WHO inasema mlipuko unaoshukiwa kuwa wa ugonjwa wa Marburg umeua watu 8 katika maeneo ya mbali ya Tanzania
Januari 15, 2025 9:00 AM
Picha maktaba FILE - Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus akihutubia mkutano na waandishi wa habari kuhusu mlipuko wa virusi vya Marburg katika Kituo cha Mikutano cha Kigali huko Kigali, Rwanda, Oktoba 20, 2024.
ARUSHA, Tanzania —
Shirika la Afya Ulimwenguni lilisema Jumatano mlipuko wa ugonjwa unaoshukiwa kuwa wa Marburg umeua watu wanane katika sehemu ya mbali ya kaskazini mwa Tanzania.
"Tunafahamu kuhusu kesi 9 kufikia sasa, ikiwa ni pamoja na watu 8 ambao wamefariki," mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema katika taarifa yake.
"Tungetarajia kesi zaidi katika siku zijazo kadiri uchunguzi wa magonjwa unavyoboreka."
Kama vile Ebola, virusi vya Marburg huanzia kwa popo wa matunda na huenea kati ya watu kwa kugusana kwa karibu na maji maji ya mwili ya watu walioambukizwa au kwa nyuso, kama vile shuka zilizochafuliwa na mgonjwa.
Bila matibabu, Marburg inaweza kuwa mbaya katika hadi 88% ya watu ambao wanaugua ugonjwa huo. Dalili ni pamoja na homa, maumivu ya misuli, kuhara, kutapika na wakati fulani kifo kutokana na kupoteza damu nyingi. Hakuna chanjo iliyoidhinishwa au matibabu ya Marburg.
WHO imesema tathmini yake ya hatari kwa mlipuko unaoshukiwa kuwa nchini Tanzania iko juu katika ngazi za kitaifa na kikanda lakini chini duniani. Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa mamlaka za afya ya Tanzania.
Mlipuko wa Marburg nchini Rwanda, ulioripotiwa kwa mara ya kwanza Septemba 27, 2024 ulitangazwa kuwa umekwisha Desemba 20, 2024.
Maafisa wa Rwanda waliripoti jumla ya vifo 15 na visa 66, huku wengi wa wale walioathiriwa wahudumu wa afya ambao walihudumia wagonjwa wa kwanza.
Mlipuko wa mwaka 2023 wa Marburg huko Kagera, mkoa ambao una mpaka na nchi ya Rwanda, uliua takriban watu watano.