kuipa nguvu serikali haramu ya Kasavubu, Mobutu na ile ya Katanga chini ya Moise Tchombe, Ili kuivuluga (paralized) serikali halali ya Lumumba.

Sasa turudi mpaka Leopardville (Kinshasa), ilikuwa ni asubuhi ya saa 10:00, Tarehe 11July 1960, pale Jimbo la Katanga lenye utajiri mkubwa wa madini, lilipo jitangazia uhuru wake chini Waziri wake Mkuu,Moise Tshombe, huku akiungwa mkono na Ubelgiji na makampuni makubwa ya uchimbaji madini. Kujitenga kwa Katanga ilitoka mapema tu baada ya uhuru, kwani siku chache baadae ya uhuru kuliibuka machafuko yaliyosababishwa na wanajeshi wa jeshi la Congo ambao pamoja na kutaka maslahi zaidi na kupandishwa vyeo, lakini walishinikiza kuondolewa kwa wanajeshi wa kibelgiji ndani ya jeshi la Congo.

Lumumba alijibu malalamiko ya askali hao kwa kuwapadisha vyeo askali hao, kwa kumteua mkuu wa majeshi wa kwanza mweusi Victor Lundula kuwa mkuu wa jeshi, na Joseph Desire Mobutu kuwa mnadhimu mkuu wa jeshi.Ukiachilia mbali madai ya wanajeshi hao, pia kuliibuka na jaribio la jimbo la katanga na kasai kutaka kujitenga. Hali hii ilichochea mapigano zaidi kwani wanajeshi wa Tshombe walikuwa wakipambana na wanajeshi wa serikali ya Kasavubu. Hali hiyo ya machafuko, ilipelekea Vikosi vya umoja wa mataifa 'UN' kuingilia kati Kwa lengo la kuzuia machafuko na kutuliza Amani. Umoja wa mataifa wakaunda kikosi maalumu cha " ONUC" chini ya Mswedeni General Carl Von Horn

Lakini ikatokea kwamba Patrice Lumumba hakuridhishwa na utendaji kazi wa vikosi vya ONUC-UN kwani aliona havifanyi kazi ipasavyo. Hivyo basi alielekea upande wa Umoja wa Usovieti 'USSR' Kwa kuwaomba misaada zaidi juu ya kurejesha katanga iliyokuwa imeasi, Pasina kuchelewa, majeshi ya Usovieti yaliingia Congo na kuanza kushambulia wapiganaji wa Katanga waliokuwa wanataka kujitenga. Kitendo cha Lumumba kuomba misaada USSR, kiliwachukiza sana mataifa ya magharibi na Marekani, na kuwafanya kuharakisha operation yao haraka, kwani walihofia kuenea kwa itikadi za kikomunisti nchini Congo. Ndipo wakaanza kumshinikiza Rais Kasavubu kumuondoa madarakani Patrice Lumumba. Kasavubu akashawishika na mwishowe akamfuta kazi Lumumba, Lumumba akapinga, Bunge nalo likapinga kitendo cha kasavubu kumfukuza kazi Lumumba kwa kukosoa hatua hiyo kuwa ni kinyume na katiba.

Bunge lilibatilisha maamuzi ya Kasavubu na Lumumba kufukuzana, lakini tayari mtafaruku huo ulikuwa umeingiza wahasimu wakubwa wa kimataifa kutia ndani Marekani na nchi za Ulaya upande wa Kasavubu, na kambi ya kikomunisti upande wa Lumumba.

Septemba14, 1960, Kanali Joseph Mobutu akiwa mnadhimu wa jeshi, akashawishiwa kufanya mapinduzi kwa kuhaidiwa madaraka na ulinzi, baada ya makubaliano baina ya Marekani na Mobutu na kwa kupewa nguvu na CIA, alitangaza kuingilia kati mtafaruku huo kwa kunyakua madaraka akidai kushikilia hadi mwishoni mwa mwaka tu, yaani Desemba 1960. Kisha akaagiza kufukuzwa nchini Warusi na Wachek wote. Lumumba akawekwa kizuizini ndani ya Makazi ya Waziri Mkuu kwa kisingizio cha kumpa ulinzi, lakini akambakiza Kasavubu madarakani kama Rais, kisha kuwatupa nje ya serikali wafuasi wote wa Lumumba.

Kwa kuhofia Lumumba angeweza kurejea madarakani, November 19, 1960, Baraza la Usalama la umoja wa mataifa, chini ya shinikizo la Rais Dawight D. Eisenhower, ulitangaza kuitambua serikali ya Kasavubu na Mobutu, hata hivyo maafisa wa ujasusi wakawasilisha mpango wa mwisho wa kumwua Lumumba, mbele ya rais Dwight Eisenhower na Allan Dulles, operation Barracuda ikaenda kutekeleza kwa kumuua kabisa Lumumba, operation hiyo iliratibiwa chini ya mwanasayansi Dakta Sidney Gottlieb, Frank Carlucci na James Angleton

Wakati operation hiyo Barracuda ikiendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa, na kwakushirikiana, Wabelgiji nao walikuwa na mpango wao upande wa pili huku wao wakiwa wamepewa jukumu la kuvuruga na kuchochea moto, kwa kuwashirikisha wakina Mobutu, Tshombe na wataalamu wa nje, huku operation hiyo Ikiwa imepewa baraka na Mfalme Boudouin wa Ubelgiji. Lumumba akiwa kizuizini nyumbani kwake kwenye makazi ya Waziri mkuu mjini Leopardville, tarehe hiyo 12/9/1960, huku nyumba yake ikiwa imezungukwa na askari wa Umoja wa Mataifa waliosheheni silaha nzito nzito.Usiku huo huo akiwa chini ya ulinzi mkali, wafuasi wake walijipenyeza na kufanikiwa kumtorosha Lumumba na kumkimbiza mafichoni Stanleyville, Lumumba aliamua kuhamia Kasai ngome yake kisiasa, ili kuanzisha utawala wake huko kwa lengo la kuikomboa Kongo.

Safari yake ilichukuwa siku kadhaa kwa vile alikuwa anasimama mara kwa mara kusalimia umati wa watu uliokuwa wanamngojea, bila kujua kuwa taarifa za kutoloka kwake Kinshasa zilimfikia Mobutu, na tayali askali wa Mobutu walikuwa wakimfatilia kwa nyuma, hatimae Lumumba akakamatwa Desemba1, 1960, akiwa nusu ya safari kabla ya kuingia Stanleyville. Kutokana na kunyimwa ulinzi wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa, alipigwa sana, kisha akarejeshwa Leopoldville kwa ndege chini ya ulinzi na alipofikishwa mbele ya Mobutu, alifungwa kamba mikononi na kutemewa mate usoni na Mobutu huku akiambiwa: “Haya sema! Uliapa ungenimaliza, sasa ni mimi ndiye nitakayekumaliza”.

Kufatia kukamatwa Lumumba Wafuasi wa Lumumba kule Stanleyville, walipata taarifa hizo za kukamatwa kwa Lumumba, wakiwa wanaongozwa na Antoine Gizenga, walijitangazia serikali yao ya *“Free Republic of the Congo” (FRC)* na kuanzisha Jeshi la Jamhuri hiyo., kufatia hali hiyo Congo ikasambaratika kwa kugawanyika katika tawala nne, huku kila moja na mfadhili wake wa kigeni. Wakati Serikali ya Mobutu na Kasavubu ikisimamiwa na kupewa nguvu na nchi za Magharibi, Serikali ya Gizenga ilipata misaada kutoka Kambi ya Urusi, na kwa viongozi wanamapinduzi kama Rais Abdel Gamal Nasser wa Misri, wakati Serikali ya Katanga (Elizabethville-Katanga) chini ya Moise Tshombe, ilitegemea msaada wa Ubelgiji ambapo Serikali ya Kasai Kusini, chini ya Albert Kalonji, nayo pia ilipokea usaidizi kutoka kwa Wabelgiji.

Serikali ya Gizenga kwa kushirikiana na Pierre Mulele iliyoundwa kwa jina la Lumumba, na kujiita jeshi la simba ilizidi kupata nguvu kiasi kwamba kufikia Desemba 20, 1960, Serikali ya Jimbo la Kivu, Mashariki mwa Kongo, iliangukia mikononi mwa majeshi ya Gizenga. Kwa kufadhaika na tukio hilo, Mobutu alituma vikosi vyake, lakini vilinyukwa vibaya na kutawanyika. Siku saba baadaye, majeshi ya Gizenga yakaingia na kuteka Katanga ya Kaskazini chini ya Mkuu wa kikosi Laurent Desire Kabila (Baba yake Joseph kabila),na kuanzisha Jimbo la “Lualaba”, huku kukiwa na habari za vuguvugu la mapinduzi nchi nzima kwa lengo la kumrejesha Lumumba madarakani.

Kwa sababu hiyo, Serikali ya Mobutu na Kasavubu iliamua kumhamishia Lumumba jimboni Kasai karibu na katanga kwa Moise Tchombe, kwenye Gereza la Thysville karibu na Elizabethville, kwa mhasimu wake mkubwa, Moise Tshombe, hatua iliyotafsiriwa sawa na kumhukumu kifo, kwa kuwa asingeweza kusalimika mikononi mwa hasimu wake huyo. Alisafirishwa kwa ndege mpaka Katanga, alipo fika huko mpango wa kuuwawa ukaandaliwa, maaskali wa Tchombe ukitaarifu Uberigiji, maafisa usalama wa Uberigiji, CIA na M16 pamoja na askali maalumu wa shabaha (sniper) kutoka Marekani na Uingeraza ukawekwa sawa kwa kummaliza Lumumba.

Januari 17, 1961, Lumumba na mahabusu wenzake wawili, yani Waziri wa Vijana, Mourice Mpolo na Makamu wa Rais wa Seneti, Joseph Okito, ambao walikamatwa pamoja wakiwa njiani kutoroke Stanleyville, awalichukuliwa kutoka Kambi ya kijeshi ya Thysville iliyopo Jimboni Kasai na Mkuu wa Usalama wa Mobutu, Victor Nendaka, akifuatana na askari watatu wa kabila la Baluba na kupelekwa uwanja wa ndege wa Moanda. Alipo wasili uwanjani, walikaribishwa kwa vipigo vizito kutoka kwa askari wa Kibelgiji na Katanga, kisha kutupwa nyuma ya gari kupelekwa kwenye nyumba pweke, maili mbili kutoka hapo, nyumba iliyolindwa na majeshi ya Kibelgiji na Polisi chini ya Afisa wa Kibelgiji. Hapo tena, Tshombe na mawaziri wake walishiriki kumpiga na kumtesa kinyama bafuni, kisha watesi hao wakatoka wametapakaa damu mwilini. Huku wakiwa wamelewa chakali, walitangaza Lumumba “auwawe mara moja”.

Ilipo usiku wa saa 4:00, tarehe hiyo hiyo 17/1/1961 Lumumba na wenzake wawili walichukuliwa kwa gari hadi kwenye vichaka, maili 30 toka Thysville, Tshombe akiongoza msafara, akiwamo pia Kamishna wa Polisi wa Kibelgiji, Frans Verscheure na walengaji shabaha kutoka Marekani. Walipofikishwa eneo lililokusudiwa wakipekuliwa, wakiwa wamevaa kaptura na fulana tu, walianza kuuwawa. Huku Lumumba alikuwa wa mwisho kuuawa kwa kupigwa risasi na kikosi cha Askari wenye shabaha na kisha kuzikwa huko huko porini. Kesho yake ya tarahe 18/1/1961 serikali ya Moise Tchombe ikatangaza habari za uongo kwamba Lumumba na wenzake waliuawa na wanavijiji wenye hasira walipokuwa wakijaribu kutoroka kizuizini.

kwa kuhofia kuvuja kwa taarifa za unyama walio fanya, Usiku uliofuata, askali hao wa Uberigiji walikwenda kufukua miili ya Lumumba na wenzake, baada ya kufukuliwa ilisafirishwa hadi Kasenga, maili 120 Kaskazini Mashariki mwa Elizabethville, ambako ilikatwakatwa vipande vipande na kutupwa kwenye pipa la tindikali (Sulphuri acid), na kuyeyuka, mafuvu yao yakasagwa unga; mifupa na meno yakatupwa kwa kutawanywa porini wakati wauaji walipokuwa wakirejea Elizabethville. Asubuhi ya tarehe 20/1/1961, jasusi Larry Devlin aliitaarifu Washington DC kwa code kuwa "Mission 009321 operation Barracuda is over".

Kule Washington mtu wa kwanza kupata taarifa juu ya kukamika kwa operation barracuda alikuwa Waziri wa kigeni Jonh Dulles, haraka akamtaalifu mkurugenzi wa CIA, Allan Dulles, na baadae taarifa zikamfikia rais Dwight Eisenhower. Wakati huo Dwight Eisenhower ndio alikuwa anakwenda kumaliza muhura wake wa mwisho madarakani, hata rais aliye mfuata wa 35 Jonh F Kennedy aliendeleza kulinda masrahi ya Marekani nchini Kongo kupitia Shirika lake la Ujasusi la CIA, liliendelea kuhakikisha na kudhibiti nyendo za watawala wa Kongo ili wasije kuegemea upande wa Ukomunisti. Kwa kuthibitisha hili mwandishi Martin Meredith Kwenye kitabu chake: The State Of Africa, ameandika, kuwa *"Mobutu kwenye safari yake ya kwanza Washington, Mei, 1963, akiwa Mkuu wa Majeshi kwenye Serikali ya Joseph Kasavubu, Rais wa Marekani, John Kennedy alimtamkia Mobutu, "Jenerali, isingelikuwa wewe, Ukomunisti ungetamalaki Kongo", huku Mobutu akimjibu, "Ninafanya niwezalo mheshimiwa raisi"*.

Martin Meredith kwenye kitabu chake cha "The State Of Africa" ameandika "After operation barracuda completed and his coup in 1965, Mobutu remained on the CIA's payroll for sometime and received regular briefings from Larry Devlin , the CIA station chief in Leopoldville." ( Meredith, State Of Africa, pg 294).

Baada ya "operation Barracuda" kukamilika na Lumumba kuuwawa, hatimae tarehe 21 January 1961, Kasavubu alimteua Mobutu kuwa mkuu wa majeshi ya Kongo, na miezi kadhaa iliyofuata Cyrille Adoula akachaguliwa kuwa Waziri mkuu. Kwa kipindi hiko chote,kulikua na mapambano yaliyokuwa yakiendelea kati ya majeshi ya Mobutu wakishirikiana na vikosi vya UN dhidi ya wapiganaji wa Serikali ya Antone Gizenga na yale ya katanga iliyoongozwa na Moise Tshombe, majeshi ya Moise Tshombe yalishindwa nguvu na Tchombe mwenyewe kukimbilia Northern Rhodesia (Zambia kwa sasa) na baadae Uhispania.Lakini mwaka 1964, Tshombe aliitwa kurudi nchini, ambapo Kasavubu alimteua kuwa waziri Mkuu.

Katika kipindi chake cha uwaziri mkuu Tchombe, alikabiliwa na machafuko kutoka kwa waasi, wakiongozwa na bwana Pierre Mulele na Gizenga. Huyu Pierre Mulele alikuwa mfuasi wa Patrice Lumumba, na aliongoza mapambano dhidi ya serikali kwa lengo la kutaka kumuondosha madarakani Rais Kasavubu. Mapigano yaliendelea kwa muda mrefu sana kati ya wapiganaji wa Mulele na majeshi ya serikali yakishirikiana na majeshi ya UN. Mwisho wa siku Mulele alizidiwa nguvu na kukimbilia nchini Congo-brazzaville.

Kwenye uchaguzi wa March 1965, Moise Tshombe alishinda uchaguzi, kwa hiyo ilibidi awe waziri mkuu wa Congo tena. Lakini kilichotokea ni kwamba Rais Kasavubu alimteua Évariste Kimba kuwa waziri mkuu, Kitendo hiko kiliamsha migogoro zaidi ndani ya nchi ya Congo. Jambo lilomrudisha Mobutu na kuichukua nchi tena kijeshi na kumfuta kazi kasavubu, Mobutu alichukua nafasi hiyo kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi tarehe 25 November 1965.

Hotuba yake ya kwanza baada ya kuchukua madaraka, Mobutu aliuambia umati wa watu mjini Leopoldville katika uwanja mkuu kuwa ‘’tangu wanasiasa wamechukua nchi wameharibu nchi basi kwa miaka mitano hatutakuwa na chama cha siasa wala shughuli za kisiasa’’. Nguvu za bunge zilibaki kuwa ni mhuri tu kabla ya kufutwa kabisa lakini baadae zilirudishwa, na Mobutu alijiimarisha vya kutosha.

Huyu Patrice Lumumba tunaye azimisha miaka 58 ya kifo chake leo alizaliwa tarehe 2 Julai 1925, na kuuwawa tarehe 17 Januari 1961, Patrice Lumumba alizaliwa na François Tolenga Otetshima, na mama yake aliitwa Julienne Wamato Lomendja, ambao walikuwa wafugaji katika kijiji cha Katakokombe, wilaya ya Kanyalwaunga, katika Jimbo la Kasai. alikuwa muumini wa kanisa Katoliki, jina alilopewa alipo zaliwa Patrice Lumumba lilikuwa akiitwa Élias Okit'Asombo. Jina hili likiwa na maana "heir of the cursed"ambalo lilitokana na kabila la Tetela ambayo ni miongoni mwa makabila ya congo okitá/okitɔ́ ('Mrithi') na asombó ('cursed or bewitched people who will die quickly').

Lumumba alilelewa katika makuzi ya familia ya Kikatoliki, alisoma katika shule ya msingi ya kanisa la Protestant, Shule ambayo ilikuwa inamilikiwa na wamisionari wa Kanisa Katoriki, na baadaye alipata mafunzo katika chuo kimoja cha serikali, alipo maliza masomo, alipata kazi katika mji wa Léopoldville (Kinshasa ya sasa) na baadaye katika mji wa Stanleyville (Kisangani ya sasa), ambapo alifanya kazi kama kalani wa posta, na pia alikuwa akifanya kazi ya uuzaji wa bia kwa wasafiri.

Mnamo mwaka 1951 alimuoa Pauline Opangu. Mwaka 1955, Lumumba alipanda cheo na kuwa Cercles wa mji wa Stanleyville, na baadaye alijiunga na chama cha Liberal Party of Belgium, ambapo alifanya kazi ya uharariri na usambazaji wa kijarida la Chama cha Kiliberali cha Ubeljiji. Baadae alijihusisha na siasa, wakati Kongo inapata uhuru chama chake kilikuwa kimeenea nchi nzima, na kupelekea chama chake cha MNC kushinda uchaguzi wa serikali wa mwaka 1960, na kuwa Waziri mkuu wa kwanza wa Kongo huru.

Lumumba atakumbukwa kwa uzalendo wake, ndani ya Kongo na Afrika kwa ujumla. Viva Kongo, Viva Afrika, Viva "Patrice Emery Élias Okit'Asombo Lumumba"


Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com
IMG_20190507_092818_289.jpeg
 
Viongozi wa mama Afrika hakika wameuwawa mno je ? nani nasi atakaye tulipizia kisasi dhidi ya mabeberu?
 
Back
Top Bottom