RC aiasa BoT izibane benki zipunguze Riba ili Wananchi waweze kumudu kukopa

kbm

JF-Expert Member
Joined
Oct 5, 2012
Posts
5,224
Reaction score
1,677
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Said ameishauri Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuzibana benki na taasisi za fedha nchini kupunguza riba ili wananchi wengi wamudu kukopa na kuanzisha biashara.

Alitoa rai hiyo juzi jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na United Bank Limited (UBL) kwa ajili ya wateja wake kufuatia ujio wa Rais wao ambaye pia ndiye Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Wajahat Husain.

Alisema hivi sasa wananchi wengi wanatamani kukopa ili kuanzisha biashara lakini wanashindwa kwa kuogopa riba kubwa wanayotozwa na benki na taasisi hizo za fedha na kusisitiza kuwa lazima serikali iingilie kati.

“Wananchi wengi wanatamani kukopa, lakini wakiangalia riba watakayokatwa wanakimbia, riba katika benki nyingi ziko juu sana sasa tukiendelea na hali hii hatutakuwa tunawasaidia wananchi wa kawaida ambao wengi hawana dhamana wala hawawezi kumudu riba kubwa,” alisema.

Aidha, alisema benki na taasisi za fedha zinapaswa kuendelea kufungua matawi mikoani ili wananchi wengi wapate huduma hizo wakiwa huko badala ya kujazana maeneo ya mijini pekee.

“Wananchi wa maeneo ya vijijini nao wana haki ya kupata huduma za kibenki wakiwa huko badala ya kulazimika kuja maeneo ya mijini hivyo wito wangu ni kwamba benki na taasisi za fedha ziwafikirie wananchi hawa kwa kufungua matawi huko huko,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Wajahat Husain, alisema amani na utulivu ni moja ya sababu zilizowavutia kuja kuwekeza hapa nchini miongoni mwa nchi nyingi walizotaka kuwekeza.

Alisema benki hiyo pia ilivutiwa na ukuaji wa pato la taifa kwa mwaka ambalo limefikia asilimia saba na kwamba Tanzania ni nchi ambayo imekuwa kiungo muhimu kwa nchi nyingi ambazo hazina bandari.

“Tuliangalia nchi yenye mazingira mazuri ya uwekezaji Afrika lakini tukaona Tanzania ndiyo kituo chetu cha kwanza tunakoweza kufanya biashara nzuri kutokana na ukuaji wa uchumi na pato la taifa, hivyo tunaahidi tutaendelea kuwahudumia Watanzania,” alisema.


CHANZO: NIPASHE
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…