SoC04 Programu ya SANIFU, mkombozi wa lugha ya Kiswahili

SoC04 Programu ya SANIFU, mkombozi wa lugha ya Kiswahili

Tanzania Tuitakayo competition threads

Jaber2024

New Member
Joined
Jun 17, 2024
Posts
2
Reaction score
1
Utangulizi
Lugha ya Kiswahili ni moja kati ya lugha zinazokua kwa kasi ndani na nje ya bara la Afrika. Mpaka sasa, takribani nchi zaidi ya kumi zinatumia Kiswahili barani Afrika kama lugha ya kwanza au ya pili, huku mwamko wa matumizi ya lugha hii ukiwa mkubwa sana. Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, Kiswahili kina wazungumzaji kati ya milioni 60 mpaka milioni 150 na pengine zaidi.

Tanzania ina wazungumzaji wengi sana wa lugha ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha ya taifa inayounganisha zaidi ya makabila 120 yaliyopo nchini. Aghalabu, hata pale ambapo Kiswahili kinatajwa basi neno Tanzania hutajwa pia kama mmiliki wa lugha hii.

Moja ya mafanikio ya lugha ya Kiswahili ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani. Kwa mafanikio kama haya, Tanzania inapaswa kuwekeza na kukibidhaisha barabara Kiswahili ulimwenguni.

Tupo zama za Sayansi na Teknolojia; mambo mengi sasa hivi yanarahisishwa na kuboreshwa kuanzia katika upatikanaji mpaka utendaji wake ili kurahisisha maisha ya binadamu.

Kukibidhaisha Kiswahili katika teknolojia
Ukikitafuta Kiswahili kimataifa katika teknolojia, mara nyingi utakikuta kwenye kamusi mbalimbali za mitandaoni, videoni, vitabuni na kadhalika, na hivi karibuni kiko katika masuala ya programming.

Lipo wazo lingine la namna ya kukiuza Kiswahili mitandaoni na pia likawa msaada mkubwa katika ukuaji wa kimataifa wa lugha hii. Wazo hili ni kuunda programu itakayotumika kuhariri na kuboresha maandishi ya Kiswahili. Programu hii itaitwa SANIFU.

Programu ya SANIFU ni nini?
Hii ni programu ambayo itatumika kuhariri, kusahihisha na kuboresha maandishi/maneno yaliyo katika lugha ya Kiswahili na hata kutoa mapendekezo ya ziada ili kuboresha kile kinachoandikwa.

Pia, itampa mtumiaji maana ya neno au maneno atakayoandika katika programu hii pamoja na kisawe/visawe vyake na maana za visawe hivyo endapo atahitaji huduma hiyo. Hivyo, hakutakuwa na haja ya kutoka katika programu ili kutafuta maana ya neno au kisawe chake.

Mfano:​
  • Mtumiaji akiandika neno dhamiria. Programu itamletea visawe kama kusudia, nuia, azimia, yakinia, pania, shupalia nk. ili kumpa utajiri wa misamiati ya kutumia kuboresha andiko lake.​
  • Mtumiaji akiandika, balua hii ikufikiepo apo uripo. Programu itamsahihisha kwa kumwonyesha usahihi wa sentensi yake ni barua hii ikufikie hapo ulipo.​
Programu itazingatia usahihi wa sarufi – kwa kuangazia aina za maneno, upatanisho wa maneno kisarufi, mofimu, muundo wa sentensi na kadhalika. Pia, itazingatia sintaksia ya lugha ya Kiswahili kwa kushughulikia jinsi maneno yanavyounganika, uakifishaji na kupangika katika sentensi kwa kufuata kanuni, ili kuleta maana sahihi iliyokusudiwa, na kumfanya mtumiaji kuandika kwa Kiswahili sanifu.

Programu hii itaundwa vipi?
Kwa uwekezaji makini kwenye utaalamu wa Sayansi ya Kompyuta, ukusanyaji taarifa (Data) sahihi: kuzipanga vizuri na kuhakikisha zina ubora wa juu. Kujenga mifumo ya Algorithimu kwa kuzingatia Deep Learning inayofanania jinsia akili ya binadamu inavyofikiri na NLP (Natural Language Processing) inayoruhusu kompyuta kuelewa, kuchambua, na kuzalisha lugha kisha kugundua makosa ya kisarufi, matumizi ya maneno, mtindo, na mengineyo.

Yatafanyika majaribio na ufuatiliaji ili kuhakiki usahihi wa programu na kuiboresha mara kwa mara ili kukabiliana na mabadiliko ya lugha na kuongeza utendaji wake. Bila kusahau uwepo wa sera zinazohakikisha taarifa za watumiaji ziko salama.

Programu hii itawafaa akina nani?
  • Wahariri: Itarahisisha sana kazi ya kuhariri miswada, makala na taarifa mbalimbali kwa kutambua kwa haraka makosa ya kisarufi na yale ya kisintaksia.​
  • Waandishi: Itarahisisha uandishi wa Kiswahili sanifu na kupata utajiri wa misamiati inayoboresha maandiko yao.​
  • Wanafunzi: Watapata programu inayowasaidia kuandika vizuri na kujifunza lugha kwa kutumia maneno sahihi hivyo kuendana na kasi ya teknolojia katika elimu.​
  • Wakufunzi: Itawasaidia kusahihisha kazi zilizoandikwa kwa Kiswahili kwa urahisi zaidi.​
  • Watu wanaojifunza Kiswahili: Watatumia Programu kujifunza miundo ya sentensi, misamiati sahihi, upangaji wa maneno na mengine yenye manufaa kwenye kujifunza lugha ya Kiswahili.​
  • Vyombo vya habari, vyuo, shule, balozi, ofisi/taasisi binafsi na za serikali nk: Taarifa, miradi, barua, makala, ripoti, matangazo na vyote vitakavyoandaliwa kwa Kiswahili vitakuwa na ubora unaostahili.​
  • Watu binafsi: Wanaweza kutumia kuhariri kazi zao ndogondogo kwa usahihi.​
  • Watengeneza maudhui wa mitandaoni: watakuwa na njia rahisi ya kufikisha maudhui yao (Captions & Subtitles) kwa kuandika, kusoma au kufasiri kwa Kiswahili sanifu hivyo kukuza Kiswahili sanifu.​
  • Wafasiri: Baada kufasiri kazi kutoka lugha ngeni kwenda Kiswahili. Mfasiri anaweza kuitumia programu hii kuhakiki kazi yake na kuifanya kuwa bora zaidi.​
  • Watafiti: Itakuwa rahisi kuandika ripoti za tafiti mbalimbali kwa Kiswahili, kwani misamiati ya taaluma tofauti tofauti itapatikana kwenye programu.​
Ukuaji
Ukuaji utakuwa wa hatua kwa hatua. Kuanzia katika uundaji wa programu hadi kutumika kwenye kompyuta na sehemu zifuatazo:​
  • Kwenye Kivinjari cha Wavuti (Web Browser Extension) ambapo itatumika kusaidia kurekebisha na kuboresha machapisho na maoni kwenye mitandaoni kama vile Jamii Forum, Facebook, X, LinkedIn, blogu mbalimbali na majukwaa mengine ya majadiliano na tafiti. Pia, katika uandishi wa barua pepe na sehemu kama Google Docs na Microsoft Office.​
  • Kwenye programu za Simu (Mobile Apps)
Kwa hatua hizo hapo juu, lugha ya Kiswahili itakua zaidi na kutumika popote duniani. Na hata kurahisisha kufarisi maandishi mbalimbali mitandaoni kwa Kiswahili sanifu.

Biashara
  • Huduma za programu hii zitatumika kwa kulipia ada ya mwezi, miezi mitatu, sita au mwaka. Bei itapangwa kwa kuangalia gharama za uwekezaji, watumiaji na uhitaji wa soko.​
  • Ushirikiano na majukwaa mengine ya kimataifa yanayohitaji huduma hii utaleta ubia wenye faida.​
  • Biashara yoyote lazima iwe na mikakati thabiti ya masoko na upanuzi ili kufikia watu wengi kwa urahisi zaidi hasa kwa masoko ya kidijitali.​
Kwanini itaitwa SANIFU?
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) neno SANIFU lina maana ya kufanya jambo kwa kufuata taratibu au kanuni zinazokubalika. Au, kufanya jambo kwa ufundi ili kuvutia watu kwa uhodari. Hivyo, jina hili linasadifu vyema jina la programu na kazi zake.

Hitimisho
Ipo changamoto kubwa mno ya uharibifu wa Kiswahili na kusababisha hata wenye nia ya kujifunza usahihi wake kupata taabu ya kuandika na kuzungumza kwa ufasaha. Programu ya SANIFU itakuwa sehemu ya suluhisho, huku pia ikikiuza Kiswahili kirahisi zaidi kama programu, duniani kote na Tanzania ikiwa mwaasisi wa kuundwa kwake.

Tanzania tuitakayo baada ya miaka kumi ni ile itakayowekeza ipasavyo kwenye teknolojia, ubunifu na kukiuza Kiswahili chake kimataifa kwa njia za kisasa zaidi.

Picha ya SANIFU.jpeg

Picha ya Laptop yenye neno SANIFU.
Chanzo: Akili Mnemba (AI)​
 
Upvote 1
Back
Top Bottom