baadhi yakiwa ni maduka ya kampuni kubwa na maarufu za jijini Dar es Salaam na
mengine maduka ya watu binafsi. Maduka yale ya kisasa yalikuwa yamezungukwa
na kuta kubwa za vioo visafi vinavyomwezesha mtu yeyote kuweza kuona bidhaa
zilizokuwa ndani ya maduka yale.
Ile korido ya mbele ilikuwa ikielekea katika Supermarket kubwa ya kisasa iliyokuwa
na bidhaa nyingi za matumizi ya kawaida ya binadamu yenye wahudumu waliovaa sare
maalum za kuwatambulisha na vitambulisho vyao vikiwa vimening’inizwa kwa kamba
maalum shingoni. Ile korido ya upande wa kulia ilikuwa ikitazamana na maduka
mengi ya bidhaa tofauti zikiwemo ofisi za kampuni za mawasiliano ya mitandao ya
simu. Koplo Tsega akajikuta akiyakumbuka vyema maelezo ya Aden Mawala yule
meneja wa benki ya Zanzibar Marine kuwa duka la Zanzibar Stone City Bazaar
lilikuwa likitazamana na duka la vinyago la Afrikan art craft mle ndani. Hivyo Koplo
Tsega akashika uelekeo wa upande wa kulia akiifuata ile korido iliyokuwa ikitazamana
na maduka mbalimbali.
Kulikuwa na watu wengi katika korido ile huku kila mmoja akionekana kuzama
katika hamsini zake. Koplo Tsega wakati akitembea akawa akiyatembeza macho
yake taratibu kuzichunguza sura za watu aliokuwa akipishana nao kwenye korido ile.
Hakumuona mtu yeyote wa kumtilia mashaka ingawa baadhi ya watu hawakujizuia
kumtazama huku dhahiri wakionekana kuvutiwa na mtindo wa uvaaji wake kama siyo
weusi wake wa asili.
Ilikuwa ni wakati Koplo Tsega alipokuwa mbioni kufika mwisho wa korido ile
pale alipoliona duka kubwa la vinyago lenye maandishi makubwa ya African art craft
upande wa kushoto. Ndani ya duka lile kulikuwa kijana mmoja aliyekuwa akiwaelekeza
jambo wazungu wawili,mwanamke na mwanaume waliokuwa wakikitazama kinyago
kimoja kikubwa cha kimakonde cha mti wa mpingo cha mwanamke wa kiafrika
aliyebeba mtoto wake mgongoni kwa mbeleko. Kinyago kizuri kilichochongwa kwa
umakini wa hali ya juu.
Koplo Tsega alipolifikia lile duka la vinyago akasimama mbele yake na
kuyatembeza macho yake taratibu upande wa kulia. Maelezo ya yule meneja wa
benki ya Zanzibar Marine yalikuwa sahihi kwani duka la Zanzibar Stone City Bazaar
lilikuwa likitazamana na duka lile la African art craft kwa upande wa kulia. Kwa dakika
kadhaa Koplo Tsega akasimama akilitazama duka lile kwa utulivu kama mtu ambaye
hayaamini vizuri macho yake.
Duka la Zanzibar Stone City Bazaar lilikuwa ni miongoni mwa maduka
yaliyokuwa na pilikapilika nyingi za wateja baadhi wakiingia mle ndani na kutazama
bidhaa zilizokuwa mle ndani huku wengine wakifanya manunuzi ya bidhaa. Lilikuwa
ni duka kubwa lenye maduka mengi madogo madogo ndani yake ya bidhaa kama
nguo,simu,vyakula,vyombo vya nyumbani,vifaa vya umeme,vitabu,vifaa vya
maofisini,viatu,mikoba na vifaa vingine muhimu vya mahitaji ya binadamu. Hata hivyo
wateja wengi waliokuwa ndani ya maduka yale walikuwa wanawake ambao wengi
wao walionekana kuvutiwa zaidi na bidhaa kama nguo,viatu,mikoba na vyombo vya
nyumbani.
Fikra za mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la White Sugar zikiwa zimeanza
kujengeka upya kichwani mwake Koplo Tsega akaanza taratibu kuzitupa hatua
zake akielekea kwenye lile duka la Zanzibar Stone City Bazaar huku akigeuka na
kuyatembeza macho yake huku na kule katika namna ya kuhakikisha kuwa hakuna
mtu yeyote aliyekuwa akizifuatilia nyendo zake. Wakati Koplo Tsega akiufikia mlango
wa duka lile pale mlangoni akapishana na mwanaume mmoja mrefu na mweusi akiwa
katika mavazi yake ndhifu ya suti ya kijivu ya Marks & Spenser,shati la rangi nyeusi na
tai ya rangi ya zambarau.
Mtu yule alikuwa amenyoa upara na macho yake alikuwa ameyafunika kwa miwani
kubwa nyeusi yenye kumwezesha kuiona dunia pasipo usumbufu wowote. Mkononi
alikuwa amevaa saa ya gharama sana ya dhahabu aina ya Maurice Lacroix huku akiwa
amebeba briefcase nyeusi inayotumia mfumo wa codenumber maalum katika kuifungua.
Miguuni alikuwa amevaa viatu vyeusi nadhifu vya ngozi huku marashi yake ya gharama
yenye harufu nzuri ya tafsiri ya ukwasi yakiongeza ziada nyingine katika utanashati
wake.
Akionekana ni mwenye haraka mara tu mtu yule alipopishana na Koplo Tsega pale
mlangoni akaanza kutembea kwa kuharakisha akishika uelekeo wa upande wa kushoto
wa ile korido pana mbele ya lile duka huku mara kwa mara akiunyanyua mkono
na kuitazama ile saa yake ya mkononi kama mtu aliyekuwa nyuma ya muda katika
tukio fulani. Kwa sekunde kadhaa Koplo Tsega akajikuta amesimama pale mlangoni
na kumtazama yule mtu namna alivyokuwa akitokomea kwenye ile korido kama
kimbunga kisha akageuka na kuingia mle ndani ya lile duka huku akiyapuuza macho
ya watu waliokuwa wakimtazama eneo lile kana kwamba alikuwa amebabaishwa na
kutekwa na muonekano wa yule mwanaume aliyetoka kwenye lile duka.
Jina la White Sugar likiwa limerudi tena kwenye fikra zake mara tu alipoingia
ndani ya lile duka Koplo Tsega akajisogeza upande wa kulia sehemu kulipokuwa na
duka la simu za mkononi za kisasa zilizopangwa ndani ya rafu nzuri ya vioo. Kijana
mmoja wa kiume aliyekuwa akihusika na biashara ile haraka akasimama kutoka
kwenye kiti alichoketi nyuma ya ile rafu ya vioo na kusogea karibu na Koplo Tsega
kama afanyavyo kwa wateja wengine waliokuwa wakiingia mle ndani na kuonekana
kuvutiwa na bidhaa zake.
“Mambo vipi dada?’’ yule kijana akamsalimia Koplo Tsega kwa makeke
“Poa” Koplo Tsega akaitikia huku usoni akiumba tabasamu la kirafiki
“Karibu sana”
“Ahsante” Koplo Tsega akaitikia huku akigeuka na kuyatembeza macho yake
kuzichunguza sura za watu waliokuwa mle ndani kabla ya kuyarudisha tena mbele
yake na kuanza kuzitazama simu zilizokuwa ndani ya ile rafu ya vioo ingawa dhahiri
mawazo yake hayakuwa katika zile simu. Yule kijana muuzaji wa lile duka kuona vile
akasogea karibu akijitahidi kuyapatiliza kwa ukaribu macho ya Koplo Tsega. Koplo
Tsega alipoyainua macho yake kumtazama yule kijana akavunja ukimya akiuliza swali
la hila.
“Hili ndiyo duka la Zanzibar Stone City Bazaar?”
“Maduka ya humu ndani yote ni ya Zanzibar Stone City Bazaar” yule kijana
akafafanua huku akishindwa kuelewa hoja muhimu katika swali lile.
“Ninashida na meneja wa hili duka,unaweza kunisaidia nikaonana naye?’’Koplo
Tsega akamuuliza yule kijana kwa utulivu huku akimtongoza kwa tabasamu lake
maridhawa.
“Shida gani?’’ yule kijana akauliza huku akimtazama Koplo Tsega kwa udadisi
“Shida binafsi inayohusu biashara” Koplo Tsega akadanganya huku akimtazama
yule kijana kwa makini.
“Umepishana naye sasa hivi pale mlangoni wakati ulipokuwa ukiingia humu
ndani” jibu la yule kijana likapelekea mshtuko mkubwa kwa Koplo Tsega,moyo wake
ukalipuka kabla ya baridi nyepesi kuanza kusafiri mgongoni mwake huku kijasho
chembamba kikichomoza taratibu katika sehemu mbalimbali za mwili wake na
hatimaye utulivu kupotea kabisa moyoni mwake ingawa alijitahidi kuumeza mshtuko
ule kwa kila hali.
Kwa sekunde kadhaa akili ya Koplo Tsega ilishindwa kabisa kuamini kuwa yule
mwanaume aliyepishananaye muda mfupi pale mlangoni wakati akiingia kwenye lile
duka ndiye angekuwa White Sugar,mtu aliyekuwa akimtafuta. Koplo Tsega akajikuta
akishawishika kuwa muda uleule atoke kwenye lile duka na kuanza kutimua mbio
akashika ule uelekeo wa yule mtu kule alikotokomea. Hata hivyo baada ya kufikiri kwa
kina Koplo Tsega akajikuta akiuweka kando mpango ule pale alipohisi kuwa kwa ule
muda uliopita yule mtu angeweza kuwa tayari amekwishafika mbali sana na eneo lile
kwa vile alivyoonekana kuwa na haraka ya kupita kiasi istoshe hakufahamu mtu yule
alikuwa akielekea wapi.
“Oh! masikini mimi nimekuwa mzembe kwa kuchelewa” Koplo Tsega akalaani
kitendo kile huku akishindwa kuamini.
“Kwani hamfahamiani?” yule kijana akauliza
“Hatufahamiani ila kuna mtu anayefahamiana naye ndiye aliyenielekeza kwake”
Koplo Tsega akadanganya wa hila
“Pole sana basi uache business card yako ili siku atakaporudi nimpe akutafute”
yule kijana akatoa wazo huku akimtazama Koplo Tsega katika mtazamo wa kimapenzi
hata hivyo Koplo Tsega akampuuza.
“Bahati mbaya sana leo nimesahau kutembea na business card yangu. Kwani
hatorudi tena leo?” Koplo Tsega akamuuliza yule kijana
“Hapana hatorudi tena na imekuwa ni bahati sana kumuona kirahisi namna
ile kwani mara nyingi sana huwa yupo safarini nje ya nchi” yule kijana akaendelea
kutanabaisha na Koplo Tsega alipomtazama akagundua kuwa maelezo yake yalikuwa
yamekomea pale katika kumfahamu White Sugar na ile ndiyo ilikuwa salama yake.
“Ameelekea wapi?” Koplo Tsega akauliza kwa utulivu huku akimtazama yule
kijana kwa makini.
“Anawahi boti ya kuelekea kisiwani Zanzibar”
“Kwani anaishi Zanzibar?”
“Ndiyo maskani yake yalipo’’ yule kijana akafafanua huku akionekana kuwa na
hakika na maelezo yake na hapo kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku Koplo
Tsega akizidi kujilaani kwa namna alivyopishana na bahati ile pasipo kujua. Mwishowe
akavunja ukimya kuuliza
“Unaweza kunisaidia namba zake za simu?’’
“Namba zake za simu nilizonazo ukimpigia huwa hapatikani” yule kijana
akaendelea kufafanua na kupitia maelezo yake Koplo Tsega akatambua kuwa
asingeweza kupata ziada nyingine kutoka kwake hivyo haraka akaunyanyua mkono
na kuitazama saa yake ya mkononi na alipomaliza na kuyahamishia macho yake kwa
yule kijana akaumba tabasamu jepesi lisilo na maana yoyote usoni mwake kabla ya
kuvunja ukimya
“Nashukuru sana wacha niende nitakuja siku nyingine”
“Pole sana dada yangu kama vipi niachie namba yako ya simu ili siku yoyote
atakaporudi nikufahamishe” yule kijana akasisitiza akijaribu bahati yake na Koplo
Tsega alipomtazama akayaona macho yake yalivyojawa na uchu wa ngono hali
iliyompelekea atabasamu kidogo na kuanza kumtajia namba ya simu ya kufikirika
kichwani isiyopatikana. Yule kijana akawahi kuinakili haraka ile namba kwenye simu
yake na wakati alipomaliza kubofya tarakimu ya mwisho na kuinua macho yake
kumtazama Koplo Tsega mbele yake,Koplo Tsega tayari alikuwa amekwisha toka nje
ya lile duka na kutokomea.