Soma gazeti la Tanzania Daima la tarehe 6 Oktoba 2010 ili kuona jinsi alivyovuta watu wengi zaidi pale Tunduma. Sehemu ya gazeti hilo inasomeka hivi:
"... MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbroad Slaa ametoboa siri ya mahusiano ya karibu kati ya Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulhaman Shimbo, na mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete.
Alisema uhusiano wao wa karibu, ulimfanya Luteni Jenerali Shimbo apate zabuni tata ya kuingiza matrekta madogo (Power Tillers) na ndio sababu ya kiongozi huyo wa jeshi kutoa kauli ya kuwatisha wapiga kura ili kulinda maslahi yao.
Dk. Slaa, alifichua siri hiyo jana wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Tunduma, kwenye uwanja wa michezo katika mkutano huo mkubwa unaoelezewa kuwa umevunja rekodi ya mahudhurio tangu kuanza kwa kampeni za urais.
Dk. Slaa ambaye amekuwa akivuta hisia za wengi kwenye mikutano yake ya kampeni, alisema Shimbo yuko kwenye mtandao wa Rais Kikwete, aliojiunga nao mwaka 2005 na ndio sababu ya kuamua kutoa kauli ya vitishio ili kumlinda Kikwete ambaye ni mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), asing'oke madarakani. Akifafanua madai dhidi ya Luteni Jenerali Shimbo, Dk. Slaa alisema aliingizwa kwenye mtandao wa Rais Kikwete mwaka 2005, hivyo alimtaka afafanue kwamba kauli aliyoitoa hivi karibuni kuhusu usalama wa nchi ni ya JWTZ au yake binafsi inayolenga kulinda mahusiano yake na Kikwete..."