SoC02 Peni na jembe vishikwe pamoja

SoC02 Peni na jembe vishikwe pamoja

Stories of Change - 2022 Competition

Erny1165

Member
Joined
Jul 31, 2022
Posts
8
Reaction score
5
Kwa kitambo sasa nchi yetu imekua ikiamini kuwa kilimo ndio uti wa mgongo kwa ukuaji wa uchumi wa taifa letu. Lakini vijana wengi bado wanakosa moyo wa kuamua kufanya kilimo.

Kila kukicha tunasikia vilio juu ya ukosefu wa ajira kwa vijana, kutwa vijana hawa wanazunguka na bahasha mitaani wakisaka nafasi za kuajiriwa serikalini au hata kwenye sekta binafsi na wanapokosa hukaa wakilaumu kuwa wamesoma na hakuna ajira.

Licha ya hayo yote serikali haijaacha kupeleka na kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao shule hata kama hamna nafasi za kutosha kuajiri watoto hao. Imani ya serikali ni kuwa huyu kijana anapomaliza kusoma basi aweze kuhusianisha "peni yake na jembe" yaani taaluma yake na jembe ama fursa nyingine yoyote ya kujiajiri ila zaidi ni kufanya kilimo chenye tija, lakini je ni kijana gani aliye tayari kwa hilo?

Kwa muda sasa nimekaa na kujiuliza ni kwanini vijana hawaendi shambani?
Majibu yanakuja mengi sana ila linaloshikiliwa na wengi ni kuwa vijana ni wavivu kulima.
Ni kweli kabisa vijana wengi wa karne hii hususani walio wasomi ni wavivu sana kufanya kilimo wengi wetu tunapenda pesa nyepesi ndiyo maana tunahangaika kutafuta maofisi tuajiriwe tukae ofisini na kuweka sahihi tu ila hatuko tayari kujishughulisha moja kwa moja kwenye kilimo licha ya faida kubwa iliyopo kwenye shughuli hii. Kwani chakula cha majumbani, viwanda, makampuni ya vyakula na vinywaji, vyote hivi vinategemea mazao ya kilimo

swali jingine nililojiuliza baada ya kusikia hoja za uvivu ni.

Je, vijana wote hawajihusishi na kilimo kwasababu ya uvivu?
Jibu ni hapana sio wote hawashughuliki na kilimo kwa sababu ni wavivu wengine wanatamani sana ila zipo sababu kadhaa ambazo zimeendelea kuwavunja moyo kwa mda mrefu kama vile

Kwanza wanakatishwa tamaa na hali duni za kiuchumi walizonazo wakulima wengi, hali za wakulima walio wengi kwa sasa nchini mwetu ni ngumu kwelikweli hivyo kupelekea vijana wengi kutoona umuhimu wa kufanya kilimo, lakini! huyu kijana kabla ya kufikia kuhitimisha kwamba kilimo hakina faida akaacha kulima hajiulizi kwanini wafanyabiashara wa mazao ya kilimo wanakua vizuri kiuchumi, hii inajenga picha kuwa bidhaa za kilimo zina faida sana ila changamoto kubwa inayowarudisha nyuma wakulima ni kukosa elimu muafaka juu ya kilimo chenye tija.

Mifumo ya uendeshaji wa shughuli ya kilimo kwa wakulima walio wengi imekua ni ya kiholela bila kuhusisha utaalamu ndiyo sababu nikasema "Peni na Jembe vishikwe pamoja", Kilimo kikifanywa kitaaluma zaidi tutapata mazao yenye ubora na ya kuaminika sokoni hivyo kumnufaisha mkulima.

Aidha vijana wanakata tamaa kutokana na kukosa mitaji kwaajili ya kufanya kilimo, ni ukweli usiofichika kuwa ni lazima uwe na mtaji kwaajili ya kununulia pembejeo, vifaa vya kulimia, eneo la kulimia n.k ili uweze kufanya kilimo lakini vijana wengi wamekua wakishindwa kutokana na kukosa mahala pa uhakika wanapoweza kupata fedha hizo ili kufanya kilimo hali inayopelekea wengi kukata tamaa ukizingatia asilimia kubwa wanatokea mazingira ya kipato cha chini.

Kukosekana kwa sera za mda mrefu za kilimo zinazoongeza tija kwa mkulima ni changamoto ambayo imefanya hali za wakulima kuwa duni na hata kukatisha vijana tamaa.

Lakini pia bei nyong'onyeshi ya bidhaa za kilimo kwenye masoko ukilinganisha na gharama za pembejeo hivyo kufanya kilimo kuonekana hakina faida.

Je, ni nini kifanyike ili kutatua haya yote?
Mifumo ya elimu iwe ni yenye kulenga kumjengea kija uwezo wa kufanya mang'amuzi juu ya kilimo chenye faida na si kufanya kilimo cha holela au cha kufata mikumbo ili kuongeza faida kwenye sekta hii na kama ikiwezekana kwenye kila taasisi ya kielimu patolewe elimu ya kilimo kama somo la ziada lisilokua la hiari ili kupa wataalamu wengi zaidi.

Uwepo wa sera endelevu za muda mrefu zinazochagiza kuongeza tija kwenye kilimo mfano sera ya "KILIMO KWANZA" ya JM Kikwete iligusa moja kwa moja kilimo na hata ile sera ya "TANZANIA YA VIWANDA" ya JP Magufuli iligusa kilimo na ni ya mda mrefu maana asilimia kubwa ya viwanda vinategemea mazao ya kilimo.

Kuwapa vijana mikopo yenye riba nafuu ili kusudi kwamba suala la mtaji lisiendelee kuwa changamoto kwao.

Pia serikali ijitahidi kutoa ruzuku za kutosha ili bei za pembejeo na vifaa vyote vya kilimo iwe kwenye kiwango ambacho kinabebeka kwa vijana walio wengi.

Lakini pia bei elekezi za bidhaa za kilimo masokoni ziendane na gharama za maandalizi ili kumletea mkulima faida, hivyo kabla ya kuweka bei utafiti ufanyike kuona wastani wa gharama anayoweza kutumia mkulima kwenye shughuli nzima ya ulimaji wa bidhaa yake.

Mpaka sasa nimeona wizara ya kilimo chini ya waziri Hussein Bashe ikifanya kazi kubwa ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kwa sekta hii kazi kubwa inaendelea kufanyika ili kuhakikisha vijana wanasaidiwa kuhakikisha wanajishughulisha na kilimo kutokana na umuhimu mkubwa wa sekta hii kwenye taifa letu.

Hivyo basi niwasihi vijana, tufunguke fikra zetu tutumie fursa na mianya iliyopo kwenye sekta hii kujiajiri, elimu tuliyonayo na nguvu tulizonazo tuziunganishe na kuzipeleka shambani kwani huko kuna faida kubwa sana badala ya kuzunguka na bahasha tukidai tumesoma tunahitaji ajira. Serikali inaendelea kufanya wajibu wake basi na sisi kama vijana tucheze kwenye nafasi yetu ONYESHA UTHUBUTU SASA.

"Kumbuka kwa kuthubutu kwako kuingia shambani leo unaweza kuwatengenezea ajira mamia kwa maelfu ya vijana watanzania leo"

Fanya maamuzi sasa na uingie shambani "Rudi shambani kumenoga"

Makala hii imeandaliwa nami
Ernest Modest Mpira
 
Upvote 0
Back
Top Bottom