John Haramba
JF-Expert Member
- Feb 4, 2022
- 365
- 1,374
Kundi la watuhumiwa wa uhalifu ambao wengi wao ni vijana maarufu kwa jina la ''Panya Road'' wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Kinyerezi Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za unyang'anyi wa kutumia silaha (mapanga).
Mtuhumiwa wa kwanza Daud Abdallah, 22, Mkazi wa Tungini pamoja na wenzake 16 walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Fadhili Luvinga kusomewa mashtaka nane yanayowakabili.
Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Serikali, Michael Ng'hoboko, Avelina Ombock na Nancy Mushumbusi walidai kuwa watuhumiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo tarehe 24/04/2022 maeneo ya Chanika Ilala Jijini Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao kwa pamoja na wengine ambao bado wanatafutwa walifanya matukio kwa Wananchi mbalimbali kwa kutumia mapanga na kujeruhi kwa lengo la kupora mali.
Waendesha Mashtaka walidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na waliomba tarehe kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali.
Watuhumiwa wote walikana mashtaka yao. Kesi hiyo iliahirishwa mpaka tarehe 27/5/2022 na wamepelekwa rumande kwa kuwa makosa waliyoshtakiwa nayo hayana dhamana.