...ninakubaliana na wewe 100% kuhusu chimbuko la matatizo yetu yote yanayotukabili nchini mwetu nayo ni UBORA WA ELIMU YETU na hiyo inaanzia chini kabisa na sio chuo kikuu tu, ni bado hatujaweza kuweka msingi imara ktk elimu yetu ya chini kwa maana nyingine mfumo wetu hautuandai vyema kuweza "kuelimika"...kwa mfano ktk maisha yangu yoote nchini mwetu sijawahi kusikia hata siku moja serikali ikiongelea urekebishwaji na uboresishwaji wa mitaala ya shule za msingi sekondari, mfumo uliopo ndio ule ule alioacha mkoloni... kuna mambo mengi hapa kwa mfano ukweli ni kwamba ktk nchi yetu lugha ambayo inatumiwa na kueleweka bila matatizo yeyote na watu wetu ni KISWAHILI sasa ni kwa nini mtoto afundishwe masomo yote kiingereza?? mimi nikichukulia uzoefu wangu shule ya msingi tulifundishwa kila kitu kiswahili, baada ya hapo nikabahatika kusoma tabora boys ambayo ilikua inajulikana kama shule maalumu kwa watu wenye vipaji maalaumu, na kule kila kitu kikabadilika ghafla na kuwa kiingereza na ukweli ni kwamba mimi pamoja na wenzangu tulipata shida sana na tukawa hatuelewi mwalimu anachosema kwa hiyo tukawa tuna buruzwa tuu na miaka inakwenda.. swali langu ni kwamba Je ni kwa nini mtu anashindwa kuliona hilo?? hauwezi ukafanikiwa ktk masomo yako vizuri kama hata lugha unayofundishiwa hauilewi vizuri... Na hii inajionyesha ktk mambo mengi nchini mwetu sasa ukija kwenye mikataba ni kwa nini mkataba uandikwe kiingereza? kwa nini usitafsiriwe? Je hauoni kwamba kama mkataba ungeandikwa kwa lugha yetu yule aneusoma labda ingeongeza uelevu wake na kisha labda ingesaidia kiasi fulani? Kwa hiyo mambo ni mengi na yote chanzo chake ni kimoja nacho ni kuutambua na kuukubali UKWELI nakisha baada ya hapo kuanza kuufanyia kazi, na mimi nafikiri kwanza kabisa tukubali kwamba sisi kiingereza sio lugha yetu hivyo basi haiwezekani kama mtu amezaliwa na kukulia Tz kuweza kukimudu vizuri Kiingereza kiasi cha kuweza kuelewa vizuri kinachoongelewa darasani au kwenye vitabu (mtanzania wa kawaida ni yule anaeshi magomeni au sinza au temeke)...
Kimsingi, nakubaliana na wewe kwa hoja ulizozijadili. Kwanza, ni kweli elimu yetu ina matatizo kuanzia elimu ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu. Mwalimu fulani alikuwa akisema elimu ya msingi ina matatizo sana na yanaletwa na uongozi mbaya ngazi za juu. Alisema waalimu wanapewa malengo, wakiambiwa 'ushindi ufikie asilimia fulani'.
Kwa hiyo, wanafanya juu-chini wanafunzi wao wawe karibu na ushindi huo ili kulinda kibarua chao. Hiyo inatoa mwanya wa rushwa (kuibia mitihani na kununua vyeti bandia). Alisema pia yeye alishapata matatizo kwa kuwa na msimamo wa kuwakatalia waalimu wenzake alipoambiwa awaachie wanafunzi wajaribu bahati yao.
Kwa hilo, alilaumiwa na waalimu na wanafunzi kuwa haitakii shule yake ushindi mzuri. Hivyo, aliwekwa kwenye listi ya kufukuzwa na akaamua aondoke pale (shule ya binafsi) na kuajiriwa shule ya serikali. Alisema pia hata huko anakumbana na matatizo yaleyale.
Pili, lugha siyo tatizo - tatizo ni waalimu kukosa motisha au kuwa na waalimu wasio na uwezo mkubwa na utaalamu wa kufundisha. Baadhi ya waalimu hawataki kuulizwa maswali darasani. Wanataka wanafunzi waelewe tu hata kama hawajafundishwa vizuri kiasi cha kuelewa.
Kuna Watanzania wanaofahamu lugha ngeni vizuri sana: Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kichina, Kiarabu... na hata lugha zingine za Afrika. Mimi naamini kuwa mwanafunzi akifundishwa vizuri lugha yoyote ataelewa tu. Tatizo kwetu hapa ni kwamba wanafunzi wanafundishwa kukariri majibu ya mitihani na siyo kukuza ubunifu, uwezo wa kufikiri na kuhoji vitu na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya jamii au mazingira yanayowazunguka. Elimu ya namna hii haijengi bali inabomoa tu.
Vilevile elimu lazima ijenge dhamiri njema na maadili mema (informed conscience & moral standing) ili kwamba mwanafunzi anapohitimu masomo yake awe pia na uwezo kwa kutofautisha chema na kibaya na siyo kuona hivyo viwili vikifanana. Elimu inayokuza ubinafsi haiwezi kamwe kuwa elimu bora na haijenge dhamiri/maadili mema.
Tuondokane na elimu inayotufanya tuendelee kula mapanki, kuua kundi fulani la watu na kutumia baadhi ya viungo vyao au kuwaingilia watoto wetu kinyume na maumbile ili tufanikiwe kibiashara, kuharibu miundo mbinu ili tufanye biashara ya vyuma chakavu, kuingiza bidhaa feki, kuendela kuvaa 'Kafa Ulaya' na kufuja mali ya umma.
Tatu, hata lugha yetu ya Kiswahili hatuijui vizuri. Tunaongea Kiswahili kibaya (siyo sanifu) kama tusivyoweza Kiingereza (sanifu). Ndiyo maana mimi naamini tatizo siyo lugha ni ubora wa elimu nzima ndio tatizo. Hata lugha zetu za kiasili hatuzijui sawasawa. Na tukishaondoa Kiingereza (tunachosingizia), hata baadaye tutaona Kiswahili kinatushinda na tutaanza kujifunza kwa lugha zetu za asili.
Na baadaye tutaona pia hatuwezi na tutarudia lugha za kigeni. Kuondokana na tatizo hili, kwanza tuwe na waalimu bora (waliobobea vizuri katika masomo wanayofundisha na wapewe nafasi za kujiendeleza) na wapewe motisha.
Nne, baada ya kuwa na soko huria, serikali yetu imeshindwa kabisa kusimamia vizuri vipaumbele: elimu, afya, usafiri na huduma nyingine muhimu. Kwa upande wa elimu, tunaona kuna vitabu vingi sana ambavyo havijahakikiwa vizuri (yaani, vina makosa mengi ya kitaaluma na lugha) likini vitabu hivyo vimeruhusiwa kutumika shule za msingi na sekondari. Elimu imekuwa mradi wa watu fulani wajanja na badala ya kuipanua na kuiboresha wanaendelea kuiangamiza. Watanzania, tuamke!