Norbert Mporoto
Member
- Jul 18, 2020
- 14
- 12
Na. Norbert Mporoto.
Tanzania.
Mei 15, 2021
Uhuru wa taifa la kenya ulibisha hodi kwa furaha, lakini utawala wenye mizizi na mabaki lukuki ya chembechembe za kikoloni uliitia doa historia ya taifa hilo. Miaka miwili mara baada ya uhuru, historia iliandika kifo cha kwanza cha mwanasiasa, mwanaharakati na mwandishi wa habari mashuhuri aliyeuawa katika mazingira tatanishi.
Anafahamika kwa jina la Pio Gama Pinto, mwenye asili ya India na mzaliwa wa Kenya. Historia ya maisha yake ilianza kuandikwa mapema Machi 3, mwaka 1927. Alitokea kwenye familia ya kawaida, baba yake akifanya kazi ya Afisa katika serikali ya kikoloni na mama yake akiwa mama wa nyumbani. Wawili hawa walipata mtoto kutoka kwenye familia hii yenye asili ya Goa Konkani, jimbo la Maharashtra. Pio alilelewa katika misingi na malezi ya kikatoliki hadi alipofikisha umri wa miaka nane, hapo ndipo alipopelekwa nchini India ili kuanza elimu yake.
Waswahili husema nyota njema huonekana asubuhi. Akiwa nchini India alisoma kwa miaka tisa na kufaulu mtihani wake wa elimu ya msingi na baadaye kujiunga na shule ya sekondari ya St. Joseph, Arpora. Baada ya hapo alijiunga na chuo cha sayansi cha Kurnatak, Dharwar kwa miaka miwili na baadaye kujiunga na jeshi la anga la nchini India mnamo mwaka 1944. Baada ya kuhitimu mafunzo ya jeshi alipata kazi ya ukarani mjini Bombay, wakati akiendelea na kazi hakuacha kujihusisha na harakati za kupinga mifumo ya kidhalimu iliyofanywa na utawala wa kireno wakati huo. Alishiriki migomo na maandamano ya kupinga utawala wa serikali ya kikoloni iliyofanyika mjini Bombay na hatimaye akafanikiwa kuanzisha Goa National of Congress, ikiwa ni taasisi itayohakikisha inauondoa utawala wa Kireno nchini India.
Harakati zake zilipoanza kuwa mwiba kwa utawala wa Kireno, Pio Gama Pinto alilazimika kurejea nchini Kenya akikimbia sekeseke la kuwekwa kizuizini nchini Cape Verde, kisiwa ambacho wanaharakati wengi waliopingana na utawala wa kireno walitupwa huko. Na wakati huo akirejea nchini Kenya, nchi ilikuwa bado mikononi mwa Waingereza. Mara baada ya kurejea alibahatika kufanya kazi kama mwanahabari katika gazeti la Colonial Times na baadae The Daily Chronicle.
Mwangaza mbili mbambo mwenga kumuengaenga. [Mshika mawili moja humponyoka]. Ni misemo tu ya hapa nyumbani, Afrika. Safari ya kurejea nchini kenya ilitosha kuwashawishi waliomzunguka kumtaka Pio Gama Pinto kuongeza majukumu mengine ya kifamilia. Ama hakika penye penzi hapapotei.
Mwaka 1953 nchini Kenya, familia moja ya kabila la Goa ilitembelewa na mlimbwende aliyeitwa Emma. Uzuri wake, tabasamu na kila kitu kilichomtafsiri mwanamke mzuri kilikuwa ndani yake. Kilichowashangaza wengi ni kwamba mrembo Emma hakuwa na mpenzi, basi ikawa purukushani miongoni mwa wanaume ambao walitamani kutia nia. Wakati huo Pio Gama Pinto alikuwa hakauki vinywani mwa watu, wengi wakimchukulia kama mmoja wa askari wanaounda jeshi la MAU MAU, wengine wakimtizama kama mwanaharakati mwenye mrengo wa kushoto wa kisiasa, na skendo nyingi zaidi zilikuwa juu yake. Anton Filipe Da Gama Pinto, baba mzazi wa Pio aliamini ndoa ndiyo kitu pekee kitachoweza mtuliza mwanae na kuachana na masuala ya harakati za ukombozi. Basi baba yake hakusita kuratibu mipango ya Pio kuonana na Emma jijini Nairobi kwani aliamini Emma ni mwanamke atayemfaa mwanae.
Pio alimuaminisha Emma kuwa ni mtu sahihi kwake, kama ujuavyo penzi ni kama majani huota popote palipo rutuba. Miezi mitatu baadae jina la Emma halikukamilika bila Gama Pinto, jijini Jinja nchini Uganda Emma Gama Pinto na mumewe waliifurahia fungate yao. Hatimaye wakarejea jijini Nairobi, katika chumba kidogo ambacho Pio alikuwa akiishi katika nyumba ya rafiki yake, naam hapakuwa kwake. Hilo halikuwa jambo lililofifisha upendo wa wawili hawa, kwani uzito wa upendo toka katika vilindi vya mioyo yao haukuwa na tafsiri iliyopimwa kwa mzani wa thamani ya vito, ila upendo wenyewe. Itoshe kusema Emma hakuwa kama dada zangu wa Buguruni Kimboka au Manzese Uwanja wa Fisi. La! Hakuwa miongoni mwa wale ‘slay queen’ wenye tamaa mithili mchwa. Nachombeza tu, ila kuna cha kujifunza.
Baada ya muda wazazi wake Emma walimtembelea binti yao nchini Kenya, furaha yao iliwaisha baada ya kuona binti yao anaishi katika mazingira ya ufukara jambo ambalo liliwafanya kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwawezesha wanandoa hawa kujikimu. Licha ya fedha, waliwapa pia zawadi ya gari. Maisha ya ufahari haikuwa kipaumbele kwa Pio, hakusita kuchukua kiasi cha fedha alizopewa na wakwe zake na kwenda kulipia katika ofisi moja ya uchapishaji kwa ajili ya kuandaa jarida aliloliita “The Uzword” kwa madhumuni ya kupigania uhuru wa watu wake, jarida ambalo baadae lilifungiwa muda mchache baada ya kuanzishwa.
Mwaka 1954 miezi mitano baadaye baada ya kuoa, akiwa mbioni kuanzisha ‘The East African Goan National Association’ Pio Gama Pinto alikamatwa kufuatia operesheni maalumu na kuwekwa kizuizini katika kisiwa cha Manda kwa muda wa miaka mine. Licha ya swaiba zake walioshirikiana na J.M Nazareth kuanzisha taasisi watu wa Goan katika Afrika Mashariki, jitihada zao ziliangukia mikononi mwa serikali ya wakoloni walioshirikiana na Wareno. Hatimaye taasisi hiyo ilifutiliwa mbali. Haikuishia hapo kwani huo ulikuwa mwanzo tu wa masaibu hayo, baada ya kuachiwa mwaka 1958 aliwekwa kizuizini tena na kuzuiwa kutoka nje ya maeneo ya Kabarnet.
Linalokuwepo machoni na moyoni lipo pia, hulka ya Pio Gama Pinto kunako mawanda ya ukombozi wa bara la Afrika na uhuru wa mtu mweusi ulionekana machoni na moyoni mwake. Historia yake ilivuka mipaka na kushika hatamu kwenye nchi tofauti baada ya kukutana na rafiki yake wa fikra na itikadi, pia mwanaharakati mwenzake Malcom X mwaka 1959. Kama ilivyo ada ndege wafananao huruka pamoja, ikawa hivyo kwao. Kitu pekee kilichowakutanisha ni mfanano wa ufikiri na mipango ya harakati zao juu ya ukombozi wa watu weusi. Hapa ndipo heshima ya Pio Gama Pinto itakumbukwa katika bara la Afrika hasa kwa ushawishi wake wa kumtaka Malcom X aendeshe harakati zake katika nchi za kiafrika chini ya vuguvugu la umajumui wa kiafrika [Pan-Africanism]. Kwa ushawishi huo inasadikika Pio Gama Pinto ndiye aliyemkutanisha Malcom X na viongozi wa kiafrika wa nyakati zile akiwepo Patrice Emile Lumumba.
Katika harakati zake Pio alifanya kazi kwa ukaribu na chama cha FRELIMO cha nchini Msumbiji, mara kadhaa alifika jijini Dar es Salaam na kuonana na wanachama wapigania Uhuru wa Chama hicho ili kujadili mikakati ya kuisaidia Msumbiji katika harakati zake za kujinasua na ukoloni. Hata katika siku chache kabla hajauawa alinukuliwa akisema anataraji kujiuzulu na kazi za Bunge ili akaishi mikoa ya Lindi au Mtwara kwa ajili ya kusaidia mapambano ya Uhuru nchini Msumbuji.
Harakati zake zilizidi shamiri kwa kasi pamoja na kupitia misukosuko lukuki. Mwaka 1960 mara baada ya kutoka kijijini Kabarnet alianzisha Kampuni ya uchapishaji aliyoipa jina ‘PAN AFRICAN PRESS LTD’ ambapo alianza kuchapisha gazeti la Sauti ya Afrika (Voice of Africa), Pan Africa na Nyanza Times huku yeye akiwa Mkurungenzi na Katibu wa magazeti hayo. Ufanisi na weledi wa kuifikia jamii yake ulifanya watu kumjengea imani kubwa na kufanya mwaka 1964 kuteuliwa kuwa mwanachama pekee wa baraza la wawakilishi ndani ya serikali kupitia chama cha KANU. Mwaka huohuo alianzisha Taasisi ya Lumumba ambayo ilikuwa ni chombo cha kuwafunza maafisa wa vyama juu ya masuala ya kisiasa na utawala bora.
Pio Gama Pinto akiwa ameiva na kuusimamia vyema ujamaa alikuwa na mikakati mingi ikiwemo kuunda serikali ya kijamaa nchini Kenya. Kupitia kuundwa kwa serikali hiyo aliamini huo ndiyo utawala pekee ambao utaondoa matabaka na unyanyasaji wa watu weusi katika bara la Afrika na walio nje ya bara la Afrika. Jambo kubwa katika mikakati yao waliyojiwekea na kuafikiana ilikuwa ni kwenda mbele ya Umoja wa Mataifa kuishutumu Marekani juu ya vitendo vyake vya kibaguzi kwa watu weusi.
Yote hii ilikuwa ni jitihada za kuusimamia ukweli! Lakini kama ilivyokuwa kawaida ya wapigania uzalendo (acha wale ambao walilewa sifa) kupotezwa, basi Pio Gama Pinto aliangukia mikononi mwa kinywa cha mabepari hao. Akiwa na miaka thelathini na nne tu, ndoto yake ya kuutetea ujamaa na mipango mingine mingi iliishia tarehe 25 Februari, 1965 ikiwa ni siku tatu tu baada ya kifo cha nduguye Malcom X. (Inadhaniwa wauaji walidhamiria kuwaondoa wawili hawa kutokana na mikakati yao waliyokuwa wameazimia juu ya ukombozi wa watu weusi).
Kunako matanga pamekufa mtu. Pinto akiwa ametoka kumpeleka mkewe kazini ili naye ajiandae kuelekea kazini ndipo umauti ulibisha hodi, akiwa nje ya geti akisubiri afunguliwe mlango ndipo risasi nne zilimiminika zikielekezwa kwenye gari lake kupitia mlango wa dereva. Sababu za kifo chake hazikuwekwa wazi, ila kwa sababu ilikuwa ni kawaida ya wazalendo hawa kupotezwa basi iliaminika kwamba Pinto alipita mkondo ule ule.
Mlenga jiwe kundini hajui limpatae, mara baada ya umauti kifo chake kiligubikwa na sintofahamu kiasi kwamba ukweli ulijichimbia kaburi. Kijana chipukizi wa miaka ishirini na moja, Kisilu Mutua alijikuta hatiani akishikiliwa kwa mauaji hayo. Baada ya kesi kurindima kunako Mahakama, kuta nne zilisikia sauti ya Jaji akitoa hukumu ya kifo kwa Kisilu Mutua kufuatia mauaji ya Pio Gama Pinto. Kwa sauti ya uungwana na yenye kujawa uchungu Kisilu alisikika akisema “sikuua, sikuua” huku Jaji akisistiza kwamba hatoi hukumu hiyo kwa mtuhumiwa kana kwamba yeyé ndiye muuaji bali anamuhukumu kwa kuhusika na walioua. Maamuzi ambayo yalimuacha kinywa wazi mtuhumiwa akihoji “je muuaji ni nani?”
Miaka thelathini na sita baadae, baada ya sekeseke la kunusurika na hukumu ya kifo mnamo mwaka 2000 Kisilu Mutua alitoka gerezani kwa msamaha wa Rais Daniel Arap Moi, huku akikanusha tuhuma hizo na kuelekeza kwa genge la Kiambu “Kiambu Mafia” kuwa ndiyo waliotekeleza shambulio hilo, lakini hakuna ukweli unaothibitisha moja kwa moja ni nani hasa alihusika na mauaji hayo!
“Pio ni sehemu ya historia yetu, ni sehemu ya sisi tulivyo. Tuliuona upendo wake juu ya nchi hii kupitia kazi zake. Ni lazima tuwape heshima wale ambao kupitia nguvu zao nasi tunaweza simama imara” alinukuliwa mama Wangari Muta Maathai.
Ni kweli, chanda chema huvikwa pete na kivuli cha mavuno hufunika walio mbali; baada ya miezi michache (takribani saba), Septemba 1965 mkewe Bi Emma Pinto alialikwa mjini Santiago jijini Chile, katika hafla ya utoaji tuzo za waandishi wa habari wa kimataifa. Katika hafla hiyo alipokea tuzo ya heshima ya mumewe ikiwa ni kuthamini mchango wake katika habari na ukombozi wa bara la Afrika kutoka mikononi mwa tawala za Kikoloni.
Pumzika pema shujaa na mwanamapinduzi wa kiafrika, Pio Gama Pinto.
#UhuruniFikra #Mporotowrites #MashujaawaAfrika #AfrikaNyumbaniView attachment 1786201
View attachment 1786202