KIJIJINI KWA BIBI--53
...ila sauti yake haikumfikia Mkuu wa Polisi, Sajenti Minja akarudi ndani ya choo, kisha akafunga mlango, akawa anachungulia kupitia tundu la ufunguo, akamshuhudia Mkuu wa Polisi akielekea nje.
"Amekuja kufanya nini huku? Au amejipa likizo na yeye kutokana na kifo cha mwanae? Au anatufuatilia?" Sajenti Minja alikuwa anajiuliza mwenyewe huku akiwa bado yupo ndani ya choo.
Baada ya dakika tano, Sajenti Minja alitoka chooni na kuelekea walipo wakina Kayoza,
"vipi anko, mbona umekaa muda mrefu sana?",Kayoza alimuuliza Sajenti Minja,
"tumbo limenishika si mchezo, mimi naona nirudi nikapumzike, nyie endeleeni na ziara",Sajenti Minja hakutaka kusema ukweli, ingawa mshtuko wa kumuona Mkuu wa Polisi ulimfanye achoke ila hakuwa na sababu ya kuwaambia wenzake ukweli kutokana na yeye kutokuwa na jibu haswa juu ya uwepo wa Mkuu wa polisi katika eneo lile,
"sisi tumeshamaliza, tulikuwa tunakusubiri wewe tu",Kayoza alimwambia Sajenti Minja,
"haya bwana, mimi naelekea mjini, nyie nendeni tu nyumbani, njia si mnaikumbuka?",Mwenyeji wao aliwauliza,
"tunaikumbuka bwana mkubwa",Sajenti Minja alijibu huku akijilazimisha kutabasamu,
Kisha wakaagana na mwenyeji wao, na wao wakashika njia ya kurudi nyumbani.
Sajenti Minja akaona huo ndio muda mzuri wa kuwaambia alichokiona, ingawa alitaka kuwaficha ila akaona haitakuwa vyema kuwaficha kwa kuwa wao ni wamoja na wamefika mkoa ule kwa lengo moja.
"jamani nimemuoona Mkuu wa Polisi pale hotelini",Sajenti Minja aliongea kisha akawa anasubiri swali,
"Mara hii umeshaonana na mkuu wa polisi wa mkoa huu, kweli nyie maaskari mnajuana sana" Omary aliongea huku akishangaa,
"Sio wa mkoa huu, yule wa Shinyanga" Sajenti Minja alitoa Maelezo yaliyowafanya wenzake washtuke,
"itakuwa umemfananisha",Omari aliongea huku akiwa bado anamshangaa Sajenti Minja,
"nimemfananisha vipi?, wakati namfahamu fika",Sajenti Minja aliongea kwa kupaniki,
"sasa huku kafuata nini?",Omari akamuuliza,
"huwezi jua bwana, yule ni polisi, inawezekana anatufatilia sisi",Sajenti Minja aliongea kwa uhakika,
"duniani wawili wawili mjomba",Kayoza aliongea baada ya kuwa kimya muda mrefu,
"ok, mmeshinda, ila mtaniambia wenyewe",Sajenti Minja alimaliza, kisha wakaendelea na stori nyingine, huku Sajenti Minja akiwa hana amani kabisa katika moyo wake.
Walipofika nyumbani, wakapelekwa moja kwa moja hadi kwenye chumba cha Bibi yake Kayoza, wakamsalimia, kisha wakatambulishwa, Bibi Kayoza alifurahi sana, alipomuona Kayoza, waliongea sana,
"ila bibi pamoja na kukusalimia, kuna jingine lililonileta huku",Kayoza alimwambia Bibi yake,
"hata usiniambie mume wangu, najua lililokuleta",Bibi yake Kayoza alimkatisha Kayoza,
"nateseka sana bibi, naishi maisha ya kutafutwa na askari kama jambazi",Kayoza aliongea kwa majonzi,
"ilikua lazima upitie hiyo hali mume wangu",Bibi yake Kayoza alisema na kumfanya Kayoza avute kamasi kwanza,
"kivipi bibi?",Kayoza alihoji huku akifuta machozi,
"bila ubishi wa baba yako na kiburi cha mama yako, yote yasingekukuta hayo",Bibi Kayoza alisema, kisha akawapa hadithi ile ile waliyopigiwa na Mama Kayoza.
"yote hayo yamepita, kilichonileta huku ni dawa ya kuniachanisha na hili dudu",Kayoza aliongea kwa upole,
"Futa kauli yako, usiseme hili dudu, kusema hivyo ni kosa kama mwananchi kumtukana rais wake" Bibi Kayoza alimwambia mjukuu wake tena hata sura yake ilionesha hakufurahishwa na kauli ya Kayoza,
"Sasa ni jina lipi unaona linafaa kuitwa?" Kayoza aliuliza na yeye alipaniki baada ya kuna Bibi yake akikitetea kile kiumbe kinachomnyima yeye Furaha ya maisha,
"Heshimu mazingira kama unataka kupona, kinyume na hapo hakuna kitakachowezekana" Bibi Kayoza aliongea maneno ambayo yalieleweka vizuri kwa Kayoza,
"Sawa nimekuelewa bibi, sasa hapa nimekuja kufuata dawa" Kayoza alimwambia bibi yake,
"dawa ipo, ila nitakupa usiku",Bibi yake kayoza alimwambia mjukuu wake,
"kwani ni dawa gani bibi?",Kayoza aliuliza,
"utaijua usiku huo huo",Bibi yake Kayoza alijibu,
"Na kwanini iwe usiku bibi?" Kayoza aliendelea na udadisi wake,
"Usiku kwa sababu ya kuwa watu wote wa hapa walioenda kazini watakuwa wamerudi nyumbani" Bibi Kayoza alijibu,
"Kwani ni lazima wawepo?" Kayoza aliendelea kuuliza,
"Ndio ni lazima wawepo, kwa sababu haya mambo yamekaa kimila, kwa hiyo basi ni lazima wanaukoo wote washiriki" Bibi Kayoza alijibu na kisha wakaendelea na hadithi zao binafsi kwa kushirikiana na Sajenti Minja na Omary ambao muda wote walikaa kimya ili kumuachia Kayoza uwanja mpana wa kuuliza maswali yake.
**************
Mkuu wa Polisi alifanikiwa sio kupajua tu mahali walipofikia wakina Sajenti Minja, alipajua mpaka Mahalia wanapolala yaani chumba walichokuwa wanakitumia wakina Sajenti Minja.
Mkuu wa polisi akapanga kuwa usiku huo ndio itakuwa mwisho wao kuvuta hewa safi ya duniani.
********************
Usiku ulipoingia, wakakusanyika wanaukoo wote, kisha wakatangaza lengo la kuitwa pale, ambalo lilikuwa ni kumuamisha mzimu kutoka kwa Kayoza na kwenda kwa Baba yake mdogo. Watu wasiokuwa wa ukoo ule hawakuhusika kujumuika pale, kwa hiyo Sajenti Minja na Omari waliambiwa wakae vyumba vya uwani. Wakina Sajenti Minja wakaondoka na kuelekea uko uwani.
Shughuli ikaanza ya kuuhamisha mzimu, yakaletwa maji masafi, mbuzi jike mwenye mimba na majani ya mitishamba ambayo waliyajua wao wenyewe.
Kayoza akalazwa chini, na pembeni yake alikuwa baba yake mdogo, bibi akaanza vitu vyake.
Muda wote huo, mkuu wa Polisi alikuwa anafuatilia kila kitu, mpaka kile kitendo cha wakina Sajenti Minja kuenda vyumba vya uwani alikiona, akawa anavuta muda ili akakamilishe azma yake, muda wake alioupanga ulipofika, akawa anaelekea kwenye chumba walichokuwepo Sajenti Minja na Omari, alipofika akagonga, bila ya kufikiria kuuliza mgongaji nani?, Omari akaundea mlango kisha akafungua, hakuamini macho yake alipomuona mkuu wa Polisi amesimama mlangoni huku kashika bastola, Omari kabla hajafanya chochote, alipigwa risasi kama nne hivi za kifuani, na kuanguka chini kwa kishindo mithili ya embe kubwa ambayo halijakomaa lililopopolewa mtini.
Na kule nje kwenye tambiko, wakati bibi anaendelea na tambiko, ulisikika mlio wa risasi ulisababisha mstuko na kumpelekea bibi kuanguka na kufa kwa presha iliyotokana na mshtuko wa ulisababishwa na mlio wa risasi, Bibi akawa amekufa bila hata kufanikisha zoezi la kuuhamisha mzimu.
Baada ya mlio wa risasi kusikika na bibi kuanguka chini kama mzigo, watu wote katika eneo lile walikurupuka, wingine wakiundea mwili wa bibi na wengine walikimbilia eneo ambalo mlio wa risasi ulitokea, wakakuta mtu akitokomea gizani kwa mbele yao mlangoni alikuwa Omary aliyekuwa amelala chini huku damu zikiwa zimemtapakaa,
Sajenti Minja akamsogelea na kukaa chini huku machozi yakimtoka na kuchukua kchwa cha kayoza na kukiweza mapajani mwake, akawa anamuangalia Omary aliyekuwa anatabasamu huku kila akitoa funda la pumzi lilikuwa likitoka huku limeambatana na damu.
Wenyeji wa pale walikuwa wanashangaa na wasijue la kufanya.
Omary akafumbua macho na kumuangalia Sajenti Minja aliyekuwa analia, kisha Omary akaongea maneno machache tu,
"Mk....uu ...wa...pol...isi" Omary aliongea kauli ambayo watu wengine hawakuielewa isipokuwa Sajenti Minja pekee.
Omary baada ya kutamka maneno hayo, shingo yake ililegea na kuanguka, huo ndio ukawa mwisho wa maisha ya Omary, roho yake ikatengana na mwili akiwa ugenini, kauli ya babu yake ikatimia.....
********ITAENDELEA**"****"***
the Legend☆