Riwaya; CONNECTION

RIWAYA YA CONNECTION EP 06
Mtunzi: Robert Heriel
Mwaka 2024
Kazi hii itarushwa katika mitandao kwa akaunti hizi:
Facebook: Robert Heriel Tz
Jamii Forum: Robert Heriel Mtibeli
WhatsApp +255693322300
ILIPOISHIA
“ Nashukuru Boss kwa kunisindikiza. Nimefurahi sana. Nje ya kazi naweza itumia namba yako?”

“ why not?”

“hayo ndio maneno” Lucy akasema akiwa amefurahia kukutana na Kijana yule ndiye Amini. Wakaachana huku Lucy akiapa moyoni mwake kumteka Amini awe Mpenzi wake.

********************
ENDELEA


GAZETI LA NYUKI;

MIMI SIJUI, uk 03


“Ongezeko la kutisha la idadi ya watu limegeuka zimwi lenye kutisha. Kadiri siku ziendavyo mambo yanazidi kuwa mabaya na magumu. Ile dhana ijulikanayo kuzaa ni Baraka kwa jamii za Afrika wakisema kila mtoto huja na sahani yake imekuwa dhana yenye sumu kali kuliko bomu la nyukilia. Ongezeko kubwa la watu limegeuka mchwa mbaya mwenye kutafuna rasilimali na kumomonyoa maadili ya maadili ya dunia. Ni kweli kuzaa ni Baraka lakini kuzaa pasipo kipimo wala mahesabu haiwezi kuwa Baraka tena zaidi ya mzigo mzito uliobeba laana ambayo dunia itashindwa kuhimili uzito wake. Dunia itaanguka na watu wake watakwisha. Hapo maisha yanaweza kukoma kama hatua Fulani zenye kuumiza hazitachukuliwa,

Wapi tutakaa na kujenga nyumba zetu. Wapi tutakapolima kwenye mashamba yatakayozalisha mazao yatakayotupa chakula. Vipi shughuli zingine za uzalishaji. Kwa kweli bado sijajua ni wapi tutatupa takataka tutakazozizalisha kama ni ardhi au angani pengine baharini je huko samaki na viumbe bahari watasalimika. Sina hakika kama tutashindana kuweza kuzifanyia recycling baadhi ya malighafi. Wapi itapatikana hifadhi ya wanyama na makazi yao. Kunyang’anyana rasilimali kunakotokana uhaba wa rasimali kutachochea vita baina ya jamii za dunia.

Mimi sijui matokeo ya kamari inayoendelea katika mabadiliko ya tabia ya nchi. Hali ya hewa haipo vile ilivyokuwa. Sio upepo sio mvua. Sio joto wala baridi kwenye jotoridi. Wala sio Miale ya jua na nani mwenye kujua haya mawingu ipo siku yatatoweka tusiyaone tena. Mimi sijui labda ningekuwa na tumaini katika maji yaliyohifadhiwa ardhini baada ya mito na vijito kwenye vyanzo vya maji kuharibiwa vilivyo. Lakini ni tumaini lisilo na hakika. Kama tumeshindwa kulinda maji yaliyorahisi kuyapa juu ardhi nay ale ya angani yasafiriyo na mawingu, tutaweza kweli kutunza maji yaliyochini ya ardhi yanayotembea mamia kwa maelfu ya kilometa katika mikondo ya miamba ya chini ya dunia. Hilo sijui.

Njia mbadala ni zipi. Zitatufikisha wapi hasa. Kila mtu anataka kufurahia maisha pasipo kuangalia hatma ya dunia. …..”

Peter Mirambo alikuwa akisoma Gazeti la Nyuki kwa makini huku akishushia na juisi ya miwa katika mgahawa uliokuwa katikati ya jiji. Alikuwa akimfuatilia Amini ambaye siku hiyo kwake ilikuwa siku ya mapumziko ya kazi hivyo akaamua kwenda kupumzika katika mgahawa huo. Pasipokujua kuwa kuna mtu anamfuatilia, Amini aliendelea na kujivinjari akila samaki mkubwa aliyekaangwa na ugali wa dona chakula ambacho alikuwa akikipenda sana.

Kilichomfanya Peter anunue gazeti hilo ni picha ya mwanamitindo ambaye aliuawa wiki kadhaa kuwa mbele ya gazeti, alafu kulikuwa na kichwa cha habari kilichoandikwa “Blackmail ilivyomwondoa Mwanamitindo Jack Ha Uk 04” Kabla ya kufungua ukurasa wa nne Peter alivutiwa na kichwa cha habari kilichopo ukurasa wa 03 “MIMI SIJUI” ambapo kumbe ilikuwa habari ya mabadiliko mabaya ya hali ya hewa ambayo mwandishi aliamini yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko kubwa la watu.

Peter akafungua ukurasa uliofuata ambao ulikuwa ukurasa wan ne. “Blackmail ilivyomwondoa Mwanamitindo Jack Ha”

“ Mtandao hatari usiojulikana ambao kazi yake kubwa ni kuwa Blackmail watu wakubwa, matajiri, wafanyabiashara na viongozi wa kisiasa umepiga mhuri safari ya mwisho ya Jack Ha ambaye alikuwa Miss Tanzania aliyeshinda Miss World. Inadaiwa kuwa mtandao huo unaohusisha watu tofautitofauti tena wengine wakiwa ni vigogo wakubwa waliopo serikalini umekuwa ukitesa kwa siri baadhi ya watu ambao wamenaswa katika mitego yao.

Jack Ha alikutwa katika mtego mbaya baada ya kukutana na kijana aliyetambulika kwa jina moja, Bizanda ambaye ndiye aliyeonekana kwenye video ile iliyovuja. Chanzo changu ambacho kilinambia nifiche utambulisho wake kiliniambia kuwa Bizanda ndiye aliyemrubuni Jack Ha. Huku Bizanda akijihusisha na biashara ya madini kutokea Congo. Hata hivyo nilipouliza chanzo changu kuwa ni lini na wapi mahusiano ya Bizanda na Jack Ha yalianzia kilisema hakijui. Bado nafuatilia kisa hiki. Macho ya gazeti hili bado yanaendelea kufuatilia tukio hili mpaka pale ukweli wote utakapopatikana. …”

Ingawaje ilikuwa ni habari ya kusikitisha inayohusu kujiua kwa Jack Ha aliyekuwa Miss World lakini iligeuka kuwa habari yenye kuvutia kwa Peter Mirambo. Aliamini habari ile inauhusiano wa namna asiyoijua na kile anachokichunguza. Alipoangalia mwandishi wa ile habari, alikuta jina moja, COCO. Ghafla akamwona Amini akitoka kwenye ule mgahawa, Petee akaamka akiliacha lile gazeti na kinywaji chake cha juis ya miwa kikiwa nusu glasi. Akawa anamfuata nyumanyuma Amini. Kumbe kwa nje ya Mgahawa ilikuwepo imepaki gari ya Lucy. Amini akapanda kisha gari ikaondoka. Peter naye akaingia kwenye gari yake na kuwafungia mkia.

Wakaenda mpaka ilipofukwe ya watasha iliyopo Maeneo ya Masaki, wakashuka bila ya kujua wanafuatiliwa. Peter akashuka akaenda kinyemela mpaka lilipokuwa limepaki gari la Lucy. Akatoa funguo maalumu ya magari akafungua mlango kisha akaingia ndani ya gari la Lucy. Akaweka vinasa sauti na Kamera kisha akashuka akarudi kwenye gari yake. Akawa anawatazama akiwa ndani ya gari.

Usingizi ulianza kumpitia baada ya kusubiri kwa takribani masaa mawili, tayari ilikuwa inaingia saa moja za jioni. Alikurupuka baada ya kusikia sauti, ilikuwa mngurumo wa gari la kina Lucy uliokuwa umenaswa na vile vinasa sauti. Walikuwa wameshaingia ndani ya gari na tayari walikuwa wanaondoka.

“Mimi nafikiri acha nikafanye hiyo kazi mpya. Huko kuna hela kuliko hii ambayo ungenipa wewe. Siwezi acha Dollar elfu tano Amini kwa mwezi. Ninachohitaji ni pesa tuu” Lucy alikuwa akiongea na moja kwa moja Peter alikuwa akisikiliza mazungumzo hayo kupitia vinasauti alivyoviweka kwenye gari lake.

“ Lakini kama ungefanya kazi pale kwetu kama mwanasheria wa kampuni ungepata faida kubwa ya uzoefu kuliko kuenda kufanya kazi iliyonje ya fani yako”

“ Faida ya kazi ni kupata kipato Amini. Hakuna faida nyingine zaidi ya hiyo”

“ Vipi kuhudumia jamii?”

“Kwani hii kazi mpya sihudumii jamii? Amini bhana! Siwezi acha hii nafasi. Hata wewe ni daktari lakini mbona uko pale kwa kazi zingine ambazo sio za kitabibu”

“ Hofu yangu kukupoteza honey”

“Hahah! Nilijua ni wivu wako tuu. Mimi ni mwanamke ninayejitambua. Hakuna mwingine ninayempenda zaidi yako” Lucy akasema,

“Unajua mimi nakupenda sana, Nitakufa mimi kama atatokea mtu aninyang’anye Lucy wangu”

“Mimi nilivutiwa na wewe tangu siku ya kwanza. Wewe ndiye mwanaume wa kwanza kuuteka moyo wangu. Amini wewe ni mwanaume wa ajabu ambaye nashindwa kuzuia hisia zangu pale nikuonapo. Naomba usije niletea mapichapicha”

“Siwezi Lucy. Kwako nimelia kadi ya mwisho”

Hapo wote wakacheka. “Kwa hiyo unaanza lini kazi?” “ Bado sijajua. Kazi ile ni mpaka nipigiwe simu. Bila simu siwezi kwenda. Sio kazi ya kila siku”

“Kazi gani hiyo?” Peter akawaza baada kusikia maneno ya Lucy. Tayari ilikuwa saa mbili usiku. Amini alishushwa Ubungo Shekilango mahali alipokuwa anakaa. Kisha Lucy akaendelea na safari kuelekea nyumbani kwake.

***************

Kesho yake kama kawaida Amini alienda kazini. Alipofika alishangaa kumkuta Kolowa ameketi kwenye kiti.

“Kulikoni Boss!”

“ Wiki mbili zimepita. Kazi yako inaenda vizuri. Sasa ni wakati wa kukupa jukumu letu lile”

Hapo pakawa kimya kwa kitambo.

“Hivi yule mwanamke mrembo mweupe ulimwambia ungeonana naye lini ili tumuingize kwenye majukumu yetu?”

“Tulikubaliana naye vizuri kwamba wiki mbili ningewasiliana naye. Lakini jana alinipigia simu na kunijulisha kuwa ameshapata kazi sehemu nyingine”

“Kazi sehemu nyingine? Ungemwambia aje tuonane tuzungumze kuhusu maslahi yake”

“amesema kule analipwa dolla elfu tano”

“wapi huko wanalipa pesa nyingi kiasi hiko. Ila ni uzembe wetu. Liwezekanalo leo lisingoje kesho. Unaona sasa. Lakini haidhuru. Mtafute mwambie tutaongeza dau atalipwa dolla elfu saba”

“Boss! Dolla elfu saba unamaanisha milioni kumi na saba za kitanzania”

“Mimi simaanishi hivyo, hiyo niliyotaja ndio sahihiu. Dolla kila siku inapanda shilingi inaporomoka. Leo ni milioni kumi na saba kesho kutwa utashangaa milioni arobaini na saba” Akameza mate kisha akaendelea.

“Hakikisha unamtafuta umweke kwenye nafasi yetu. Ni muhimu. Mimi naondoka”

“Unaondoka bila kunipa majukumu mapya lakini”

“Majukumu mapya yanahitaji yule mrembo awepo. Ukishampata nijuze. Zingatia majukumu mapya yanaenda sambamba na maslahi mapya ambayo yatabadilisha maisha yako ankol. Tutawasiliana “

Akaondoka akiwa amemuacha Amini akiwa na maswali mengi. Ni kazi gani hiyo ya kumlipa Lucy mahela yote hayo. “Kuna jambo silifahamu kuhusiana na hii kampuni” akawaza. Huku akiwa anaingia ofisini kwake.

**********

“Nafahamu kuna mtu anakufuatilia. Nina mpango wa kumpumbaza huyo mtu. Jiandae”

Kalage alikuwa akiongea na Lucy kwenye simu.

“Mtu gani?”

“Nimekuambia jiandae. Kuna mtu anakuja kukuchukua” Kalage akasisitiza.

“Namwona mtu ameletwa na bodaboda”

“Ndio mwenyewe huyo. Fuata maelekezo yake” Kalage akaongea kisha simu ikakatika. Wakati huo Peter alikuwa yupo kwenye gari yake akiwa ameegesha umbali kidogo kutoka ilipo nyumba ya Lucy. Kitendo cha kuiona ile bodaboda iliyombeba kijana mmoja kilimfanya azidi kuwa makini kutazama. Akamwona yule kijana aliyebebwa kwenye bodaboda akishuka, kisha akatoa pesa akamlipa yule dereva bodaboda, kisha bodaboda ikaondoka. Yule kijana wala hakuangalia huku na huku, yeye akaenda kugonga moja kwa moja kwenye geti la Lucy. Punde Geti likafunguliwa na yule kijana akaingia ndani.

Peter akataka kushuka lakini akili yake ikamuonya. Punde akasikia kupitia vinasa sauti watu wakiingia kwenye gari la Lucy. Akamsikia Akizungumza na yule kijana.

“ Nafikiri wakati huu hamtaniletea mambo kama ya wakati ule. Mlinikera sana” Alimsikia lucy akiongea.

“Hapana Boss. Yale yalikuwa tuu makosa. Wakati huu hayatajirudia”

“Ndio maneno yenu siku zote. Haya nipeleke upesi” Lucy akasema,

Kisha gari akianza kunguruma, lakini ghafla vinasa sauti vikawa vinakwaruza kwaruza, jambo hili lilimshangaza sana Peter. Akiwa anashangaa punde pakawa kimya. Yaani ni kama vile vitu alivyokuwa ameviweka kwenye gari la lucy vimezima.

Akiwa anashangaa punde akaona geti linafunguka kisha gari ya lucy linatoka likiwa na vioo vya tinted. Akainama kwa chini. Likapita. Akawasha gari kisha akalifungia mkia. Hao wakiwa njia wanatoka Mbweni kupitia barabara ya ununio akapishana na gari jingine jeusi. Hakulizingatia. Alikuwa makini sana asije akalipoteza Gari la Lucy, alitaka kujua ni wapi alipokuwa anaelekea. Alikuwa akitaka kujua ni kazi gani mpya Lucy kaipata na wapi eneo lake la kazi.

Alitembea mpaka walipofika bahari Beach, hapo palikuwa na Super market, gari ya Lucy ikasimama, akashuka yule kijana pekeake. Peter akapitisha gari yake na kuisimamisha mbele kidogo. Kisha akamwona yule kijana akitoka akiwa kabeba mfuko wenye nembo ya ile supermarket, yule kijana akapanda kwenye gari la lucy na kunza kuendesha. Mpaka walipofika Mbezi Beach ile gari ya Lucy ikasimama kwenye Bar moja, akashuka yule kijana tena. Jambo hili likaanza kumpa mashaka Peter. “Haiwezekani mara mbili zote ashuke pekeake huyu kijana kuna ujumbe hapa ninapewa siupati. Hii inamaanisha nini” akawaza pasipo majibu.

Ilipita nusu saa bila ya yule kijana kurudi, Peter akatoka akamwona yule kijana anakunywa zake pombe hana habari. Akajua amechengwa akili, akaenda kwenye gari ya Lucy kuchungulia hakuna mtu.

**********

“Yes Hello. Ninaongea na nani?”

“ Sidhani kama hilo ni muhimu kwa sasa. Unapaswa kujua kuwa kama hutafuata maelekezo nitakayokupatia maisha yako yanaenda kuharibika” Kolowa alisema akiongea na mwanamke kwenye simu.

“ Hivi unajua nani unayezungumza naye? Unajua hatari ambayo unajaribu kuiita. Usitafutie watu ubaya kijana”

“Hujiulizi wapi nimepata namba zako. Enhee! Kama nimeweza kupata mawasiliano yako kwa nini usiamini kuwa ninaweza kuharibu maisha yako tangu sasa” Kolowa akasema,

“ Usijiamini sana kijana. Ninaweza kukupata popote ulipo. Simu yako hiyohiyo ndio itakayotumika kukutia mikononi”

“Sikia Mhe. Nisikupotezee Muda. Jana yote uliyoyafanya kwenye gari na Mwanamuziki maarufu zaidi niliyashuhudia kwa macho yangu mawili”

“Wait….! Unazungumzia nini?”

“unaanza kubabaika eenh! Nimekuambia ninauwezo wa kuyaharibu maisha yako. Kwa sasa mtu pekee ambaye ameshikilia maisha yako ni mimi.”

“ Uliona nini?”

“ Sitaki kuelezea jinsi usivyojiheshimu, uchafu wako wa siri kama nikiuanika hadharani unafikiri nini kitatokea? Fikiria vizuri Mhe.”

“ Kama uliniona unaushahidi gani?”

“Unataka ushahidi? Mumeo ndio atakuonyesha kile ulichokuwa ukikifanya siku ya jana. Nakuonea huruma Mhe”

“ Unamaanisha una video au picha uliyotupiga?”

“ Nakuambia mumeo baada ya muda mfupi atakujibu kuwa ni video au picha kisha baadaye tutarusha mtandaoni..”

“Subiri kwanza! Please naomba usifike huko.. hello! Hello!” Yule mwanamke kwenye simu hofu ilikuwa imemuingia. Sasa alianza kuona kwamba anayeongea naye akimletea mzaha anaweza kuyaangamiza maisha yake. Kitambo kidogo kilipita Kolowa alikuwa kimya akimpa adhabu ya kisaikolojia Yule mwanamke aliyekuwa akimuita Mhe.

“Hello! Kijana!”

“Sasa umeona jinsi ulivyokalia kuti kavu”

“Ndio! Kijana naomba unisamehe sana. Unataka nifanyeje?”

“Hayo ndio maneno. Tangu mwanzo tungeelewana sana”

“ Nakusikiliza kijana. Unahitaji nifanye nini ili unipe huo ushahidi?’

“ Nahitaji Milioni mia moja..”

“Milioni Mia moja?”

“ Una masaa arobaini na nane kuzitafuta hizo pesa. Hiyo ndio njia pekee ya kujiokoa na janga hili.”

“ Mdogo wangu! Aaah sorry sijui kama wewe ni mdogo au mkubwa lakini naomba unisaidie hiyo pesa ni nyingi. Sina. Nitapata wapi mimi?”

“Kazi yangu sio kujua utapata wapi hizo pesa. Hata hivyo ninyi si ndio mnaokula keki ya taifa mpaka mnavimbiwa. Kwa nafasi yako huwezi kosa hiyo pesa. Kwani ni kiasi gani mnawaibia wananchi mpaka useme huna hiyo pesa?”

“Nisikie Mhe. Baada ya Masaa arobaini na nane nitakupigia simu mwenyewe nikupe maelekezo ya namna ya kunipatia. Nakutahadharisha, usije mhusisha mtu mwingine katika hili. Sio rafiki wala polisi. Ujanja wowote ninakuahidi utakurudia mara kumi. Nitakupa pigo baya na chafu kuliko kile mlichokifanya ndani ya gari jana usiku. Nafikiri utakuwa umenielewa Mhe. Kwa kheri” Kolowa alikata simu. Kisha akamgeukia Kalage aliyekuwa anavuta sigara huku akisikiliza mazungumzo hayo.

“ Hahahaha! Ameshanasa kwenye mtego. Mama mzima hajiheshimu, kazi kutembea na vijana wadogo. Yule Mwanamuziki ni kama mtoto wake lakini bila aibu anamvulia nguo. Ni zaidi ya uchafu! Kujidhalilisha. Sasa hii itakuwa dawa ya watu wa namna hii. Wanaharibu Future ya vijana” Kalage akasema,

“Lakini huyu mwanamuziki naye lazima tumnyooshe.” Kolowa akasema

“Huyu hana pesa, vile anajikosha mbele za watu anatumia pesa za huyu Mama. Pia anajihusisha na biashara zingine haramu. Unazijua bila shaka”

“Kwa hiyo yeye tumuache?”

“Kete yake tutaisukuma baadaye. Najua watasumbuana na Mhe”

Kimya kidogo kilipita huku wawili hao wakivuta sigara na kunywa pombe.

“Ushaandaa mazingira ya kuchukua hizo pesa?” Kalage akamuuliza Kolowa.

“Yeah! Mpango ulionipa unaendana na mazingira ya haya…” Anamuonyesha, kisha Kalage anachukua ile IPAD kisha anaanza kuiangalia kwa umakini.

“ Vizuri! Mengine niachie mimi” Kalage akasema.

***************

“ Hivi nani asiyeogopa nafasi yangu kwenye hii nchi? Nani asiyejua kucheza na mimi ni kuyachezea maisha yake? Uuuh! Kwamba Jay Love amenichezea mchezo mchafu? Mhh! Sidhani! Jay hawezi kunifanyia huu mchezo. Sasa nani mwingine anataka kuniharibia. Adui yangu mkubwa ni Mhe. Casto. Nani mwingine? Yeye ndiye anaweza kufanya mambo kama haya. Lakini kwa jinsi anavyomuogopa Mume wangu sidhani kama angeweza kufanya kitendo kama hiki. Sasa ni nani?” Mhe. Jenifer Basta Makaroni ambaye ni mke wa Rais alikuwa akiwaza akiwa ofisini kwake.

“Lakini vipi kama kijana huyu ananichezea akili na hana huo ushahidi?” akawaza lakini wazo jingine likamwambia “Vipi kama ni kweli anao ushahidi?” hapo akasimama na kuanza kutembea tembea kwenye ofisi yake.

“Sikuwahi kupitia wakati mgumu kwenye maisha kama wakati huu. Lakini bado sielewi ilikuwaje kuwaje mpaka tukaonekana. Mbona mazingira yote hakukuwa na mtu” akawaza mwenyewe huku filamu ya kumbukumbu yake ikianza kupita katika akili yake. Kumbukumbu yake ilimuonyesha akiwa anatoka ofisini kwake na moja kwa moja akaelekea kwenye nyumba yake iliyokuwa nje ya mji ambapo zilikuwepo nyumba za kisasa na kifahari na hakukuwa na watembea kwa miguu labda mmojammoja hasa walinzi. Tayari Msanii wa muziki Jay Love alikuwa ameshatangulia na gari yake nyingine ambayo sio maarufu. Mhe. Jenifer alimkuta Jay Love akiwa hajashuka kwenye gari lake, isipokuwa alikuwa amekaa siti ya mbele ya gari akiwa amefungua mlango wa gari akiwa anabonyeza bonyeza simu.

Mhe. Jenifer alipofika wala hakuwa na muda wa kupoteza akakumbatiana na Jaylove kisha wakaingia wote ndani ya gari la Jaylove.

“Jamani Jay wangu. Polepole mbona unaharaka. Hatufunga milango ya gari” Jenifer aliongea kwa madeko. Milango ya gari ikafungwa. Yaliyoendelea huko waliyajua wao wenyewe.

Kumbukumbu hizo zilimfanya Mhe. Jenifer aone kuwa huenda kuna rafiki wa Jay Love ndiye anamchezea akili. Lakini wazo akalikataa.

“Sina njia. Acha kwanza nizitafute hizo pesa kisha nikishamalizana na huyo mwehu. Lazima nifuatilie. Yeyote anayehusika na mchezo huu lazima alipie”

“Huna haja ya kumshirikisha mtu aibu zako. Hili pambana nalo mwenyewe. Hakunaga siri ya watu wawili” Akaendelea kuwaza.

***************

Masaa arobaini na nane yaliisha, Mhe. Jenifer alikuwa akisubiri simu ya maelekezo ya wapi apelike zile pesa. Lakini punde akawaza “Yaani nimpe pesa zote hizi. Kutoa pesa zote hizi kirahisi bila kutumia njia yoyote ni dalili ya akili yangu kuzidiwa na huyu kijana mwanaharamu. Lazima nimwonyeshe kuwa mimi sio mwanamke wa kuchezewa. Ajue kuwa mimi pia ni mafia”

Akachukua simu, akampigia rafiki yake ambaye walikuwa wakifichiana mambo mengi ya sirini. Akamwomba wakutane katika Hotel moja iliyopo nje kidogo ya mji. Haikuchukua masaa mawili walikuwa wameshakutana.

“ Kwa hiyo ndio hivyo Best. Nipo kwenye mtego nimenasa. Sijui ninajinasuaje hapa. Mbaya zaidi mtego umenikamata sehemu ambayo sina uwezo wa kufurukuta” Mhe. Jenifer aliyasema hayo akiwa na wasiwasi ulioonekana kabisa.

“Kweli huo ni mtego. Lakini unahakika kwamba huyo kijana anaushahidi”

“Kwa kweli sina. Ila mpaka ananipigia simu na kile alichonieleza kwa vile ni kweli nilifanya lazima niamini kuwa ushahidi anao”

“Kabisa! Hapo chakufanya itatupasa tuandae mpango. Kwani amekuambia unampelekea hizo pesa au unamtumia kwa akaunti?” Rafiki wa Mhe. Jenifer akasema,

“Bado! Alisema atanipigia baada ya masaa arobaini na nane tangu juzi ambapo yametimia tangu saa saba mchana. Muda huu ni zaidi ya maasa matatu tangu yatimie”

“Hapo kazi ipo. Ngoja tumsikilize kwa maana hatuwezi kupanga mpango wowote kama hatujui ni njia gani ya kumpa hizo pesa”

“ uuumm! Yaani nimechoka Best. Tunapaswa tuwaze mbele yao kama tunataka tuwashinde hawa”

“ Sahihi lakini nao wameweka mtego. Naogopa tusije jichanganya. Unakumbuka ulinimbia alikuambia kuwa usimshirikishe mtu yeyote na ujanja wowote hautafanikiwa zaidi ya kukuumiza zaidi” Kabla Rafiki yake hajamaliza kuongea simu ya Mhe Jenifer ikawa inaita. Akawa anaitazama.

“Ndio mwenyewe?” Rafiki yake akauliza,

“Yes!” “Pokea tumsikilize”

Akaipokea simu.

“Mhe.Jenifer nafikiri umeipata pesa niliyokuagiza. Hakuna kilichobadilika kwenye makubaliano yetu. Ujanja wowote utajibiwa kwa nguvu itakayokuangusha mpaka chini kabisa. Ninahakika litakuwa pigo ambalo hautainuka kabisa. Sasa sitaki tufikie huko. Tunaelewana?” Sauti ya mwanaume kwenye simu ilikuwa ikiongea. Jambo lililomshangaza Mhe. Jenifer ni kusikia sauti mpya tofauti na ile sauti aliyoongea nayo siku mbili zilizopita. Jambo hilo likamfanya awe kimya bila kujibu akiwa anatazamana na Rafiki yake aliyekuwa anampa ishara ya kujibu mazungumzo ya kwenye simu.

“Mheshimiwa!”

“Aaah! Abee! Ndio tupo pamoja. Nimekuelewa”

“Vizuri! Sasa utachukua hizo pesa kisha utakuja nazo mpaka hapa Kariakoo mtaa wa Aggrey kama unaelekea Mnazo mmoja. Kuna bango la simu lenye maandishi ya Bluu tofauti na mabango mengine. Chini yake kuna mtu anauza juisi ya miwa. Nunua Juisi glasi moja. Wakati unakunywa nitakuja nikiwa nimevalia tisheti ya ugoro lakini inapicha ya barakoa kwenye kifua. utanisalimia na na kuniambia kuwa umenisubiri sana. Baada ya hivyo mengine utafuata maelekezo yangu baada ya kukutana ukiwa na hizo pesa. Umeelewa?”

“Subiri! Uje na huo ushahidi vinginevyo hutozipata hizi pesa”

“Usihofu! Nasisitiza, kama jinsi ulivyokuwa unatumia hila na kuficha siri kwa kutoka na Mwanamuziki Jaylove jitahidi ufanye vivyohivyo katika hili pia. Usiniulize ulinzi uliopewa utakuwa wapi. Na wala usifikiri ni namna gani ya utatumia watu wako uliopewa wakulinde wakusaidie katika hili. Unajua jinsi ya kuja huku. Sasa ni saa kumi. Saa kumi na moja na nusu uwe hapo nilipokuelekeza” Kisha simu ikakatika.

“Mmmh! Mwenzangu unajua huyu ni mwingine. Yule niliyeongea naye siku ile alikuwa na sauti nzito kidogo. Huyu yake ni nyepesi. Sidhani kama tutafanikiwa Best”

“Sikia, tena huko alikokuchagua ndio kuzuri. Tutaenda wote lakini hatutaongozana. Mimi nitatangulia na kukaa kwenye duka jingine nikiwa nasoma mchezo. Kazi itakuwa rahisi sana. Nilifikiri watasema uende sehemu Fulani uache hizo pesa. Kumbe wajinga kiasi hiki” Yule rafiki yake akasema,

“Lakini vipi ikishindikana”

“Hawawezi kutushinda akili. Mimi tayari nitakuwa nimewasiliana na vijana wangu kwaajili ya kukamilisha sehemu iliyobaki. Mbona watakoma kujiingiza kwenye mdomo wa mamba..”

“Itanipasa nikavae Hijabu ili nisionekane sura yangu. Itashangaza mke wa rais kupita katikati ya soko la kariakoo. Watu watanishangaa Best”

“Hata mimi nilifikiri hivyo. Nami nitavaa. Unashangaa umepigwa picha. Unahakika walinzi wako hawakufuatilii lakini?”

“Wananijua. Nikiwaamabia nahitaji faragha wanajua namaanisha nini. Mimi sio mtoto nichungwe muda wote”

“Lakini ni First Lady”

“Kwamba First Lady sipaswi kuwa na Faragha yangu. Kuna muda nahitaji kuishi kama watu wengine kwa uhuru”

“Hilo haliwezekani Jenny. Nafasi uliyonayo ni kubwa ndani ya nchi. Katika hili huna budi. Subiri hiyo miaka ya uongozi wa shemeji ukiisha kidogo ndio unaweza kuwa huru.

“Muda ndio huu. Tunalisaa limoja tuu. Tuondoke. Itabidi kila mtu achukue gari yake. Utakuwa wa kwanza kufika. Pitia shortcut mimi nitatumia njia ndefu” Mhe. Jenifer akasema.

“Nguo tutapata wapi?”

“ Nishaongea na Mage kariakoo aniandalie Hijabu. Duka la Mage lipo pale msimbazi. Kwa hiyo wewe tangulia mwambie umeagizwa na mimi uchague nguo yoyote” Mhe. Jenifer akasema kisha wote wakaamka wakaelekea mahali yalipo magari yao. Wakapanda kisha wakaondoka.

*************

Tayari Mhe. Jenifer alikuwa ameshafika Kariakoo akiwa tayari ameliona lile Bango lenye tangazo la simu lenye maandishi ya Bluu. Chini yake alimuona muuza juisi ya miwa akiwa anakamua juisi ya miwa na mashine. Akiwa amevaa hijabu lililofunika uso wake na kuacha uwazi katika macho yake. Watu walikuwa wengi, pirikapirika za jioni ziliwafanya watu wawe mbiombio kuwahi kununua vitu kabla maduka hayajafungwa. Msongamano huu wa watu ulikuwa chaguo sahihi kwa Kalage katika kuchukua pesa hizo.

Mhe. Alifika kwa Yule muuza juisi ya miwa, upande wa pili wa barabara alikuwepo rafiki yake aliyekuwa makini kuangalia kila aliyekuwa eneo lile hasa ambaye alikuwa amesimama. Ulikuwa ni mtego ambao walikuwa wameundaa katika kumkamata Kalage.

Mhe. Jenifer akiwa amesimama akaagiza juisi ya miwa kama alivyoelekezwa. Alipokuwa akinywa mashaka na hofu vikianza kukita katika moyo wake. Lakini alishangaa kutokumwona yeyote aliyevalia Tisheti ya ugoro yenye picha ya barakoa mbele ya kifua. Alikuwa akishtuka kila alipomwona mtu aliyevaa Tsheti ya ugoro lakini wote aliowaona tsheti zao hazikuwa na picha ya barakoa. Akiwa amebakisha robo ya juisi punde alifika kijana mmoja mchafumchafu akiwa amevaa tisheti ya ugoro yenye barakoa. Mapigo yake ya moyo yaliongezeka zaidi na zaidi lakini hakusahau kuongea alichoelekezwa;

“Habari yako! Nimekusubiri sana”

Wakati anaongea hayo kwa upande wa pili rafiki yake anaguswa begani na kijana mwingine akiwa amevalia tisheti ya ugoro akiwa amebeba chupa yenye juisi ya miwa. Anatabasamu na kumsalimia rafikiake Mhe. Jenifer kisha anamwambia ameagizwa ampe ile juisi na Yule mwanaume aliyesimama pale. Rafiki wa Mhe. Jenifer anaangalia upande wa nyuma anakoelekezwa na Yule kijana. Anamwona kijana mmoja aliyevalia miwani usoni akiwa na kata mikono iliyoacha makwapa wazi, huku sehemu yake ya mikono ikiwa na michoro ya tattoo. Anamwona Yule mwanaume akiondoka na kupotelea kwenye kona. Akiwa bado ametahamaki akakumbuka Yule kijana aliyempa juisi ya miwa, alipogeuka hakumwona naye alishakuwa ameondoka. Alipotazama upande wa pili alipokuwa Mhe. Jenifer anashangaa hamwoni. Kwa upesi akaamua kuvuka barabara kumfuata Yule muuza juisi ya miwa.

“:Habari kaka”

“Salama kabisa. Karibu juisi tamu ya miwa”

“”Ahsante! Huyu mwanamke aliyekuwa anakunywa juisi hapa ameelekea wapi?”

“Amepanda ile bajaji, Ile inayovuka mataa. Kapanda na kijana mmoja”

Rafikiake Mhe. Jenifer alikuwa akiiona ile bajaji ikiendelea kwenda lakini punde akashangaa imesimama. Hapo akawa anaitazama, huku asitake kuipoteza machoni. Akamwona Yule kijana aliyevalia tsheti ya ugoro akishuka. Kisha ile bajaji ikaendelea na safari. Kwa upesi akaanza kutembea huku akipiga simu macho yake yakiwa yanamfukuzia Yule kijana mwenye tisheti ya ugoro.

Sasa alikuwa karibu naye ingawaje msongamano wa watu ulikuwa ukimzuia asimfikie kirahisi. Yule kijana hakuwa na habari yoyote zaidi alikuwa akihesabu noti za shilingi elfu kumikumi. Ghafla alishtuka amesimamiwa na wanaume wawili pamoja na Mwanamke mmoja aliyevalia hijabu uso wake ukiwa umesitiriwa. Kabala hajasema chochote mwanaume mmoja alimwonyeshea bastola kwa kificho bila ya watu wengine kuona. Wakamkokota moja kwa moja mpaka walipotokea mtaa wa pili ambapo wale wanaume walikuwa wameegesha gari lao. Kisha wakampakiza na kuondoka naye.

****************
ITAENDELEA

0693322300
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…