Pole shetani

balozi SDG 10

Member
Joined
Apr 17, 2024
Posts
8
Reaction score
8
Mbinguni kuna hukumu,amewaita manani
Malaika walo zamu,aridhi na samawini
Idadi wameshatimu,walo watu na majini
Umeonewa shetani?

Mikao ni kwa kaumu,watu wa zama fulani
mitume yao hashimu,ilotumwa duniani
Wamekaa kwa nidhamu,kikao kiso amani
Umeonewa shetani?

Mkuu wa mahakimu,aliyeketi enzini
Baada ya kusalimu,akaanza na shetani
Huyu bwana mdhalimu,aloleta tafarani
Umeonewa shetani?

Bwana shetwani rajimu,mkazi wa duniani
Upelekwe jahanamu,miaka ya sulemani
Kwa kosa la kuhujumu,kutia watu dhambini
Umeonewa shetani?

Machozi kwikwi za pumu,akigaa gaa chini
Imemzidi hukumu,anaomba afueni
Kulea ana jukumu,mama watoto nyumbani
Umeonewa shetani?

Utungo nime ukimu,jambo nawaelezeni
Yatawakuta magumu,mkijitia dhambini
Tuishini kwa nidhamu,haki usawa na dini
Umeonewa shetani?

#Mwl.Bakari
#Muungwana
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…