Raslimali zetu na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania – Nini hatima ya Gesi Asilia?

Raslimali zetu na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania – Nini hatima ya Gesi Asilia?

TheAnalyst

New Member
Joined
Feb 5, 2013
Posts
3
Reaction score
9
Na TheAnalyst

Kila linapotokea jambo zito hapa nchini, kunajitokeza pande nyingi za wadau, ambao kila mmoja hudai kuwa na mantiki ya kuelezea kiini cha jambo hilo, huku wale wenye kuujua ukweli, kwa sababu zao, huamua kukaa kimya kwa kuhofia, pengine, kuumbuliwa na ukweli huo. Hapo ndipo tatizo linazidi kuwa kubwa, kwani wananchi ambao wana haki ya kuujua ukweli wanabakia gizani, huku migogoro ikizidi kuwa mikubwa na pengine hata kusababisha maafa na hasara kubwa, vikiwemo uharibifu wa mali na hata maisha ya watu kupotea. Hili tayari limetokea Mkoani Mtwara, sina haja ya kulirudia kwani taarifa zimetolewa kwenye vyombo vya habari na mamlaka husika. Maelezo yake ni kama ifuatavyo.

Kabla ya kuendelea, tujikumbushe jambo moja muhimu sana ambalo pengine wengi wetu tayari tumelisahau, ambalo ni uteuzi alioufanya Mhe. Rais, Jakaya Kikwete, wa kumteua Nape Nnauye kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, mwaka 2010, muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Wengi waliuliza: Nape aliteuliwa kwenda Masasi kufanya kazi gani? Lakini cha ajabu zaidi, Mhe. Rais hakutangaza kutengua cheo chake hizo, kwani, kimya kimya, mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 kumalizika, Nape aliondoka Masasi na kurejea Dar es Salaam, ambapo amebakia hadi sasa akiwa Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Umuhimu wa uteuzi huo wa Nape kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi nitauzungumzia hapo baadaye, kwani hiki ni kitendawili ambacho kitateguliwa leo hii.

Kabla ya kuendelea, napenda kusema ni kwa nini nimeamua kujiunga leo rasmi na mtandao huu wa kijamii, ambao ni muhimu sana kwa kujadiliana masuala nyeti yanayotugusa sisi Watanzania. Mimi ni Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yangu. Ni mzaliwa wa Mkoa wa Kilimanjaro, lakini naweza kusema pia kwamba Mkoa wa Mtwara ni nyumbani kwangu, kwa sababu ambazo sina uhuru wa kuzitaja hapa leo.

Ninavyowafahamu watu wa mkoa huu, si kwa kuambiwa, bali kwa kuona, ni kwamba ukarimu wao umepita kiasi. Watu wote wa Mkoa wa Mtwara si wakorofi; ni wakarimu, wenye busara, wakulima na wafanyakazi hodari na pia ni watu wenye uvumilivu mkubwa. Lakini, kama mjuavyo, kila uvumilivu una kikomo chake. Hata mbwa wako anayekulinda huchoka kuvumilia ukiwa unampiga kila siku bila sababu, na iko siku utakapompelekea chakula, au utakapojaribu kumpiga, ATAKUUMBA! Lakini nisieleweke kwamba nimewakosea ndugu zangu hawa wa Mtwara kwa kuwalinganisha na mbwa; ashakum si matusi. Nimetoa mfano tu kwamba, kila kiumbe chenye uhai kina ukomo wa uvumilivu wake. Lolote linaweza kutokea na kuwa kama cheche inayowasha moto, ambao ulikuwa ukifukuta na kutoa moshi kidogo kidogo – uvumilivu wenyewe – ukisubiri cheche ziwake na hatimaye ulipuke. Wataalam wa lugha ya Kiingereza wanatuambia: “Every outcome is the result of a long term process.” (Tafsiri: Kila tukeo linasababishwa mchakato wa muda mrefu.) Kilichotokea Masasi ni “mchakato” wa muda mrefu.


MCHAKATO WA WILAYA YA MASASI
Kwanza kabisa, napenda nisieleweke kwamba nimetumwa na mtu yeyote. Hata hawa ambao nitawataja kwenye makala haya ya uchambuzi hawana habari kabisa kwamba leo hii nimeamua kuamka na kuandika makala haya. Sijatumwa. Nimefanya haya kwa mapenzi mema niliyonayo, kwa watu ambao walitoa mchango wao mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao, lakini hatimaye wakaonekana kuwa vikwazo kwa watu ambao, sio tu wana uchu wa madaraka, bali pia, wana uroho wa kupitiliza wa kujishibisha wao wenyewe na jamii zao, huku wakiwaacha wakazi wa Mtwara kuzidi kuendelea kuishi kwenye maisha duni, huku mikoa mingine ikineemeka na kutaka kuneemeka zaidi kupitia hizo rasilmali za Mtwara!

Katika watu waliotoa mchango wao mkubwa, wa binafsi na kipekee, ni Mhe. Raynald Alfons Mrope, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Masasi, kupitia Chama cha Mapinduzi, kwa vipindi viwili mfululizo, kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 alipoenguliwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM kwa hila, mizengwe na ufisadi mkubwa. Hilo sitalizungumzia hapa. Nataka kuzungumzia mchango wa Mhe. Mrope, yale aliyoyapanga, yale aliyoyatekeleza na nini kimetokea baada ya kuondolewa kwake kwenye nafasi hiyo. Daima, umuhimu wa mtu huonekana zaidi pale ambapo anapoondoka kwenye nafasi ya madaraka, na si wakati anapokuwa madarakani. Ingawa kwa Mrope hali ilikuwa tofauti, ni uroho wa madaraka, uchu wa fedha na ufisadi, ndivyo vilivyotumika kumuondoa kwenye nafasi hiyo ya ubunge, na wala si kwamba hakuwa mtekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. La hasha! Pia, ieleweke kwamba mimi si mwanachama wa CCM; ni mwanachama wa Tanzania, ninamuunga mkono mtekelezaji yeyote yule anayefuata miiko na maadili ya uongozi bora hapa nchini, hata kama akiwa ni mwanachama au kiongozi wa CCM. Chama changu, kama ilivyo kwa Mhe. Mrope, ni TANZANIA!

Sekta ndogo ya Maji
Mhe. Mrope aliweka mikakati ya muda mrefu kuhakikisha anamaliza kero ya maji kwenye Jimbo la Masasi. Hadi wakati anamaliza muda wake wa miaka kumi, ikibaki muda wa miaka tano, yaani kuanzia 2010 hadi 2015, pesa za mradi mkubwa wa maji kutoka kwenye chemchem ya Mbwinji, ambapo mradi mkubwa wa maji ulipaswa kujengwa na kusambaza maji kwenye Jimbo la Masasi na mkoa mzima wa Mtwara, zilikuwa zimepatikana. Kilichobakia kilikuwa ufuatiliaji tu, kazi ambayo Mrope alikuwa tayari amekwishaifanya. Wakati akijinadi kwa wanachama wa CCM na wapigakura kwa ujumla, Mrope aliwaeleza wananchi yale aliyoyafanya, kupitia kitabu kidogo alichokiandaa na kukichapisha, ambacho kilisambazwa bure na kueleza yale yote aliyoyafanya katika kipindi cha 2005 hadi 2010. Binafsi nilikisoma kitabu hicho, ila kwa bahati mbaya nakala yangu imepotea. Wapo wenye nakala ya kitabu hicho sehemu mbali mbali; warejee kukisoma.

Sekta ya Umeme
Wakati alipokuwepo madarakani, Mrope alifanya kazi kubwa na kampuni ya uwekezaji na uendeshaji wa miradi ya umeme, kwa kupitia gesi asilia, iliyotoka nchini Canada, yaani, Artumas Group Incorporated. Kwa kupitia nafasi pekee aliyokuwanayo, kama mwakilishi wa kuchaguliwa wa wananchi wa Masasi, na pia, kama Mwenyekiti wa Wabunge wa Mikoa ya Kusini kwa wakati huo, Mrope aliteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Government Negotiation Team (GNT) ya Wizara ya Nishati na Madini, ambapo alikuwa kiungo muhimu kati ya Artumas na Serikali kupitia Wizara ya Nishati. Mrope alifanikiwa kuwaunganisha wawekezaji hao na Serikali hadi wakaweka mipango thabiti ambayo ilianza kutekelezwa. Wananchi wa Masasi watakumbuka “maajabu” ya teknolojia rahisi (rejea hata Hansard za Bunge wakati huo) ya “Red Board”, ambapo Artumas ilianza kuwafungia wakazi wa Mtwara umeme kwa gharama nafuu ya Shilingi Elfu Sitini tu za Kitanzania (TZS 60,000.00), bei ambayo – kwa mujibu wa taarifa nilizozipata (aliyeniambia siwezi kumtaja) – TANESCO waliipinga vikali mno, kwani walidai kwamba inawaharibia soko lao. Jamani, hebu fikirieni: Muda wote huo, TANESCO walishindwa – hata kwa bei walizozipanga wao – kupeleka umeme wa uhakika huko Lindi na Mtwara. Amepatikana mwekezaji, anataka watu wote waupate umeme kwa bei nafuu, TANESCO wanapinga? Kulikoni? Kuna mengi zaidi ambayo naweza kuyasema kuhusu jinsi ambavyo TANESCO walikuwa wakiupinga mradi wa Artumas, lakini kwa kuwa ni taarifa ambazo ni “siri” ya Serikali, nahofia watu walioniambia kuingia matatani. Lakini ukweli ni kwamba, licha ya jitihada kubwa za kufanya kazi ya kupeleka umeme Mtwara, haswa kule vijijini, ambayo aliifanya Mrope, na maandalizi hayo yakiwa yanasubiri mkataba rasmi kuwekwa baina ya Serikali na Artumas, BADO haikutosha. Mrope alienguliwa. Umeme huo ungetokana na gesi asilia, ambayo inaliliwa kama lulu hivi sasa. Kisa nini?

Sekta ya Elimu
Hapa napo Mrope aliwajibika ipasavyo. Katika muda wa kipindi cha miaka kumi aliyokuwa Mbunge wa Masasi, Mrope alifanikiwa kujenga – kwa kuhamasisha michango ya wapigakura na kupata fedha nyingine kutoka mfukoni mwake – shule mbili kwa kila kata, kwa jumla ya shule kumi na sita (16), yaani, shule mbili kwa kila kata, kwa jumla ya kata nane (8). Taarifa hii ipo kwenye kitabu cha ripoti ya utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Masasi, alichokichapisha na kukisambaza mnamo mwaka 2010. Walimu wa kutosha walikuwapo, madawati hayakuwa tatizo, kimsingi, watoto walisoma na kiwango cha ufaulu kilionekana. Wenyewe mmejionea jinsi kiwango cha utoro wa wanafunzi kilivyoongezeka BAADA ya Mrope kuondoka madarakani. Ninavyokumbuka, taarifa za magazeti ziliandika zaidi ya nusu ya wanafunzi wa kike wa shule za msingi waliacha shule kutokana na kupata mimba, huku takriban asilimia 30 ya wanafunzi wa kiume kuacha shule kutokana na utoro. Hii ilitokea baada ya mwaka 2010, wakati ambapo Mrope hakuwa tena Mbunge wa Masasi.

Sekta ya Afya
Utekelezaji wa kipekee, wa kihistoria, alioufanya Mrope kwenye sekta ya afya, ambao haujawahi kufanywa na mbunge yeyote wa CCM, uliweza kufanyika mnamo mwaka 2003 (kama sikosei), ambapo Mhe. Mrope alifanikiwa kupata msaada wa vifaatiba, dawa na mahitaji mengine ya kiafya, ikiwemo vifaatiba vya upasuaji wa moyo, vitanda, dawa, na kadhalika, vyote ambavyo alivigawa kwa Hospitali ya Wilaya ya Masasi, Mkomaindo, na Hospitali ya Ndanda, pamoja na vituo vya afya vikiwemo kile cha Lukuledi na vinginevyo. Nasema haya kwa kuwa NILISHUHUDIA ugawaji huu kwa macho yangu; sikuambiwa. Thamani ya msaada huu ilizidi Shilingi Bilioni TATU za Kitanzania! Haijawahi kutokea, haitakaa kutokea!

Miradi ya Maendeleo kwa Kinamama
Mhe. Mrope, kwa kutambua umuhimu wa maendeleo ya wanawake, alimtuma mke wake kuanzisha na kusimamia miradi ya wanawake kwenye Jimbo la Masasi, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Sera Nzuri za CCM, jambo ambalo lilifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana. Miradi mingi ilianzishwa, ambapo wanawake walijifunza mbinu mbali mbali za ujasiriamali, ikiwa ni pamoja na biashara, kazi za mikono na kilimo. Walihitimu mafunzo na kuunda vikundi ambapo walipatiwa mikopo, kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Hakika akinamama walipendeza Jimboni Masasi.


KIINI CHA MGOGORO
Sasa, baada ya mafanikio haya yote, nini haswa kiini cha mgogoro huu? Kwa nini hili suala la gesi limekuwa kubwa kiasi cha wana-Masasi kushindwa kuvumilia, na kuingia barabarani na kufanya vurugu zilizozua hasara ya zaidi ya Shilingi Bilioni Moja, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mali na watu kupoteza maisha?

Kumbukeni, kila tokeo lina mchakato wa muda mrefu. Mchakato mmeuona. Mafanikio makubwa.

Mchakato ulianza pale uhalifu na uasi dhidi ya Mrope ulipoasisiwa, na wale waliotaka kunufaika na gesi asilia wao binafsi. Ishara zote zilionesha kwamba Mrope asingekubali gesi itumike kinyume na makubaliano rasmi kati ya mwekezaji Artumas na Serikali. Makubaliano ya msingi, kama mlivyoyasikia, yalikuwa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kiwango cha MegaWati 300, ambapo viwanda viwili vingenufaika na sehemu ndogo ya umeme huo, ambapo, kiwanda cha saruji na kiwanda cha mbolea vingejengwa. Umeme ambao ungebakia, takriban Megawati 240, ungeingizwa moja kwa moja kwenye mtandao wa umeme wa taifa (national power grid). Mradi huo mkubwa ulitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 3,000, ambapo ajira tegemezi zaidi ya 30,000 zingepatikana. Ulikuwa mpango madhubuti ambapo kama ungefanikishwa, leo tungekuwa tunaongelea suala la wapi tukafanye sherehe ya kufanikiwa kwetu, si kwenda mitaani kuchoma moto magari na ofisi za serikali.

Wale ambao waliona kwamba mradi huu ulikuwa kikwazo kwao, waliamua kuuvuruga na kumshawishi vibaya Rais, wakafanikiwa kwa hilo. Artumas walijua kwamba bila ya Mrope wasingefanikiwa; huwezi kulinganisha “kichuguu” na “mlima”.

Mbunge wa Masasi (kwa sasa), Mariam Kasembe, alikuwa mmoja wa wasaidizi wa Mrope. Niliwahi kumfahamu wakati huo. Aliingia kwenye siasa kupitia kwa Mrope, na alipotaka kuwa Mbunge, aliyeweza kumshawishi Mama Anna Abdallah (wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM) kumtafutia namna ya kumpa Ubunge wa Viti Maalum, kazi hiyo ilifanywa na Mrope. Kumbe Mariam Kasembe alikuwa na dhima ya kuja kumpindua mwalimu wake wa siasa, akidhani yeye anaweza kufanya kazi nzuri zaidi, au labda kwa kudhani kwamba kwenye Ubunge kuna lolote la maana. Kumbukeni, ruzuku nyingi zaidi hutolewa kwa wabunge wa Viti Maalum kuliko wale wa kuchaguliwa. Kasembe hakulijua hilo; hata kabla hajamaliza miaka tano ya awamu yake ya kwanza ya Ubunge wa kuchaguliwa, Kasembe amejisahau, anaanza kubwabwaja, anawaambia wapigakura wa Masasi: “Ninyi ni watu wa Mrope. Hamkunichagua. Siwatambui!” Mimi namwuliza Kasembe: “Kwani wewe bila ya Mrope ungekuwa wapi?”

Mchakato uliundwa kumwengua Mrope kutokana na ukweli kwamba alikuwa mtendaji mzuri na angeyasimamia yote aliyoyapanga. Gesi ingezalisha umeme, nchi ingenufaika. Inashangaza. Badala ya kuwathamini watendaji wazuri, nchi hii inawadhalilisha na kuwaondoa madarakani. Kwa kweli, hali hii ya Mikoa ya Kusini imeandaliwa na watu wenye hila, wenye nafsi za kifisadi, wenye dhima ya kujinufaisha binafsi na kuwaacha walio wengi wakibaki kwenye lindi la umaskini na ufukara.

Watu hawa waliona kwamba ni heri gesi isibaki Mtwara, iende moja kwa moja Dar es Salaam, ambako kunadaiwa kwamba soko ni kubwa zaidi. MAWE! Nadhani sasa mnaelewa vema ni kazi gani aliyotumwa Nape Nnauye kwenda kuifanya huko Masasi. Sisemi zaidi!

Artumas waliamua kuuza hisa zao kwenye mradi wa Mnazi Bay, wakijua kwamba aliyechaguliwa kuwa Mbunge wa Masasi asingeweza kuchukua nafasi ya Mrope, na hakukuwa na mbunge mwingine yeyote ambaye angeweza kuimudu kazi hiyo ya ufuatiliaji. Waliona mbali. Madai kwamba Artumas ilipata matatizo ya kifedha hayana ukweli; hiyo ilikuwa ni “cover story”, ili wasiulizwe maswali mengi kwa nini waliondoka hapa nchini. Ukweli ni kwamba walikata tamaa. Kukosekana kwa Mrope, ambaye ndiye angeweza kuwasemea wananchi wa Mtwara hata leo, kumekuwa pengo kubwa sana.

Napenda nieleweke kwamba SIKUTUMWA na mtu yeyote kuandika makala haya. Ninamheshimu sana Mhe. Mrope kutokana na mimi kumfahamu binafsi kwa muda mrefu. Akipata kuyasoma makala haya atashangaa, kwani hajanituma nimtetee, wala hajanituma niseme kwa niaba yake. Simetetei, sisemi kwa niaba yake. Ninachosema ni ukweli, ambao wengi wanaujua. Ninafahamu kwamba hata yeye Mhe. Mrope ameamua kukaa kimya kutokana na kuchukizwa kwake na yale yote yaliyotokea; amenawa mikono na kumuachia Mungu uamuzi wa mwisho. Lakini mimi si Mungu, mimi ni mwanadamu.

Nimeumizwa kwa kuwaona watu ambao nawaita “ndugu” zangu kuumizwa, kutokana na kudangangwa kwao kwa pesa ndogo ndogo. Watendaji wakuu wa mchakato wa kumwengua Mrope kwenye ubunge kupitia Kura za Maoni, walikuwa viongozi wa CCM wa Wilaya ya Masasi, ambapo wenyeviti na makatibu wa kila kata walihusika moja kwa moja. Pesa nyingi sana zilitembezwa kuwarubuni watu kumpigia kura Mariam Kasembe, cha ajabu, vijana wa TAKUKURU walikuwa nyuma ya Mrope kila alipokwenda, wakimlinda asijaribu kutoa rushwa. Kwa kuwa Mrope alijiamini, kutokana na utendaji wake mahiri, hakuwa na sababu ya kuutafuta uongozi kwa njia ya pesa. Yule anayetoa pesa ili achaguliwe – jambo ambalo ni dhambi kubwa – kwa kweli hajiamini! Rushwa imeharamishwa kwenye vitabu vyote vitakatifu; Biblia na Kurani. Naamini hata kwenye dini nyingine, kama vile Bah’ai na Ubuddha, rushwa ni haramu pia, kwani HAKIKA INAMCHUKIZA MUNGU!


HITIMISHO
Iwapo Serikali ya CCM inataka kurejesha imani ya wananchi wa Lindi na Mtwara, ili iweze kubaki madarakani huko Lindi na Mtwara, haswa kwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 ni sawa na keshokutwa, inapaswa kufanya yafuatayo, na huu ni ushauri wa BURE kabisa!


  1. Kutekeleza miradi yote ya maendeleo katika sekta ya gesi asilia, kama ilivyokuwa imepangwa, na kuunda Tume Maalum ya Rais ya kusimamia mradi huo. Ninapendekeza kazi hiyo apewe Mhe. Mrope, kwani yeye ndiye aliyeasisi mradi huo. Gesi itumike kuzalisha umeme ikiwa Lindi na Mtwara; viwanda vya saruji na mbolea vijengwe. Utalii utakuzwa, haswa kwa kuwa wakati huo wataalam mbali mbali watakuja kufanya kazi nchini kutoka nje ya nchi, watahitaji makazi ya kudumu na ya muda. Wananchi wa Lindi na Mtwara watapata fursa ya kujenga hoteli mpya na za kisasa. Kwa sasa, hakuna hoteli za kutosha hata nyumba za wageni huko Lindi na Mtwara. Serikali ikipuuzia, sio tu kwamba ajira hazitapatikana, bali hata maendeleo ya uchumi kwa ujumla yatadorora. Sekta ya utalii ni moja ya sekta nyeti zinazochangia kwa kiwango kikubwa pato la taifa.
  2. Miradi ya maji, afya, elimu na maendeleo ya wanawake na vijana irejeshwe kama awali. Hili halina maelezo mengi, wala ubishi mwingi.
  3. Migogoro yote ya wakulima ya korosho iondolewe mara moja na mpango wa stakabadhi za ghalani ufutwe, kwani umekuwa ukiwanyonya wakulima hao kwa kuwalazimisha kuweka korosho kwenye ghala hizo kwa gharama kubwa sana. Pia, wakulima hao wa korosho waruhusiwe kutafuta masoko ya mazao yao kwa nguvu zao, vyama vya ushirika vivunjwe kwani vimeshindwa kuwatetea. Wasilazimishwe kuweka korosho zao kwenye maghala hayo. Pia, Bodi ya Korosho ivunjwe, badala yake liundwe Baraza Huru la Korosho, ambalo litasimamiwa na wakulima wenyewe. Viongozi wote wa Bodi ya Korosho watakaobainika kuhusika na vitendo vya hujuma wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na kisheria.
  4. Ujenzi wa Barabara ya Dar-Lindi-Mtwara ukamilike mara moja, haswa eneo korofi la kilometa 60, ambalo lipo kwenye kipande cha Kibiti-Somanga-Lindi, kwani eneo hili limekuwa kikwazo kikubwa na cha muda mrefu kwa ukamilishwaji wa barabara hii muhimu sana kwa taifa. Kipande hiki cha barabara kimekuwa kikijengwa kwa zaidi ya miaka kumi sasa, kiasi cha kustaajabisha na kuwafanya watu wahisi, pengine, ni “mradi” wa watu fulani walioko wizara husika. Makandarasi lukuki wamepewa mikataba na kushindwa kuikamilisha kwa wakati, huku wananchi wakibaki bila maelezo ya uhakika wa sababu ya kushindwa kwao huko.
  5. Bandari ya Mtwara iimarishwe na kuwa Bandari Kuu, haswa kwa biashara za Tanzania na nchi jirani, kwa mfano, Comoro, Msumbiji na Madagascar. Bandari ya Mtwara ndiyo yenye kina kirefu zaidi hapa nchini, lakini haina magati ya kutosha kupokea meli kubwa za mizigo aina mbali mbali.


Haya ndiyo mambo ya msingi ambayo Serikali ya CCM inapaswa kuyatekeleza, kwa Mpango Mkakati wa Dharura (Emergency Action Plan), ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Lindi na Mtwara wanarejesha imani yao kwa Serikali ya CCM. La sivyo, vyama vya upinzani vitakuwa na kila haki ya kuzoa kura zote za wana-CCM waliochoshwa na vijembe, kejeli, dhihaka, matusi, na udanganyifu wa muda mrefu sana, walioupata kutoka kwa watendaji wabovu, wakiwemo Anna Abdallah, Hawa Ghasia na Mariam Kasembe, ambao wamefanikiwa kuwatenganisha wananchi wa Mtwara na chama chao, CCM.

Napenda kuhitimisha makala haya leo kwa kuwapa pole nyingi ndugu zangu wa Mtwara. Nina imani kwamba Uongozi Mkuu wa CCM una uwezo wa kuingilia kati yaliyotokea, na kuhakikisha hayarudiwi. Makala haya ni ombi rasmi kwa Rais Kikwete, okoa jahazi hili linalozama kwa kasi kubwa. Linda heshima yako, linda heshima yako kwa wakwe zako. Utaacha kumbukumbu ya kudumu kwa wananchi wa Lindi na Mtwara, ambao watakushukuru daima. Wenzako waliopita hawakufanya lolote la msingi kwa mikoa hii. Hata ile reli ya Kusini iling’olewa na Serikali ya TANU. Mtwara itaendelea kuwa “Cinderella Province” mpaka lini? Au Lindi na Mtwara waamue kujitenga na kujiunga rasmi na Msumbiji, ili kieleweke?

Nawatakieni nyote mafanikio mema katika ujenzi wa Taifa letu.

Ni mimi,

[TheAnalyst]
 
Hongera kwa kumfahamu Mrope............pamoja na maneno yako ya kumuhusu Ndg Mrope.....inaonyesha kuna udhaifu mkubwa kwenye iliyokuwa mipango yake....
....kuna harufu ya "vijisenti"...kati ya hao wawekezaji na huyo Mrope............yaani kwa kuwa yeye Mrope aliondolewa asigombee ubunge.....na hao wawekezaji nao wakaamua kuondoka!!!!!!!!!!!!!.........huo ni upuuzi....hatutaki wawekezaji wa aina hiyo..........kama wao walikuwa for real.....uwepo au kutokuwepo kwa Mrope kusingebadilisha dhamira ya uwekezaji.......inaelekea kulikuwa na zaidi ya uwekezaji.......naufananisha uwekezaji huo na ule wa KITAPELI aliotuletea Balozi Ami Mpungwe........

......pamoja na kwamba waliochaguliwa wanaweza kuwa mafisadi pia...lakini story yako nzima haina mashiko.....in my opinion......
 
Back
Top Bottom