HUJUMA NZITO-PART 08
Kachero Manu akapata wasaa sasa wa kufanya utalii wa bure kwa kutumia macho yake kuichunguza nyumba ya Meja Marwa pale sebuleni walipoketi. Kwa msaada wa mwangaza hafifu pale sebuleni akaanzia juu kushuka chini, kwenye mbao za dari zinazoshikilia bati kuukuu aliona kikundi cha panya bila aibu wanakimbizana usiku ule kama vile wanacheza mchezo wa kitoto wa foliti, huku buibui wakiwa wametandaza nyumba yao sehemu kubwa ya dari.
Akaanza kuyashusha macho yake taratibu mpaka yakatua kwenye madirisha ya mbao yaliyoanzwa kutafunwa na mchwa. Akaona vipande vya kanga kuukuu na vipande vya maboksi vimetumika kuziba uwazi uliopo kwa ajili ya kupunguza makali ya upepo wa baridi la usiku.
Hakuchoka kufanya taftishi zake, alipotupa macho yake sakafuni akakutana na udongo ulioshindiliwa vyema ukamwagiwa maji kwa ajili ya kutuliza vumbi lisitimke mle ndani. Huku sebule ikiwa imepambwa na samani chakavu na za kizamani zenye umri wa zaidi ya miaka 15 kwa mtazamo. Zikionekana kabisa hazijawahi kung'arishwa tokea zilipoingizwa kwenye nyumba hii.
Akiwa amezama kwenye lindi la tathimini yake, ghafla akashtushwa na kelele za kulalamika za mlango wa bati wa kuelekea uani. Mwenyeji wake Meja Marwa akarejea toka msalani na kuisogeza karibu yao karabai inayoangazia pale sebuleni huku mkononi akiwa sasa ameshikilia kidaftari chake kidogo chakavu.
"Nimechelewa kidogo kuna nyaraka hii nilikuwa naitafuta stoo huko uani, bahati nzuri nimeliona daftari langu la kumbukumbu. Hii taa imeshaanza kupunguza mwangaza, sina uwezo wa kuvuta umeme, pensheni yangu ya mwezi ni ya kijungu meko haitoshi hata kuilisha familia lishe bora" alizungumza Meja Marwa kwa sauti ya manung'uniko akionyesha kabisa hajaridhishwa na namna wazalendo, walinda usalama waliochangia nchi hii kuitwa kisiwa cha amani namna wanavyopunjwa maslahi yao.
Baada ya mazungumzo kadhaa nje ya mada, Meja Marwa akaendelea na simulizi yake. "Kupata majibu ya maswali nani chachu ya maasi hayo, hatuna budi kuangalia kwa ufupi matukio kadhaa yaliyotangulia maasi ya nchi hizo tatu, kuona kama yana uhusiano wowote. Tanganyika ilirithi Jeshi kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza baada ya uhuru, Desemba 9, 1961, likijulikana kama Kings African Rifles (K. A. R) na baadaye kuitwa Tanganyika Rifles (TR) na kutokana na maasi hayo ya Januari, 1964 likaitwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Katika kipindi kufuatia uhuru, ili kukidhi matarajio ya Watanganyika, zilitakiwa hatua za haraka kuhakikisha nafasi zote za juu serikalini na taasisi zake, zinashikwa na Wazalendo. Huu ni utamaduni uliokuwa umejengeka kwa nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikipata uhuru.
Hiyo hali ilikuwa ndio inaonekana kuwa uhuru wa kweli umepatikana kinyume chake watu walikuwa wanaona ni kama kiini macho tu, wamepewa uhuru wa bendera. Baadhi ya vigogo ndani ya chama cha TANU wakawa mbogo, wakaona Nyerere anawalea wakoloni hataki kuwafurumusha, anapeleka mambo aste aste, hapo ndipo yakaanza malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Tawala, Tanganyika African National Union (TANU).
Wapo waliomuambia Nyerere wazi wazi kuwa alikuwa anairudisha Tanganyika katika enzi za Ukoloni.
Hivyo kwamba uhuru haukuwa na maana kwa Watanganyika kwa kushindwa kwake kuwapa vyeo Waafrika. Na kwamba wapo waliopoteza mali zao, kazi zao na hata kuhatarisha uhai wao ili tu kumfurusha mkoloni sasa iweje uhuru umepatikana yeye anawadekeza tena!.
Ili kuepusha shari, na ili Chama kisifarakane, wakawapa nafasi wafitini, Mwalimu akaachia ngazi nafasi yake ya Uwaziri Mkuu Januari 16, 1962 na kurejea kijijini kwake Butiama kuimarisha Chama kama Mwenyekiti wa Taifa wa TANU; na Rashid Mfaume Kawawa akachukua Uwaziri Mkuu wa nchi.
Naye Oscar Kambona, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Elimu, akawa Waziri wa Mambo ya Ndani badala ya George Kahama. Wote wawili hao wakaachiwa jukumu zito la kazi ya kuwaondoa Wazungu katika vyeo walivyokuwa bado wanashikilia haraka bila visingizio. Kazi ya kwanza ya Oscar Kambona sasa akiwa kama Waziri wa Mambo ya ndani ilikuwa ni kumtimua Kamishna wa Polisi Mwingereza, 'Mr. M.S Wilson' na kumteua mzalendo 'Elangwa Shaidi' kuchukua nafasi hiyo.
Zoezi hili la kuwapokonya madaraka wazungu lilifanywa kwa kasi ya kutisha kiasi cha kuishitua jamii ya Kimataifa. Desemba 1962, ulifanyika Uchaguzi Mkuu ambapo Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Rais Mtendaji wa kwanza. Kwa hiyo, Januari 1963, Mwalimu alirejea madarakani kama Rais wa kwanza wa Tanganyika na kusitisha mara moja zoezi hilo.
Hali ambayo ilichochea hasira kali toka kwa viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, ambao waliapa kutolala usingizi, wala kuupa nafasi uamuzi wa Mwalimu wa kusitisha zoezi la kuwapa madaraka Watanganyika. Wakaanza kumuona Mwalimu kuwa kama nae ni mkoloni tofauti ni rangi tu, Waingereza nyeupe na Nyerere nyeusi.
Kwa ujumla Nyerere alikuwa yupo sahihi, unapotaka kufanya mabadiliko hufanyi kwa ghafla tu lazima kuwe na maandalizi. Hata mtoto mchanga hapelekwi moja kwa moja toka kuacha kunyonya ziwa la mama mpaka ugali, lazima aanze uji mwepesi, uji mzito kisha ndio ugali mlaini mpaka anafikia hatua ya kula ugali mgumu.
Matata yalianza usiku wa Januari 20, kuamkia 21 usiku huo, siku ambayo Okello alikuwa na mazungumzo na Mwalimu, Ikulu usiku. Lakini ilipofika saa 7:50 alfajiri, Januari 21, Mkuu wa Kikosi cha kwanza cha Tanganyika Rifles (TR), Brigedia Patrick Sholto Douglas, aliamshwa nyumbani kwake na sauti ya baruji na vingora, karibu na kambi ya Jeshi ya Colito (sasa Lugalo Barracks).
Alipotoka nje, aliona askari wake 12 wakikamatwa na wenzao wenye silaha na kutiwa mahabusu. Ndipo alipofahamu kwamba, nusu ya askari 800 wa Kikosi hicho walikuwa wameasi. Aliweza kutoroka yeye na familia yake hadi katikati ya Jiji, akaiacha familia kwa Balozi wa Australia, kisha akakakimbilia kwa Afisa mwenzake, eneo la Oyster Bay. Akiwa huko, akampigia simu Oscar Kambona, akamwomba msaada naye akakubali, kupeleka ndege tatu Kikosi cha Pili huko Tabora, kuleta askari waliokuwa bado waaminifu kwa Serikali.
Douglas na Kambona hawakujua kwamba, tayari waasi walikuwa wamefunga barabara iendayo uwanja wa ndege; kwa hiyo, marubani walirudi mbio; naye Douglas akakimbilia kwenye Ubalozi wa Uingereza, akajificha kwa siku tano hadi Januari 25. Douglas alikuwa amempigia simu Mkuu wa Polisi, ambaye alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Makamu wa Rais, Rashidi Kawawa, eneo la Ikulu na kumwamsha, kisha hao wawili kwa pamoja, wakaenda kumpa habari Mwalimu. Mwalimu alipoelezwa juu ya maasi hayo, alilipuka kwa hasira na ghadhabu kubwa papo hapo; akataka kwenda yeye mwenyewe kukutana na Waasi hao ili wamweleze sababu za kitendo hicho cha aibu.
Ndipo watu wa Usalama walipojenga hoja nzito kumzuia, na hoja hiyo ikamwingia. Akakubali kuteremka matawi ya chini, kisha yeye, Kawawa na Mama Maria Nyerere, wakatorokea mahali kusikojulikana wakitoroshwa na mlinzi wao Bwana Peter Bwimbwo.
Wakati huo, tayari waasi walikuwa kwenye lango kuu la Ikulu wakimtafuta. Mwenyezi Mungu ni mwema kwetu Watanzania huenda waasi wangempata wangefanya tukio la kuistaajabisha dunia.
Kufikia saa 9:00 alfajiri, waasi walikuwa tayari wamekamata kambi ya Colito, hii kambi ya jeshi inayoitwa Lugalo hivi sasa, kisha waasi wakajigawa vikundi vitatu na kuingia mjini. Kikundi kimoja kilibakia kulinda kambi ya Colito, mimi nilibaki kwenye kile kinacholinda kambi ya hiyo ya Colito. Kikundi cha pili, kikiongozwa na Sajini Francis Higo Ilogi, ndicho kilichokwenda Ikulu kumtafuta Rais; wakati kikundi cha tatu kililinda barabara kuu zote mjini.
Kikundi cha Sajini Ilogi kilipofika Ikulu, kilishauriwa na mmoja wa Maafisa Usalama wa Taifa, wamwone kwanza Waziri Oscar Kambona; nao wakakubali kufanya hivyo. Wakaenda hadi kwa Kambona na kumleta Ikulu, na kumweleza kwamba walikuwa wamewakamata na kuwaweka mahabusu maafisa wake (Wanajeshi) 16; na kwamba, kama alikuwa tayari kusikiliza malalamiko yao, afuatane nao hadi Colito. Kambona hakuwa na budi bali ni kukubaliana nao.
Hapa sasa nisikilize kwa makini mjukuu wangu, Ni ujasiri gani huo; ni kujiamini vipi kwa Kambona, kwamba bila ulinzi wala woga, tena akiwa amepanda gari la Mkuu wa Polisi tu, aliweza kukubali kuandamana na askari wenye silaha, na hasira kali, kwenda Colito Barracks (Lugalo)?. Hilo ni swali gumu sana linalohitaji majibu ya kina sio ya kurashiarashia tu.
Ukimwondoa Nyerere na Kawawa, ambao walikuwa na kila sababu ya kujificha, kulikuwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Malecela Lusinde; kwa nini Kambona hakumshirikisha, kama aliona mambo yalikuwa salama kiasi hicho?. Hapo ndipo baadhi ya watu wanakwenda mbali zaidi kusema kwamba, huenda Kambona alihusika na maasi hayo" Kachero Manu akaanza kutikisa kichwa kuonyesha somo sasa linaanza kumuingia huku akabaki anatabasamu kwa jinsi Babu Meja Marwa anavyojua kujenga hoja na kuzitetea kiustadi mkubwa wakati anaunganisha na kunyumbulisha matukio.
"Huko Colito Barracks, walipompeleka walimweka Kambona mtu kati, wakimtaka aamue papo hapo, pamoja na mambo mengine, kuondolewa mara moja kwa Maafisa wa Kiingereza Jeshini, na nafasi zao zishikwe na Wazalendo. Walitaka pia mishahara iongezwe maradufu, kwa zaidi ya asilimia mia, kutoka shilingi 105/= hadi shilingi 260/= kwa mwezi. Bila kuonyesha kwamba ameyakubali au kuyakataa madai yao, Kambona aliomba wateue wawakilishi wachache ili wafuatane naye hadi Ikulu kwa mashauriano na Mwalimu Nyerere.
Ndipo Kiongozi wa waasi, Francis Higo Ilogi mzaliwa wa Bukene, Tabora, mtu mmoja mwenye roho ngumu, na mkomavu kama mti mkavu asiyetaka masikhara wala utani kwenye jambo lake akiamua, alikataa mara moja na kusema, Tunataka kila kitu leo hii, Yowe zikasikika, Apigwe risasi, apigwe (Kambona) huyo!. Tayari baadhi ya wanajeshi wakakoki silaha zao wakimnyooshea midomo ya mitutu yao Bwana Oscar Kambona kusubiria amri ya kumpiga risasi itoke kwa kiongozi wao Bwana Hilogi.
Kambona alipoona hali ni tete akauliza haraka haraka: Mnataka nani awaongoze? Lilitajwa jina la Alex Nyirenda; lakini likakataliwa kwamba alikuwa na majivuno, madahiro na kujisikia sana hafai kuwa kiongozi. Akatajwa Luteni Elisha Kavana, akapitishwa kwa kauli moja na kuvishwa kofia ya Brigedia Douglas.
Kambona alikataa kutia sahihi makubaliano, kwa madai kwamba mpaka ashauriane kwanza na Rais. Ndipo kikundi chote cha Ilogi kikafuatana naye sako kwa bako kwenda Ikulu kwa Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kubatiza uteuzi huo wa Luteni Elisha Kavana.
Walipofika huko, askari hao walijipanga barabara yote iingiayo Ikulu, lakini Sajenti Ilogi aliwakataza wasiingie ndani, alitumia nguvu kweli kwelikweli kuwatuliza mpaka wakamuelewa. Ndipo wakamruhusu Kambona pekee ndio aingie ndani Ikulu kwenda kuonana na Nyerere. Wakati huo kumbe Nyerere alikuwa ametoroka zaidi ya saa mbili zilizopita. Baada ya mashauriano kwa muda na wasaidizi wa Rais pamoja na mama mzazi wa Mwalimu, Kambona alitoka nje na kuwatangazia waasi hao kuwa Rais ameyakubali madai yao.
Lakini askari hao wakapiga kelele mwongo huyo! Rais hayumo ndani; mpige risasi, mwongo huyo!. Kambona akawa ametindinganya mambo tena kwa mara ya pili. Hata hivyo sudi bado ilikuwa upande wake Kambona, waliondoka wameridhika, wakarejea kambini siku hiyo. Hima, Kambona aliwaondoa maafisa wa Kiingereza na kuwasafirisha kwao kupitia Nairobi.
Akiwatangazia wananchi kupitia Redio Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC), Kambona alisema: Huyu ni Waziri wenu wa Mambo ya Nje na Ulinzi; Serikali ingalipo Kumekuwa na kutoelewana baina ya askari Waafrika na maafisa wa Kiingereza katika Jeshi. Baada ya kuingilia kati shauri hili, sasa askari wamerudi kambini.
Hata hivyo, hakusema lolote juu ya Nyerere, wala mahali alikokuwa. Je, ni kweli mambo yalikuwa yamekwisha? Kwa nini Nyerere hakutokea hadi siku mbili baada ya askari kurejea kambini? Kwa nini askari hao waliasi tena siku nne baadaye na Nyerere kulazimika kuita majeshi ya Uingereza kuja kuzima maasi?.
Haya maswali yote mjukuu wangu ni magumu hatuwezi kupata majibu kwa haraka haraka kwa uchambuzi wa usiku huu pekee!.
Ninachoweza kukuambia ni kuwa kwa kawaida Kambona alijua au alikuwa amearifiwa mapema kuhusu maasi ya Dar es Salaam katika vitengo vya usalama vya Tanganyika na maofisa wa Kiingereza ambao bado walikuwa wakiitumikia Serikali ya Tanganyika, lakini hakuchukua hatua yoyote kuikabili hali hiyo hadi pale ilipotokea. Mmoja wa maofisa hao ni Luteni Kanali Rowland Mans. Ilidaiwa kuwa mara kwa mara, Kambona, akiwa Waziri wa Ulinzi, alikuwa akiwatembelea maofisa wa ngazi za chini katika kambi ya Colito, na mara nyingine bila kuonana na viongozi wakubwa wa kambi hiyo.
"Leo asubuhi nilikuwa nasoma kitabu kimoja cha utafiti wa Ndugu Nestor Luanda katika kitabu hicho "Tanganyika Mutiny", ameeleza humo kuwa Kambona alianza kufika mara kwa mara katika Makao Makuu ya Jeshi mwishoni mwa 1963 na aliwaambia maofisa wa kijeshi wa Kiingereza kwamba alitaka wawe wameondoka nchini ifikapo mwishoni mwa 1964, je hayo maelezo yana ukweli kwa kiasi gani?" Kachero Manu aliingilia kati mazungumzo ya Meja Marwa kwa swali, huku akijiandaa kunukuu majibu ya swali lake.
"Unajua mjukuu wangu Kambona alitaka maofisa wengi wa Kitanganyika wapewe vyeo haraka, jambo ambalo Waingereza walidai haliwezi kutendeka kwa ghafla kama alivyotaka. Kuanzia hapo maofisa hao wakaanza kuwa na wasiwasi kuwa chochote kinaweza kutokea. Ingawa uhusiano wa maofisa wa kijeshi wa Uingereza na Waziri Kambona ulianza kupungua, huo si ushahidi wa kutosha kueleza kuwa Kambona alihusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja", alijibu kimtego wa kijanja akiwa hataki kumhukumu Kambona moja kwa moja jambo ambalo Kachero Manu alishamshtukia kuwa Meja Marwa ni mjanja kama sungura, anaingia na kutoka kwenye mtego.
"Sasa kuna mwanajeshi mmoja anaitwa Kapteni Wandawanda alikuwa anatokea Mbamba Bay ni Mnyasa nasikia nae mlikuwa nae jeshini kipindi hicho lakini akapata utajiri wa maajabu maajabu akawa anamiliki mali lukuki kipindi hicho zilizotokana na uasi, je unamkumbuka vizuri?" Kachero Manu sasa aliona muda umeshakwenda sana akamuulizia swali la kumchomekea mlezi wa mapacha Dr.Pius na Alex Chilembwa, na hili swali ndio lilikuwa swali haswa lililomleta.
"Huyo mtu unayemtaja hafai kabisa ni hayawani mkubwa. Kwenye yale machafuko kama ujuavyo kwenye msafara wa mamba na kenge wapo, sisi lengo lilikuwa ni kudai wazungu waondoke na maslahi bora lakini baadhi ya wenzetu akiwemo Kapteni Wandawanda walikosa maadili walikuwa wanapita mitaani kupora mali za wananchi. Kwa namna hiyo wapo baadhi yetu akiwemo yeye walitajirika sana kwa uhalifu huo walioufanya mitaani. Baadae aliachana na jeshi na kwenda kuishi nchini Uingereza akitumbua utajiri haramu aliojikusanyia.
Mfano nakumbuka tukio moja kipindi maasi hayo yalivyosababisha ghasia nyingi mitaani, hususani Mtaa wa Msimbazi maeneo ya Kariakoo. Maeneo mengi ya katikati ya mji risasi zilirindima. Mwarabu mmoja eneo la Magomeni, kwa kuona duka lake linavamiwa, kwa hasira zake alimpiga risasi mwanajeshi mmoja aliyejulikana kwa jina la Kassim na kumuondosha duniani hapo hapo bila kuomba maji. Koplo Nashon Mwita, ninatoka nae mkoa wa Mara, ambaye alishuhudia mauaji hayo, alirudi kambini kujizatiti. Akiongozana na askari mwingine, Luteni Mwakipesile, pamoja na wanajeshi wengine, walifika Magomeni na kummiminia risasi Mwarabu huyo, kulipiza kisasi kama mbwai iwe mbwai tu. Kana kwamba haikutosha, waliiteketeza nyumba yake kwa moto. Katika nyumba hiyo, inasemekana, Mwarabu huyo aliteketea na familia yake ya watu 15" alijibu kiufasaha Meja Mwita huku akionekana hana hata lepe la usingizi na kumbukumbu yake kichwani inachaji mithili ya ghulamu wa miaka 15 vile.
"Sasa je Wanyasa mlikuwa nao jeshini hawakuwa wanajivuna kuona mtu wa kabila lao kama Kambona ndio katuliza machafuko hivyo wao ni watu muhimu sana katika nchi hii?" alichomekea swali la kimtego ili apate penyenye zinatakazompa mwangaza zaidi wa upelelezi wake.
"Aaaaah...hiyo kujivuna mtu wenu akiwa anafanya vizuri ni kawaida mbona, sio wao tu Wanyasa peke yao mbona hata sisi watu wa mkoa wa Mara tulikuwa tunajivuna Nyerere katokea kwetu, hivyo hiyo sio mbaya. Ubaya ni kama kuna upendeleo yule kiongozi anaufanya kwa watu wa kabila lake huku anawabagua wa makabila mengine hilo ndio jambo baya sana kwa ustawi wa jamii yenye usawa, machafuko yanaweza kutokea wakati wowote ule kama vita vya Watusi na Wahutu kule Rwanda.
Ila nakumbuka Siku za usoni baada ya Nyerere na Kambona kutofautiana mitazamo mbalimbali ya kiitikadi katika namna ya kuiendesha Tanzania mpaka kupelekea Kambona kutoroka nchini Tanzania na kuhajiri nchini Uingereza, baadhi ya Wanyasa jeshini na hata huko mitaani walijisikia vibaya sana.
Huyo Firauni Kapteni Wandawanda alikuwa anaropoka maneno hatari kwa ustawi wa Umoja wa nchi kuonyesha kuwa Kambona kaonewa na nadhani pia jambo hilo lilichangia yeye kuacha kazi. Maana Kambona alikuwa anaonekana ni kama mtu namba mbili kwa ubora wa uongozi akitoka Nyerere. Hasa sononeko kwao lilizidi sana baada ya nyimbo mbalimbali za kashfa na kejeli dhidi ya Kambona zilipokuwa zinaimbwa mashuleni na jeshini.
"Sasa baada ya kupatikana Uongozi mpya wa Jeshi, je wale waliofanya fujo walichukuliwa hatua zozote au walisamehewa?" alichomekea swali la mwisho huku muda ukiwa umeenda sana karibia saa saba kasorobo za usiku alipotupa jicho kwenye saa yake ya mkononi.
"Mjukuu wangu ilipofika Jumamosi ya Januari 25, 1964, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mwalimu Nyerere aliomba msaada kutoka Serikali ya Uingereza kunyamazisha maasi ya kijeshi yaliyokuwa yanazidi kusambaa katika Tanganyika, yalifika mpaka kambi ya Tabora na Nachingwea huko Lindi. Hatimaye makomandoo wa Uingereza waliwasili kwa helikopta na kuwanyanganya silaha waasi. Jioni ya siku hiyo hiyo maasi ya Tabora nayo yakazimwa. Maasi hayo, hasa katika kambi ya Colito( Lugalo), yalizimwa baada ya makomandoo hao wa Uingereza kutua na kuanza kulipua lango la mbele la kambi hiyo.
Mara moja askari walioasi walijisalimisha. Kikosi cha Uingereza kiliongozwa na Brigedia Patrick Sholto Douglas. Waasi watatu waliuawa katika operesheni hiyo. 20 walijeruhiwa na wengine 400 walikamatwa, na wengine walitoroka, sisi wengine tulishatubia tulikuwa tunaiunga mkono serikali ya Nyerere, tuliona maji yameshazidi unga.
Kwa njia hiyo Rais Nyerere alirejea madarakani, lakini historia ya Tanganyika ikabadilika moja kwa moja.
Wiki tatu baada ya maasi (Feb. 16, 1964), Nyerere aliitisha mkutano wa hadhara Viwanja vya Jangwani na kuwaambia Watanganyika hivi: "Wanajeshi walioasi walidanganywa na wahuni wachache. Wendawazimu walikuwa wawili, watatu. Wale wengine waliswagwa tu kama ng'ombe wanaoenda malishoni. Wakivutishwa bangi, wakaja mjini kutenda maovu. Tukaenda kwa Mwingereza. Bwana Mwingereza tusaidie utuondolee balaa hili". Baada ya maasi hayo, Mwalimu Nyerere alianza kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa hakuna kosa linalorudiwa.
Hatua ya kwanza alianza kukamata wote waliohusika, kisha akapiga marufuku gazeti la Nation la Kenya linalomilikiwa na Aga Khan kutouzwa katika Tanganyika. Kwanini marufuku hayo? Gazeti hilo (Nation) lilitoa taarifa sahihi lakini yenye raghba na chumvi nyingi kuhusu kuangushwa kwa serikali yake. Kupunguza uwezekano wa mfarakano wa mawazo, akawabadilisha makamanda wa Kiingereza akaweka wa Kiafrika. Wakati huo huo, akateua kamati ya kutafakari mabadiliko ya kikatiba ambayo yataifanya Tanganyika kuwa nchi ya kidemokrasia ya chama kimoja kisheria na kiuhakika. Uso wake Nyerere ulikuwa na simanzi sana.
Hakuna hata Mtanganyika mmoja aliyeuawa kwa miaka yote 17 ya kupigania Uhuru wa Tanganyika. Lakini sasa baada ya uhuru Watangayika wameuawa. Jumanne ya Aprili 21, Mwalimu Nyerere alimwapisha Sir Ralph Wildham ndani ya Ikulu ya Dar es Salaam kuwa Jaji Mkuu wa Tanganyika, na kumwambia awashughulikie kikamilifu wanajeshi waliofanya jaribio la kuipindua serikali yake hapo Januari 19, 1964.
Ndipo Sir Wildham akatangaza rasmi kuwa wanajeshi wa Kambi ya Colito waliotaka kuiangusha serikali watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu, Aprili 27, 1964. Wakati huo huo Rais alimteua Kapteni Abdallah Twalipo (35) na Kapteni Lukias Shaftaeli (39), wote wakiwa ni wanajeshi wa jeshi la Wananchi, kuwa wajumbe wa mahakama ya kijeshi. Sir Wildham akawa Rais wa mahakama hiyo.
Baada ya uteuzi huo, Mkurugenzi wa Mashitaka, Herbert Wiltshire Chitepo, alisema angewaita mashahidi 25. Kesi hiyo iliendeshwa kwa siku chache na hatimaye hukumu ikatolewa. Ijumaa ya Mei 15, 1964, siku 19 baada ya kufanyika kwa Muungano wa Tanzania, wanajeshi walioasi katika Kambi ya Colito walihukumiwa, lakini adhabu zao zilikuwa tofauti.
Sajini Francis Hingo Ilogi alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, Koplo Aliche miaka 10, Koplo Baltazar miaka 10, Private Jonas Chacha miaka 10, Private Pius Francis miaka 10. Wengine ni Private Patric Said John aliyehukumiwa miaka 10, Sajini Lucas miaka 10, Kapteni Kamaka Mashiambi miaka 10, Kapteni Benito Manlenga miaka 10, Private Dominicus Said miaka 10, Kapteni Andrea Dickson miaka 5, Private Hamidus miaka 5 na Roger Mwanaloya miaka 5.
Wanajeshi walioshitakiwa lakini hawakupatikana na hatia na hivyo kuachiwa huru ni Koplo Peter Mbasha, Private Ernao Msafiri, Private Gerado Raphael, Kapteni Mahara Magom na Kapteni Moses Kawanga" alimalizia mazungumzo yake huku anawasoma majina wanajeshi hao kupitia kwenye daftari lake kuukuu la kuhifadhia kumbukumbu zake alilolifuata pindi alipoelekea msalani.
Hapo ndipo Kachero Manu akang'amua kwanini aliporudi msalani alisogeza taa karibu yake, kumbe alikuwa anajiandaa kumsomea majina ya waasi.
Baada ya mazungumzo hayo wakaagana na kuahidi kumfanyia mpango wa kumsaidia kumvutia umeme nyumbani hapo kwa kutumia tashiwishi yake kwenye idara ya usalama.
"Nilichojifunza hapa inaonyesha akina Kapteni Wandawanda na baadhi Wanyasa wenzake wachache waliona kama wameonewa hivyo waliamua kujipanga, wajukuu zao waje kuchukua uongozi wa nchi kulipiza kisasi cha Babu yao Kambona. Ndio maana hata hawa akina Dr.Pius Chilembwa walipelekwa wakawasomeshwe elimu bora ughaibuni ili watumie elimu yao kuandaa mapinduzi ya kiakili sio kwa kutumia nguvu" yalikuwa ni baadhi ya mawazo yanayopita kichwani mwa Kachero Manu wakati anasukuma gari lake kwa mwendo wa wastani anaelekea nyumbani Mbweni. Muda ulikuwa umeshasonga mno usiku ule na yeye alishaanza kushikwa na uchovu wa usingizi.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]
SURA YA TANO
Jina la Kachero Manu chungu midomoni mwa wahujumu kama shubiri..
"Jamaa ni hatari sana, anatisha kama njaa, anashambulia kwa kugonga kama nyoka mwenye sumu kali, kamuua kikatili sana Kapteni Koba, ambaye ni komandoo wa kutegemewa kwenye operesheni nyingi za kijeshi nchini Tanzania.
Tulimrudisha makusudi toka Darfur kiujanja anapohudumu kwenye jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa (UN) ili aje kumshughulikia huyu Kachero Manueli Yoshepu, lakini tahamaki kachemsha, na kwa ujumla tumegonga mwamba. Mwili wa Kapteni Koba nimeushuhudia kwa macho yangu ukiwa mochwari kule hospitali ya Muhimbili.
Kusema ukweli umechakazwa vibaya hautamaniki huwezi kuuangalia mara mbili. Utasema amegongwa na gari barabarani kumbe ni vipigo vitakatifu toka huyu mshenzi, mjuba Manueli Yoshepu. Ripoti ya polisi ilivyoandikwa ni kuwa ameuawa kwenye tukio la ujambazi, hivyo hatozikwa kwa heshima za kijeshi kwa hadhi ya cheo chake ni kama ameliaibisha jeshi.
Kiongozi wetu ukiongea na Mkubwa kwa busara zake naomba umwambie awape kifuta jasho familia ya Kapteni Koba ili kuwafuta machozi maana alikuwa ni mshirika wetu muhimu katika harakati za kuisimika Dola ya Nyasa nchini Tanzania. Pia itatupa moyo sisi wa kupambana kuhakikisha ndoto yetu ya kuisimika Dola ya Nyasa inatimia tena kwa haraka".
Chew Master kama anavyojulikana na washirika wenzake wa mpango dhalimu, lakini ni kigogo mkubwa wa jeshi la polisi alikuwa anatoa taarifa ya kuhuzunisha kwenye kikao cha dharura kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili tukio lililoshindikana la mauaji ya Kachero Manu.
Jukumu la mauaji alibebeshwa Chew Master na akaahidi kulitekeleza kwa ufanisi ndani usiku huo huo lakini, Kachero Manu amegeuka fupa la chupa lililomshinda fisi kutafuna.
"Halafu mmepata taarifa ya kustusha kijijini Kwembe, kule kaburini kwa Dr.Pius Chilembwa feki?" aliuliza mmoja wapo wa wana kikundi kile mle kwenye chumba cha mkutano wao. "Wewe ndio wa kutujuza maana shughuli za mazishi yote yalikuwa ni jukumu lako, kuanzia usafiri, mazishi, chakula mpaka ulinzi..!" alichangia mmoja wapo, huku kila mmoja akipatwa na wahaka wa moyo wa kutaka kufahamu kumetokea nini huko maziarani.
ITAENDELEA