Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Mkutano wa TANU Mnazi Mmoja, mwaka wa 1954
(Picha ya Tanganyika Information Services)
Hiyo hapo juu ni picha ya Viwanja Vya Mnazi Mmoja kama ilivyokuwa katika miaka ya 1950.
Nimejaribu kutambua baadhi ya nyumba lakini sikuweza kwa kuwa mimi nilizaliwa 1952 na hadi kuwa na akili ya utambuzi ni katika miaka ya 1957 lakini hizo nyumba upande wa kulia ni nyumba zilizokuwa New Street mtaa uliokuwa ukianzia Arab Street ukamalizikia Morogoro Road.
Ikiwa hivi ndivyo nyumba ya mwisho mkono wa kushoto itakuwa Kiungani Street na mtaa unafuatia ukielekea Morogoro Road ni Somali Street (Mtaa wa Omari Londo), Kirk Street (Mtaa wa Lindi ) na hiyo nyumba inayoonekana mwisho itakuwa iko Kipata Street (Mtaa wa Kleist Sykes).
Kuanzia hapo Somali kwa sasa katika Mtaa wa Lumumba liko jengo la Elimu ya Watu Wazima na Jumba la Washirika.
Kushoto ni sehemu tupu hapo ni Kidongo Chekunde. na mbele zaidi kuelekea Mtaa wa Msimbazi hapakuwa na majengo yoyote na nakumbuka kulikuwa na lingo la kuni kubwa watu wakija kununua kuni na miti ya kujengea ikiitwa, ''milingo.''
Saad Juma Mzee mtu mashuhuri sana katika historia ya vilabu vya mpira Dar es Salaam akiwa kiongozi wa Sunderland Football Club (Simba Sports Cub) alikuwa na biashara kubwa ya lingo la kuni.
Sehemu hiyo karibu na lingo la kuni palikuwa panapigwa kilua ngoma ya Wamanyema siku za Jumapili.
Sehemu hiyo pia palikuwa na biashara nyingi zikifanywa na akina mama kama kuuza togwa na biashara nyingine ndogondogo.
Hivi sasa sehemu hiyo ndipo palipojengwa viwanda vidogovidogo vya SIDO.
Watu wengi mashuhuri katika siasa za kupigania uhuru na ndani ya TANU waliishi katika mitaa hiyo.
Ukoo wa Sykes walikuwa na nyumba mbili New Street na Kipata na ndipo aipoishi baba yao Kleist Sykes kabla ya kuhamia Aggrey Street 1942, Zuberi Mtemvu akiishi Somali Street, Dossa Aziz, Mbaruku Street ambako babu yangu alikuwa na nyumba lakini akiishi Kipata Street nyumba iliyokuwa ikitazamana na nyumba ya Kleist Sykes.
Ibrahim Hamisi mmoja wa waasisi wa African Association alikuwa akiishi Kipata Street na Congo Street nyumba ya ya kwenye kona.
Mwanzo wa mtaa wa Kipata ndipo akiishi Abdallah Matimbwa mmoja wa wanaushirika wa mwanzo na alitoa gari yake kama mtaji wa kuanzia.
Mbele ya nyumba ya Abdallah Matimbwa kulikuwa na uwanja mkubwa ambako kulikuwa na chuo cha Sheikh Omar Mtiro, baba yake marehemu Balozi Abdulkarim Mtiro (Cisco) na Sheikh Hassan bin Ameir katika miaka ya 1940 alikuwa akidarsisha hapo.
Katika uwanja huu hapo Kipata watu wakileta biashara zao kuuza hasa akina mama na inasemekana haleti mtu biashara hapo ila itanunuliwa yote.
Wazee wanasema ilikuwa ni barka ya Qur’an iliyokuwa ikisomeshwa hapo.
Hapo sasa unauona Mtaa wa Msimbazi na Shule ya Kitchwele Girls School alipokuwa akisoma dada yangu na akisomeshwa na Mwalimu Maunda Plantan na Mwalimu Blandina aliyekuwa shoga wa mama yetu.