The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Ripoti kuhusu hali ya haki za kidijitali Kusini mwa Afrika imepongeza juhudi za nchi za ukanda huo kuweka sheria za ulinzi wa data kama moja ya njia za kuboresha haki za kidijitali miongoni mwa wananchi.
Ripoti hiyo yenye kichwa “Kulinda Haki za Kidijitali Kusini mwa Afrika: Wito wa Hatua kwa Wadau,” iliyoandikwa na Profesa Admire Mare wa Denhe Reruzivo Consultancy Hub, ni ya nne katika mfululizo wa ripoti zinazojadili masuala ya haki za kidijitali katika nchi kumi zinazounda Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Ripoti hiyo Iliyochapishwa na Shirika la Association for Progressive Communications na Namibia Media Trust, imechunguza kiwango ambacho nchi za ukanda huo zinatimiza wajibu wa kulinda haki ya uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari, haki ya faragha na haki ya usalama wa mtandao katika zama za kidijitali.
Ripoti hiyo inasema kwamba ingawa kumekuwa na maendeleo chanya katika kuboresha haki za kidijitali kama vile kupitishwa kwa sheria za ulinzi wa data na kuanzishwa kwa mamlaka za ulinzi wa data miongoni mwa hatua nyingine, pia kumekuwa na mambo hasi kama inavyoonekana katika vitendo vya uangalizi katika baadhi ya nchi, sheria kandamizi zinazozuia uhuru wa kujieleza na hata masuala kama usajili wa laini za simu kwa lazima.
“Kupitishwa kwa sheria na sera za ulinzi wa data, maendeleo ya sheria za haki za kidijitali na ongezeko la utetezi kutoka kwa wadau wa jamii kuhusu haki za kidijitali ni baadhi ya mafanikio makubwa katika miaka mitano iliyopita,” inasomeka sehemu ya matokeo ya ripoti hiyo.
Inaeleza pia kuwa, kwa mfano, nchi kama Zambia na Zimbabwe sio tu kwamba zina sheria za upatikanaji wa habari katika vitabu vyao vya sheria, bali pia zina sheria za ulinzi wa data. Hali kadhalika eSwatini, na Afrika Kusini ambayo imekuwa na sheria ya ulinzi wa data binafsi tangu mwaka 2013.
Licha ya hatua hizi, ripoti inabainisha kuwa matukio ya ukiukaji wa haki za kidijitali pia yameripotiwa katika baadhi ya nchi, jambo linaloibua wasiwasi miongoni mwa wanaharakati kuhusu athari na uendelevu wa mafanikio yanayorekodiwa.
“Shida kubwa imekuwa ongezeko la matukio ya aina mbalimbali za uangalizi haramu (unlawful surveillance) katika nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), eSwatini, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia na Zimbabwe,” ripoti inasema, ikibainisha kuwa “mengi ya matukio haya ni kama vile kufuatilia watu kupitia simu za mkononi (mobile phone tapping), kufuatilia mitandao ya kijamii (social media monitoring), mifumo ya utambuzi wa nyuso, n.k.”
Ripoti hiyo inamalizia na kile mwandishi anachokiita "wito wa kuchukua hatua" kwa wadau mbalimbali kama vile serikali, mamlaka za ulinzi wa data, vyombo vya habari, mashirika ya kiraia, na wasomi, kufanya jitihada za kivitendo za kutetea haki ya uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari, haki ya faragha na usalama wa mtandao katika zama za kidijitali.
Mwezi Aprili, serikali za Afrika zilihimizwa kuhakikisha uwepo wa ulinzi wakati wa utekelezaji wa mipango ya utambulisho wa kidijitali katika ripoti iliyochanganua hali ya haki za kidijitali na ujumuishaji katika nchi 26 za Afrika.
Akizungumza hivi karibuni kwenye The World Summit on the Information Society (WSIS), Afisa Mkuu wa Kidijitali wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Robert Opp, alieleza kazi ambayo shirika hilo la Umoja wa Mataifa limekuwa likifanya kusaidia miradi ya mabadiliko ya kidijitali inayotilia mkazo faragha na haki za watu.
Hii, alisema, ni sehemu ya mchakato unaoendelea wa kuunda mfumo wa ulinzi unaohitajika kuhakikisha ujumuishi, uaminifu na uwazi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya umma ya kidijitali.