Azizi Mussa
JF-Expert Member
- May 9, 2012
- 9,186
- 7,492
Mara zote katika kipindi cha uchaguzi kama hiki, tumekuwa tukijadili nani ni ‘kiongozi wa wanyonge’. Ijapokuwa ni kweli kwamba jamii yetu ina ‘wanyonge’ wengi, lakini kwa kuwa unyonge sio sifa ya kujivunia; badala ya kujadili nani ni ‘kiongozi wa wanyonge’, ni vyema kujadili jamii yetu inatokaje kwenye unyonge.
Unyonge unasababishwa na matatizo sugu yanayoisumbua jamii yetu. Aidha, ni wazi kuwa tatizo sugu kupita yote kwa sasa ni ukosefu wa ajira kwa vijana na tatizo hilo linatarajiwa kukua siku hadi siku na hatimae kufikia kiwango kisichoelezeka. Kwa mantiki hiyo, tunaweza kusema wanyonge namba1, ni vijana wasio na kazi na hivyo kutoingiza kipato.Suala hili lisipoangaliwa kwa umakini wa ziada, huenda badae likazua janga kubwa la kiuchumi, kijamii na kiusalama pia.
Tatizo hili linasababishwa na mambo makuu mawili. Kwanza mfumo wa elimu unaoua vipaji na kumfundisha mtoto vitu ambavyo havifanyi kazi kwenye maisha ya kawaida hivyo elimu kutomsaidia kijana kuwa na uwezo wa kukabiliana na mazingira yake na pili ukosefu wa mitaji unaosababisha kijana kushindwa kujiajiri.
Wakati tuna durusu muelekeo wa kisera 2020-2025-2030; ni muhimu kufanya mapinduzi ya kisera na kimuelekeo kulenga kutatua changamoto tajwa hapo juu ili tutoke kwenye kile kiitwacho ‘Unyonge’.Tunaweza kuangalia uwezekano wa kufanya yafuatayo;-
- Elimu ya msingi ibaki kama ilivyo ili kumuwezesha kila mtoto kujua mambo ya msingi kwa mhutasari,
- Kuanzia ngazi ya sekondari, watoto wachague masomo kama matatu tu wanayopenda wenyewe (kwa ushauri wa waalimu wao) ili waweze kuyamudu vizuri. Ikumbukwe kwamba imethibitika kisayansi kwamba ili mtu afanikiwe kimaisha, hapaswi kufahamu kila kitu bali anatakiwa ku ‘master ‘ maeneo machache.
- Kuanzia kidato cha kwanza (pamoja na masomo matatu aliyochagua hapo juu) kila mtoto aruhusiwe kuchagua fani 2 anazopenda na anahisi anazimudu na aanze kuzifanyia kazi kwa ubinifu wake binafsi. Kazi ya mwalimu itakuwa ni ‘coaching’ kwa mtoto na sio kumfundisha kwa sababu mtoto atakuwa ana uelewa na mapenzi zaidi kwenye fani hizo kuliko mwalimu, Hivyo akiwa 'coached' kwenye anachokipenda na kukimudu, anaweza kufanya maajabu.
- Siku ya mtihani, (kwenye fani husika)mwanafunzi atapimwa kutokana na mwenendo wake kwa kipindi chote ambacho amekuwa ‘coached’. Aidha, mwanafunzi anaweza kujitungia mtihani wake mwenyewe kwenye fani ambazo amekuwa anazifanyia kazi, na jopo linatathmini uwezo wa mtoto kutatua matatizo aliyochagua kutatua.
- Ikifika kwenye level ya kwenda kwenye vyuo vikuu, wakati wachache wakipewa mikopo waende vyuo vikuu, wengi watapewa mikopo wakatekeleze miradi yao ambayo tayari wameshajenga umahiri kwayo. Aidha, wataendelea kuwa ‘coached’ na wataalam kwa miaka kadhaa kabla ya kusimama wenyewe.
Kinyume chake tukiendelea na mfumo huu wa elimu za vijana wote wanapiga madesa, kukariri, kupata vyeti, kukariri wakoloni walivyotupiga na kutunyanyasa, tulivyofanywa watumwa na kisha vijana kusubiria ajira ambazo kimsingi hazipo; tutakuwa hatujitendei haki, hatutendei haki nchi yetu, na hatutendei haki vizazi vijavyo.
Aidha, Tukichagua kuendelea na mfumo kama ulivyo, pamoja na athari tajwa hapo juu, tutakuwa tumeamua kuendelea kuwapa ‘mabeberu wa ubeberuni’ nafasi za kutuonesha kazi. Nadhani ni vyema tukalitafakari suala hili na kuona namna ya kufanya mapinduzi makubwa yatakayofuta hili jina la ‘wanyonge’ na kuingia kwenye level nyingine.