Nimefurahi umenukuu sehemu husika ya Katiba. Huielewi. Maana yake ni kuwa Rais atateua wale tu waliotajwa hivyo na Katiba au Sheria. Kama Katiba au Sheria haikuwataja kuwa wateuliwe na Rais, ni makosa Rais kuwateua. Iko kwenye Mabadiliko ya 13 ya Katiba ya mwaka 2000, na yaliwekwa baada ya mjadala mkali kuwa Rais alikuwa na madaraka mengi kupitiliza ya kuteua.
TAFSIRI POTOFU YA JF MEMBER NDUGU TATHMINI YA IBARA YA 36 (2) YA KATIBA KUHUSU UTEUZI WA RAIS WA MTENDAJI MKUU WA TANROADS.
1. UTANGULIZI.
Ndugu yangu
Tathmini ambaye ni Member mwenzangu wa JF amekosoa vikali makala yangu hapa JF yenye kichwa cha habari kifuatacho;
( Rais Samia ana mamlaka ya kumteua mtendaji mkuu wa TANROADS ). Hoja ya Ndugu
Tathmini ni kwamba Rais ana mamlaka ya kuteua viongozi wa Umma au Watumishi Waandamizi wa Umma ambao wametajwa katika Katiba na Sheria tu kuwa watateuliwa na Rais na sio vinginevyo na hoja yake hii imejikita katika
Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Tatu ya Katiba, 2000 na kinachoitwa historia iliyoambatana na mabadilio ya 13 ya Katiba ya mwaka 2000 . Ndugu
Tathmini ameenda mbali zaidi na kusema kuwa mimi sijui katiba ya nchi, hatahivyo, kwa unyenyekevu mkubwa sana ninawiwa kusema kuwa yeye mwenyewe Ndugu
Tathmini ndo hajui vizuri Katiba ya nchi na historia iliyozunguka na kuambatana na Katiba ya nchi na
Kunga za Tafsiri za Sheria na Katiba pamoja na
Jurisprudensia iliyonyuma ya Katiba ya Nchi na kwa ufupi ni kwamba Ndugu
Tathmini ana uelewa potofu (misconception) kuhusu Katiba ya nchi na hususani
Ibara ya 36 ya Katiba.
Kutokana na hoja hii ya Ndugu
Tathmini, kwa heshima na taadhima ninaomba kutofautiana naye na kwa kuanzia ni maoni yangu kuwa Ndugu
Tathmini haujui Katiba ya nchi na historia na jurisprudensia ambayo imeizunguka na kuambatana na Katiba ya nchi na haujui Kunga za Tafsiri ya Katiba na Sheria (Canons of Constitutional and Statutory Interpretation) ndo maana ametafsiri kwa makosa masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba.
The legal adage by Scottish Novelist one
Sir Walter Scott goes that
“A lawyer without history or literature is a mechanic, a mere working mason; if he possesses some knowledge of these, he may venture to call himself an architect.”
2. TAFSIRI SAHIHI YA KATIBA.
Kwa mujibu wa masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba, kwa kuyatafsiri kwa kutumia
Tafsiri Sisisi (Literal Interpretation), Rais ana mamlaka ya kuteua viongozi wa umma au watumishi wa umma wa aina nne zifuatazo;
(a) Viongozi wa Umma wenye mamlaka ya kutunga sera za Idara na Taasisi za Serikali (e.g Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi na Tume)
(b) Watendaji Wakuu Idara na Taasisi za Serikali ( CEO wote wa Idara na Taasisi za Serikali ikiwemo mashirika ya Umma kama Tanesco, TTCL, NIC etc).
(c) Viongozi wa umma na watumishi wa umma ambao wametajwa na Katiba kuwa watateuliwa na Rais.
(d) Viongozi wa umma na watumishi wa umma ambao wametajwa na sheria zilizotungwa na Bunge kuwa watateuliwa na Rais.
N.B. Pia ni muhimu kuzingatia kuwa masharti ya
Ibara ya 36 (3) ya Katiba, yamepiga marufuku au kuzuia Tume ya Utumishi wa Umma, Tume za utumishi nyingine na mamlaka nyingine za uteuzi kuteua Viongozi na Umma wanaowajibika kutunga sera na Watendaji wa Kuu wa Taasisi za Serikali kwa kuwa mamlaka hayo yako mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na badala yake Tume ya Utumishi wa Umma, Tume za Utumishi nyingine na mamlaka nyingine vimeruhusiwa kuteua watu katika nafasi ambazo sio za Watunga sera na sio watendaji wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali.
Pia, ni muhimu kutambua kuwa Kunga za Tafsiri ya Sheria na Katiba zinaelekeza kwa lazima kuwa katika kutafsiri Katiba au Sheria lazima maneno yaliyotumika katika Katiba au sheria lazima ya tafsiriwe kwa kutumia
Tafsiri Sisisi (Literal Interpretation) yaani yatafsiriwe kwa kupewa tafsiri ya maana ya asili, bayana na ya kawaida ya maneno husika (
Words used in constitutional or statutory text must be given natural, plain and ordinary meaning) labda tu kama matokeo ya kutumia
Tafsiri Sisisi yanaleta maana yenye utata (
ambiguity) au maana yenye upumbavu uliopindukia (
absurdity) au inaleta mzozo au chokochoko (
mischief) ambayo sheria ililenga kuitatua ndipo hapo mbinu tafsiri za katiba na sheria nyingine zinaweza kutumika katika kutafsiri katiba na sheria kama vile (1) Tafsiri ya Kanuni ya Dhahabu (Golden Rule), (2) Tafsiri Chokochoko (Mischief Rule), Tafsiri Lengo (Purpose Approach) nakadhalika. Msimamo huu wa kisheria umewekwa na Mahakama katika kesi kadhaa zenye nguvu ya kisheria na nguvu ya ushawishi nchini Tanzania ikiwemo kesi zifuatazo;
(i) Sussex Peerage Case (1844;1 Cl & Fin 85 (Tindal CJ);
(ii) Singida Regional Trading Company Vs Tanzania Posts & Telecommunication Corporation [1979] L.R.T No. 11 (Chipeta, J);
(iii) Mwinyimadi Ramadhan Vs Republic Criminal Appeal No. 150 of 1963 (Weston, Biron and Reffe, JJ);
(iv) Grey Vs Pearson (1857) 6 HL Cas 61, 106; 10ER 1216, 1234 (Lord Wensleydale);
(v) Becke Vs Smith [1836] 2 M & W 191 (Parke, B).
Pia, msimamo huu unaungwa mkono na Mwanazuoni wa Sheria (Legal Scholar) na Mwanafalsafa wa Sheria (Jurist),
John W. Salmond katika kitabu chake kiitwacho
"Jurisprudence", (Toleo la 12) kuanzia ukurasa wa 132 mpaka ukurasa wa 133 ambao Mbinu hii ya Tafsiri ya Sheria ameipa jina la
Ita scriptum est Principle na pia msimamo huu unaungwa mkono na waandishi wa kitabu maarufu kuhusu tafsiri ya sheria kiitwacho
“Statutory Interpretation” ambao ni Sir Rupert Cross, John Bell and George Engle hususani ukurasa wa 47 wa kitabu hiki.
Sasa, Ndungu yangu Tathmini, ametafsiri masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba kwa kutumia hisia zake binafsi badala ya kutumia
Tafsiri Sisisi (Literal Interpretation) kama inavyoelekezwa na Kunga ya
Ita scriptum est Principle kama ilivyoibuliwa na kutumiwa na mahakama katika kesi tajwa hapo juu ambazo zina nguvu ya kisheria katika Jamhuri ya Muungano kwa kuwa maneno yaliyotumika katika
Ibara ya 36 (2) ya Katiba hayana utata wowote na hayana chokochoko yoyote na upumbavu uliopindukia (absurdity) ndani yake.
3. HISTORIA ILIYOZUNGUKA IBARA YA 36 YA KATIBA.
Maudhui au Masharti ya
Ibara ya 36 ya Katiba ya Nchi hayakuwa katika
Ibara ya 36 ya Katiba wakati Katiba hii ilipotungwa na kuanza kufanya kazi tarehe 26 April, 1977 bali maudhui haya yalikuwa katika
Ibara ya 20 ya Katiba kuanzia mwaka 1977 mpaka mwaka 1985. Masharti ya
Ibara ya 20 ya Katiba yalimpa mamlaka Rais pekee yake ya kuteu viongozi wa umma na watumishi wa umma katika utumishi wa Serikali lakini kwa masharti kwamba pasiwepo na masharti ya Katiba au sheria inayomzuia Rais kufanya uteuzi huo na maana yake ni kwamba Rais hakuwa na uwezo wa kumteua kiongozi wa umma au mtumishi wa umma kama sheria ya mabadiliko ya Katiba au sheria kuu (principal legislation) iliyotungwa na bunge imeelekeza vinginevyo kuwa nafasi hiyo itateuliwa na mamlaka nyingine na hali ilikuwa hivi mpaka mwaka 1985 yalipofanyika mabadiliko ya 5 ya Katiba. Mwaka 1985 maudhui ya
Ibara ya 20 ya Katiba yaliamishiwa katika
Ibara ya 36 ya Katiba kupitia
Kifungu cha 9 cha Sheria ya Mabadikiko ya Tano ya Katiba, 1985 (Sheria Na. 15 ya 1985).
Sheria ya Mabadiko ya Tano ya Katiba, 1985 ilimpunguzia mamlaka Rais ya kuteua Viongozi wa Umma na Watumishi wa Umma kwa namna 3 zifuatazo;
(a) Mamlaka ya kipekee (exclusive power) ya Rais kuteua viongozi wa Umma yalifutwa hivyo mamlaka haya yaliiwekwa mikononi mwa (i) Rais, (ii) Tume ya Utumishi na (iii) Mamlaka za Umma nyingine.
(b) Bunge lilikuwa na mamlaka ya kumnyang'anya Rais mamlaka ya kumteua Kiongozi yoyote wa umma kwa kuhamishia mamlaka ya uteuzi husika kwa tume ya utumishi wa umma au mamlaka nyingine ya Umma kupitia Sheria iliyotungwa na Bunge ikiwemo Sheria ya Mabadiliko ya Katiba , hii ni kutokana na Bunge kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Tano ya Katiba, 1985 kuweka katika
Ibara ya 36 (2) ya Katiba maneno yafuatayo;
"Bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na masharti ya sheria yoyote inayohusika", hii sentensi ilidhibiti mamlaka ya Rais ya kipekee na yasiyokuwa na kikomo kuteua viongozi wa umma na watumishi wa umma.
(c) Mabadiliko ya Katiba hayakutaja kwa bayana (expressly) kuwa Rais ana mamlaka ya kuteua Viongozi wa Umma Watunga Sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali (kama ilivyo bayana kwa sasa hivi kupitia mabadiliko ya 13 ya katiba ya mwaka 2000).
Kinyume na anavyosema Ndugu yetu
Tathmini kuwa madaraka ya Rais kuteua viongozi wa umma yalipunguzwa kupitia
Sheria ya Mbadailiko ya Kumi na Tatu ya Katiba, 2000, hii si kweli bali ni uongo, ukweli ni kwamba kupitia
Kifungu cha 6 cha Sheria ya Mabadikiko ya Kumi na Tatu ya Katiba, 1985 (Sheria Na. 3 ya 2000) madaraka ya Rais yaliongwezwa maradufu kwa namna 4 zifuatazo;
(i) Kwanza, Bunge lilipokonywa au kunyang'anywa mamlaka ya kumdhibiti Rais katika eneo la uteuzi wa viongozi wa umma wakiwemo Watendaji Wakuu wa Idara naTaasisi za Serikali kwa kuwa mamlaka ya Rais ya uteuzi wa viongozi wa umma hayawajibiki tena(not subject to) kwa masharti ya Katiba na masharti ya sheria iliyotungwa na bunge kwa kuwa Rais alipewa mamlaka yasiyokuwa na mipaka ya kuteua Viongozi wa Umma Watunga Sera na Watendaji WaKuu wa Idara na Taasisi za Serikali na mamlaka ya Rais ya uteuzi yasiyokuwa na mipaka yalitokana na
"kufutwa" katika
Ibara ya 36 (2) ya Katiba kishazi (clause) au maneno yafuatayo;
"Bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na masharti ya sheria yoyote inayohusika", hii sentensi iliondoa madaraka ya Bunge kudhibiti mamlaka ya Rais ya kuteua viongozi wa umma watunga sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali kupitia kutunga sheria kwa kuwa hatua yoyote ya kumnyang'anya Rais mamlaka ya kuteua Viongozi wa Umma Watunga Sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali kupitia sheria iliyotungwa na bunge inakuwa ni kinyume na
Ibara ya 36 (2) ya Katiba hivyo hatua hiyo inakuwa batili tangia mwanzo (null et void abnitio) chini ya masharti ya
Ibara ya 64 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama yalivyotafsiriwa na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya
Kukutia Ole Pumbun & Another Vs Attorney General & Another [1993] TLR 159 , baina ya nyingine (among others).
(ii) Mabadiliko ya 13 ya Katiba, 2000 yametaja kwa baya (expressly) kuwa Rais ana mamlaka ya kipekee (exclusive power) ya kuteua Viongozi wa Umma Watunga Sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali, sasa maana ya hii (legal implication) ni kwamba Tume ya Utumishi wa Umma na Mamlaka nyingine wakiwemo mawazi walipokonywa madaraka ya kuwateua Viongozi wa Umma Watunga Sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali.
(iii) Mabadiliko ya 13 ya Katiba, 2000 yaliongeza
Ibara Ndogo ya (3) kwenye
Ibara ya 36 ya Katiba ambapo masharti ya
Ibara ya 36 (3) ya Katiba yalipiga marufuku au kuzuia Tume ya Utumishi wa Umma na mamlaka nyingine kuteua Viongozi na Umma wanaowajibika kutunga sera na Watendaji wa Kuu wa Taasisi na Idara za Serikali kwa kuwa mamlaka hayo yaliwekwa mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kama mamlaka ya kipekee (exclusive power) na badala yake Tume za Utumishi (ikiwemo Tume ya Utumishi wa Umma) na mamlaka nyingine vimeruhusiwa tu kuteu watu katika nafasi ambazo sio za Viongozi wa Umma Watunga sera na ambao sio watendaji wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali.
(v) Kutokana na kufutwa kwa Kishazi (clause) au maneno ;
"Bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na masharti ya sheria yoyote inayohusika", katika masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba kupitia Sheria ya Mabadiliko ya 13 ya Katiba, 2000, moja kwa moja (automatically) bunge lilipoteza uwezo au mamlaka ya kuhamishia mamlaka ya uteuzi viongozi wa umma Watunga Sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali kutoka kwa Rais kwenda kwaTume za Utumishi au mamlaka nyingine ya Umma kama ilivyokuwa hapo awali ambapo bunge lilikuwa na mamlaka hayo kupitia Sheria ya Mabadiliko ya 5 ya Katiba,1985.
4. MSIMAMO WA SHERIA KWA SASA (CURRENT LEGAL POSITION).
Kutokana na maelezo au ufafanuzi huu hapo juu, msimamo wa sheria kwa sasa ni kama ifuatavyo;
(a) Kwa mujibu wa masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba, Rais ana mamlaka ya kuteua viongozi wa umma au watumishi wa umma wa aina nne zifuatazo; (1) Viongozi wa Umma Watunga sera za Idara na Taasisi za Serikali (2) Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali (3) Viongozi wa umma ambao wametajwa na Katiba kuwa watateuliwa na Rais na (4) Viongozi wa umma ambao wametajwa na sheria zilizotungwa na Bunge kuwa watateuliwa na Rais.
(b) Masharti ya
Ibara ya 36 (2) na
(3) ya Katiba, yamepiga marufuku au kuzuia Tume za Utumishi na mamlaka nyingine wakiwemo Mawaziri kuteua Viongozi wa Umma wanaowajibika kutunga sera za idara na taasisi za serikali na Watendaji wa Kuu wa Idara na Taasisi za Serikali kwa kuwa mamlaka hayo ni mamlaka ya kipekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na badala yake Tume ya Utumishi wa Umma na mamlaka nyingine vimeruhusiwa kuteu watu katika nafasi ambazo sio za Watunga sera na ambao sio watendaji wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali.
(c) Rais ana mamlaka ya kipekee (exclusive power) ya kuteua Viongozi wa Umma Watunga Sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali akiwemo Mtendaji Mkuu wa Tanroads.
(d) Masharti ya
Kifungu cha 9 cha Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 245 ( the Executive Agencies Act, Cap. 245) yanakinzana na masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Wakati
Kifungu cha 9 cha Sheria ya Wakala wa serikali, Sura ya 254 kinaelekeza kuwa Mtendaji Mkuu wa Tanroads atateuliwa na Waziri ambaye taasisi au idara husika hiko chini ya Wizra yake huku
Ibara ya 36 (2) ya Katiba inaelekeza kuwa mamlaka ya kuteua
Watendaji Wakuu wa Idara na taasisi za Serikali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yako mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(f) Ni Kunga (principle) ya Sheria bayana (it is a settled principle of law) kwamba iwapo sheria iliyotungwa na Bunge yaani
Sheria Kuu (principal legislation) inakinzana na
Katiba basi sheria iliyotungwa na bunge itakuwa batili tangia mwanzo (
null et void ab initio) kwa kiwango ambacho inakinzana na katiba ya nchi, hii ni kwa mujibu wa masharti ya
Ibara ya 64 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama yalivyotafsiriwa na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya
Kukutia Ole Pumbun & Another Vs Attorney General & Another [1993] TLR 159 , baina ya nyingine (among others).
(g)Masharti ya
Kifungu cha 9 cha Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 254 ni batili tangia mwanzo (
null et void ab initio) kwa kuwa yanakinzana na masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Kwa kuwa masharti ya
Kifungu cha 9 cha Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 254 ni batili tangia mwanzo basi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana mamlaka ya kuwateua Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo
Mtendaji Mkuu wa Tanroads chini ya masharti ya
Ibara ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
(h) Iwapo Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inatoa mamlaka ya kuteua Viongozi wa Umma Watunga Sera za Idara na Taasisi za serikali na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Seikali kwa Waziri, Tume ya Utumishi wa Umma au mamlaka nyingine ambayo sio Rais basi Sheria hiyo ni batili tangia mwanzo chini ya masharti ya
Ibara ya 64 (5) ya Katiba kwa kukiuka Masharti ya
Ibara ya 36 (2) na (3) ya Katiba.
(i) Kwa sasa Bunge halina uwezo au mamlaka ya kuhamishia mamlaka ya uteuzi wa viongozi wa umma Watunga Sera na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali kutoka kwa Rais kwenda kwa Tume ya Utumishi, Waziri au mamlaka nyingine ya Umma.
Imeandaliwa na Matojo M. Cosatta
2, August, 2021.