PEMBETATU YA USHINDI: KUELEKEA MABADILIKO
Na. M. M. Mwanakijiji
Njia ya Dr. Slaa kuingia Ikulu inapitia moja kwa moja katika migongo na mabega ya Zitto Kabwe na Freeman Mbowe. Na pamoja nayo inapitia katika pembetatu ya watu hawa watatu kuongoza shambulizi la mwisho katika wiki hizi mbili zilizosalia kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010.
Kama kuna kiongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema anayeamini kuwa ipo nafasi nyingine ya kugombania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushinda nje ya nafasi hii ya 2010 basi mtu huyo anajidanganya. Kama wapo wanachama na mashabiki ambao wanaamini kuwa wakati wa kugombea Urais na kushinda siyo sasa na hivyo wasubiri hadi 2015 au 2010 watu hao vile vile wanajizuga wao wenyewe. Endapo viongozi, wanachama na mashabiki wa Chama hicho maarufu cha upinzani nchini hawatafanya yote wanayopaswa na wanayoweza kufanya katika wiki hizi mbili za mwisho za kampeni basi ndoto ya kuupata Urais itatoweka kama umande wa alfajiri.
Nalazimika kuandika hili kama kuwatia shime wale wote ambao wanataka kweli mabadiliko nchini kupitia chama hicho kuondoa vizuizi vyote vya kihisia na kiakili na kutumia nafasi hii ya kihistoria kuweza kuigombania ipasavyo nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano.
Mkakati wowote wa kutaka kupata wabunge wengi zaidi na siyo kupata Urais wa Jamhuri ya Muungano ni mkakati uliokubali nafasi ya kudumu ya upinzani. Kama viongozi na mashabiki wa Chadema wanapita na kuhamisha watu wawachague wabunge ili kuwe na wabunge zaidi Bungeni ili kwa kufanya hivyo waanze kusikilizwa zaidi na CCM basi watu hao wanakuwa wamekubali nafasi ya upinzani na hawako tayari kuwa watawala. Mkakati wa kupata wabunge wengi ni mkakati mzuri isipokuwa pale tu unapoendana na lengo zima la kutaka nafasi ya urais vile vile.