Ripoti ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2022/23

Ripoti ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2022/23

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Ripoti hii ya mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2022/23 imetolewa kwa mujibu wa Ibara ya 143(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 34 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sura 418.

Ripoti hii imeangazia matokeo ya ukaguzi na mapendekezo ya hatua stahiki za marekebisho zinazohusiana na kuchochea uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya rasilimali za umma.


MUHTASARI

Ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2022/23 ina sura 19. Maeneo yafuatayo yamejadiliwa kwa kina katika ripoti hii:

Hati za ukaguzi

Kwa mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni 2023, nilikamilisha kaguzi 215 za mashirika ya umma ambapo nilitoa hati za ukaguzi. Kati ya hati za ukaguzi 215 nilizotoa, 211 zilikuwa zenye kuridhisha, na nne zilikuwa zenye shaka. Idadi ya hati zinazoridhisha imeongezeka kutoka asilimia 97 mwaka jana hadi asilimia 98 mwaka huu. Hali hii inaashiria uboreshaji endelevu katika uandaaji wa taarifa za fedha ambao unazingatia mifumo na viwango vya kimataifa vya uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za fedha kama vile Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu (IFRS) au Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Taasisi za Umma (IPSAS).

Utekelezaji wa mapendekezo ya kaguzi zilizopita na maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali

Ukaguzi wangu ulibaini, kati ya mapendekezo ya ukaguzi 6,151 niliyotoa kwa mashirika ya umma 215, mapendekezo 2,413 (asilimia 39) yalitekelezwa kabisa, mapendekezo 2,776 (asilimia 45) yalikuwa chini ya utekelezaji, mapendekezo 720 (asilimia 12) hayakutekelezwa, wakati mapendekezo 242 (asilimia 4) yalikuwa yamepitwa na wakati.

Pia, nilibaini kati ya maagizo 136 ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali yaliyotolewa hadi mwaka wa fedha 2022/23, maagizo 45 (asilimia 33) yalitekelezwa, maagizo 89 (asilimia 65) yalikuwa katika hatua za chini ya utekelezaji, na maagizo mawili (asilimia 2) hayakutekelezwa.

Kwa ujumla, kasi ya kutekeleza mapendekezo ya ukaguzi na maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali inahitaji kuboreshwa ili kushughulikia vihatarishi ambavyo vilikuwa vimekusudiwa kupunguzwa au kuondolewa.

Utendaji wa kifedha wa mashirika ya umma

Nilikagua utendaji wa kifedha wa mashirika ya umma 215 kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Nilibaini mashirika ya umma 58 ambayo yaliripoti hasara au nakisi, ama kwa miaka miwili mfululizo 2021/22 na 2022/23 au kwa mwaka mmoja wa fedha 2022/23. Hii ni kutokana na dosari za kiutendaji zinazosababisha utendaji usioridhisha katika uwekezaji au uendeshaji wa biashara, au kupata msaada wa fedha kutoka Serikalini.

Pia, nilibaini mashirika ya umma 11 yalikuwa na mtaji hasi katika mwaka wa fedha uliomalizika tarehe 30 Juni 2023. Sababu kuu za mtaji hasi kwa mashirika hayo zilikuwa malimbikizo ya hasara kwa muda mrefu na madeni makubwa wanayoingia mashirika haya ili kufadhili shughuli zao.

Vilevile, nilibaini mashirika 63 yenye madeni ya muda mfupi zaidi kuliko mali za muda mfupi; ambapo 13 kati ya hayo yalikuwa mashirika ya umma ya kibiashara, huku 50 yalikuwa mashirika yasiyo ya kibiashara. Uwiano wa ukwasi ulikuwa kati ya 0.01 hadi 0.98. Hivyo basi, taasisi hizi zinaweza kushindwa kulipa mikopo na kuchelewesha malipo kwa wazabuni.

Aidha, nilibaini mashirika ya umma 28 (12 ya kibiashara na 16 yasiyo ya kibiashara) yalikuwa na uwiano mbaya wa madeni (jumla ya madeni yote dhidi ya jumla ya mtaji) kwa zaidi ya asilimia 100. Hii inaonesha mashirika haya, kwa kiasi kikubwa, yanategemea mikopo kujiendesha. Hii inasababisha kuwa na hatari kubwa ya kifedha kutokana na gharama kubwa za kuhudumia madeni.

Ufanisi wa mashirika ya umma katika kuimarisha biashara

Katika ukaguzi wangu wa ufanisi wa uendeshaji wa mashirika ya umma ya kibiashara yenye jukumu la kuweka mazingira mazuri ya biashara nilibaini:

Licha ya kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere tarehe 12 Desemba 2018, pande mbili za mkataba bado hawajasaini makubaliano ya kina ya utekelezaji wa miradi ya kijamii yenye thamani ya shilingi bilioni 262.34, ikiwa yamechelewa kwa zaidi ya miaka minne. Mkataba wa kina wa miradi ya kijamii ulipaswa kutiwa saini ifikapo tarehe 13 Januari 2019. Hivyo, hakuna mradi wowote wa kijamii umetekelezwa.

Ukaguzi wangu katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ulibaini wastani wa muda wa kuingia na kutoka kwa meli kwa sasa ni siku 6.5 kwa meli za kontena, na hadi siku 13.7 kwa meli za zinazobeba vimiminika badala ya siku tatu na tano zilizopangwa mtawalia.

Usimamizi wa mapato katika mashirika ya umma

Ukaguzi wangu ulibaini kuwapo kwa ukusanyaji wa mapato nje ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) kwa shilingi bilioni 21.46 kwa mashirika ya umma saba. Hili ni ongezeko la shilingi bilioni 18.14 (sawa na asilimia 546) kutoka shilingi bilioni 3.32 za mwaka uliopita.

Aidha, katika Shirika la Umeme Tanzania, nilibaini wateja 6,905 waliosajiliwa katika mfumo wa kufanya maombi kwa njia ya mtandao (N-Konekt) walikuwa bado hawasajiliwa katika mfumo wa LUKU kwa siku moja hadi 438 kufikia tarehe 30 Juni 2023. Pia, nilibaini ucheleweshaji katika usajili wa wateja 12,666 katika mfumo wa LUKU kuanzia siku 7 hadi 366 toka wateja hao wajiunge kwenye mfumo wa Ni

– konekt. Ucheleweshaji wa usajili wa wateja unaathiri mapato ya TANESCO. Pia, nilibaini mashirika ya umma 66 yaliyoripoti madeni ya muda mrefu yanayofikia shilingi trilioni 2.92.

Vilevile, nilibaini hakukuwa na uhamishaji wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 192.44 zilizokusanywa kwenda kwenye akaunti ya Mfuko wa Miundombinu ya Reli, ambapo fedha hizo zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilipelekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Usimamizi wa matumizi katika mashirika ya umma

Katika ukaguzi wangu kwenye usimamizi wa matumizi kwa mwaka ulioishia 30 Juni 2023, nilibaini mashirika ya umma 17 yenye matumizi ya jumla ya shilingi bilioni 72.36 yasiyo na tija. Hii inamaanisha kuwapo kwa ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo kulikuwa na mashirika ya umma 12 yenye jumla ya shilingi bilioni 63.77. Pia, nilibaini mashirika ya umma 11 yenye matumizi yasiyostahili ya jumla ya shilingi bilioni 4.64 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 94 ikilinganishwa na shilingi bilioni 77.75 kwa mashirika ya umma 21 kwa mwaka uliopita.

Vilevile, kuna uwezekano wa kutopata tija kwa malipo ya shilingi bilioni 3.09 kwa ajili ya vifaa vya kukagulia magari katika Shirika la Viwango Tanzania ambapo huenda visitumike kama ilivyokusudiwa kufuatia agizo la Serikali la kusitisha ukaguzi wa magari ndani ya nchi kama ilivyokusudiwa awali.

Pia, nilibaini kutokuwapo kwa uhakika juu ya urejeshwaji wa shilingi bilioni 14.7 za kodi na tozo za uingizaji wa mafuta nchini. Fedha hizi zilizolipwa na Kampuni ya Uwekezaji ya TANOIL kwenye shehena za mafuta zilizokuwa na zuio kwa kushindwa kulipa gharama za mafuta kwa mzabuni na baadaye kuuzwa kwa kampuni zingine za uuzaji wa mafuta; ambapo Kampuni ya Uwekezaji ya TANOIL haikurejeshewa kodi na tozo ilizokuwa imelipia.

Usimamizi wa bajeti katika mashirika ya umma

Nilibaini Serikali haikutoa shilingi trilioni 1.01 kwa mashirika 50 ya ya Umma kama ilivyopangwa katia mwaka wa fedha 2022/23.

Vilevile, nilibaini mashirika ya umma 66 hayakukusanya fedha kiasi cha shilingi bilioni 284.71 kutoka katika bajeti ya vyanzo vya ndani katika mwaka wa fedha 2022/23.

Pia, nilibaini mashirika ya umma nane yalitumia zaidi ya bajeti kwa kiasi cha shilingi bilioni 21.14 bila idhini ya Afisa Masuuli au Bodi ya Wakurugenzi.

Usimamizi wa mikataba na ununuzi

Nilibaini kuendelea kuwapo kwa mapungufu katika mashirika ya umma 22 yaliyochelewa kupokea bidhaa na huduma zenye thamani ya shilingi bilioni 14.84 kwa kipindi cha kuanzia siku 30 hadi 1,140 ikilinganishwa na mashirika ya umma 12 yaliyoripotiwa katika ripoti yangu ya mwaka wa fedha 2021/22.

Pia, nilibaini kutofuatwa kwa sheria ya ununuzi katika Kiwanda cha Dawa Keko kwa ununuzi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 4.97. Katika ununuzi huo, hapakuwa na bodi ya zabuni wala timu iliyoteuliwa kufanya tathmini ya zabuni. Hii ilisababisha michakato yote kufanywa na Mkurugenzi wa Fedha pamoja na Afisa Masuuli pekee. Aidha, nilibaini kuwa uchapishaji katika Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania ulifanywa nje ya Kampuni pasipo mchakato wa ununuzi wala kuingia mkataba. Uchapishaji huo ulikuwa na jumla ya thamani ya shilingi bilioni 1.71.

Vilevile, nimeendelea kubaini mashirika ya umma ambayo yalitekeleza mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 31.11 bila dhamana ya utendaji kazi. Aidha, nilibaini taasisi nne hazikuwasilisha mikataba kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Afisa Sheria kwa ajili ya uhakiki kabla ya kusainiwa yenye thamani ya shilingi bilioni 9.89 na dola za Marekani milioni 2.95.

Tathmini ya rasilimali watu na utawala

Nilibaini mashirika ya umma nane yalikuwa yanafanya kazi bila Bodi za Wakurugenzi. Hii inapunguza uwezo wa kufanya majukumu ya uongozi na usimamizi kwenye mashirika ya umma husika.

Aidha, nilibaini mashirika ya umma 40 hayakuwa na nyaraka za uendeshaji kama vile mwongozo wa hesabu uliosasishwa, sera na kanuni za kifedha pamoja na sera ya usimamizi wa vihatarishi.

Vilevile, nilibaini mashirika ya umma nane hayakufuata maelekezo ya Serikali yanayohitaji shirika kuhakikisha linawasilisha mpango wa motisha, mpango wa mazungumzo ya hali bora, posho, na muundo wa shirika ili kupitishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Usimamizi wa kodi katika mashirika ya umma

Nilibaini kesi za rufaa ya mapato ambazo hazijaamuliwa wa kipindi cha kuanzia mwaka mmoja hadi mitano katika Bodi ya Rufani za Kodi na Baraza la Rufani za Kodi zenye jumla ya shilingi bilioni 3,681.36 na dola za Marekani milioni 4.66 mtawalia.

Pia, nilibaini mashirika ya umma 16 hayakuwasilisha makato ya kodi yenye jumla ya shilingi bilioni 33.45 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Vilevile, nilibaini mashirika ya umma 12 yalichelewa kuwasilisha makato ya kodi yenye jumla ya shilingi bilioni 29.09 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mwaka 2022/23. Kadhalika, nilibaini malipo ya jumla ya shilingi bilioni 2.17 yaliyofanywa na mashirika ya umma tisa hayakuambatanishwa risiti za kielektroniki za kodi ya mapato.

Utendaji wa benki za Serikali na taasisi zingine za fedha

Mapitio yangu ya mikopo chechefu nilibaini kuwa Benki ya Maendeleo ya TIB ilikuwa na mikopo chechefu ya asilimia 21.50 kufikia tarehe 31 Desemba 2023 (2022: mikopo chechefu asilimia 20.28), wakati Benki ya Azania ilikuwa na mikopo chechefu asilimia 7.44 hadi 31 Desemba 2023 ( 2022: mikopo chechefu asilimia 18.25). Pamoja na kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu kutoka mwaka uliopita kwa Benki ya Azania, ni vyema kutambua kuwa benki zote mbili bado zilivuka kiwango kinachokubalika na kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania cha asilimia 5.

Nilibaini Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wana mikopo ya muda mrefu ambayo ilitolewa kwa taasisi za Serikali yenye thamani ya shilingi trilioni 1.73 ambayo haijalipwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka mmoja hadi 16. Hali hii imesababisha kupunguza uwezo wa mifuko ya jamii kufanya uwekezaji zaidi.

Pia, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi haikukusanya michango ipatayo shilingi bilioni 856.78 kutoka kwa wanachama; hivyo kudhoofisha uwezo wa mifuko kuhudumia wanufaika.

Vilevile, nilibaini Shirika la Bima la Taifa, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma hawakuweza kukusanya kodi ya shilingi bilioni 47.20 kutoka kwa wapangaji katika vitega uchumi vyao. Kadhalika, Shirika la Bima la Taifa lina madeni kutoka kwa wapangaji shilingi bilioni 7.95 ambapo wadaiwa wake hawajulikani walipo.

Tathmini ya sekta ya utalii nchini Tanzania

Ukaguzi wangu katika sekta ya utalii ulibaini yafuatayo: Kutolewa kwa bajeti isiyotosheleza kwa ajili ya kuendesha Kituo cha Kidijitali na kutangaza utalii wa kimataifa kupitia Bodi ya Utalii. Hali hiyo inakwamisha ufikiwaji wa lengo lililokusudiwa la kutangaza utalii kwa ufanisi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Kadhalika, nilibaini ukosefu wa huduma za kuwezesha utalii (ikiwamo uwezo mdogo wa malazi, umeme usiokuwa wa uhakika, kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi wa uwanja wa gofu). Vilevile, nilibaini hali ya kutokuendeleza na kutotangaza kreta za Empakai na Olmoti.

Aidha, niliona hatari ya kushindwa kukamilika kwa mradi wa kuwahamisha wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na makadirio hafifu ya gharama zilizotakiwa katika zoezi hilo. Hii ni kwa sababu, katika hali halisi, mkopo uliochukuliwa hauwezi kukamilisha zoezi hilo. Mradi huu unatekelezwa ili kurejesha mazingira na uoto wa asili ulioharibiwa; hivyo kuifanya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kuwa endelevu.

Utendaji wa mamlaka za maji

Ukaguzi wangu ulibaini hapakuwa na uhakika wa thamani ya fedha za miradi katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Songea. Miradi hii iligharimu shilingi bilioni 17.29.

Pia, nilibaini kuwapo kwa muendelezo wa hasara ya shilingi bilioni 163.93 kutokana na upotevu wa maji (mwaka 2021/22 kulikuwa na hasara ya shilingi bilioni 162.14). Hasara hii inasababishwa na miundombinu chakavu inayovujisha maji.

Aidha, nilibaini ongezeko la madeni ya mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira kutoka shilingi bilioni 126.23 (mwaka 2021/22) hadi shilingi bilioni 136.17 (mwaka 2022/23). Hii inatokana na utoaji wa huduma za majisafi na majitaka kwa taasisi za Serikali kuu, mashirika mengine, pamoja na wateja binafsi.

Tathimini ya utendaji wa taasisi za mafunzo, utafiti na elimu ya juu

Ukaguzi wangu katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ulibaini yafuatayo: kutokuwapo kwa utambulisho wa lazima, wakutegemewa na wa kipekee, kwa wanafunzi wanaopokea mikopo; kutokuwapo kwa mfumo wa kuwashirikisha wadau katika mkakati wa kuwatafuta wanufaika wanaodaiwa mikopo ya elimu.

Pia, nilibaini kuwapo kwa upungufu wa udahili wa wanafunzi ukilinganishwa na malengo; na kuwapo kwa mapungufu katika shughuli za utafiti na ushauri katika taasisi za kitaaluma.

Aidha, nilibaini: kulikuwa na programu ambazo zimepata ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania lakini bado hazijaanza kutolewa katika Chuo Kikuu cha Dodoma; na programu zilizoisha muda wake hazikupatiwa ithibati mpya katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Ufanisi wa mamlaka za udhibiti katika kutekeleza majukumu yao

Wakati wa ukaguzi nilibaini yafuatayo: kuwapo kwa mapungufu katika usimamizi na matumizi ya TEHAMA katika mamlaka za udhibiti ikijumuisha Soko la Bidhaa Tanzania, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji na Bodi ya Usajili wa Makandarasi ambapo unazuia ufanisi katika utoaji wa huduma za udhibiti.

Aidha, katika Bodi ya Usajili wa Makandarasi, nilibaini kutokuwa na hatua zisizotosheleza za kusimamia wanachama waliofutiwa usajili. Hii inaweza kusababisha umma kupata huduma bila kujua kutoka kwa watu au taasisi ambazo hazijasajiliwa na hawastahiki kutoa huduma, na ambapo ubora wa kazi zao haujahakikiwa.

Pia, katika Bodi ya Usajili wa Makandarasi na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania nilibaini matumizi duni ya tafiti kama zana ya kutambua, kutathmini, na kushughulikia mapungufu ya udhibiti ndani ya nchi.

Vilevile, nilibaini kuwapo kwa mikataba ya kipekee ya usambazaji yenye vifungu vya kupinga ushindani katika ununuzi wa magari ya Serikali ambayo yanainyima nchi fursa ya kufanya ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wa magari au wauzaji wakubwa, ili iweze kununua maguri kwa bei ya chini.

Ufanisi wa mashirika ya umma katika sekta ya afya

Mfuko wa Bima ya Afya ulipata nakisi ya shilingi bilioni 156.77 kwa mwaka wa fedha 2022/23. Pia, Mfuko unayadai mashirika ya umma jumla ya shilingi bilioni 280 kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Pia, nilibaini kiwanda cha Dawa cha Keko kilipata hasara kwa miaka minne mfululizo ambapo mwaka 2019 (shilingi bilioni 3.27), mwaka 2020 (shilingi bilioni 1.35), mwaka 2021 (shilingi bilioni 1.48), na mwaka 2022 (shilingi bilioni 1.35).

Vilevile, nimekuwa nikibaini bidhaa zilizoisha muda katika Bohari Kuu ya Dawa kwa miaka mitatu mfululizo. Dawa hizo zilikuwa na thamani ya kati ya shilingi bilioni 5.92 hadi bilioni 11.75 kati ya mwaka 2020/21 na 2022/23.

Mazao na bodi za mazao

Nilibaini mapungufu ambayo yanazuia ufanisi na tija. Mapungufu hayo yanajumuisha: Uwezo mdogo kwa bodi za mazao ili kutekeleza majukumu yao; Matumizi hafifu ya teknolojia ya kilimo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya kuboresha tija ya kilimo; Udhibiti duni wa ubora wa mazao; Usimamizi duni wa upatikanaji na usambazaji wa ubora na wingi wa mbolea; na hatua zisizofaa za kudhibiti upungufu wa sukari. Udhaifu huu unahitaji kushughulikiwa kwa kina kwa ajili ya kilimo endelevu cha mazao ya biashara na mazao ya chakula.

Pia, nilibaini hatua zisizotosheleza za kuzuia mapungufu katika programu za ruzuku ya mbolea. Vilevile, nilibaini dosari katika mchakato wa usajili wa wakulima chini ya mpango wa ruzuku ya mbolea.

Utendaji katika sekta ya uziduaji

Nilibaini ukosefu wa mpango kamili na utoaji duni wa huduma za kitaalamu kwa wachimbaji wadogo nchini kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania. Hii inapunguza kasi ya ukuaji katika sekta ya madini.

Pia, katika Shirika la Maendeleo ya Petroli, nilibaini ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani; na kutokuwapo kwa Hifadhi ya Taifa ya Petroli ya Kimkakati ambayo itasaidia upatikanaji wa nishati ya mafuta wakati wa upungufu.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali RK/MASHIRIKA/2022/23

Pia soma
CAG Kichere: Licha ya kupewa Ruzuku ya Tsh. Bilioni 31.55, ATCL imepata hasara ya Tsh. Bilioni 56.64, ongezeko la 61% kutoka hasara ya Mwaka 2021/22
- Ripoti 21 za CAG zatua Bungeni kwa ajili ya kuanza kujadiliwa
 

Attachments

Back
Top Bottom