Kilango amjibu Kisumo
na Martin Malera
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM), ameeleza kusikitishwa na matamshi yaliyotolewa dhidi yake na mwanasiasa wa siku nyingi, Peter Kisumo.
Kilango, mmoja wa wabunge walio mstari wa mbele kukemea vitendo vya ufisadi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali wakiwa bungeni na nje, alisema tuhuma zilizotolewa na Kisumo dhidi yake ni za kutumwa.
Mbunge huyo ambaye ni mke wa Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela, alitoa matamshi hayo jana wakati alipofanya mahojiano ya simu na Tanzania Daima.
Kilango ambaye alifikia hatua ya kusema kwamba alikuwa akiwafahamu waliomtuma Kisumo hata kutoa matamshi hayo, alisema ataendelea kusimama kidete kupambana na mambo ambayo yanakitia doa chama chake na serikali.
Pasipo kuwataja kwa majina wale anaoamini kuwa wamemtuma Kisumo, mbunge huyo alisema alikuwa bado haamini sawasawa iwapo kauli dhidi yake zimetolewa na mwanasiasa wa kariba ya Kisumo, aliyejijengea heshima ndani ya chama na serikali kwa miaka mingi iliyopita.
Hivi kweli maneno hayo ni ya Kisumo ninayemfahamu mimi! Kisumo yupi? Kisumo ninayemjua mimi ni yule mwanachama mkongwe wa CCM, anayepaswa kuilinda CCM na serikali ili isidhalilishwe na mafisadi.
Kisumo ninayemfahamu mimi ni kiongozi wa siku nyingi, ambaye amewahi kuwa mbunge, waziri na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, anapaswa kujielekeza kwenye majukumu ya chama, alisema Kilango kwa kujiamini na kwa sauti kali.
Akifafanua kuhusu kutumwa kwa Kisumo, mbunge huyo machachari, alisema maneno aliyotumia mwanasiasa huyo dhidi yake yanatokana na mazungumzo ya ndani kati ya wabunge wa CCM na Katibu Mkuu wa chama chao, Yussuf Makamba.
Kisumo si mbunge. Haya maneno ya kikao cha ndani cha wabunge wa CCM na Makamba cha sisi kuzuiliwa kuikosoa serikali kayatoa wapi? alihoji Kilango.
Pamoja na hilo, Kilango alieleza kushangazwa na maneno aliyotoa Kisumo akidai kwamba yeye (Kilango) alikuwa hana sifa ya kuwa hata naibu waziri katika serikali.
Kisumo anasema eti mimi sina hata sifa ya kuwa naibu waziri. Amepata wapi sifa za watu wanaotakiwa kuwa mawaziri au naibu mawaziri? alihoji Kilango.
Alisema Kisumo anapaswa kujua kuwa, yeye (Kilango) ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na analifahamu Azimio la Butiama na madhara ya kutokemea maovu yanayotendwa na baadhi ya viongozi wa serikali ya CCM.
Alisema Kisumo, mtu aliyepata kushika nyadhifa za juu za ukuu wa mkoa na uwaziri zama za Serikali ya Awamu ya Kwanza, anapaswa kujua kuwa yeye (Kilango), alichaguliwa kwa kura kuingia bungeni na akala kiapo cha kukijenga chama, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ufisadi unaangamizwa nchini.
Kutokana na kulitambua hilo, alisema ataendeleza msimamo wake wa kuikosoa CCM, na kwamba yuko tayari kwa lolote wakati anapokabiliana na kukemea vitendo vya kifisadi.
Nataka Kisumo ajue, nitasimamia ninachokiamini, nitaendelea kukemea kwa nguvu zangu zote viongozi na watendaji waovu, kwa sababu wanakidhalilisha chama na serikali, na mawazo ya Kisumo wala hayanishughulishi, alisema Kilango.
Mbali ya hayo, Kilango alieleza kusikitishwa pia na tuhuma za Kisumo dhidi ya mwana CCM mwingine, Aggrey Marealle, za kuhoji sababu za kutoa misaada Moshi Mjini hata kufikia hatua ya kusema hana sifa za kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Katika hili, Kilango alisema matamshi hayo ya Kisumo yamemfanya agundue sababu za CCM kushindwa katika jimbo hilo la uchaguzi kila wakati.
Alisema anaamini kwamba, moja ya sababu za chama hicho tawala kulipoteza jimbo hilo kwa wapinzani ni kuwapo kwa wanachama wenye mawazo kama ya Kisumo. Kwa vipindi viwili mfululizo jimbo hilo linaongozwa na Mbunge wa CHADEMA, Philemon Ndesamburo.
Sizungumzii nani anapaswa kuwa mbunge Moshi Mjini, lakini Kisumo hawezi kutoa kauli ya kuonyesha nani anafaa au nani hafai kuwa mgombea, hii maana yake, yupo mtu anayemtaka yeye na hilo si jambo zuri, alisema Kilango.
Kwa upande wake, Marealle, alikataa kuzungumzia kwa undani kauli ya Kisumo kumponda, akisema asingependa kutoa kauli yake pamoja na kusisitiza kuwa, alikuwa anayo haki ya kutoa msaada wowote kwa chama chake pale anapoona inafaa.
Mjadala huu umeibuka siku moja tu, baada ya Kisumo kuzungumza na waandishi wa habari akimshutumu Kilango kwa msimamo wake wa kuikosoa CCM na serikali kila wakati.
Kisumo katika mazungumzo yake hayo ya juzi, alisema Kilango amejivisha jukumu la wapinzani kwa kuishutumu serikali juu ya tuhuma za ufisadi, wakati yeye mwenyewe akiwa mwanachama na mbunge anayetokana na chama hicho.
Kauli hiyo ya Kisumo kwa wadadisi wa mambo inaweza kukumbusha msimamo wa mwanasiasa huyo mkongwe aliyejitokeza hadharani kumpigia Rais Jakaya Kikwete debe wakati akitangaza azima yake ya kugombea urais mwaka 2005, kwa kuwataka wazee wenzake kuwaachia vijana kulitumikia taifa.
Kauli hiyo ya Kisumo dhidi ya wazee kwa kiwango kikubwa ilionekana kumlenga zaidi Malecela, ambaye ni mume wa Kilango, aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kutoa upinzani mkali kwa wagombea wengine wa urais, akiwamo Kikwete.