Ntawajibu wote kwa mpigo!
Ni miaka karibu 50 sasa tangu tupate Uhuru wetu, kutoka makucha ya Wakoloni na Ubepari, lakini kama jamii inayojitawala, bado hatujaweza kuzinduka kutoka kwenye Usingizi wa Pono na Cherekochereko za kuelewa kwa nini tumepata Uhuru.
Tumelewa nderemo na vifijo, lakini kujituma na kujitutumua kujitumikia na kujiboresha ina kuwa ni vigumu kwetu bila kusukumwasukumwa na hivyo masikio na mategemeo yetu yote ni kuwa tutakuwa na Kiongozi fulani atakayetuletea neema kama Mana kutoka mbinguni.
Watanzania tunatabia mbaya sna ya Utegemezi na kusubiri tufanyiwe kazi au tuletewe matunda tuyafurahie. Ama ni asili yetu kutokana na Vizazi vya Mababu wa Mababu zetu waliishi maisha ya kuridhika kwa kujipatia kile cha kutosha na bila kufikiria kile cha kesho au ni dhahiri kuwa sisi ni jadi yetu kuwa Wavivu na tuna mategemeo makubwa na mengi kuliko uwezo wetu.
Suala la kusoma au kujielimisha si la mtu kwenda Chuo Kikuu, kuwa mtaaluma au mtaalamu au umahiri fulani wa kunyumbulisha au kukokotoa mambo, bali ni hata vitu vidogovidogo na dhahiri ambavyo havihitaji mtu awe na Udaktari!
Fikiria jukumu dogo sana la Uraia la mtu kuwa na uwezo wa kupima mbunge au mwakilishi wake. Je ni elimu ya daraja gani inahitajika kubaini kuwa mbunge huyu ambaye kawakilisha jimbo tangu mwaka 1965 ni mbabaishaji mwenye kauli bila vitendo, lakini kila wakati wa kupiga kura tunaruhusu udhaifu na kumpa dhamana ya kuendelea kuwa kiongozi?
Nikimsoma Mwalimu Mbele, naona nasoma fasihi ambayo ni tata na si lazima ipokelewe kuwa anaifagilia CCM au kumfagilia Kikwete. Waweza niita Ngwini, lakini mimi nimepokea anachosema Mwalimu Mbele kwa kujipima nafasi yangu kwanza kabla ya kunyooshea Serikali na Kiongozi Mkuu kidole.
Ni kweli tuna udhaifu wa hali ya juu katika safu ya Uongozi na mfumo wa Kisiasa Tanzania na inajionyesha mapokeo yake hata kwa jamii tunavyofanya mambo yetu.
Tulianza safari yetu baada ya kupata Uhuru vizuri sana kwa kuwa na mshikamano na msisimko wa kujitawala na kujiongoza. Lakini katika safari hii, hatukuwa na nidhamu au uwezo wa kuhimili safari na ugumu wa safari yenyewe kwa kuwa tulidhania kuwa kwa kujitawala na kuwa huru, basi kama Mgogo mambo ni Mswano na kama Mnyiramba tutasema ni wakati wa kujiogoga.
Mara nyingine inakuwa kana kwamba tumekwama kwenye tope au tumepotea jangwani bila kujua tunakoelekea wala kujua ni mbinu gani zinahitajika tujikwamue kutoka kwenye tope.
Tumeridhika sana na udhaifu na umasikini na kama mkimwangalia Kikwete anavyolalama kila siku kuwa hajui ni kwa nini Taifa letu ni masikini au kutokuelewa kwake yeye Kikwete kuwa vitu havipatikani kwa urahisi bali vinahitaji si mikakati tuu, bali pia ufuatiliaji, utaona taswira karibu ya kila Mtanzania inafanana na Rais wetu.
Sasa kama safu ya viongozi wetu tumeshaizoea kuwa ni ya watu kama Kikwete au kama sisi ambao hatujitumi au kujitutumua, kwa nini tuogope kumpa dhamana mtu mpya tusiyemjua ili naye tujifunze kwake? Au lile la Zimwi likujualo lina pande mbili la sisi kama Raia na Wananchi kuridhika na mfumo butu na mfumo wetu kuridhika na sisi Raia na Wananchi BUTU?
Unapokubali kuonewa na kuburuzwa kila siku bila kusimama kidete na kutunisha misuli kulinda utu wako na haki yako, daima utaendelea kuwa mnyonge na kuamini kuwa ni haki yako kuwa mnyonge. Ni mpaka pale utakapo amka na kujitutumua na kupukuta mavumbi na kuanza kutetea na kujivunia utu wako na kuweza kusimama na kuitetea nafsi yako bila woga kwa ujasiri, ndipo utakapoanza heshimika na yule aliyemnyanyasaji ama atalegeza kamba au kufungasha virago na kuondoka.
Tulipigania Uhuru kwa nguvu sana, je ili kuwa ni kwa sababu gani? Je ni ile chuki yetu ya kufanyishwa kazi na Mkoloni katika nchi yetu? mbona tabia hiyo bado tunaendelea nayo popote pale ambapo tupo nje ya kujitawala wenyewe?
Angalia Watanzania walioko Diaspora, wengi ni mahiri na wanajituma kwa bidii katika kila nyanja hata kama ni Udereva Teksi. Watanzania walioko nje ya nchi wanafanya kazi kwa kujituma, juhudi ,maarifa na kwa nidhamu za hali ya juu, inakuwaje nyumbani tunashindwa kuwa na nidhamu na mvuto ule ule wa kuwa wachapakazi hodari wenye kutumia juhudi na maarifa?
Je tutalaumu mishahara na ufinyu wa vipato? mpaka lini tuendelee kulialia kuwa tunapunjwa? Je tumeshasimama na kumhoji yule tuliyempa dhamana ya kutuongoza na kufanya mipango ya maendeleo nchini mwetu na kutaka kujua ni lini tutaona maendeleo chanya au msukumo chanya?
Wakati wa Nyerere, tulikuwa na mategemeo mengi, tuliposhindwa kupata tulichotaka (ambacho ukweli mpaka leo hatukijui), tukasema hafai na katuletea umasikini. Ndio maana kuna wengine wanaamini kwa dhati kuwa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ndio chimbuko la Umasikini wa Mtanzania.
Akaja Mwinyi ambaye tukamshangilia kwa utawala wake unaofanana na Babu au Mjomba poa, maduka yakajaa, tukaanza kuchekelea neema ya fahari ya macho na kuimba ruksa kama vile basi tumefika ile nchi tulioahidiwa. Tukachukua bilauri na kata na kuanza kujipongeja kwa maduka na bidhaa kuongezeka, lakini sisi wenyewe kufanya kazi kujizalishia ikawa ni shida.
Mkapa akatuambia sisi ni wavivu na wenye wivu, tukakasirika na kuzira, akahamasisha mipango ya sisi kujihujumu wenyewe na kuwa Taifa linalotegemea uagizaji na si uzalishaji wa ndani kama vile Mwinyi alivyofanya, tukanyamaa kwa miaka 10 akishirikiana na wenzake ambao walishaamini kuwa sisi ni Zimwi liliwalo, haliwezi kwisha kulika kutokana na UBUTU wetu, na kama zawadi ya kazi nzuri aliyofanya ambayo imelihujumu Taifa, akahakikisha tunapewa mtu dhaifu kama kiongozi na tukampokea Kikwete kwa vifijo na nderemo!
Sasa Kikwete kafanya lile tulilojua mapema na kwa hiari tukampa dhamana, leo tunahamaki?
Msishangae kwa Mchungaji kuunganisha nafsi yake katika kujisuta pamoja na kuwa wengi wenu mnamshangilia anavyomchambua Kikwete na uongozi wa CCM. Siwezi kujitoa kutoka lawama kisa nimeandika s c r ew Muungwana au Ajizi ya Kibuge.
Ninachofanya ni kukubali wazi kuwa sisi kama jamii, tutaendelea kutaabika mpaka pale tutakapoanza kubadilisha mienendo kwa kujipima wenyewe kwanza, kujihakiki na kujiwekea nidhamu na malengo katika ubinafsi na nafsi zetu kama mtu mmoja mmoja, ndipo tutakapoweza kwenda kwa umoja kama Taifa.
Lakini, nimewahi kuuliza mara kadhaa hapo awali, je tafsiri ya Mtanzania ya maendeleo na utajiri ni nini? sijapata jibu la uhakika na hata kama leo tutasoma majedwali ya kimataifa yanayoonyesha viwango vya umasikini na utajiri, je tunavielewaje kwa nafsi zetu na mazingira yetu?
Mmeuliza kwa nini nilihoji watu kukaa vijiweni Dar, nitawaambia hili, pale Dar na hata mikoani ambako niliona watu wakiamka asubuhi kwenda kulibwia tembo na si kufanya kazi, kuna nafasi nyingi sana za Watanzania kuweza kujiendeleza kiuzalishaji mali na si lazima iwe kwa kupitia kuajiriwa.
Ndio maana nikakaa chini na kuhoji kama tulilipokea Azimio la Arusha kwa makosa na hivyo sera za Ujamaa na baadhi ya vipendele tulivyoviimba kwa nguvu kuwa hatutaki Ubepari au watu binafsi kuwa wazalishaji huru ni sehemu moja na nyeti inayohusiana kwa kiwango kikubwa na Umasikini, Unyonge na Udhaifu wa Mtanzania (na hili la UUU ni kwa mtazamo wangu, mtu mwingine anaweza kusema karidhika na alichonacho na hana tatizo!).
Hivyo, binafsi, Mwalimu Mbele, JMushi, Tumain, Mwanakijiji na Michuzi tunajukumu la kujihoji nafsi na kujichambua na kujipima je tunajipimaje kama wananchi na ni halali kwetu kuelekeza vidole vyote vya lawama kwa mtu mmoja au Serikali bila kuhoji nafasi yetu katika matatizo yanayotukabili?
Uchanga wa Tanzania na Watanzania na ufinyu wa upeo, si jambo la kupuuziwa, na ndio maana Mzee Mwanakijiji ana kampeni ya kuleta mabadiliko mwaka huu. Lakini mabadiliko si kumuondoa Kikwete na kutuletea Mwakyembe kisa eti tunapiga vita Ufisadi. Je tukimwondoa Kikwete na kumleta Mwakyembe, Sitta, Lipumba au Sitta basi ndipo tutabadilika fikra?
Nakumbuka wakati Mzee Mwinyi na Azimio la Zanzibar lilipokuja, nakumbuka suala la cost sharing lilipokuja, sisi tulidumaa na kupoteza nafasi muhimu kuhoji madhumuni na mbinu zitakazotumika katika mfumo huo mpya. Kama bendera inayofuata upepo, tukaridhika kimya kimya na kukubali kuburuzwa bila kuelezwa kinagaubaga kuwa mabadiliko haya yana maana gani na kwa manufaa ya nani?
Imekuwa ni kawaida yetu, kutafuta mchawi wa kumtupia lawama. Kikwete ana gunia elfu za lawama kutupiwa, CCM ina magunia laki ya lawama kubebeshwa, lakini mimi, wewe na yule na wote katika nafsi yetu ya binafsi kama mtu mmoja mmoja na kwa umoja kama Taifa, tujitwishe magunia yetu Milioni kadhaa ya lawama!
Reverend,naomba nami nikujibu kwa ujumla.
Tulipopata uhuru tulikuwa na matumaini makubwa kwamba wakati umefika wa kusimamia maendeleo yetu wenyewe kwa faida yetu (japo mie nilikuwa sijazaliwa wakati huo).Lakini tusiilinganishe nchi na ndoa,kwamba kama umeoa na kisha kugundua mke/mume ni bomu basi jitihada zitafanyika chap chap ili atalikiwe.Uhuru uliambatana na kuundwa kwa taasisi za utawala na uongozi.Waliojaribu mapema kupambana na kile walichokiona "mwelekeo mbaya wa vioungozi/watawala wetu" waliishia kuwekwa vizuizini.Hapa nazungumzia harakati za kuiondoa serikali madarakani zilizopelekea kesi za uhaini.Whether walikuwa na nia ya dhati ya kubadilisha mambo kwa niaba ya umma au walifanya hivyo kama vibaraka,mie siko katika nafasi nzuri ya kutoa hitimisho.Ninaloweza kusema ni kwamba some tried/dared to try....na matokeo yake tunayafahamu.
Ni rahisi kuwalaumu Watanzania iwapo anayelaumu ana-neglect mfumo wa siasa uliotawala nchi yetu tangu kipindi cha uhuru hadi mwanzoni mwa miaka ya 90 watawala wetu walipolazimika kwa shingo upande kukubali kubadili mfumo wa kisiasa,uchumi na maeneo mengineyo.Hata hivyo,takriban miongo miwili baadaye,Tanzania bado kwa kiasi kikubwa imeendelea kukumbatia mfumo wa kidikteta usioruhusu mawazo mbadala hata kama mawazo hayo ni kwa manufaa ya wananchi walio wengi.Reverend,unatarajia nini kwa mwananchi wa kawaida wakati watawala wetu wanamwaga mamilioni ya fedha za walipa kodi kuhakikisha nafasi zao zinaendelea kuwa salama?Hapa nazungumzia matumizi mabaya ya vyombo vyetu vya dola na usalama ambavyo vimeendelea kuwa sehemu muhimu ya hegemony ya CCM.
Kwa anayesoma juu juu mtazamo wa Reverend,anaweza kuamini kuwa Watanzania ni sado-masochists wanaopata raha kutoka kwenye mateso na uonevu wanaokumbana nao kila kukicha.Ukweli ni tofauti sana.Laiti siku itapokuja tukabaini, kwa mfano, ni namna gani CCM imekuwa ikivutumia vyombo vya dola kudumisha utawala wake,ni dhahiri kuna wenzetu watakaolazimika kuwaomba radhi Watanzania wenzao waliokuwa wakiwatuhumu kwa uzembe wa kutofanya jitihada za kuleta mabadiliko.
Sie hatuna tofauti sana na Wapalestina.Hawafurahii mateso wanayoshushiwa na Waisraeli lakini hawana uwezo wa hapo kwa hapo kukomesha mateso hayo.Na kwa namna hiyohiyo,mateso yanayoendelezwa na tawala kama za Korea ya Kaskazini,Iran,China,Cuba na kwingineko-kama ilivyokuwa kwenye tawala za kikomunisti-sio kitu kinachowapendeza "wateswa" lakini kuendelea kwa mateso hayo ni matokeo ya watawala husika kujenga mazingira ya kuhakikisha kila aina ya upinzani unakuwa crushed na kudhibitiwa kabla haujaathiri "ulaji" wao.Comparative analysis ni muhimu katika kubaini namna mfumo wa kikandamizaji unavyodhibiti kila avenue ya wanyanyaswaji kujikomboa.
Tunapowalaumu Watanzania kwa "kuridhia kila baya" tunapaswa pia kutafiti kwanini "wanaridhia mateso hayo".Na ni muhimu pia kutambua kuwa umasikini wetu unawanufaisha sana watawala.Ikumbukwe kuwa kwa mwenye njaa,pishi ya mchele na sukari inaweza kabisa kumfanya asahau haki yake.Tumbo lenye jaa haliwezi kuelewa habari za "kutumia kura yako vizuri".Watawala wetu wanalitambua hilo na,I hypothise,umaskini wa Watanzania ulio wengi unatumika kama mtaji wa kisiasa kwa watawala wetu kwa vile unawasaidia kuepuka maswali muhimu kama "unatuomba kura sasa wakati miaka mitano iliyopita hukutufanyia lolote kati ya uliyoahidi".Busara zinatueleza kwamba "mpe mtu umaskini na atakuwa mtumwa wako kwa muda mrefu sana".Iliwezekana kwenye slavery na feudalism, na sasa pia inawezekana pia.
Naomba nifafanue kidogo kuhusu mtizamo wako unaposema "
Angalia Watanzania walioko Diaspora, wengi ni mahiri na wanajituma kwa bidii katika kila nyanja hata kama ni Udereva Teksi. Watanzania walioko nje ya nchi wanafanya kazi kwa kujituma, juhudi ,maarifa na kwa nidhamu za hali ya juu, inakuwaje nyumbani tunashindwa kuwa na nidhamu na mvuto ule ule wa kuwa wachapakazi hodari wenye kutumia juhudi na maarifa?
.Hivi umeshajiuliza kwanini wengi wanajituma?Lakini hata pasipo kujiuliza,kwa hapa UK kuna ushahidi wa kutosha wa baadhi ya wenzetu waliobwetekwa baada ya kupewa "makaratasi yao" na wameridhika na social benefits kutoka Idara ya Kazi na Pensheni (DWP).Hawataki kuajiriwa au kuajiriwa kwa vile tu wanajua kila baada ya wiki mbili kuna fedha zinazoingia kwenye akaunti zao.Ukitaka kufanya utafiti,nakushauri uanzie Milton Keynes,Coventry,Birmingham,Reading,Leicester na hata London.However,I noticed you said BAADHI,nami nasema ni section ndogo tu ya wenzetu.
Jibu langu fupi kuhusu ufanisi wa baadhi ya wabongo wanaojituma huku ughaibuni ni kwamba kwa kiasi kikubwa waajiri wa huku wanathamini service ya mwajiriwa.Kama unalipwa kinachotosheleza kumudu maisha yako-na pengine hatimaye kumudu kufanya "vurugu za hapa na pale mtaani"-kwanini usimnyenyekee mwajiri wa aina hiyo?Ni banadamu gani mwenye akili timamu ataipenda kazi inayokulipa mshahara kiduchu kana kwamba mwezi una siku 5?Morali na ufanisi wa watumishi unachangiwa sana na malipo mazuri yanayoendana na mazingira mazuri ya kazi.Lakini pia sheria zinazozuia ubabaishaji pia zinasaidia kuhakikisha kuwa hakuna fursa za wazi kwa "wababaishaji".
Hiyo ni kinyume na ajira za upendeleo zinazotolewa kwa kuangalia majina ambapo si ajabu bosi wako akawa hana hata robo ya sifa za kitaaluma au ujuzi ulionao.Add to that,mshahara kiduchu usio na hakika ya kutoka in time,na mazingira mabaya ya kazi (kwa mfano walimu wanaofundisha watoto wanaokaa chini).Mwajiriwa mwenye utashi hapaswi kufikiri mshahara tu bali pia kile kinachompatia mshahara.
Lakini pia tusiwasahau wakulima walioajirajiri wenyewe mashambani.As I mentioned earlier,hawa ni chaguo rahisi la kuonewa na watawala.Wanashinda mshambani,wanahangaika kupata mazao bora huku mifuko ya pembejeo na mbolea ikirutubisha nyumba ndogo za watawala,lakini wanapopata mavuno wanashurutika kuyapeleka vyama vya ushirika,ambapo mazao hayo yanageuka mtaji wa bure wa viongozi wa vyama vya ushirika...wanakopa na kukopa na baadaye "kuua" vyama huku mkulima akiendela na dua zake kutarajia miujiza ya kulipwa deni lake.
Wamachinga nao.Wanajitahidi kununua bidhaa waziuze kama mobile shops.Badala ya kutengenezewa mfumo mzuri wa ku-encourage kujiajiri,wanageuka maadui nambari wani wa mgambo wa jiji (ambao nao wana uchu wa bidhaa za wamachinga kwa kisingizio cha 'kutekeleza sheria za jiji/manispaa).Akina mama ntilie nao wamegeuzwa migahawa ya bure kwa mgambo hao.Ma"baa meidi" nao wanalipwa mshahara mdogo kuliko idadi ya bia wanazohudumia kwa siku,hali inayowalazimisha kutegemea fadhila za wateja wao huku wakiomba dua wasivunje glasi au chupa za bia-suala linaloweza kuwageuza permanent sex slaves wa bar managers."Mahauzigeli" na "mahauziboi" wameendelea kuwa watumwa waliohalalishwa hasa kwa vile watawala wetu ni miongoni mwa waajiri wao wakuu.Taasisi zisizo za kiserikali zinazoanzishwa kuwatetea zimegeuka miradi muhimu ya kuongezea nyumba ndogo.Badala ya kuletewa mipango ya kujiajiri,watu wale wale wenye majukumu ya kusaidia ajira wanakuja na "dili" za kuwapeleka vijana "shamba" kuleta "unga" utakaozidi kuhujumu uwezo wa nguvukazi ya taifa.Na miongoni mwa "wabuni miradi" hao ni wale wenye jukumu la kupambana na mihadarati!
Na mtizamo wako kuhusu Azimio la ARUSHA ni kana kwamba ilipigwa kura ya maoni ku-seek opinions za wananchi.Tulishurutishwa kulifuata,kuliamini na kulitekeleza.Actually,baadhi ya wachambuzi wanadai kwamba moja ya sababu ya kutofanikiwa kwa Azimio hilo ni namna lilivyowasilishwa kwa umma i.e. kuwalazimisha wananchi walitekeleze pasipo kutaka ridhaa yao.Na hatukulazimishwa kulipokea na kulitekeleza tu bali pia tulishurutishwa kulitukuza kwa nyimbo,mashairi na chereko chereko nyinginezo.Naamini Reverend ulipitia mfumo wa elimu wa enzi hizo,na utakumbuka "ulazima" wa kukupenda chama,kuamini itikadi zake,kukubali usahihi wa viongozi wake na upuuzi mwingine kama huo.Je tulifanya hayo kwa hiari?Nah!Ni katika namna hiyohiyo tawala dhalimu kama za enzi za Taleban,au huko Korea ya Kaskazini zinavyolazimisha matakwa yao kwa watawaliwa.
Naafikiana nawe kwamba ni muhimu kwa Watanzania kujiangalia wenyewe,na ikibidi kujilaumu kwa mapungufu yao (hakuna kiumbe hai aliye absolutely perfect,mie and you included) lakini lawama hizo pia ziendane na hali halisi ya namna wangeweza,wanaweza na wataweza kujikwamua na mfumo dhalimu.Kuna usemi maarufu wa kisiasa kwamba "kwa Afrika chama tawala hakipaswi kushindwa uchaguzi bali 'kinajishindishwa' chenyewe".Suala sio chaguzi zinazoweza kupelekea kuangushwa kwa vyama tawala bali hofu ya watawala kuwa "kikija chama kingine basi tumekwisha".Tuna wakuu wa vyombo vya dola wanao-abuse madaraka yao kwa vile wanafahamu kuwa watawala hawakuwateua kuutumikia umma bali wao (watawala).Wanafahamu fika kuwa "zikija sura mpya zisizo na ubia nao" patakuwa hapakaliki.Na kwa vile wao ni sehemu ya mfumo,kama ilivyo kwa watwala,wanafanya kila wawezalo kuhakikisha mfumo huo dhalimu unadumu as long as it takes.
Labda ufumbuzi ni kizazi cha kujitoa mhanga kama suicide bombers (hapa simaanishi watu wajilipue bali nashauri wajitolee kwa ajili ya manufaa ya wengi).Unless watu wataacha lawama na kuonyesha nini wanachoweza ku-sacrifice kurekebisha madhila yaliyodumu kwa takriban miaka 40,tusitarajie mabadiliko yoyote.Unahitajika ujasusi,hujuma,na kila aina ya mbinu kupambana na mfumo huu dhalimu.Si CCJ wala chama mbadala kinachoweza kuleta mabadiliko ya haraka kwa vile wanausalama wameshapenyezwa huko zamani ili kuharibu mambo pindi utapojiri wakati mwafaka.Adui yetu yuko well-equipped na yuko tayari kwa lolote kuhakikisha anaendelea kutukandamiza.
Bahati nzuri kwake ni kwamba ana nia,sababu,nguvu na nyenzo za kufanya hivyo.
Tuna safari ndefu.