Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, ameisifu Katiba ya mwaka 1977 huku akitoa rai kwa vyama vya upinzani, hususan Chadema, kuheshimu na kushiriki kikamilifu kwenye chaguzi kwa mujibu wa Katiba iliyopo.
Padri Kitima alieleza kuwa, licha ya kuwepo mijadala kuhusu katiba mpya, Katiba ya sasa bado ina uwezo wa kuhakikisha uwazi na ushiriki wa kila mtu katika siasa.
“Katiba hii imerekebishwa mara kadhaa na bado inatosha kutuongoza kushiriki siasa kwa ufanisi. Muhimu ni kuielewa na kuzingatia ili kuimarisha demokrasia yetu,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa msingi wa Katiba hiyo uliwekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. “Hii ni Katiba nzuri iliyoundwa na Nyerere, mtu wa Mungu. Msisitizo wetu kama TEC ni kuendeleza katiba hii ya Nyerere,” aliongeza.
Kauli ya Padri Kitima imekuja wakati ambapo Chadema na baadhi ya vyama vingine vya upinzani vimeonekana kusitasita kushiriki uchaguzi hadi katiba mpya itakapopatikana, hatua iliyozua mjadala mkubwa nchini.
Your browser is not able to display this video.
Tunachokijua
Padre Charles Kitima ni katibu wa baraza la maaskofu katoliki Tanzania (TEC) ambaye alipata daraja takatifu ya upadre takribani miaka 27 iliyopita ambapo mwaka 2022 aliadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Upadre katika Parokia ya Kristu Mfalme Siuyu Jimbo Katoliki Singida mahali alipozaliwa.
Mnamo Oktoba 26, 2024 katika Viwanja vya parokia ya Kristu Mfalme Tabata lilifanyika adhimisho la Misa Takatifu na Warsha kwa Waamini Wakatoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, misa hiyo ikiongozwa na Mhashamu Stephano Musomba Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Katika warsha huo kwa waamini wakatoliki jimbo kuu la Dar es salaam yalifanyika mawasilisho yenye mafundisho kuhusu mada mbalimbali ambapo padre Charles Kitima aliwasilisha mada inayosema “Utume wa siasa”
Kumekuwepo na chapisho la video liloambatanishwa na maandishi yenye yanayomtaja padre Charles Kitima kuwa amesema hatuhitaji katiba mpya, CHADEMA waheshimu katiba tuliyonayo.
Je ni upi uhalisia wa chapisho hilo?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa video na maandishi katika chapisho hilo vinapotosha uhalisia wa kile ambacho kilizungumzwa na Padre Charles Kitima kwa sababu video hiyo imekatwa katika vipande vidogovidogo kutoka kwenye video halisi na kuunganishwa hatimaye kupotosha ujumbe wa msingi uliotolewa na padre Kitima.
Hata hivyo kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya Jambo TV haijachapisha video hiyo inayoonesha kuwa ya televisheni hiyo ya mtandaoni wala maneno hayo yanayodaiwa kuwa yamesemwa na Padre Kitima.
Katika wasilisho lake padre Kitima alisema hapingi mchakato wa katiba mpya, lakini kwa sasa taifa linaweza kuendelea kutumia katiba iliyopo licha ya mapungufu yaliyopo lakini inaweza kufanya watu wakashiriki siasa vizuri huku akikumbushia juu ya vyama vya siasa akivitaka kuendelea na katiba iliyopo wakati mchakato wa katiba mpya ukiendelea.
Video halisi iliyochapishwa na Tumaini TV katika mtandao wa Youtube inapatikana hapa, ambapo unaweza kuanza kuitazama kuanzia 3:53:41
Attachments
Fr. Dr Charles Kitima Secretary-General of the Tanzania Episcopal Conference (TEC).jpg