Mimi ndiye Mheshimiwa Raisi wenu, mmenichagua kwa ridhaa yenu tena kwa ushindi wa kishindo. Mlinijua kiutendaji na kitabia bado mkaridhia kunichagua; nasisitiza tena kwa ridhaa yenu bila kulazimishwa na yeyote. Ninaendelea kumalizia muda mfupi uliobaki kumalizia miaka yangu mitano ya kwanza.
Kwa kweli nimefanikiwa kuzunguka sehemu nyingi za dunia hii, kama wengi wenu mjuavyo. Nimejionea mengi huko nje. Watanzania ni watu wenye uvumilivu wa hali ya juu; na ukarimu na upole wa hali ya juu. Pamoja na matatizo tuliyonayo lakini amani ndio kitu cha msingi.
Hivi sasa najipanga kwa ajili ya miaka mitano ijayo. Nafikiri safari za kipindi cha pili zitakuwa marudio; sana sana tu hasa kwenye sehemu nilizonoti wana utalii mzuri. Nashukuru nina watendaji wazuri chini yangu ambao mimi mwenyewe sihitaji kuwepo nchini kufukuzana nao. Wanajituma na wanachapa kazi vizuri. Hawa nitahakikisha wanabaki kwenye nafasi zao ili mimi nipate muda zaidi wa kujenga mahusiano na nchi za nje.
Katiba yetu ya nchi nayo imekaa vizuri sana. Inanipa mimi kama raisi madarka na uhuru mkubwa wa kutenda kazi ninavyojisikia. kuna wachochezi wachache wanaizungumza zungumza hii, naona wana chuki binafsi tu na uhuru nilio nao. mie kipenzi cha watanzania bwana.
Sera zoooote zilizoandikwa kwenye ilani ya uchaguzi ya chama changu, sikuziandika mimi. Hili nilishalisemea mara nyingi tu. Kwa hiyo mtu asije akajipa matumaini eti kwenye ziara zangu nitamletea mtu yeyote maisha bora. Haya ni mambo ya kisiasa tu ndugu zangu.
Pale mwanzoni nilikuwa nikiwafuatilia watendaji wangu kwa vikao vya kushtukizia, lakini baadaye nikagundua wao ni watendaji wazuri tu bila hata ya kufuatiliwa. Hivyo siku hizi wala sina presha. Mimi nazunguka huku na baadhi yao, huko nyumbani nao wanachapa kazi tu. Ukikaa nyumbani sana kero haziishi bwana, bora kutuliza akili huku nje. Hukawii kudondoka jukwaani bure! Maisha yenyewe mafupi nugu yangu.