Source: Gazeti la mwananchi
CHENGA ya mwili ambayo serikali iliipiga Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika utoaji wa ripoti ya utekelezaji wa maazimio dhidi ya kashfa ya Richmond, ilihitimishwa jana baada ya suala hilo kuyeyuka, bila ya wabunge kupata nafasi ya kuhoji.
Hali ilikuwa ya utulivu wakati spika wa Bunge, Samuel Sitta akiorodhesha shughuli ambazo zilitakiwa zijadiliwe kwenye mkutano huo wa 17 wa Bunge, ikiwemo suala la ripoti ya utekelezaji wa maazimio hayo dhidi ya kashfa ya Richmond, sakata la mgodi wa Kiwira na kampuni ya Reli (TRL), lakini haikuwezekana kujadiliwa kwa sababu mbalimbali.
âHili ni Bunge ambalo liko makini na linalotaka kutatua matatizo ya wananchi,â alisema Spika Sitta na kuongeza kuwa shughuli zote ambazo hazikuweza kujadiliwa, zitashughulikiwa kwenye mkutano ujao.
âNinasikitika kwamba tumefikia muda wa kuahirisha mkutano huu wakati bado kuna viporo. Liko suala la ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Richmond, suala la mgodi wa Kiwira, suala la (Kampuni ya Reli) TRL na Ticts (kampuni inayoendesha kitengo cha makontena Bandari ya Dar es salaam).â
Sitta alisema ilikuwa ni nia yake kwamba suala la utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge kuhusu Richmond lifikie mwisho mkutano huo, lakini jambo hilo limeshindikana.
Baada ya kutoa maneno hayo yaliyoonekana kuwa na nia ya kuwatuliza, Sitta aliwataka wabunge waunge mkono hoja ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ya kuahirisha mkutano huo, lakini hakukuwepo na sauti kubwa za kuunga mkono hoja hiyo kama ilivyo kawaida kiasi cha Spika Sitta kulazimika kutumia mbinu nyingine.
âSasa matokeo ya kura hii nitayatoa baada ya wimbo wa taifa,â alisema Sitta na kuruhusu wimbo huo upigwe.
Mara baada ya kumalizika kwa wimbo huo, Spika Sitta alisema kuwa baada ya kuuliza ni wabunge wangapi wameafiki hoja ya kuahirisha mkutano huo wa Bunge, amegundua kuwa waliosema ndio wameshinda na kuahirisha rasmi hadi Januari.
âTumeshangaa sana maana jana (juzi) serikali ilituahidi kwamba ingeleta ripoti hiyo leo(ya Richmond jana) ili Jumamosi iwasilishwe bungeni, sasa sijajua nini hasa kimetokea,â alidokeza mjumbe mmoja wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Mbunge wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai (CCM) alisema: âtuko stranded (tumekwama)... wananchi hawatatuelewa kuhusu kuahirishwa kwa suala la Richmond na kwa kweli linazidi kutuchanganya.â
Mbunge wa Karatu, Dk Willibroad Slaa (Chadema) alisema kitendo serikali ya CCM ni kielelezo kingine cha ubabaishaji akisema suala hilo si miliki ya chama hicho pekee.
âJambo pekee litakalofanywa na Chadema ni kwenda kwa wananchi kwa sababu ndio mahakama kubwa kuliko zote,â alisema katibu huyo wa Chadema.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti alisema alitegemea serikali ingetoa taarifa ya nini kilichotokea kwa sababu hata mpangilio wa ratiba ulikuwa ni wa kubalikabadilika.
Serikali ilishindwa mara mbili kuwasilisha ripoti hiyo kwa Kamati ya Nishati na Madini jijini Dar es salaam kwa kutoa sababu tofauti, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo nchini kwa Waziri William Ngeleja na aliporejea nchini waziri huyo aliwaambia waandishi kuwa wamekubaliana suala hilo lipelekwe moja kwa moja Dodoma.
Hata hivyo, suala la kuwasilishwa kwa hoja hiyo likawa kitendawili baada ya mkutano huo wa 17 kuanza baada ya kutojumuishwa kwenye shughuli za Bunge na iliripotiwa baadaye kuwa suala hilo lingerejeshwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini.
Juzi mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shelukindo aliiambia Mwananchi kuwa ana uhakika suala hilo lingejadiliwa leo lakini katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alikaririwa akisema kuwa Richmond haitajadiliwa tena kwa kuwa mjadala wake ni malumbano ambayo hayana faida kwa nchi.
Miongoni mwa maazimio hayo 23 ni kuwajibishwa kwa mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah.