Riwaya: Bondia

RIWAYA: BONDIA
MTUNZI: HUSSEIN ISSA TUWA


SEHEMU YA KUMI NA NANE


"Namaanisha huo utaratibu wa kukusubiri urudi na Deus aongee nawe...lakini mambo yaliharibika pale Rachel aliposhika ujauzito..."
"Deus akamkana...!" Roman alidakia kwa jazba, sasa machozi yakimtiririka waziwazi. Sada alitikisa kichwa kwa simanzi. "Hapana. Akamtaka atoe ile mimba...!"
"Ama!?" Roman alimaka kwa mshangao, "Yaani...kwa nini?"
"Kuna sheria kali sana dhidi ya wanaume wanaowatia mimba wanafunzi kaka Roman. Deus alikuwa akiogopa hilo, lakini Rachel hakutaka kutoa mimba. Alimwambia akupigie simu huko uliko akueleze kila kitu...Deus hakuwa tayari, alisisitiza msimamo wake kuwa Rachel atoe mimba. Ikawa mizozo na majibizano. Rachel akaanza kukosa kuhudhuria masomo, kutwa barabarani akimtafuta Deus. Hali ilipozidi kuwa mbaya, Rachel akamtishia kumshitaki kwa wakuu zake wa kazi. Deus alikuja juu, na hapo ndipo alipomtakia kuwa haujui ule ujauzito..."
"Hah!"
"Ndiyo kaka...Rachel alichanganyikiwa!"
Kufikia hapa Roman alikuwa akilia waziwazi. Uchungu aliokuwa nao haukuwa na mfano. "Kwa...kwa...kwa hiyo nd'o mdogo wangu akanywa sumu kwa hilo...? Why Rachel...? Why...?" Roman alisema huku akizongwa na kwikwi za kilio. Sasa na Sada naye alikuwa akilia pamoja naye. Mark alitikisa kichwa huku naye akitiririkwa na machozi. Ilikuwa ni hali ya kutia uchungu sana. Lakini uchungu bado ulikuwa haujatimia.
"Hapana kaka Roman...hilo silo lililosababisha Rachel achukue uamuzi aliochukua..." Hatimaye Sada alimjibu. Roman alimtazama kwa mshangao.
"Sio hilo...?" Aliuliza kwa kutoamini, akitembeza macho baina ya Mark na Sada. "Sasa kuna ubaya gani tena zaidi ya huu ambao mdogo wangu amefanyiwa jamani? Hebu niambie Sada...ni nini tena Deus alichomfanya mdogo wangu...?"
"Ah, kaka Roman...we' acha tu..." Sada alisema na kuangua kilio upya.
"No! Nieleze tafadhali...niambie tu mdogo wangu...ni nini kilichosababisha Rachel ajiue?"
Sada alilia kwa muda, kisha akajilazimisha kumueleza.
"Siku hiyo...kiasi cha wiki moja baada ya Deus kuukana ujauzito wake, Rachel aliniomba nimsindikeze nyumbani kwa Deus ili ajaribu kuzungumza naye..." Sada alitulia kidogo, akipenga kamasi na kujifuta machozi, "...huko tulimkuta Deus akiwa na mwanamke mwingine!" Sada alimalizia kauli yake na kuangua kilio kizito.
Duh!
Mark na Roman walitazamana, uchungu aliokuwa nao Roman ukijiweka wazi machoni mwake.
"Ilikuwa ni vurugu kubwa...Rachel akilia na kumshutumu Deus kwa kumlaghai, yule mwanamke mwingine naye akimshutumu Deus kwa kumlaghai, Deus naye akimkana Rachel na kumuita malaya...."
"Ah, jamani...hivi ni Deus huyu huyu nimjuaye ndiye aliyefanya mambo hayo?" Roman alisema kwa mshangao na uchungu.
"Ndiye kaka...ndiye." Sada alimjibu huku akishindana na kwikwi za kilio, kisha akaendelea, "...na kitendo alichomfanyia Rachel pale nyumbani kwake siku ile ndicho kilichogongelea msumari wa mwisho...pamoja na kuwa nilikuwa naye muda wote siku ile baada ya kutoka kule kwa Deus...Rachel aliamka usiku wakati wote tumelala, na kunywa sumu...nilikuja kuamshwa na sauti zake akikoroma na kugumia...nilipogundua alichofanya, niliwaarifu waalimu na tukamkimbiza hospitali..." Sada alimalizia na kuangua kilio. Hakuweza tena kuendelea. Alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa.
"Mimi nilipigiwa simu na mmoja wa waalimu wao...Rachel aliandika namba yangu na ya Deus pale shuleni kwa ajili ya dharura yoyote itakayotokea...walisema namba ya Deus ilikuwa haipatikani. Nilipofika hospitali na kukuta hali ilivyo, ndipo nilipokupigia simu. Baada ya hapo nimekuwa nikijaribu kumafuta Deus kwenye simu bila mafanikio. Jamaa hakuwa hewani kabisa...nadhani aliamua kubadilisha namba kabisa." Mark aliingilia kati na kufahamisha zaidi.
"Lakini mi' nilimpata...wakati Rachel anahangaika usiku ule, kabla hata sijawaita waalimu nilimpigia na nikampata...nikamwambia kuwa amesababisha Rachel anywe sumu...na kwamba nitahakikisha namfikisha mbele ya sheria...nadhani baada ya hapo ndio akaamua kufunga kabisa simu yake!" Sada alisema huku akilia.
Roman alilia! Alilia sana. Alilia kwa uchungu, majuto na hasira pia. Alilia kweli kweli.
"Kwa hiyo...Rachel hakuacha ujumbe wowote kueleza sababu za uamuzi wake ule?" Hatimaye Roman aliuliza.
"Hapana...hakuacha chochote..." Sada alisema.
Roman alibaki akitikisa kichwa kwa masikitiko.
"Na ndio maana tunashindwa kumchukulia Deus hatua yoyote sasa Roman...mimi nilishindwa kwenda polisi...nigekuwa na ushahidi gani? Ni ushuhuda wa Sada tu, ambao unakanika kirahisi sana..." Mark alisema kwa uchungu.
"Dah! Ni kweli Mark...hakuna ushahidi wa kushikika na kuukabidhi kwa polisi...lakini ushahidi wa kuwa Rachel...mdogo wangu, amekufa upo...she is dead Mark! Dead! Bado binti mbichi kabisa!" Roman alisema kwa uchungu, "...na Deus ndiye anayehusika...lazima alipe! Hii haina mjadala kabisa, lakini kwanza nataka nisikie kutoka kwake mwenyewe...anasemaje kuhusu kifo cha mdogo wangu niliyemkabidhi kwake?" Hatimaye alisema.
"Mimi nilikwenda kumuona Deus jana kabla sijaenda uwanja wa ndege kukupokea Roman..." Mark alisema, na kuendelea, "... hakukana kabisa kuwa alikuwa na uhusiano na Rachel...alisema ni jambo la bahati mbaya naye hakulitegemea...hakutegemea kuwa Rachel angechukua uamuzi ule...na hakika alikuwa na majuto makubwa..."
"Sasa mbona hakuja hata kwenye maziko Mark...?"
"Alisema hataweza kuja...hataweza kukutazama tena usoni baada ya yote yaliyotokea..."
Roman alilia sana. Alilia kwa muda mrefu.
"Basi ana bahati mbaya sana... kwa sababu mimi nataka nimtazame yeye usoni..." Hatimaye Roman alisema huku akijifuta machozi.


***
Kapten Deusdelity Macha aliteremka kutoka kwenye gari la jeshi na kutembea kiaskari kuuelekea mlango wa nyumba yake. Upande wa pili wa barabara, Roman alijiinua kutoka kwenye benchi alililokuwa amekalia lililokuwa mbele ya kibanda cha mkaanga chipsi na kumfuata taratibu. Usoni alikuwa amevaa miwani ya jua na ndani ya kifua chake alikuwa akihisi mfukuto wa ghadhabu wakati akimtazama Deus akifungua mlango wa nyumba yake na kuanza kuingia ndani.
"Hallo Deus...!" Aliita taratibu, sasa akiwa hatua si zaidi ya tano kutoka mlangoni kwa Deus. Deus aligeuka, na mara tu alipomuona uso ulimbadilika na kusajili mshituko mkubwa sana.
"Roh...Roman!" Alisema kwa kitetemeshi na kubaki akimtazama.
Walitazamana.
"Un...nataka nini...umekuja lini...?" Deus alijikuta akiuliza bila kufikiri. Roman alibaki akimtazama, chuki isiyo kifani ikijijenga moyoni mwake.
"Rachel is dead Deus."
Deus alitazama chini.
"Na...naomba uende Roman...nasikitika kwa msiba uliotokea, lakini..."
"Sijakuona msibani hata kidogo Deus...sasa najiuliza, kwa mtu ambaye ndiye niliyekukabidhi mdogo wangu wakati naondoka nchini, kwa nini usitokee msibani?" Roman alimwambia kwa sauti ya utulivu. Deus alianza kufunga mlango, akimuacha Roman nje. Haraka sana Roman aliweka kiatu chake mlangoni na kuuzuia ule mlango kufunga. Deus aliinua uso wake na kumtazama Roman kwa mshangao.
"Toka bwana!" Alisema huku akimsukuma kwa ule mlango. Roman hakutetereka.
"Umemuua Rachel Deus...."
"No! Amejiua mwenyewe Roman, na naomba usinilaumu kwa hilo...mi' sikuwa na nia mbaya kwake, nilimpenda kikweli kabisa, lakini..."
Hapo Roman alishindwa kuzuia ghadhabu zake. Aliukamata mlango kwa nguvu na kumsukumia ndani Deus huku naye akimfuata nyuma yake.
"Kelele wewe! Ulimpenda mdogo wangu wewe? Mi' nilikukabidhi ili umrubuni na kumtelekeza?" Alimfokea huku akimsukuma kwa mikono yake yote miwili kifuani. Hapo hapo Deus alimtandika ngumi kali ya uso, na Roman akayumba hadi ukutani huku akiachia mguno wa maumivu. Deus aligeuka na kukimbilia ndani zaidi ya nyumba yake na kujifungia chumbani kwake, ambako alienda moja kwa moja hadi kwenye simu iliyokuwa kando ya kitanda chake.
"Hallo Polisi? Mimi ni kapteni Desudelity Macha! Nahitaji msaada haraka sana nimevamiwa nyumbani kwangu...haraka!"
Nyuma yake Roman alikuwa akibamiza mlango wa kile chumba.
"Fungua mwanaharamu, fungua!" Roman alifoka huku akiubamiza mlango ule kwa hasira.
"Ondoka Roman, ondoka! Mi' nimeita polisi...yatakayokukuta tusilaumiane!" Deus alimpgia kelele kutokea chumbani kwake.
"Umemuua mdogo wangu Deus! Nimekukabidhi nikiamini kuwa u-binaadamu kumbe ni shetani usiye haya?"
"Sikudhamiria Roman! Hebu ondoka upesi Roman...ondoka nyumbani kwangu!"
Roman alipandwa na ghadhabu. Alirudi nyuma na kuurukia kwa nguvu ule mlango. Lakini ule mlango ulikuwa mgumu sana naye aliishia kuanguka chini kwa kishindo.
"N'takuua mwanaharamu! N'takuua kama ulivyomuua mdogo wangu shenzi wee!" Roman alipiga kelele kwa hasira. Nje ya nyumba ile majirani walisikia mayowe na wakaanza kukimbilia kwenye ile nyumba kujua kulikoni. Roman aliubamiza mlango kwa nguvu bila mafanikio. Alitoka mbio na kuingia jikoni. Akachukua chupa ya mafuta ya taa na kuitupia pale mlangoni, chupa ikapasuka na mafuta ya taa yakiilowesha pazia iliyokuwa imetundikwa mbele ya ule mlango.
Akaliwasha moto lile pazia.
"Utatoka humo ndani paka we! Utatoka! Kama hutoki basi utaangamia humo humo ndani kwa moto baradhuli mkubwa we!" Alimtupia maneno ya ghadhabu. Moto ukapamba kwa kasi, mlango ukaanza kuugua, moshi ukatanda kila mahali. Kule chumbani Deus alianza kukohoa kwa taabu, moshi ukimuelemea. "Roman! Roman...acha ujinga...acha..." Alipayuka kwa taabu.
Sasa moto ulikuwa umetawala mlango wote, na bila kufikiri Roman aliurukia ule mlango na kupita nao mzima mzima mpaka ndani, huku nyuma akisikia mayowe ya majirani na ving'ora vya magari ya polisi.
Deus alimshitukia Roman akitua ndani ya chumba kile kwa kishindo. Alijitupa pembeni na kujaribu kumzunguka Roman ili akimbilie nje ya ya chumba kile, lakini Roman alimrukia na kumdaka kiuno na wote wawili wakaenda chini. Deus alimsukumia Roman teke lililomtupa pembeni. Wote waliinuka kwa wakati mmoja na Roman akamsukumia konde kali la uso, lakini Deus aliliona, akabonyea likapita hewani naye akamtandika ngumi nzito ya tumbo. Roman aliguna kwa maumivu na hasira huku akiyumba. Sasa ule moto uliokuwa mlangoni alitambaa mpaka ndani na kupamba kwenye shuka la kitanda.
Roman akamrukia Deus mzima mzima na kumshidilia kichwa cha mwamba wa pua, na Deus alipelekwa mpaka ukutani, akiachia kilio cha maumivu huku akijishika pua iliyokuwa ikibubujika damu. Roman alimuendea na kumchapa konde kali la mbavu na Deus alijipinda huku akigumia kwa uchungu. Roman akamshindilia konde jingine la ubavu wa pili, Roman akajipindia upande wa pili. Roman akampa konde jingine zito la tumbo, Deus akajipinda kwa mbele. Roman akamkamata kichwa na kumsihdilia kwa goti usoni na Deus alienda chini kama mzigo. Sasa chumba chote kilikuwa kimetanda moto, kitanda chote kilikuwa kikiwaka moto, na ndimi za moto ule zilirukia kwenye pazia za madirisha, nayo yakashika moto.
"Acha Roman...acha!" Deus alikuwa akibwabwaja huku akijitahidi kuinuka. Sasa Roman alikuwa amepandwa wazimu wa ghadhabu. Alimdaka ukosi wa gwanda lake la jeshi na kumuinua, kisha akamshindilia kichwa kingine kilichotua sawia mdomoni.
Deus alichia yowe kubwa huku akienda tena chini.
"Umemuua mdogo wangu, Deus! Umemuua mdogo wagu halafu unaniambia nitoke nyumbani kwako? Nyama we, sasa nawe utaenda kuzimu kunakokustahili!"
"Roman, I am sorry...! Nisa...me...he...brother!" Deus alibwabwaja, lakini Roman alikuwa ameshapanda mzuka wa kulipa kisasi. Huku wakiwa wamezongwa na moshi kila upande, alimkamata na kuunyofoa kwa nguvu mkanda wa gwanda la kijeshi alilokuwa amelivaa Deus na kumzingira nao shingoni.
"Roman Nooookkhhhh!" Deus alipiga kelele lakini hapo hapo Roman alianza kumkaba kwa kutumia ule mkanda, akimkata mayowe yake na kumuacha akikoroma.
"Utamfuata Rachel alipo ili ukamuombe msamaha nyau we!" Roman alisema huku akitweta na akizidi kumkaba kwa ule mkanda. Macho yalimtoka pima Deus, alianza kutupa mikono huku na huko, akijitahidi kufurukuta bila mafanikio kutoka kwenye kifo dhahiri kilichokuwa mbele yake.
"Polisi! Jisalimishe sasa hivi!" Sauti kali ya kiaskari ilifoka kutokea mlangoni. Roman aliinua macho yake yaliyowiva kwa ghadhabu na moshi uliotanda mle ndani, na aliona kivuli cha mtu akiwa amesimama pale mlangoni.
"Sijisalimishi mimi! Naua! Namuua bazazi huyu! Niacheni nimmalize halafu nanyi mkaninyonge!" Aifoka huku akizidi kumkaba. Mara hiyo mlio wa bastola ulisikika, na kabla hajatanabahi, Roman alishuhudia kiumbe kikijitupa mle ndani na kujibiringisha sakafuni, kisha akajikuta akiwa amewekewa kabali shingoni kwake na mdomo wa bastola ukiwa umekandamizwa kwenye upande wa kichwa chake.
"Uko chini ya ulinzi mwanaume! Muachie huyo mtu sasa hivi, ama si hivyo napasua bichwa lako kwa risasi!"
Ilikuwa ni sauti kali ya kike.
Roman alizidi kumkaba Deus kwa ule mkanda, pua zikimtutumka, akitweta kwa ghadhabu.
"Niue nami nakufa naye afande!" Alisema kwa hasira, kisha akamalizia, "...huyu mwanaharamu kasabaisha kifo cha mdogo wangu gaddemitt, afande!"
"Utakufa wewe kwanza, naye utamuacha akitapatapa kutafuta pumzi, lakini akiwa hai. Muachie huyo askari sasa hivi!" Fatma, wakati huo akiwa koplo, alisema kwa msisitizo, bastola yake ikiwa kichwani kwa Roman. Na hata alipokuwa akisikia maneno yale, Roman alishuhudia askari wengine watatu wakivamia mle ndani, bunduki aina ya SMG zikiwa mikononi mwao, zote zikiwa zimemuelekea yeye, huku moto ukizidi kupamba mle ndani. Alihema kwa pumzi za haraka haraka, na huku bado akizidi kumkaba Deus kwa ule mkanda, alisogeza mdomo wake sikioni kwa yule rafiki yake aliyebadilika na kuwa adui yake mkubwa, na kumnong'oneza kwa sauti nzito ya kongofya.
"Umeokolewa na askari safari hii Deus, lakini ujue kuwa bado kifo chako kiko mikononi mwangu...I will kill you one day Deus...that's a promise (nitakuua tu siku moja Deus...nakuahidi hilo)!" Kwisha kusema hivyo, alimsukuma mbele kwa nguvu, akimuacha Deus akisambaratika ovyo sakafuni, naye akijikuta akisukwasukwa kwa nguvu na wale askari, mikono yake ikivutwa nyuma na akipachikwa pingu.


***ROMAN aliahidi ataua......je ataua kweliiiii


TUSUBIRI MPAMBANO.....


davidson689 Toplady ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy Khantwe mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrango mangimeza muuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru
 
Khaaa Casuist fupi sana bwana....
 
Last edited by a moderator:
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…