Kamakabuzi
JF-Expert Member
- Dec 3, 2007
- 2,903
- 1,360
A) MUHIMILI WA MAHAKAMA UMEWEKWA CHINI YA RAIS:
Kuna mahakama 2, mahakama ya juu na mahakama ya rufani:
146.-(1) Bila ya kuathiri masharti yoyote yaliyotangulia katika Sehemu hii, kutakuwa na Muundo wa Mahakama katika Jamhuri ya Muungano utakaokuwa kama ifuatavyo:
(a) Mahakama ya Juu; na
(b) Mahakama ya Rufani.
147.-(1)Kutakuwa na Mahakama ya Juu ya Jamhuri ya Muungano au kwa kifupi itaitwa "Mahakama ya Juu" ambayo itakuwa na:
(a) Jaji Mkuu ambaye atakuwa Rais wa Mahakama ya Juu;
(b) Naibu Jaji Mkuu ambaye atakuwa Makamu wa Rais wa Mahakama ya Juu; na
(c) Majaji wengine wa Mahakama ya Juu wasiopungua saba.
Uteuzi wa jaji mkuu uko hivi:
151.-(1) Jaji Mkuu atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa majina ya watu watatu yaliyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na kabla ya kuapishwa jina lake litawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge.
(2) Jaji Mkuu ndiye atakuwa Mkuu wa Mhimili wa Mahakama katika Jamhuri ya Muungano.
Uteuzi wa naibu Jaji mkuu uko hivi:
152.-(1) Naibu Jaji Mkuu atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa majina ya watu watatu yatakayopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na kabla ya kuapishwa jina lake litawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge.
Uteuzi wa majaji wengine saba wa kuunda Mahakama ya juu uko hivi:
153.-(1) Majaji wa Mahakama ya Juu watateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa majina yatakayopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na wataapishwa na Rais.
Uteuzi wa mwenyekiti wa mahakama ya rufani, na majaji wa mahakama hiyo unafuata mlolongo huohuo rejea vifungu vya 162 na 163
Hiyo Tume ya utumishi wa mahakama inaundwa ifuatavyo:
172.-(1) Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo itaundwa na wajumbe tisa watakaoteuliwa na Rais kama ifutavyo:
(a) Jaji Mkuu ambaye atakuwa ni Mwenyekiti;
(b) Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(c) Jaji mmoja wa Mahakama ya Juu;
(d) Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani;
(e) Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria wa Tanzania Bara;
(f) Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar;
(g) Wakuu Wawili wa vitivo vya sheria kutoka vyuo vikuu, mmoja kutoka Tanzania Bara na moja kutoka Zanzibar watakaopendekezwa na Jaji Mkuu; na
(h) Mtendaji Mkuu wa Mahakama ambaye atakuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Wajumbe a,b.c.d, na h ni wateule wa Rais; yaani watano kati ya tisa, bado hata hao wa namba g watapendekezwa na jaji mkuu ambaye ni mteule wa Rais!
Na kitu kingine ni kuwa Rais anaweza kutengua masharti ya katiba yanayohusu uteuzi wa watu wa muhimili huu, hasa sharti la muda (uzoefu),
Kifungu cha 153 "……na amekuwa na sifa hizo mfululizo kwa muda usiopungua miaka kumi.
basi Rais anaweza kutengua sharti la kuwa na sifa kwa muda usiopungua miaka kumi, na baada ya kushauriana na Tume ya Utumishi wa Mahakama, kumteua mtu huyo kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu."
Hapa Rais anapewa uwezo wa kutengua masharti ya katiba. Kumbuka hii ni katiba ya wananchi wote lakini Rais napewa uwezo wa kutengua uamuzi wa wananchi!
Hii inaacha nafasi ya Rais kumteua mtu kuwa Jaji wa mahakama ya juu au ya rufani ambaye hana uzoefu kwa kushauriana na tume ya utumishi ambayo ameiteua yeye mwenyewe!
Kwa kuruhusu kipengele hiki, Rais anapewa uwezo wa kutengua masharti ya katiba. Kumbuka hii ni katiba ya wananchi wote lakini Rais anapewa uwezo wa kutengua uamuzi wa wananchi
NAPENDEKEZA HII TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA IWE HURU NA RAIS ASIPEWE NAFASI YA KUTENGUA MASHARTI YA KATIBA. Kama ni lazima kutengua masharti basi wa kumruhusu kufanya hivyo si tume aliyoichagua mwenyewe bali Bunge ambalo limechaguliwa na wananchi kwa madhumuni ya kurekebisha katiba kwani katiba ni ya wananchi.
B) KUJAZA NAFASI WAZI ZA WABUNGE
Katika utangulizi wa Katiba ambao unaonyesha misingi yya Katiba ambayo imekubaliwa na wananchi, kuna kipengele kinasema:
"NA KWA KUWA, tunaamini kuwa misingi hiyo inaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye mfumo wa demokrasia na utawala bora ambayo Serikali yake inasimamiwa na Bunge lenye Wabunge waliochaguliwa na wanaowawakilisha wananchi na Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa na kudumishwa na kwamba wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu";
Hii inaonnyesha kuwa wananchi wanaamini katika bunge lenye wabunge wa kuchaguliwa na wanaowakilisha wananchi (yaani wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa au dini nk)
Pia kifungu cha 105 kinasaema :
105.-(1) Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
(2) Wajumbe wa Bunge watakuwa wa aina zifuatazo:
(a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi;
(b) Wabunge watano watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuchaguliwa kuwa wabunge kuwakilisha watu wenye ulemavu kwa kuzingatia uwiano wa Washirika wa Muungano.
Yaani kifungu hiki kinasisitiza kuwepo kwa wabunge waliochaguliwa na wananchi kuwakilisha majimbo (na hao watano tu walemavu wa kuteuliwa)
Pia kifungu cha 119 kinasisitiza wabunge wa majimbo wawe wa kuchaguliwa na wananchi:
"119.-(1) Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi watachaguliwa na wananchi kwa kufuata masharti ya Katiba hii na vile vile masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba hii, inayoweka masharti kuhusu uchaguzi wa Wabunge.
SASA Kifungu cha 106 kinaua kabisa msingi ambao wananchi wanauamini
"116 (4) Endapo Mbunge anayetokana na chama cha siasa atapoteza sifa
za kuwa mbunge kwa sababu yoyote isiyokuwa ya Bunge kumaliza muda wake, Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri, kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na sheria itakayotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, itamteua na kumtangaza kuwa mbunge mtumwingine kutoka kwenye orodha ya majina ya wagombea iliyowasilishwa na chama hicho kwa mujibu wa Ibara ndogo ya (5)
Kwa maana ya kifungu hiki wananchi watawekewa mtu ambaye hawakumchagua kuwa mbunge wao. Suala kuwa chama husika kilimuweka katika orodha ya wagombea wake haina maana kuwa orodha hiyo ya chama ilichaguliwa na wananchi wote. Orodha hiyo inaandaliwa na chama husika kwa utaratibu wanaoujua wao ambao hauko kwenye katiba.
Je hii si kuvunja msingi iliotajwa kwenye utangulizi na kuwekewa msisitizo katika kifungu cha 105 na 119?
NAPENDEKEZA UWEPO UCHAGUZI MDOGO KUJAZA NAFASI WAZI. Tusikwepe gharama kwani hakika hiyo ni gharama ya demokrasia.
Suala hili likiachwa kama lilivyo kutajitokeza matatizo mengi kwenye uchaguzi mkuu kuzidi ilivyokuwa huko nyuma. Yaani chama kitaamua kutumia nguvu nyingi na mbinu zisizohalali ili kihakikishe kinapata kiti cha ubunge kikijua kuwa hata kama itathibitika kuwa mbinu mbaya zilitumika, chama kama chama hakitakuwa na cha kupoteza kwani kitaendelea kushikilia kiti chake.
Ni afadhali basi katiba ingesema kuwa aliyekuwa mshindi wa pili ndiye apewe hiyo nafasi hiyo kwani ana kura za wananchi, na pia itazuia nguvu na mbinu haramu kutumika wakati wa uchaguzi.
C) KUTANGAZA MALI KWA WATUMISHI WA UMMA
Kitu hiki ni kizuri na tumekuwa nacho kwa muda mrefu lakini hakionekani kuwashtua wahusika. Ni vyema basi katiba sasa ikakiwekea mkazo zaidi.
Katika kifungu cha16 kiongozi amelazimishwa kutangaza mali zake
"16.-(1) Kiongozi wa Umma atalazimika kutangaza, ndani ya siku thelathini baada ya kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na thamani zake na madeni yake katika Tume ya Maadili na Uwajibikaji.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), Kiongozi wa Umma atalazimika kutangaza mali zake na madeni:
(a) yake binafsi;
(b) ya mwenza wake wa ndoa; na
(c) watoto wake walio chini ya umri wa miaka kumi na nane,
mara moja kila mwaka, au kadri itakavyoamuliwa na sheria.
Hii sehemu ya mwisho ndiyo inapoteza uzito wa suala hili. Kama kipengele hiki kitabaki kilivyo ni wazi Katiba imejiwekea mwanya wa kutungwa sheria itakayopoteza uzito wa Katiba, Ikimubukwe pia kuwa wabunge ni miongoni wa watakaotakiwa kutangaza mali na ndio haohao ambao watatunga sheria ya kujiwekea muda; je haitatokea conflict of interest? Kumbuka sheria inaweza kubadilishwabadilishwa wakati wowote. (leo iwe kila mwaka, kesho iwe kila miaka mitano, kesho kutwa iwe miaka miwili nk)
NAPENDEKEZA KATIBA YENYEWE IWEKE MUDA ILI KILA MHUSIKA AUFUATE, KUTANGAZA KILA MWAKA NI VIZURI ZAIDI. Nina uhakika kama mtu ameongeza mali halali ndani ya mwaka mmoja hawezi kushindwa kuzitaja.
Katika suala hili la utangazaji mali naona kama Spika anadhalilishwa katika kifungu cha 128
128 (4) Spika atatakiwa kuwasilisha kwa Rais nakala mbili za taarifa rasmi ya maelezo ya mali yake, kadri itakavyokuwa, mali ya mke au mume wake.
Kwa nini spika asiwasilishe taarifa hiyo kwenye tume ya maadili kama ilivyo kwa viongozi wengine? Hii si ni kumfanya aonekane yuko chini ya Rais? Je Rais yeye anawasilisha taarifa hizo kwa spika? Je kama spika hatawasilisha taarifa hizo kwa Rais, ina maana Rais ataweza kumchukulia hatua? Au tunadhani ni rahisi kwa tume ya maadili kumuuliza Rais kama spika ameshawasilisha orodha ya mali zake kwake au la!
Huu ni udhalilishaji wa muhimili mmoja dhidi ya mwingine.
NAPENDEKEZA SPIKA AWASILISHE ORODHA YA MALI ZAKE KWENYE TUME YA MAADILI NA KWA UTARATIBU SAWA NA WA VIONGOZI WOTE WA UMMA.
D) KUPINGA UCHAGUZI WA RAIS
Hili ni suala zuri kwa maana ya kuondoa mashaka juu ya uchaguzi wa Rais, yaani Katiba inatoa nafasi ya kupingwa kwa matokeo kabla Rais hajaapishwa. Tuliona kule Kenya katika uchaguzi ulioleta vurugu jinsi Rais alivyoapishwa haraka harak an kusababisha mauaji. Katika uchaguzi ulioofuata wan chi hiyo hiyo tumeona namna matokea yalivyopingwa na baada ya uamuzi wa mahakama hakuna vurugu.
Suala hili zuri limeharibiwa na Katiba yenyewe katika kifungu cha 78(4):
"78. (4) Kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (3), Mahakama ya Juu inaweza kutoa uamuzi bila kutoa sababu za uamuzi na sababu hizo zikatolewa ndani ya kipindi kisichozidi siku thelathini tangu siku ya kutoa uamuzi."
Yaani mahakama ya juu inatoa maamuzi yawe ni ya kutengua uchaguzi au ya kuthibitisha uchaguzi na hailazimiki kuweka wazi sababu za kufanya hivyo hadi hapo itakapoona inafaa kuzitoa ndani ya siku 30! Tunatarajia nini kwa wananchi ambao watakuwa hawakurudhika na uamuzi huo wa mahakama ya juu? Kwa nini sababu ziwekwe kuwa siri? Yaani mtu anapinga matokeo, anawasilisha sababu zake na vielelezo lakini mwisho anaambiwa (kwa mfano) kuwa matokeo yanabaki yalivyo na hapewi sababu za kufanya hivyo!
Ukisoma utaratibu wa kumuapisha Rais, utagundua kuwa sababu za uamuzi wa mahakama zitatolewa baada ya Rais kuapishwa! Tunafanya hivyo ili iweje? Kwamba kwa kuwa Rais atakuwa ameshaapishwa basi atakuwa na rungu la kuwapiga walalamikaji!
HAKUNA SABABU ZA MSINGI ZA KUFICHA SABABU IWAPO MAHAKAMA NI HURU NA INA UHAKIKA IMETOA UAMUZI WA HAKI
E) MASUALA YA MUUNGANO
Hapa naomba ufafanuzi wa kifungu cha 62
Labda kama nimeelewa vibaya, sioni kwa nini mshirika wa Muungano awe na mamlaka na haki zote kwa mambo yasiyo ya muungano? Mimi nadhani mambo yasiyo ya muungano ndiyo yanashughulikiwa na washirika wa muungano kila mmoja katika eneo lake. Kwa mfano maliasili siyo suala la muungano, je Mtanzania bara atakuwaje na mamlaka na haki zote juu ya mafuta yaliyo Zanzibar? Je Mzanzibari atakuwaje na mamlaka na haki zote juu ya ardhi ya Tanzania bara?"62.-(1) Kila Mshirika wa Muungano atakuwa na mamlaka na haki zote juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano, na katika utekelezaji wa mamlaka hayo, kila Mshirika wa Muungano atazingatia misingi ya ushirikiano na mshirika mwingine kwa kuzingatia haki na usawakwa ajili ya ustawi ulio bora kwa wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano.
NAONA HILO NI KOSA LA KIUANDISHI (TYPING ERROR), NENO "yasiyo" lifutwe mara moja.
Huu mchango kutoka washirika wa muungano ungetajwa kwa uwiano na uwiano huo huo ndiyo utumike mahali popote panapohitaji uwiano kati ya Tanzania bara na Zanzibar. Yaani isiwe mshirika mmoja anachangia asilimia 60 lakini penye uwiano anapata asilimia 75 nk.215. Vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakuwa:
(a) ushuru wa bidhaa;
(b) maduhuli yatokanayo na taasisi za Muungano;
(c) mchango kutoka kwa Washirika wa Muungano; na
(d) mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano.