Padri Kitima: Pato la Mtanzania kwa sasa halina uhalisia

Padri Kitima: Pato la Mtanzania kwa sasa halina uhalisia

Papaa Mobimba

JF-Expert Member
Joined
Jan 27, 2018
Posts
882
Reaction score
3,337
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha uchumi shirikishi katika mchakato wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza Jumatatu, Januari 13, 2025, katika Mkutano wa Kamati ya Dini Mbalimbali Kuhakiki Rasimu ya Dira hiyo, uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa TEC, Kurasini, Dar es Salaam, Dkt. Kitima ameeleza wasiwasi wake kuhusu usawa wa pato la Mtanzania.

Dkt. Kitima ameeleza kuwa, ingawa pato la wastani la Mtanzania kwa sasa linakadiriwa kuwa Shilingi milioni 3 kwa mwaka (sawa na Dola 1,200), zaidi ya 60% ya Watanzania hawafikii kiwango hicho. Amesema kuwa pengo kubwa la kipato linaonekana wazi, huku pato la taifa likitegemea zaidi sekta kubwa kama madini, ambazo mara nyingi hazinufaishi Watanzania wa kawaida.

“Zile Shilingi milioni 3 zinazosemekana kuwa pato la Mtanzania kwa mwaka, hata hapa hakuna wanazozipata. Wengi wetu tunabebwa na kampuni kubwa zinazozalisha madini. Hili kundi linalozalisha mali kufikia Shilingi milioni 10 kwa mwaka (sawa na Dola 4,000) linapaswa kuwa Watanzania kwelikweli,” amesema.

Dkt. Kitima amependekeza kuwa sekta binafsi ya Kitanzania inapaswa kushika uchumi wa nchi ili kuhakikisha kuwa pato la Shilingi milioni 11.7 linalolengwa kufikia 2050 (sawa na Dola 4,700) linawafaidisha Watanzania wengi, badala ya kuwa kwa wachache.

“Kama Shilingi milioni 11.7 zitakuwa za watu wachache, hatutakubali. Hili pato la Shilingi milioni 3 limeonesha siyo za watu wote,” ameongeza.

Akigusia elimu bure, Dkt. Kitima ameipongeza serikali kwa kuwezesha watoto wengi kuhudhuria shule za sekondari kupitia ujenzi wa shule za kata. Hata hivyo, amebainisha kuwa changamoto za kiuchumi bado zimeendelea kuwakumba wazazi, ambao wengi wanashindwa kumudu gharama za sare za shule na mahitaji mengine muhimu.

“Wazazi wengi, hata baada ya kupata chakula na malazi, hawana hata Shilingi laki moja kwa mwaka ya kumudu gharama za shule. Hii inaonesha kuwa bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kiuchumi, licha ya kuwepo kwa elimu bure,” amesema.

Dkt. Kitima amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa uchumi shirikishi, akisema kuwa viongozi wa dini wanapenda kuona uchumi ambao unawahusisha Watanzania wote, ili kuhakikisha kwamba maendeleo ya taifa yanawafikia watu wa kada zote.

Mkutano huo umewaleta pamoja viongozi mbalimbali wa dini nchini ili kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Maoni yaliyotolewa yalilenga kuhakikisha kuwa Dira hiyo inajumuisha mahitaji na matarajio ya Watanzania wote kwa ajili ya maendeleo endelevu.
 
Mh! mbona wanatetea au sadaka zimepungua nini..?
 
Tunamtegemea kusimamia uchaguzi wa mwenyekiti CHADEMA kama Lissu alivyoomba.
 
Back
Top Bottom