Rajabu Ibrahim Kirama sehemu ya pili

Rajabu Ibrahim Kirama sehemu ya pili

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
RAJABU IBRAHIM KIRAMA SEHEMU YA PILI

Baada ya kupata msingi huu wa simulizi kazi yangu sasa ikawa kuingia katika historia ya Wachagga ambayo karibu yote imeandikwa na Wazungu na hapo kutazama taarifa ambazo zipo katika nyaraka za Mzee Rajabu.

Nyaraka za Mzee Rajabu zimebeba unaweza kusema historia kubwa ya Uchaggani kwa kuweza kumkutanisha mtafiti na viongozi wa nyakati zile na siasa zilizotamalaki baada ya kundoka Wajerumani na kuja Waingereza.

Nyaraka zina taarifa za Gavana George Stewart aliyekuwa Gavana wa tatu wa Tanganyika aliyetawala mwaka wa 1931 hadi 1934.

Ndani ya nyaraka hizi kuna barua walizokua wakiandikiana Mzee Rajabu na Chief Abdiel Shangali kuhusu mambo mengi yaliyokuwa yanaikabili Machame hasa kuhusu ugomvi uliozuka baina yao pale Mzee Rajabu aliposilimu na kujenga msikiti.

Nyaraka za Rajabu Ibrahim Kirama zina barua nyingi zinazoeleza yote yaliyotokea hadi kufikia kujengwa msikiti mwaka wa 1933 ambao sasa unaitwa Msikiti wa Mzee Rajabu.

Kuna barua baina ya Mzee Rajabu na Mangi Mkuu Chief Thomas Marealle.

Kuna taarifa za wanasiasa mahiri wa zama zile Petro Njau na Joseph Merinyo.

Hawa wawili walikuwa waandishi wa Mzee Rajabu wakimuandikia barua zake kwenda serikalini na kwengineko barua nyingine zikiandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

Halikadhalika wamo wanamji watu wa Moshi mjini kama Liwali Minjanga Mussa na mwanae Liwali Mussa Minjanga waliokuwa mahakama ya mwanzo Moshi Bomani wakihukumu kwa mujibu wa sharia, Shariff Muhdhar Hussein, Suleiman Nassor Gurnah, Shariff Jiwa kwa kuwataja wachache, hawa walikuwa viongozi wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS)tawi la Moshi.

Hawa wote walikuwa watu mashuhuri katika siasa za Uislam Kilimanjaro.

Nyaraka hizi zina taarifa za wanazuoni maarufu wa nyakati zile kutoka Zanzibar ambao walisubihiana na Mzee Rajabu, wanazuoni kama Sayyid Omar bin Sumeit, Sayyid Omar Abdallah Mwinyibaraka na Sheikh Abdallah Saleh Farsy.

Inasikitisha kuwa historia ya Wachagga imeandikwa na Wazungu kama Bruno Gutmann, Charles Dundas kwa mtindo wa wao kuelezwa kila kitu na wenyeji kuanzia mila na utamaduni, historia za watawala hadi vita vilivyopiganwa baina yao lakini hakuna mahali popote ambapo watoa taarifa wa historia hii wametajwa.

Machifu wanapotajwa wanatajwa kutokana na jicho la Wazungu pale waliposuhubiana na Wachagga katika historia yao ya ukoloni.

Kama isingekuwa kwanza kwa kuhifadhiwa historia hii ya ukoo wa Nkya kwa simulizi na kwa kuhifadhi nyaraka historia hii ya Uislam Uchaggani ingepotea.

Watafiti walikuwa wametosheka na historia ya jinsi Ukristo ulivyofika Uchaggani nay ale manufaa ambayo wao wanaona waliwaletea Wachagga kama shule, hospitali na mengineyo.

Mangi Shangali Ndeseruo ndiye aliyewapokea Machame Wamishionari wa Leipzig Mission kutoka Ujerumani mwaka wa 1893 na alijenga uhusiano mzuri sana na Wamishionari hawa wa dhehebu la Kilutheri.

Kitabu hiki kinaeleza maisha ya Rajabu Ibrahim Kirama ambae ndiye aliyeuingiza Uislam Nkuu Machame kwa kujenga msikiti shule na kuleta walimu kusomesha Qur’an. Hivi ndivyo Mzee Rajabu alivyoweza kuifungua Kilimanjaro kupokea Uislam.

Hapa ndipo panapoanza harakati za Uislam Machame Nkuu na kusababisha uhasama mkubwa kati ya ukoo wa Muro Mboyo na ukoo wa Mangi Ndeseruo Mamkinga.

Huu ukaja kuwa ugomvi baina ya mjukuu wa Mangi Ndeseruo Mamkinga, Chief Abdiel Shangali na mtoto wa Mkuu wa jeshi lililokuwa la babu yake kabla ya utawala wa Wajerumani, Muro Mboyo, sasa akijulikana kwa jina lake jipya la Kiislam, Rajabu Kirama.

Abdiel Shangali alipochukua utawala kutoka kwa baba yake Mangi Shangali Ndeseruo Ukristo ulikuwa umeshamiri vyema Machame na kote Uchaggani.

Mzee Rajabu alipokuja na ombi la kujenga msikiti katika himaya ya Chief Abdiel Shangali, jambo hili lilimghadhibisha sana Chief Shangali.

Chief Shangali alifanya kila juhudi aliyoweza ili Uislam usishike mizizi Machame na kwa takriban miaka 20 palikuwa na uhasama mkubwa baina yake na Mzee Rajabu.

Msikiti ulipojengwa Mangi alitoa amri uvunjwe na Waislam wakamatwe.
Halikadhalika palitokea jaribio la kumuua Mzee Rajabu.

Baadhi ya Waislam walikimbia Machame kwa kuhofia maisha yao.

Mzee Rajabu alikwenda hadi Dar es Salaam kutafuta msaada kutoka kwa Al Jameeat Islami Umumia of East Africa (Umoja wa Waislam wa Afrika ya Mashariki).

Juhudi za kutaka kujenga msikiti na baadae shule kulimpeleka Mzee Rajabu Mombasa na Dar es Salaam kutafuta vibali kutoka kwa Gavana na ofisi nyingine za serikali.

Mzee Rajabu alitumia nafasi hii ya mgogoro kuomba Machame iwe na mafungamano na Al Jameeat Islami Umumia of East Africa ili kujiongezea nguvu.

Jumuia hii katika mazingira ya kikoloni ilikuwa ikiongozwa na Wahindi na hili lilipunguza nguvu ya Waislam kwa kiasi kikubwa sana.

Mwaka wa 1933 Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ilipoundwa Dar es Salaam na vijana wanasiasa waliokuwa viongozi wa African Association Mzee Rajabu haraka aliwaunganisha Waislam wa Machame na jumuia hii mpya.

Mwaka wa 1943 Mzee Rajabu alikwenda Dar es Salaam na kumchukua Sheikh Hassan bin Ameir na kujanae Machame.

Baada ya safari hii Sheikh Hassan bin Ameir alileta walimu wanne kuja kufundisha dini Machame na Upare - Sheikh Salehe Mwamba, Shariff Alawi, Sheikh Mahmud Mshinda na Sheikh Abdallah Minhaj. Kuanzia hapa taratibu pakawa na mabadiliko makubwa katika mila za Wachagga hasa kuhusu pombe na misikiti ikawa sasa inajengwa kila walipokuwapo Waislam.

Kuja kwa Sheikh Abdallah Minhaj Machame na kuanza kusomesha kulileta mafanikio makubwa sana Machame.

Uislam ulianza kupata nguvu na Waislam wakajipembua kwa mila na tabia ikawa sasa Waislam wanaweza kutambulikana kwa muonekano wao kabla ya kudhihirika tabia zao. Waislam wakawa jamii inayotambulikana.

Sheikh Abdallah Minhaj aliacha athar kubwa sana Kilimanjaro na ndiye mwalimu aliyemsomesha Mama Ali Qur’an.

Wakati tunaagana baada ya mazungumzo yetu nilivutiwa na usomaji wa Qur’an wa Mama Ali wakati alipokuwa anasoma dua.

Sikuweza kustahamili nilimuuliza kuhusu hili na yeye akanijibu, ‘’Mimi ni mwanafunzi wa Sheikh Abdallah Minahaj.’’

Mzee Rajabu alipofariki mwaka wa 1962 alipata maziko makubwa sana Waislam kutoka kila pembe ya Uchaggani na Upareni walihudhuria mazishi yake pamoja na Mangi Mkuu Thomas Marealle.

Kaburi la Mzee Rajabu lipo katika uwanja wa msikiti alioujenga, uwanja ambao pia ilijengwa Muslim School ya kwanza Uchaggani na hii ndiyo shule aliyosoma Mama Ali na watoto wengi Uchaggani.

Wanafunzi wa shule hii walikuja kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Tanganyika na Tanzania. Maarufu katika hawa akiwa Prof. Awadh Mawenya aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kuwa Mkuu wa Idara ya Uhandisi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Ningependa kuhitimisha kwa kusema kuwa athari ya Uislam Uchaggani ilijitokeza wazi miaka ya 1950 wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika pale TANU ilipopanda mlima kumkabili Mangi baada ya kujiimarisha kupitia Waswahili wa Moshi mjini chama kikiongozwa na wazalendo kama Yusuf Olotu, Juma Ngoma, Melkezedek Simon, Gabrieli Malaika, Bi. Halima Selengia, Bi. Amina Kinabo, Mama bint Maalim, Lucy Lameck kwa kuwataja wachache.

Iliwachukua muda kwa machifu kutambua kuwa huu ulikuwa mwamko mpya tofauti na kuingia kwa Uislam Uchaggani ambao ulianza na Mzee Rajabu Kirama Machame Nkuu na kusambaa taratibu.

Mwamko huu wa uhuru na kujitoa katika minyororo ya ukoloni uliitikiwa na kila Mchagga kwa wakati mmoja bila ya kujali imani yake.

TANU ikaweza kwa kipindi kifupi cha miaka saba ya kupigania uhuru kuvunja nguvu ya Mangi iliyobakia Uchaggani chini ya utawala wa Waingereza.

Tunamuomba Allah alifanye kaburi la Mzee Rajabu Ibrahim Kirama kuwa moja ya mabustani ya peponi.
Amin.

Picha ya Rajabu Ibrahim Kirama, Gavana George Stewart (1931 - 1934) na kushoto Marealle, Chief John Maruma na Abdiel Shangali. Liwali Mussa Minjanga na Julius Nyerere Moshi miaka ya 1960.




 
Back
Top Bottom