Riwaya: Maamuzi Magumu

Riwaya: Maamuzi Magumu

Chachasteven

JF-Expert Member
Joined
Jul 4, 2014
Posts
1,941
Reaction score
2,044
JINA: MAAMUZI MAGUMU
MTUNZI: CHIAMARO MOKIRI

HAKI ZOTE ZIMEHIFADHIWA. NI MARUFUKU KUNAKILI AU KUSAMBAZA KAZI HII BILA RUHUSA YA MAANDISHI KUTOKA KWA MWANDISHI. HATUA ZA KISHERIA ZITACHUKULIWA KWA YEYOTE ATAKAYETHUBUTU.


SEHEMU YA KWANZA

JACK REACHER ALIAGIZA kahawa vikombe viwili vya take away, bila sukari na kabla haijaletwa mezani kwake aliona maisha ya mwanaume mmoja yakibadilika milele. Sio kwamba mhudumu alikuwa amechelewa kuleta alichoagizwa. Ni kwamba, tukio aliloliona lilitokea kwa kasi. Kasi ya ajabu kiasi kwamba Reacher hakuwa anafahamu nini kinaendelea. Lilikuwa ni tukio la kawaida tu, linalojirudia karibu kila sehemu ulimwenguni zaidi ya mara bilioni kwa siku: Jamaa f'lani alifungua mlango wa gari kwa funguo na kuingia ndani na kuiwasha gari kuondoka. Hivyo tu.

Lakini hicho kitendo kilikuwa kinatosha.

Ile kahawa aliyoagiza ilikuwa imetengenezwa kwa umaridadi, kwahivyo Reacher alirudi kwenye mgahawa uleule masaa ishirini na nne baadae. Haikuwa kawaida ya Reacher kurudi eneo moja mara mbili baada ya masaa 24, lakini uzuri wa ile kahawa ulimpa sababu tosha ya kuvunja kanuni yake hiyo.

Mgahawa wenyewe ulikuwa unapatikana mashariki mwa mtaa wa Six Avenue uliyopo New York, katikati ya jengo la Bleeken na Houston. Mgahawa ulikuwa floo ya chini, huku juu yake kukiwa na ghorofa nne ambazo zilionekana kama nyumba za kupangishwa.

Reacher alikaa kwenye meza na kiti kilekile alichokuwa amekalia usiku wa jana. Alijinyoosha kwenye kiti chake na kuegemea ukuta ili kuipa miguu yake nafasi kwa kuegemea ukuta. Jambo lililofanya macho yake yaangalie mashariki ambako ndiko ilikuwepo barabara ya magari na wapita njia. Alikuwa amekaa upande wa meza za nje. Hii ni kwasababu alipenda kuona watu na magari na taa za barabarani zilivyopambana na giza. Lakini pia ilikuwa njia moja wapo ya kumfariji na kumuweka huru mtu aliye mpweke

Mhudumu aliyekuwa amemhudumia usiku wa jana ndiye alikuja kuchukua oda yake: kahawa mbili kwenye vikombe vya plastiki, bila sukari na bila kijiko. Alipoletewa alilipa moja kwa moja na kuiweka chenchi aliyopewa mezani. Kwa namna hiyo alikuwa huru kuondoka muda wowote ambao angetaka bila kumkera mhudumu au mmiliki wa mgahawa kama ingetokea dharura. Reacher aliyapangilia maisha yake hadi vile vitu vidogo usivyodhania. Ilikuwa ni tabia aliyozaliwa nayo. Hakuwa anamiliki kitu chochote na hakuwa anatembea na mzigo wowote. Na kimuonekano, alikuwa na mwili mkubwa lakini kivuli chake kilikuwa ni kidogo sana.

Aliinywa kahawa yake huku akipulizwa na kijoto cha usiku. Alikuwa anaangalia watu na magari. Aliona Taxi zikipita kwenda kaskazini na magari ya kubeba uchafu yakisimama hapa na pale. Aliona makundi ya vijana wakielekea kwenye kumbi za muziki. Aliona pia wasichana ambao siku si nyingi zilizopita walikuwa ni wanaume wakipita barabara hiyohiyo kuelekea kusini. Akaona Sedan moja ya bluu ya kijerumani ikiegeshwa. Halafu akaona mwanaume aliyevalia suti ya kijivu akishuka kutoka kwenye ile gari na kuanza kupiga hatua kuelekea kaskazini. Aliendelea kumtazama yule mwanaume alivyotembea kuzivuka meza zilizokuwepo nje hadi kuingia ndani ya ule mgahawa ambako kulikuwa na wahudumu waliotapakaa.

Alimuona akiwahoji maswali wale wahudumu.

Yule mwanaume alikuwa na urefu wa katikati, hakuwa kijana, hakuwa mzee, alikuwa mkakamavu kiasi kuvuka daraja la wazembe, hakuwa mwembamba ila katikati ya unene wa mazoezi. Nywele zake kichwani zilikuwa na mvi kidogo kwa pembeni na zilikuwa zimenyolewa kuwa fupi kidogo. Midomo yake haikuwa ikicheza sana alipokuwa akiongea. Lakini macho yake yalicheza yakifumba na kufumbua kila muda. Umri wake ulikuwa kati ya miaka ya arobaini, Reacher alikadiria, na zaidi Reacher alihisi yule mwanaume alikuwa ni mzee wa kazi. Reacher alikuwa ameona watu wengi wa sampuli hii katika siku zake za uhai.

Halafu yule mhudumu aliyemhudumia Reacher akageuka na kumnyoshea mkono Reacher. Yule mwanaume mwenye suti ya kijivu akakodoa macho yake. Reacher pia akakodoa macho. Wakabaki wametazamana kupitia kioo kilichowatenganisha na bila yeyote kuondoa macho kwa mwenzake, yule mwanaume akamwambia mhudumu ahsante na kuanza kupiga hatua kuelekea nje alipokuwa amekaa Reacher. Alirudi kwa njia aliyokuwa ameingialia na kuifikia meza aliyokusudia. Reacher aliamua kuweka ukimya kwa sekunde kadhaa akiwa anafikiria uamuzi wake. Halafu akasema "ndiyo." Sio swali, ila jibu.

"Ndiyo? Nini?" Yule mwanaume aliuliza.

"Ndiyo chochote," Reacher alijibu. "Ndiyo ninaifurahia jioni yangu, Ndiyo unaweza kukaa na mimi meza moja, Ndiyo unaweza kuniuliza swali lolote unalotaka kuniuliza."

Yule mwanaume alivuta kiti na kukaa mbele ya Reacher upande wa pili wa meza, hivyo kumnyima Reacher nafasi ya kuona barabarani.

"Ukweli ni kwamba nina swali nataka kukuuliza," Alisema.

"Najua," Reacher aliingilia. "Ni kuhusu jana usiku?"

"Umefahamu vipi ninataka kukuuliza kuhusu jana?" Sauti ya yule mwanaume ilikuwa ni ya chini na lafudhi yake ilionesha ni mtu wa Uingereza.

"Yule mhudumu kakuelekeza kwangu," Reacher alianza kueleza. "Na kitu pekee kinachonitofautisha na hawa wateja wengine ni kwamba mimi nilikuwepo hapa usiku wa jana pia."

"Una uhakika na maneno yako?"

"Geukia upande wa barabara," Reacher alisema.

Yule mwanaume aligeuza kichwa chake kuangalia barabarani.

"Sasa niambie nimevaa nini?" Reacher aliuliza.

"Shati la kijani," Yule mwanaume alianza kutaja. "Umelivaa juu ya tisheti ya kijani, limetumika kwa muda kidogo na chini una suruali aina ya Chinos ya kaki, chini haujavaa soksi na viatu vyako ni toleo la Uingereza pia."

"OK," Reacher alisema.

"OK nini?"

"Una jicho la kuona. Mimi pia ninalo. Sisi ni watoto wa mama mmoja. Na mimi ndiye mteja pekee niliye hapa sasa hivi ambaye jana usiku pia nilikuwepo. Sababu pekee ambayo ndiyo imemfanya yule mhudumu akuelekezee kwangu."

Yule mwanaume aligeuka kumtazama Reacher.

"Jana uliona gari?"

"Niliona magari mengi sana jana, Hii ni Sixth Avenue. Unategemea nini?"

"Uliona Mercedes Benz ikiwa imeegeshwa maeneo yale," Yule mwanaume alisema akinyooshea mkono wake barabarani.

Reacher akasema, "Mercedes Benz ya silva, Sedan ya milango minne, S420 ikiwa na sahani ya namba za New York zinazoanzia na OSC."

Yule mwanaume akageuka kumtazama Reacher. "Uliiona hiyo gari?"

"Ndiyo," Reacher alijibu. "Ilikuwepo hapo kwahivyo niliiona."

"Na kipindi inaondoka uliiona?"

"Ndiyo, ilikuwa inaelekea saa tano na dakika arobaini na tano, mwanaume mmoja alifika akapanda akawasha akaondoka?"

"Mbona haujavaa saa leo?"

"Sihitaji saa kujua muda. Ninaujua tu bila kuangalia saa."

"Kwahivyo ilikuwa inaelekea katikati ya usiku,"

"Labda," Reacher alijibu.

"Na ulibahatika kumuona dereva?"

"Nimekuambia nilimuona anapanda gari na kuliwasha na kuondoka."

Yule mwanaume alisimama.

"Nahitaji uje na mimi," Alisema. Halafu akaweka mkono wake wa kulia mfukoni. "Nitalipia kahawa yako."

"Nimekwishalipa,"

"Kwahivyo twende sasa."

"Wapi?"

"Ukaonane na Bosi wangu."

"Bosi wako ni nani?"

"Jamaa mmoja anaitwa Lane."

"Wewe sio askari," Reacher alisema. "Kwa tabia chache nilizoziona wewe sio askari."

"Tabia zipi?"

"Lafudhi yako! Wewe ni Muingereza. Sio Mmarekani na NYPD haina uhitaji hivyo kiasi cha kuajiri watu wasio raia wa nchi yao."

"Wamarekani wengi ni watu wa Uingereza," Yule mwanaume alisema. "Lakini upo sahihi. Mimi sio askari, ni raia wa kawaida tu."

"Raia wa kawaida daraja gani?"

"Aina ya daraja ambalo litakupa faida kwenye muda wako kama utatupa ushirikiano wa kumtambua mwanaume aliyepanda na kuendesha lile gari jana usiku."

"Faida kivipi?"

"Kiuchumi," Yule mwanaume alisema.

"Kwani hakuna faida zingine ukitoa hela?"

"Kama zipi?"

"Zipo nyingi tu, kwahivyo nitakaa hapa tu."

"Hili suala ni la muhimu kuliko unavyodhani."

"Muhimu kwa kiasi gani?"

Yule mwanaume mwenye suti akakaa tena kwenye kiti.

"Siwezi kukuambia hilo suala,"

"Basi kwaheri ya kuonana."

"Sio maamuzi yangu," Yule mwanaume alisema. "Ni maelekezo ya Bwana Lane hili suala asiambiwe mtu yeyote. Anazo sababu nzuri kabisa."

Reacher alikibunua kikombe chake na kuangalia kilichokuwemo. Kilikuwa kinaelekea kuisha.

"Una jina?" Reacher aliuliza.

"Unataka kufahamu jina langu? Nijue la kwako kwanza."

"Hapana! Wewe kwanza."

Kama kujibu, yule mwanaume akaingiza vidole vyake kwenye mfuko wa kushoto wa kwenye koti la suti yake na kutoa kitambulisho. Akakiweka kwenye meza. Kilikuwa kitambulisho cha kuvutia. Kwa juu kilikuwa kimeandikwa: OPERATIONAL SECURITY CONSULTANTS.

"OSC," Reacher alisema. "Kama sahani ya namba ya lile gari?"

Yule mwanaume hakujibu kitu.

Reacher alicheka kidogo, "Yaani wewe ni mtu unayepanga operesheni za ulinzi halafu gari lako limeibiwa. Naelewa kwa kiasi gani hicho kitu kinafedhehesha."

"Shida yetu sio gari,"

Chini kwenye kile kitambulisho kulikuwa na jina: John Gregory. Kwa chini kulikuwa na maelezo mafupi: Jeshi la Uingereza, Mstaafu. Halafu cheo cha kazi kilifuata: Makamu wa Rais.

"Tangu umetoka jeshini muda kiasi gani umepita?"

"Miaka saba." Yule mwanaume alijibu.

"Kitengo gani?"

"SAS."

"Unaonekana," Reacher alisema.

"Wewe pia unaonekana," Gregory alisema. "Una muda gani upo nje ya jeshi?"

"Miaka saba," Reacher alijibu.

"Kitengo?"

"US. Army CID."

Gregory alimtazama Reacher kama mwenye matumaini.

"Kwahivyo ulikuwa kama mpelelezi?"

"Nadhani,"

"Cheo?"

"Sikumbuki," Reacher alijibu. "Nimekuwa raia kwa miaka saba sasa."

"Acha kuona aibu," Gregory alimwambia. "Kwa kukadiria ulikuwa Lieutenant."

"Nilikuwa Major," Reacher alijibu.

"Ulileta usumbufu au matatizo?"

"Kiasi."

"Una jina?"

"Watu wote wana majina."

"Lako ni nani?"

"Reacher."

"Kwahivyo sasa hivi unafanya nini?."

"Nakunywa kahawa."

"Unafanya kazi?"

"Hapana," Reacher alisema. "Sitaki kazi."

"OK! Mimi nilikuwa Sajenti," Gregory alisema.

"Nafahamu," Reacher alijibu.

"Kwahivyo utakuja na mimi twende kwa Bwana Lane?"

"Nimekwishakuambia nilichokiona. Unaweza kwenda kumsimulia."

"Bwana Lane atafurahi kama akisikia moja kwa moja kutoka kwako."

Reacher akaangalia tena kilichomo kwenye kikombe chake. "Yupo wapi?"

"Hayupo mbali. Ni safari ya dakika kumi tu."

"Sina hakika kama nina muda," Reacher alijibu. "Kama unavyoona nakunywa kahawa yangu."

"Ipo kwenye kikombe cha take away. Unaweza kubeba ukaja nayo."


"Napenda ukimya na utulivu."

"Ninahitaji dakika zako kumi tu."

"Fujo zote za nini kisa gari tu, hata kama ni Mercedes sio fujo hizo."

"Nimekuambia suala sio gari. Ni zaidi ya gari."

"Kwahivyo ni kuhusu nini?"

"Uhai na kifo," Yule mwanaume alijibu. "Na kwa muda huu ni kifo kuliko hata uhai."

Reacher aliangalia tena kilichomo kwenye kikombe chake. Yalikuwa yamebaki matone kadhaa tu. Alikiweka kikombe chini na kusimama.

"Haya, twende zetu."

ITAENDELEA...

ANGALIZO: RIWAYA ITAISHA, Ila kwa anayelipia tu. Atatumiwa binafsi. Hapa nitakuwa naweka kwa kadri ninavyohisi inafaa! Ahsante.
 
Muandishi wa riwaya hii upo vizuli na umetulia ,unandika vizuli na unajua kuipangilia, ikiwa liwaya maridhawa ya kipelelezi
 
Back
Top Bottom