- Source #1
- View Source #1
Nimekutana na hii taarifa mtandaoni ikisema mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kushirikiana na chombo cha utoaji wa huduma za Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa pamoja wametoa mkataba KANJU ENTERPRISES LDT wa kutoa huduma kwa wananchi ya kufanya marekebisho ya majina/taarifa zilizo tofautiana kwenye; Cheti cha Kuzaliwa na NIDA/Kitambulisho cha Taifa. Je ni upi uhalisia wa taarifa hii?
- Tunachokijua
- Kwa mujibu wa tovuti ya mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA, historia inaeleza kuwa Mwaka 1968 katika kikao cha 'Interstate Intelligence Gathering' kilichojumuisha wajumbe kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia, lilizaliwa wazo la kuanzisha Vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania. Kwa wakati huo nchi za Kenya na Zambia tayari zilikuwa na Vitambulisho vyao vya Taifa. Iliazimiwa kwamba ili kuimarisha mahusiano ya kiusalama yanayozingatia Utawala wa Sheria katika nchi hizo nne ni lazima nchi za Uganda na Tanzania nazo zikatoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia wao.
Hatimaye Rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alitia saini Hati ya kuidhinisha kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia Vitambulisho vya Taifa kinachojulikana kama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (National Identification Authority (NIDA).
Aidha mwaka 2006 Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) ulianzishwa rasmi kwa dhumuni la kutoa huduma za Usajili wa Matukio Muhimu ya binadamu, Ufilisi na Udhamini.
Mara kdhaa kumekuwapo na changamoto ambayo imekuwa ikiwakumba wananchi wengi katika vyeti vinavyotolewa na wakala huo pamoja na vitambulisho vya taifa kutoka NIDA, ambapo imekuwa ikitokea mtu mmoja cheti na kitambulisho kuwa na majina au taarifa zinazotofautiana hivyo kukwama kupata baadhi ya huduma hatimaye kupelekea baadhi ya watu wasio na nia njema kutumia mwanya huo kutaka kuwatapeli baadhi ya watu.
Kumekuwapo na taarifa inayosambaa mtandaoni ikidai RITA na NIDA wanafanya marekebisho ya majina au taarifa kwenye vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya taifa.
Je ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck ulibaini kuwa taarifa hiyo haikuchapishwa katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya NIDA pamoja na RITA.
JamiiCheck imebaini mapungufu kadhaa katika taarifa hiyo yanayoitofautisha dhidi ya taarifa rasmi ambazo hutolewa na mamlaka pamoja na wakala huo. Sehemu ya mapungufu hayo ni pamoja na kutofautiana kwa mwandiko (fonts), matumizi ya namba ya simu kwa ajili ya kuwasilisha nyaraka muhimu, kiwango cha pesa ambacho ni tofauti na kiwango rasmi kilichowekwa na mamlaka ya vitambulisho vya taifa endapo mtu akihitaji kubadili taarifa zake kwa kulipia kiasi cha shilingi elfu ishirini 20000/= pia uwepo wa kampuni batili iliyotajwa kupewa tenda hiyo ikiitwa ‘KANJU INTERPRISES LDT’
Hata hivyo taarifa inayofanana na hiyo ambayo haikuwa ya kweli ilikanushwa na kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya RITA na NIDA na kuwataka wananchi kupuuza taarifa hiyo.
Aidha kupitia tovuti ya NIDA unaelezwa mchakato rasmi ambao mtu anaweza kuufuata ili kukamilisha ombi la kubadili taarifa katika kitambulisho chake ambapo mtu atahitajika kuwa na Kadi ya kliniki, tangazo, cheti cha kuzaliwa, cheti cha darasa la vii, kidato cha iv ama ‘leaving certificate’
Hati ya kiapo cha kubadili jina (Deedpoll) toka kwa wakili anayetambuliwa na Chama cha Mawakili Tanzani (TLS) kisha kiwasilishwe Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kupata Usajili wa Jina unalorekebisha, pia kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali linalotolewa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuonyesha mabadiliko ya jina yaliyofanyika.
Ombi la mteja litawasilishwa kwenye kamati ya Usajili na Utambuzi wa watu, iwapo watajiridhisha kuwa ombi limekidhi vigezo ndipo watatoa kibali ili Afisa Msajili aweze kuendelea na hatua ya kufanya maboresho, ombi lisipokidhi vigezo, kibali hakitatolewa na Afisa Msajili haruhusiwi kuendelea na hatua yoyote ya maboresho.