IamBrianLeeSnr
JF-Expert Member
- Nov 10, 2022
- 2,010
- 4,179
MSURURU wa visa vya mauaji ya kutisha na vituko vingine vya ajabu vinavyoendelea kuripotiwa katika eneo la Gusii, umeibua hofu tele miongoni mwa wakazi na Wakenya kwa ujumla.
Viongozi wa kidini na wazee wa Baraza Kuu la Jamii ya Abagusii wanaungama kuwa, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, basi eneo hilo litageuka Sodoma na Gomorah.
Mauaji hayo ya kiholela yamekuwa yakihusishwa na uhalifu wa kupangwa wa hali ya juu, matatizo ya kiakili, migogoro ya kifamilia kati ya sababu nyinginezo.
Tukio la kwanza la kushtusha lilikuwa Disemba 14, 2022, wakati mtoto Junior Sagini aling’olewa macho na kisha kutelekezwa katika shamba la mahindi kijijini Ikuruma, kaunti ndogo ya Marani. Mtoto huyo kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa serikali. Inaaminika waliomng’oa macho walidhamiria kumuua ili asije kurithi shamba la babake ambaye ni mgonjwa.
Washukiwa watatu ambao ni nyanya, binamu na shangazi ya mwathiriwa wamekamatwa na wanangoja kesi yao kutajwa Jumatano ijayo.
Awali, Oktoba 26, mwanaume alimuua na kumzika kisiri mkewe ndani ya kaburi la kina kifupi lililochimbwa kando ya shamba la mahindi. Haya yalitokea katika kijiji cha Ensakia, eneobunge la Borabu, kaunti ya Nyamira.
Mume huyo aliingiza mwili wa mke wake kwenye gunia, kabla ya kuuzika. Sababu za mauaji hayo hazikubainika mara moja.
Ijumaa wiki jana, mwanaume wa umri wa miaka 31, aliwakata kinyama wanawe wawili wasichana kwa upanga na kisha kuitupa miili yao ndani ya shamba la mahindi. Watoto hao ni wa umri wa miaka miwili unusu na miezi kumi. Mshukiwa huyo kwa jina Nelson Momanyi Ontita, anasemekana kuwa na akili punguani. Jumatatu wiki hii, alifikishwa katika mahakama ya Ogembo lakini hakujibu mashtaka.
Maafisa wa upelelezi waliomba siku 14 kumaliza uchunguzi wao ikiwemo kumfanyia mshukiwa vipimo vya kiakili.
Wakenya walipokuwa wakisherehekea mwaka mpya, familia moja Nyamira ilikuwa ikiomboleza kwa kumpoteza jamaa yao aliyeuawa kikatili. Mwili wa Ezekiel Nkeere, mwalimu mkuu wa shule moja ya msingi Nyamira, ulipatikana kwenye banda lililokuwa likitumiwa kufuga kuku. Ulikuwa umekatwa vipande vipande na kisha kufunikwa kwa zulia.
Ulikopatikana mwili wa mwalimu huyo ni kwa nesi mmoja ambaye hadi kufikia sasa hajakamatwa. Familia ya mwendazake imeilaumu serikali kwa mwendo wa kobe kuwakamata waliomdhulumu ndugu yao.
Siku hiyo hiyo, mwanaume wa miaka 37 alikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii, baada ya kuumwa uume wake na mkewe. Nusura mwanamke huyo anyofoe sehemu hizo za siri, lakini madaktari walidhibiti hali yake. Ugomvi ulizuka baina ya wanandoa hao wawili katika mtaa waishio wa Nyanchwa.
Jumapili, baba mwingine wa miaka 67, alimuua mwanawe wa miaka 31 kwa kumpiga jembe utosini. Inasemekana wawili hao waligombania suala lisilojulikana kijijini Igonga, eneobunge la Bonchari.
Kulingana na padre Lawrence Nyaanga wa Parokia ya Kisii Cathedral, ongezeko la visa vya mauaji ni kutokana na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo pombe na bangi.
Padre huyo pia anahoji kuwa, katika siku za sasa, watu hawamuogopi Mungu na si wote wanaojali hali za wenzao.
Kauli yake iliungwa mkono na mchungaji Charles Mayore wa kanisa la Worldwide Gospel Churches of Kenya lililoko Otamba.“Dawa za kulevya zimeongezeka na zinauzwa kila mahali. Polisi wengi huchukua hongo kutoka kwa wauzaji na watengenezaji wa pombe haramu ili kuendelea na biashara zao. Sababu nyingine ni kutoshughulika na watu wanaoonyesha mzongo wa mawazo,” padre Nyaanga akasema.
“Watu hawawapendi wenzao siku hizi. Ikiwa unampenda mumeo au mkeo au wanao, unaweza kuwaua kweli? Hizi ni ishara za mwisho zilizotabiriwa kwenye vitabu takatifu. Suluhu tu ni kumgeukia Mungu. Makanisa na misikiti ichukue jukumu kuhamasisha umma kumgeukia Mungu,” Bw Mayore anasema.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Abagusii, Araka Matundura, anasema kama baraza, wameshangazwa na kutamaushwa na mauaji hayo ambayo sasa yamepaka tope jamii.
Alihoji kuwa kuna haja ya mikutano ya mara kwa mara kuandaliwa ili kuwapa nafasi watu wazungumze kuhusu yanayowakwaza.
“Ipo haja mikutano mingi ifanyike na watu waambiwe wafungue roho zao kuhusu yanayowasibu. Ndio, hali ya maisha ni ngumu, lakini kuna haja ya kustahimiliana,” mwenyekiti huyo anasema.
Takwimu za polisi zinadokeza kwamba, mnamo 2021, jumla ya watu 126 waliuliwa katika kaunti ya Kisii.
Kaunti ndogo ya Nyamache iliongoza kwa visa 18. Kenyenya ikafuata kwa visa 17 na Kitutu ya Kati ikawa na visa 15 vya mauaji.