RIWAYA: Mifupa 206

Katika upande ule wa kulia tulioingia kulikuwa na milango mingine. Tulipoifikia
ile milango yule msichana mbele yangu akasimama kisha akageuka na kunitazama.
Nikatabasamu kidogo katika hali ya kuonesha kuwa sikuwa na wasiwasi wowote
ingawa hali iliyokuwa ikiendelea moyoni mwangu nilikuwa nikiifahamu mwenyewe.
Yule msichana alipoacha kunitazama akageuka na kufungua ule mlango kisha
akaniashiria nisogee karibu na kuchungulia mle ndani. Nikasogea na kuchungulia mle
ndani na kwa kufanya vile nikawaona wasichana wadogo vigoli. Uzuri wa wasichana
wale kwa kweli ulinibabaisha na kuziamsha hisia zangu.
Wale wasichana wakageuka mara tu mlango ule ulipofunguliwa wakitutazama
ingawaje nilikuwa na kila hakika kuwa walikuwa wakinitazama mimi zaidi kuliko yule
mwenyeji wangu. Labda kwa sababu nilikuwa mwanaume peke yangu eneo lile. Mara
wale wasichana vigoli wakaacha walichokuwa wakikifanya na kuanza kunifuata pale
mlangoni lakini yule mwenyeji wangu aliwahi kuwakemea hivyo wakarudi.
Yule dada akanisukuma pembeni na kufunga ule mlango na hapo safari yetu
ikaendelea huku yule mwenyeji wangu akiendelea kufungua milango ya vyumba
vingine vilivyokuwa vikifuatia ambapo mle ndani kulikuwa na wasichana wengine
wazuri sana wa rika tofauti. Niliwatazama wasichana wale na kwa kweli niseme kuwa
mwanaume yeyote mkware asingekubali hazina ile impite hivihivi.
Hatimaye safari yetu ikaishia ndani ya chumba kipana chenye kitanda kikubwa
cha futi sita kwa sita kilichofunikwa kwa shuka safi zenye rangi ya kupendeza na mito
miwili ya kuegemea. Pembeni ya kitanda kile kulikuwa makochi mawili makubwa ya
sofa na meza fupi ya kioo katikati yenye kibeseni kidogo cha majivu ya sigara mfano
wa fuvu la mtu.
Nikayatembeza macho yangu na kwenye pembe ya chumba kile kulikuwa na
jokofu dogo la vinywaji lililopakana na kabati lililofungwa ambalo sikuweza kufahamu
haraka kuwa mle ndani yake kulikuwa na nini. Kiyoyozi murua kilichokuwa mle ndani
kililifukuza joto kali la jiji la Dar es Salam na kunipelekea niyafurahie sana mandhari
yale tulivu.
“Karibu uketi” yule msichana akanikaribisha na nilipomchunguza niliweza
kuukadiria umri wake kuwa ulikuwa ni kati ya miaka ishirini na mbili na ishirini nne
huku akionekana kujiamini sana. Hatimaye nikaenda na kuketi kwenye kochi moja
miongoni mwa yale makochi mawili yaliyokuwa mle ndani. Mara tu nilipoketi mbele
yangu nikajikuta nikitazamana na runinga pana iliyokuwa kwenye kona ya kile chumba.
“Ahsante!” nikaongea na kuketi.
“Utatumia kinywaji gani?” yule mrembo akaniuliza na hadi kufikia pale niliweza
kuhisi kuwa alikuwa na wadhifa wa juu mle ndani.
“Maji baridi tu tafadhali!” nikamwambia yule mrembo na hapo nikamuona
akienda kufungua lile jokofu la mle ndani kisha akachukua chupa kubwa ya maji baridi
na bilauri ya kioo halafu na yeye akajichukulia kinywaji baridi cha Malta na kuja na
kuketi mbele yangu kwenye lile kochi jingine ambalo lilitupelekea tuketi katika mtindo wa kutizamana
Kwa vile nilikuwa nikihisi kiu nikaichukua ile chupa ya maji na kuifungua kisha
nikaanza kugida mafunda kadhaa ya maji pasipo kuitumia ile bilauri. Nilipoiweka ile
chupa juu ya meza ilikuwa imebaki nusu hivyo nikachukua pakiti ya sigara kutoka
mfukoni na kutoa sigara mbili ambapo moja nilimpa yule mrembo na nyingine
nikaitia mdomoni na kuilipua kwa kiberiti changu cha gesi. Ile sigara ilipowaka na
kukolea vizuri nikamrushia kile kiberiti yule mrembo ambapo alikidaka kwa ustadi na
kujiwashia sigara yake.
“Jina lako unaitwa nani?” nikamuuliza yule mrembo baada ya kuitoa sigara yangu
mdomoni na kuupuliza moshi pembeni
“Oga” yule mrembo akanijibu kwa utulivu huku akiendelea kuvuta sigara yake
“Jina zuri”
“Na wewe je?”
“Remy” nikamdanganya
“Siyo Stephen Masika tena?” yule mrembo akaniuliza na hapo moyo wangu
ukalipuka kwani Stephen Masika lilikuwa jina langu la bandia ambalo nilikuwa
nimelitumia kujiandikisha uanachama kule Vampire Casino. Nikaumeza mshtuko
wangu kwa kuivuta sigara yangu taratibu na nilipoitoa nikamuuliza yule mrembo kwa
shauku
“Umenijuaje?”
“Ulinidanyanga ikidhani sikufahamu?” yule mrembo akaniuliza huku akivuta pafu
jingine la sigara na alipoitoa ile sigara mdomoni akaendelea huku akiupandisha mguu
wake mmoja juu ya mwingine na hivyo kulipelekea gauni lake fupi lipande juu na
hapo nikayaona mapaja yake yaliyonona. Ili kuurudisha vizuri mhimili wa nafsi yangu
nikaanza kumkemea pepo mchafu ingawa sidhani kama maombi yangu yalikubalika
kwani nafsi yangu bado iliendelea kusukwasukwa ovyo na jinamizi la ngono.
“Huwenda ukawa unajua kila kitu kuhusu mimi Oga hebu niambie” nikamwambia
yule mrembo huku nikitengeneza uso wa tabasamu.
“Kwa sehemu tu ndiyo maana nikakuleta humu ndani” Oga akaniambia kwa
utulivu kisha akaivuta sigara yake na alipoitoa na kupuliza moshi pembeni akaniuliza
“Tafadhali! niambie wewe ni nani hasa na umefika hapa kufanya nini?”
“Nahitaji kufahamu nyinyi ni akina nani na mnashughulika na mambo gani humu
ndani” nikamuuliza yule mrembo huku nikimtazama kwa makini.
“Nani aliyekuelekeza humu ndani?” yule mrembo akaniuliza na kabla sijamjibu
nikamuona akisimama na kuanza kunifuata pale nilipoketi. Kufumba na kufumbua
akaitoa bastola yangu kutoka nyuma kiunoni nilipokuwa nimeibana kwa mkanda
kisha akaifyatua magazine yake na kuitupia pale kitandani. Tukio lile likanipelekea jasho
jepesi lianze kufanya ziara kwenye sehemu mbalimbali za mwili wangu. Kitendo kile
kikanifanya nijihisi kuwa nilikuwa nimemkadiria vibaya yule mrembo. Hata hivyo
sikutia shaka yoyote.
“Nimeokota business card yenu hivyo nikaona si vibaya kuja kuwatembelea”
nikamwambia yule mrembo huku nikiendelea kuivuta sigara yangu taratibu.
“Na hiyo bastola ni ya nini humu ndani?” yule mrembo akaniuliza huku
akinitazama kwa makini.
“Kujilinda pale inapobidi”
“Nani aliyekwambia kuwa humu ndani kuna hatari?” swali la Oga likanipelekea
nimtazame mrembo yule kwa makini. Nilikuwa na uzoefu mkubwa kwa wasichana
wenye tabia kama za Oga. Hivyo nilifahamu kuwa ili kupata matokeo mazuri ya kazi
yangu nilihitajika kuwa mtulivu na mwenye moyo wa subira. Hatimaye nikaitia sigara
yangu mdomoni na kuivuta taratibu. Nilipoitoa sigara yangu mdomoni nikayakung’uta
majibu kwenye kile kibeseni cha majivu pale mezani kisha nikavunja ukimya
“Jina langu naitwa Chaz Siga” nikamwambia yule mrembo huku nikiiacha sigara
yangu ikiteketea katika pacha ya vidole vyangu.
“Vizuri!,endelea nakusikiliza” Oga akaongea huku akitabasamu.
“Mimi ni mpelelezi wa kujitegemea” nilikatisha maongezi kisha nikaipeleka sigara
yangu mdomoni na kuivuta taratibu. Nilipoitoa sigara mdomoni nikaupuliza moshi
pembeni na kuendelea
“Sikuwahi kufika humu ndani pamoja na kuzaliwa na kukulia hapa jijini Dar es
Salaam kwa muda mrefu. Lakini sasa nafurahi kupafahamu mahali hapa na huwenda
majibu ya maswali yangu yakaanza kujibiwa”
Oga alikuwa ameketi kwenye kochi mbele yangu huku mguu wake mmoja
ameupandisha juu ya mwingine na sigara yake ikiendelea kuteketea taratibu mkononi.
Ingawa Oga alikuwa akitazama dirishani lakini nilikuwa na kila hakika kuwa masikio
yake alikuwa ameyatega vizuri kunasa kile nilichokuwa nikikizungumza.
“Unapeleleza nini?” Oga akaniuliza
“Kifo cha rafiki yangu” nikaongea kwa utulivu
“Jina lake?”
“Gabbi Masebo” nilimwambia Oga na hapo nikamuona akitabasamu kidogo
kisha tabasamu lake lilipokoma akaniambia
“Okay! endelea”
“Rafiki yangu ametoweka miaka kumi iliyopita katika mazingira ambayo siyaelewi”
“Nini kinachokusukuma uje kufanya upelelezi wako humu ndani?” Oga akaniuliza
huku akiyakung’uta majivu ya sigara yake kwenye kile kibeseni pale mezani.
“Mpaka sasa bado sijafahamu kama nimefika hapa kupeleleza ua lah!” niliongea
huku nikimtazama Oga na safari hii uzuri wake ulizidi kunichanganya. Umbo lake
maridhwawa lilikuwa limechoreka vyema ndani ya gauni lake jepesi na laini alilolivaa.
Mikono yake mirefu na imara pamoja na vishimo vyake vidogo mashavuni vikaongeza
ziada nyingine katika uzuri wake.
“Hicho ndiyo kilichokupelekea kumuua mlinzi wetu?” swali la Oga likanipelekea
nigeuke na kumtazama kwa shauku.
“Wapi?”
“Vampire Casino”
“Umejuaje?” nikamuuliza Oga huku nikimkazia macho.
“Walinzi wawili uliopambana nao wakati ukijaribu kutoroka walitueleza habari
zako na kamera za usalama za casino zikatuhakikishia” Oga akaongea kwa utulivu.
“Hao walinzi wamewaeleza wewe na nani?” nikamuuliza Oga huku nikitabasamu
“That’s non of your business!” Oga akafoka kwa hasira huku akinitazama kwa makini.
“So what kind of business is yours?” nikamuuliza Oga kwa utulivu huku nikiyakung’uta
majivu ya sigara yangu kwenye kile kibeseni cha majibu pale mezani kisha nikaendelea
“Unaweza kuniambia kuwa mnawapata wapi wale mabinti wadogo kule
vyumbani?” nikamuuliza Oga na hapo akaangua kicheko kilichonishangaza.
“Nilidhani umesahau. Vipi unataka mmoja?” Oga akaniuliza huku ekiendelea
kucheka lakini ghafla kicheko chake kikakoma huku sura yake ikiwa mbali na mzaha
na tabia yake ile ya kubadilikabadilika ikazidi kunichanganya.
“Bado hujanijibu swali langu mrembo” Oga akanitazama kwa utulivu na uso wake
haukuonesha tashwishwi yoyote’’
“Tayari umechelewa kwani hata nikikupa hizo taarifa hutofanikiwa kufikanazo
kokote”
“Una maanisha nini?” nikamuuliza Oga kwa utulivu.
“Umefanya makosa sana kuingia humu ndani”
“Mbona unanitisha mrembo”
“Unadhani kuwa nakutisha basi umekosea sana kwani huu ndiyo mwisho wako
na habari zako zitaishia humu ndani’’
“Una maanisha nini?’’
“Subiri na utanielewa muda siyo mrefu. Najua umekuja humu ndani kupeleleza
kinachoendelea lakini nataka nikufahamishe kuwa hilo ni kosa kubwa sana ulilowahi
kulifanya siku za uhai wako hapa duniani. Baada ya kumtafuta Milla Cash kwa muda
mrefu na kumkosa naona sasa umeamua kufanya uamuzi wa busara kwa kujileta
mwenyewe’’
Nikamtazama Oga kwa shauku kwani kitendo cha kumtaja Milla Cash bila
shaka kilikuwa kimeanza kutanzua wingu zito lililotanda kichwani mwangu. Kwa
kweli nilianza kuhisi wepesi fulani katika fikra zangu na hapo nikaupachika mche wa
sigara yangu mdomoni na kuvuta mapafu kadhaa huku nikiupisha utulivu kichwani.
Nilipoitoa sigara mdomoni nikaupuliza moshi pembeni huku nikimtazama Oga kwa
utulivu.
“Kama ungekuwa umewahi kuniomba ushauri huwenda ningekushauri usiingie
humu ndani lakini kwa sasa nafasi hiyo huna. Huu ni mtandao mkubwa sana usioweza
kuvunjwa kwa urahisi na hivyo vijiharakati vyenu”
“Mbona unaongea kama mwoga?”
“Najua anazungumza hivyo kwa kuwa hufahamu uzito wa maneno yako ya ovyo”
Oga akafoka kwa dhihaka.
“Mbona hujaniambia kuwa mtandao wenu unahusika na nini?”
“Shut up your mouth you bastard!” Oga akafoka hata hivyo nilimpuuza na kuendelea
na maswali yangu.
“Mtandao wenu unajumuisha na viongozi wa serikali?”
“Muda wa maswali umekwisha” Oga akaniambia huku akisogeza kochi nyuma na
kusimama na nilipomchunguza nikamuona akiwa ameshika bastola yenye kiwambo
cha kuzuia sauti mkononi.
“Mbona hutaki kujibu maswali yangu. Kwani mtandao wenu unashughulika na
nini na kiongozi wenu ni nani?” nikamuuliza Oga lakini hakunijibu na badala yake
haraka nikamuona akiielekeza bastola yake kwangu. Risasi mbili alizozifyatua moja
ikachana lile kochi nililolikalia huku mimi nikiwahi kuruka pembeni. Risasi nyingine
ikachimba sakafu na hapo nikajua kuwa kweli Oga alikuwa amedhamiria kuniua.
Oga akaendelea kufyatua risasi ovyo mle ndani akinilenga lakini nilikuwa
mwepesi wa kujirusha upande huu na ule na hapo risasi moja ikanipunyua begani.
Hatari ikaanza kunikaribia kwani kila nilipojaribu kumkaribia Oga alinikwepa na
kurudi nyuma. Nilipoona hatari inazidi kunikaribia nikainua kitanda cha mle ndani
ili kujikinga na mashambulizi yale. Niliendelea kukitumia kile kitanda kuzikwepa zile
risasi na nilipopata upenyo mzuri nikajirusha upande wa pili sehemu aliposimama Oga
na kufumba na kufumbua nikawa nimefanikiwa kumfikia Oga na kumtundika kabari
matata isiyompa nafasi ya kufurukuta. Mshikemshike ule ukatupelekea tujibwage juu
ya ile meza ya kioo iliyokuwa mle ndani. Ile meza ikavunjika vipandevipande na vioo
vyake kutuchana hata hivyo kabari yangu matata haikutoka kwenye shingo ya Oga.
Tukiwa pale chini tukaendelea kugaragazana. Oga alikuwa akipigania kuichomoa
ile kibari yangu matata niliyomtundika shingoni huku akitafuta mhimili mzuri wa
kunishindilia risasi na mimi nikajitahidi kwa kila hali kuhakikisha kuwa hapati nafasi
ya kufurukuta.
Kile kitanda kilikuwa kimeangukia pembeni kikichanguka ovyo. Zile purukushani
zikaendelea pale chini na kwa kweli pale ndiyo nilipojua kuwa Oga hakuwa mwanamke
wa kuchezea kwani alikuwa na nguvu mno na maarifa ya mapigano. Katika
purukushani zile nikafanikiwa kumtandika Oga ngumi mbili za bega la ule mkono
wake ulioshika bastola. Ule mkono ukashikwa na ganzi,vidole vyake vikafunguka na
ile bastola yake ikaanguka chini na hapo nikaipiga teke na kuitupilia mbali.
Kwa kujibu mapigo Oga akanipiga kiwiko cha nguvu cha tumbo na hapo nikasikia
kichefuchefu cha ghafla huku maumivu makali yasiyo na mfano yakisambaa mwilini.
Hali ile ikanipelekea nishindwe kumdhibiti Oga vizuri hata hivyo sikumuachia. Oga
alipoona kuwa sitaki kumauchia akaanza kunikwaruza usoni kwa kucha zake ndefu na
kali. Nikawa nikiukwepesha uso wangu huku na kule bila kumuachia lakini hatimaye
alinizidi ujanja kwani mikono yake ilikuwa mirefu sana kuweza kuufikia uso wangu
bila kikwazo na hivyo zile kucha zake ndefu kunikwaruza vibaya.
Hali ile ikanipelekea niiachie ile kabari bila kupenda na hilo likawa kosa kubwa
kwani Oga akanitandika teke la nguvu la korodani. Kwa kweli nilisikia maumivu
makali yaliyonipelekea nigande kama sanamu.
Hasira za kudhihakiwa zikanivaa na hapo nikajibetua nyuma na kusimama.
Mapigo ya Oga mawili ya karate yaliponijia shingoni nikayakinga katika namna ya
kuyapunguza nguvu kisha kwa nguvu zangu zote nikapeleka ngumi moja matata na
kuuvunja mwamba wa pua yake na hapo Oga akapepesuka na kupoteza mhimili.
Sikusubiri Oga atulie hivyo nikamuwahi kwa mapigo mengine yenye malengo ya
kulitia udhaifu tumbo lake hata hivyo Oga alikuwa makini sana kuyapangua mapigo
yale kama mchezo na kunikwepa.
Nguvu nyingi nilizowekeza kwenye mapigo yale na kumkosa Oga zikanipelekea
nipepesuke kama mlevi nikikosa mhimili makini. Oga kuona vile akaruka round kick
na kunishindilia pigo jingine la teke mgongoni lililonipelekea nijibamize ukutani bila
kupenda. Hakika Oga alikuwa mpambanaji matata mwenye mwili wa kike lakini nguvu
za kiume na bila shaka alikuwa tayari kupambana na mimi mpaka tone la mwisho la
damu yake. Maumivu makali yakasambaa mgongoni mwangu.
Pigo jingine la teke lilipokuja nikawahi kuliona hivyo nikainama chini kidogo na
kulikwepa na hapo pigo lile likakata upepo bila mafanikio. Kuona vile jitahada zangu
nikazielekeza kwenye ule mguu wake mmoja sakafuni. Nikajipinda na kumchota Oga
mtama wa nguvu hewani na huwenda tukio lile lilimtia hofu kwani alipiga yowe kama
mtoto. Nikamsubiri atue lakini hayakuwa mahesabu mazuri kwani Oga alitua chini
kama paka kwa miguu yake miwili na mkono mmoja sakafuni huku akinitazama kwa
hasira.
Nilipomuwahi Oga pale chini ili nimmalize akawa ameishtukia dhamira yangu
hivyo akaanza kujiviringisha kama gurudumu la gari akienda huku na kule katika
mtindo wa Ninja. Sasa Oga akawa akinishambulia kwa hila. Akawa akinifikia haraka
na kunishambulia na kabla sijakabiliana naye vizuri anakuwa tayari ameshafika upande
wa pili wa kile chumba. Hali ile ikanipelekea nianze kuona hatari ya kupoteza pambano
lile.
Wakati nikiendelea kujihami mara wazo fulani likanijia. Sikutaka kuendelea
kuruhusu mashambulizi ya namna ile hivyo wakati Oga akinijia tena kwa kasi ya
ajabu nikalivuta shuka la kitanda cha mle ndani kisha kwa mtindo mzuri wa sarakasi
nikamrukia Oga na kumvalisha lile shuka usoni. Lilikuwa shambulizi makini la hila
lililompelekea Oga asiweze kuona na badala yake nguvu zake zote akazielekeza katika
kuliondoa lile shuka.
Oga hakufanikiwa kwani Kufumba na kufumbua akaanguka chini na hapo
mapigo matatu makini ya ngumi zangu kavu yakavunja taya lake la kushoto na
kulipasua vibaya koromeo lake na hapo Oga akapiga yowe kali huku damu nyingi
ikianza kumtoka puani na mdomoni. Nilitulia kidogo kumsubiri Oga afurukute na
nilipomuona kuwa ametulia nikalifungua lile shuka na kumtazama. Oga alikuwa tayari
wa baridi kifo kikiwa tayari kimemchukua.
Sikutaka kuendelea kupoteza muda mle ndani hivyo nikaanza kuitafuta ile bastola
yangu na nilipoipata nikaishindilia ile magazine na kuichomeka kibindoni. Halafu
nikaiokota ile bastola ya Oga na kuikamata vyema mkononi. Wakati nikiwa katika
harakati zile mara nikasikia ule mlango wa kile chumba ikigongwa kwa nje. Niliyatega
vizuri masikio yangu kusikiliza na hapo nikawa na hakika kuwa nje ya chumba kile
mlangoni kulikuwa na mtu akigonga. Mgongaji yule alikuwa makini akigonga kwa
muda na kusikilizia na alipoona kuwa hajibiwi akafungua ule mlango taratibu huku
ameitanguliza mbele bastola yake.
Niliwahi kuuona mdomo wa bastola ile ukichungulia kwani wakati ule nilikuwa
tayari nimeshajibanza nyuma ya ule mlango wa kile chumba. Nikamsubiri yule mtu
aingie mle ndani vizuri na hapo nikaubetua ule mkono wake kwa teke langu makini na
kuipelekea ile bastola imponyoke na kuruka hewani na ilipotua chini ilikuwa mikononi
mwangu.
“Tulia hivyohivyo ngedere mkubwa weh! na ukijitingisha tu nakufyeka”
nikamwambia yule mtu huku nikiufungua vizuri ule mlango wa kile chumba. Yule
mtu akataharuki sana akishangazwa na jinsi mambo yalivyotokea mle ndani huku
akishangazwa na ile maiti ya Oga pale sakafuni. Nilipomchunguza vizuri yule mtu
nikamkumbuka kuwa alikuwa ni mmoja wa wale mabaunsa walinzi wa kule Vampire
Casino walionizuia siku ile wakati nilipotaka kuingia mle ndani bila kitambulisho cha
mwanachama.
“Sogea mbele na mikono yako weka juu” nikamwambia yule mlinzi huku mdomo
wa bastola yangu mkononi ukimtazama kwa uchu. Yule mtu hakuwa na ujanja
isipokuwa kutii maagizo yangu. Hivyo akasogea mbele huku mikono yake ameiweka
juu.
“Wewe ni nani?” nikamuuliza yule mtu nikitaka kupata hakika ya maelezo yake
“Naitwa Beka Mandevu au Mbavu nene!” yule mtu akaniambia kwa woga na
nilipomchunguza nikajua kuwa jina lake bilashaka lilitokana na ukubwa wa misuli ya
umbo lake na ndevu nyingi alizokuwa nazo.
“Unafanya nini humu ndani?” nikamuuliza kwa utulivu.
“Mimi ni mlinzi tu” yule mtu akanijibu kwa hofu.
“Unalinda nini humu ndani?”
“Usalama wa watu na mali zao”
“Yule msichana aliyelala pale chini unamfahamu?” nikamuuliza yule mtu huku
nikimuonesha ile maiti ya Oga kwa bastola yangu pale chini. Yule mtu akanitazama na
kusita lakini aliponiona nikianza kumsogelea akavunja ukimya.
“Ndiyo namfahamu!”
“Unamfahamu kama nani?”
“Malkia wa humu ndani” maelezo yale yakanipelekea nimtazame yule mtu na
kumuona kama mtu aliyechanganyikiwa kwani tangu nizaliwe sikuwahi kusikia
utawala wa malkia katika nchi ya Tanzania.
“Humu ndani mnashughulika na nini?’’ nikamuuliza yule mtu huku nikimtazama
“Mimi sijui chochote,kazi yangu ni ulinzi tu’’ yule mtu akajitetea
“Nahitaji kuonana na Milla Cash ni wapi nitampata humu ndani?’’ swali langu
likampelekea yule mtu ageuke na kunitazama kwa mshangao sana kama niliyeuliza
swali lisilowezekana kuulizika.
“Milla Cash…!’’ yule mtu akaongea kama anayefikiri jambo kisha akaendelea
“Hakuna mtu yoyote humu ndani anayefahamu ni wapi anapoishi Milla Cash
isipokuwa Oga tu ambaye ndiye malkia wa humu ndani” yule mtu akaongea kwa
utulivu na maneno yake yalikuwa na hakika.
“Unaposema malkia wa humu ndani una maanisha nini?”
“Ndiye mwangalizi mkuu wa shughuli zote za humu ndani” yule mtu akaniambia
huku akiongea kwa woga.
“Na wale watu kule ukumbini wanafanya nini?” nikamuuliza yule mtu na mara hii
nilipomtazama shingoni nikaiona ile tatoo ya namba 666. Swali langu likampelekea yule
mtu anitazame tena kwa mshangao.
“Wako kwenye ibada” yule mtu akavunja ukimya na hapo nikaupisha utulivu
kichwani mwangu nikitafakari juu ya hiyo ibada kwani matendo ya mle ndani yalikuwa
yamenichanganya sana.
“Ibada ya namna gani?” nikamuuliza yule mtu hata hivyo hakunijibu na badala
yake akanitazama tu pasipo kusema kitu.
“Na wale watu waliovaa makoti meupe mle vyumbani wanafanya nini?”
“Sifahamu” yule mtu akanijibu kwa mkato
“Na wale mabinti vigoli kule vyumbani je?”
“Sijui chochote mimi ni mlinzi tu humu ndani” yule mtu akajitetea huku
akionekana dhahiri kutaka kunificha mambo fulani yaliyokuwa yakiendelea mle ndani.
“Sasa kama hufahamu kinachoendelea humu ndani unalinda nini?” nikamuuliza
yule mtu kwa hasira hata hivyo hakunijibu.
“Hili jengo linamilikiwa na nani?” nikamuuliza tena.
“Mimi sifahamu chochote!”
Ghafla wakati nikiendelea kumuhoji yule mtu mara mlango wa kile chumba
ukafunguliwa kwa kasi ya ajabu nami sikutaka kusubiri kwani nilifahamu nini ambacho
kingefuatia. Hivyo kufumba na kufumbua yule baunsa akawa ameenea vizuri kwenye
kabari yangu makini ya mkono wa kushoto huku mkono wangu wa kulia ukiwa
umeielekeza ile bastola kichwani kwake. Yule mtu kuona vile akashikwa kwa kihoro
na kuanza kuongea maneno mengi ya hofu huku akinisihi nimuachie.
Mle ndani wakaingia watu wawili warefu walionyoa vipara huku wamevaa suti
nyeusi na miwani myeusi machoni. Nilipowatazama vizuri wale watu nikagundua
kuwa masikioni mwao walikuwa wamevaa vifaa vya mawasiliano vyenye nyaya nyeusi
zilizojisokota na kupotelea kwenye kingo za makoti yao ya suti. Mmoja kati ya wale
watu nilimkumbuka haraka kuwa alikuwa miongoni mwa wale watu waliopata ajali
muda mfupi uliyopita kwenye ile Landcruiser ambaye kwa wakati ule alikuwa ndiye
pekee aliyekuwa na fahamu kabla ya kupoteza fahamu wakati nilipomnasa makofi ya
nguvu usoni.
Yule mtu sasa alikuwa akichechemea kwa mguu mmoja na hapo nikakumbuka
kuwa ulikuwa ni ule mguu wake uliyobanwa wakati wa ile ajali. Wale watu wote
mikononi walikuwa wameshika bastola ambazo haraka waliwahi kuzielekezea kwangu.
“Tupa bastola yako chini na usithubutu kufanya hila yoyote” mmoja kati ya wale
watu walioingia mle ndani kwa pupa akanionya na nilipomtazama nikagundua kuwa
alikuwa akinipigia mahesabu ya kuniondoa kwa risasi. Kwa kuishtukia hila yake yule
baunsa nikamsogeza mbele yangu vizuri na kumfanya kama ngao yangu.
“Nyinyi ndiyo ambao mtaziweka bastola zenu chini vinginevyo mtamponza huyu
ndugu yenu kama mwenzake yule pale chini aliyejidai mkaidi” nikawatahadharisha
wale watu kwa bastola yangu mkononi huku nikiwaelekeza pale chini ilipokuwa
imelala maiti ya Oga. Wale watu wakageuka na kutazama upande ule ilipolala maiti
ya Oga hata hivyo hawakuziondoa bastola zao kwangu. Walipoiona ile maiti ya Oga
wakaingiwa na taharuki.
“Nahesabu mpaka tatu nikimaliza kama bado mtakuwa mkiendelea na msimamo
wenu msije mkanilaumu” nikawatahadharisha wale watu kisha nikaanza kuhesabu.
Kuona vile kabla sijamaliza kuhesabu wale watu wakasalimu amri haraka na kuziweka
bastola zao chini.
“Very good! kwa kufanya uamuzi wa busara kwani nilidhani mngekaidi ili
mjithibitishie wenyewe ukweli wa maneno yangu. Haya rudia nyuma na kuanzia
sasa nyinyi ndiyo mtaongoza mbele tukielekea nje ya hili jengo. Nawatahadharisha
kuwa msijaribu kuleta hila yoyote kwani sitowavumilia” nikawaambia wale watu kwa
msisitizo na hawakuwa na namna zaidi ya kutii amri yangu. Hivyo wale watu wakageuka
nyuma na hapo safari ya kutoka mle ndani ikaanza huku nikiwa nimemdhibiti vilivyo
yule baunsa kwa kabari yangu matata na bastola mkononi.
Tulitembea taratibu na kwa tahadhari hadi pale tulipozifikia zile bastola mbili
za wale watu ambapo niliinama na kuziokota. Baada ya pale safari yetu ikaendelea
tena huku wale jamaa waliovaa suti wakiongoza msafara mbele yetu. Muda mfupi
uliyofuata tukawa tumetoka nje ya kile chumba na hapo tukashika uelekeo wa kurudi
kule tulikotoka na Oga hapo awali.
Tuliivuka korido ya kwanza kisha tukakunja kona na kuingia korido ya pili ambayo
kwa kumbukumbu zangu korido ile ingetupeleka hadi kwenye ule ukumbi niliyowaona
wale watu wakiwa wameketi kwenye vile viti wakimsikiliza mtoa mada mbele yao.
Kitu kilichonishangaza ni kuwa zile kelele za vilio vya watoto wachanga na
vicheko vya wanawake sikuzisikia tena wakati tulipokuwa tukitembea kwenye zile
korido za mle ndani. Wakati huu lile jengo lilikuwa limemezwa na ukimya wa aina
yake na hata tulipofika kwenye ule ukumbi wale watu niliyowaona pale awali wakati
huu hawakuwepo eneo lile. Jambo lile likanishangaza sana hata hivyo sikuwa na mtu
wa kumuuliza.
Hatimaye tukawa tumezifikia zile ngazi za kushukia mle ukumbini na kuanza
kuzipanda huku wale watu wakiwa wameongoza mbele yetu. Baada ya muda mfupi
mara tukawa tumefika juu ya zile ngazi ambapo mbele yake kulikuwa na ule mlango
wa kuingia kwenye kile chumba chenye michoro ya ajabu. Kufikia pale nikawaona
wale jamaa wakisita kuufungua ule mlango na kwa ishara fulani walizopeana kwa siri
nikajua kuwa walikuwa wamepanga kufanya hila dhidi yangu.
Wakati nikitafakari hali ile mara nikamuona yule mtu aliyekuwa akitembea kwa
kuchechemea mbele yangu akiupeleka mkono wake haraka kwenye mfuko wa koti
lake la suti. Nikajua alikuwa akiichukua bastola yake ya ziada ambayo hapo mwanzo
sikuwa nimeshtukia kama alikuwa nayo. Hata hivyo hakupata nafasi ya kuitumia
kwani alipoitoa tu nikamuwahi. Risasi moja niliyoifyatua kwa shabaha ya hali ya juu
ikakifyeka kiganja chake na ile bastola yake ikamponyoka na kuangukia kwenye uwazi
mdogo uliokuwa chini ya zile ngazi na kupotelea chini. Yule mtu akapiga yowe kali
la maumivu akirukaruka kama ndama huku ameshika kifundo cha mkono wake
kilichokuwa kikivuja damu nyingi.
“Fungua mlango au mlidhani kuwa natania!” niliongea kwa hasira huku
nikimtazama yule mwenzake kwa makini na kuzichunguza nyendo zake kwa ukaribu
zaidi. Yule mwenzake kuona vile ikabidi abonyeze vitufe fulani vilivyokuwa kando ya
ule mlango na hapo ule mlango ukafunguka.
Ule mlango ulipofunguka safari yetu ikaendelea huku wale watu wakitangulia
mbele. Lile tukio la shambulio langu la risasi lilikuwa limemuogopesha sana yule
mateka niliyemdhibiti vizuri kwa kabari yangu matata hivyo akawa akitetemeka kwa
hofu huku jasho jepesi likimtoka mwilini. Hali ile ikanifurahisha sana kwani nilikuwa
na kila hakika kuwa yule mtu alikuwa akinigwaya.
Mara tu tulipoingia kwenye kile chumba chenye michoro ya ajabu nikagundua
kuwa wale watu mbele yangu walikuwa tayari wameshaufungua ule mlango mkubwa
mweusi wa kutokea kwenye ile korido hivyo hatukuweka kituo katika kile chumba.
Wale watu mbele yangu walikuwa tayari wameshatoka kwenye kile chumba na kuingia
kwenye ile korido.
Sikutaka kutoka mzimamzima kwenye ile korido hivyo nikambana vizuri yule
mateka wangu kisha nikasogea taratibu na kuchungulia nikipeleleza usalama wa lile
eneo. Hali ya usalama katika korido ile haikuniridhisha kabisa kwani kulikuwa na watu
wapatao kama sita kwenye korido ile upande wa kushoto na wote walikuwa wamevaa
suti nyeusi huku wakiwa na bastola zao mikononi kama wale watu wawili waliotangulia
mbele kwenye msafara wetu. Hisia zikanitanabaisha kuwa wale watu walikuwa
makachero. Hisia za kuzidiwa ujanja zikaanza kunisimanga na hapo nikaanza kuiona
hatari ya kukamatwa mzimamzima endapo nisingepiga akili ya haraka ya kuutegua
mtego mle.
Wakati nikiendelea kuwaza namna ya kujinasua katika hatari ile wale watu wawili
waliokuwa mbele wakiongoza msafara wakaanza kutimua mbio wakielekea upande
wa kushoto wa ile korido walipokuwa na wale makachero wenzao. Wakati tukio lile
likifanyika mara kitu cha kushangaza kikatokea kwenye ile korido.
Kwanza nikasikia sauti kali ya mpasuka wa kioo halafu muda uleule nikamuona
yule kachero niliyemkata kiganja kwa risasi yangu akisombwa kwa nguvu za ajabu
na kutupwa hewani na alipotua chini kwenye sakafu ya ile korido kila mtu eneo lile
akashikwa na taharuki. Kiwiliwili chake kilikuwa kikirukaruka kama kuku ambaye
hajachinjwa vizuri halafu muda uleule kichwa chake kikaanguka chini na kuanza
kujiviringisha kwa kasi kikielekea upande wa kushoto wa ile korido walipokuwa wale
makachero.
Kuona vile wale makachero wakaanza kutimua mbio kwa hofu wakishuka ngazi
kuelekea ghorofa ya chini ya lile jengo. Lilikuwa tukio la kushangaza sana lililoniacha
kwenye taharuki isiyoelezeka. Eneo lote kwenye sakafu ya ile korido lilipotokea lile
tukio la kushangaza likawa limetapakaa damu.
Kwa kweli nilishtushwa sana na tukio lile hata hivyo sikumuachia yule mateka
wangu wala kutimua mbio ingawa sasa nilikuwa makini sana nikichungulia tena
kwenye ule upande niliposikia ile sauti kali ya mpasuko wa kioo kwenye ile korido.
Nilikuwa sahihi kwani kioo cha dirisha kubwa lililokuwa mwisho wa ile korido
kwenye lile jengo chote kilikuwa kimechanguliwa vibaya na kuanguka chini kwenye
sakafu ya ile korido na kutawanyika kila mahali. Nilipoupisha utulivu kichwani
mwangu haraka wazo fulani likanijia na kunitanabaisha kuwa yale hayakuwa mauzauza
isipokuwa lilikuwa tukio makini lenye uhalisia. Nilipochungulia tena kwenye ile korido
mara nikakiona kivuli cha mtu fulani kikipotelea kwenye dirisha la chumba cha jengo
lingine la ghorofa lililokuwa kando ya lile jengo letu likitenganishwa kwa barabara ya
lami. Kitendo kile kikapelekea baridi kali ya ghafla isambae taratibu moyoni mwangu.
Hisia zangu zikanitanabaisha kuwa ile ilikuwa ni kazi makini ya mdunguaji.
Hisia zile zikanipelekea nichungulie tena kwenye lile dirisha hata hivyo sikumuona
mtu yeyote na hapo nikajua kuwa mdunguaji yule hatari alikuwa tayari ameshatoweka
eneo lile. Kwa kweli sikutaka kuendelea kusubiri eneo lile kwani lile tukio lilikuwa
limenipotezea utulivu kwa kiasi kikubwa kichwani mwangu. Wale makachero
sasa walikuwa wamepotelea kwenye zile ngazi za kushukia ghorofa ya chini ya
lile jengo. Hivyo nikambana vizuri yule mateka wangu na hapo nikaanza kusota
kimgongomgongo ukutani huku yule mateka wangu nikimuweka mbele yangu kama
ngao.
Baada ya muda mfupi nikawa nimefika kwenye kile chumba cha lifti cha lile
jengo. Nikabonyeza kitufe cha lifti na chumba kile cha lifti kilipofika na mlango wake
kufunguka nikapotelea mle ndani huku yule mateka wangu nikiwa nimemdhibiti
kikamilifu. Muda mfupi mara baada ya kuingia kwenye kile chumba cha lifti tukaanza
safari ya kushuka chini ya lile jengo huku ndani ya chumba kile tukiwa wawili tu yaani
mimi na yule mateka wangu.
Mara tu kile chumba cha lifti kilipoanza kushuka chini ya lile jengo hisia zangu
zikanihamasisha kuwa nigeuke na kuangalia upande wa pili kwenye lile jengo la
ghorofa ambalo yule mdunguaji hatari alikuwa amelitumia kufanya shambulizi la
hatari kwa yule kachero wa usalama.
Katika lile jengo la ghorofa lililokuwa kando ya lile jengo letu nikakiona chumba
kingine cha lifti kilichotengenezwa kwa vioo vinavyomuwezesha mtu yeyote kuona
mle ndani bila shida yoyote. Chumba kile cha lifti sasa kilikuwa kikishuka chini ya
lile jengo. Hali ile ikanivutia na hapo nikayasimamisha macho yangu nikitazama kwa
makini ndani ya kile chumba cha lifti kilichokuwa kikishuka chini ya lile jengo.
Taswira nzuri ikajengeka machoni mwangu na tafsiri nzuri iliyofanyika katika
ubongo wangu ikanitanabaisha kuwa ndani ya kile chumba cha lifti kulikuwa na mtu.
Koo langu likakauka ghafla pale nilipogundua kuwa yule mtu aliyekuwa ndani ya
chumba kile cha lifti alikuwa ndiye yule dada aliyenitoroka kwenye lile jengo la Rupture
& Capture.
Yule dada alikuwa amevaa suruali ya jeans,viatu vyenye visigino virefu miguuni,blauzi
ya rangi ya hudhurungi na kichwani alikuwa amevaa kofia ya Sombrero na miwani
myeusi ya jua. Kama ambaye alikuwa ameshtukia kuwa nilikuwa nikimtazama naye
pia akageuka na kunitazama huku begi lake jeusi na jembamba likitengeneza kichuguu
kidogo nyuma ya mgongo wake.
Alikuwa ndiye yule mdunguaji hatari na ingawa mdunguaji yule alikuwa amevaa
miwani myeusi lakini kitendo kile cha yeye kugeuka na kutazama kwenye kile chumba
chetu cha lifti kikanipa hakika kuwa alikuwa akinitazama mimi. Nilitulia nikijaribu
kuvuta picha kuwa mdunguaji yule ungekuwa akiwaza nini juu yangu lakini hilo
lilishindikana kwani hakuna binadamu aliyejaliwa uwezo wa kutambua mwenziwe
anawaza nini. Hivyo tuliendelea kutazamana kwenye vyumba vile vya lifti vilivyokuwa
vikishuka chini ya majengo yale ya ghorofa taratibu huku mawazo mengi yakipita
kichwani mwangu. Kwa kweli nilishindwa kabisa kuelewa kwanini mdunguaji yule
hatari alikuwa akiendeleza ubabe wake kwa kuwadungua watu namna ile.
Mawazo mengi yaliyokuwa yakipita kichwani mwangu wakati tukishuka kwenye
kile chumba cha lifti ghafla yakakatishwa baada ya kile chumba cha lifti tulichopanda
kugota chini ya lile jengo kwenye ghorofa ya mwisho ama groundfloor na hapo
nikaikumbuka hatari iliyokuwa mbele yangu. Hivyo nikambana vizuri yule mateka
wangu kwa kabari matata huku bastola yangu nikiwa nimeikamata vyema mkononi.
Mlango wa kile chumba chetu cha lifti ulipofunguka sikutaka kuharakisha kutoka
nje na yule mateka wangu na badala yake nilisogea taratibu na chungulia nje ya kile
chumba cha lifti kwanza. Nikaupisha utulivu kichwani mwangu huku nikiyatembeza
macho yangu taratibu kule nje na kwa kweli hali ya usalama ya eneo lile ilinipa hadhari.
Eneo lote chini ya lile jengo lilikuwa limezingirwa na makachero wa usalama
wa taifa huku wakiwa katika suti zao nadhifu na bunduki zao mikononi. Baadhi ya
makachero wale niliwaona wakiwasiliana kupitia vinasa sauti vilivyokuwa katika kola
za makoti yao ya suti. Wale makachero walikuwa wamejipanga katika maeneo tofauti.
Wengine walikuwa kwenye vipenyo vya jengo lile na wengine walikuwa wamejibanza
kwenye kona za magari yaliyoegeshwa pale nje. Kwa hesabu ya haraka ni kuwa mitutu
ya bunduki zisizopungua kumi na tano ilikuwa imeelekezwa kwenye kile chumba cha
lifti nilipokuwa mimi na mateka wangu.
Hofu ikaanza kujenga taratibu moyoni mwangu huku nikihisi kushikwa na
kigugumizi cha kufanya maamuzi sahihi na ya haraka. Nikiwa katika hali ile nikaanza
kufikiria kuwa nirudi mle ndani kisha niiamuru ile lifti iturudishe kule juu ya lile jengo
tulipotoka mimi na mateka wangu huku nikiamini kuwa nikiwa kule ningepata wazo
zuri la kujinasua kutoka wale makachero.
Lakini baada ya kuyapa utulivu mawazo yangu wazo lile nikaliweka kando pale
nilipowaza kuwa uamuzi wa kurudi juu ya lile jengo ungeweza kuwavuta zaidi wale
makachero na hivyo kujipanga kikamilifu hali ambayo ingepunguza uwezekano
mkubwa wa kutoroka kwangu kwenye lile jengo. Hivyo njia sahihi niliyoiona ilikuwa
ni kukabiliana na wale makachero ana kwa ana huku nikiwa tayari kukabiliana na
lolote ambalo lingetokea.
Hivyo hatimaye nikamdhibiti vizuri yule mateka wangu na hapo tukaanza taratibu
kusogea tukitoka nje ya kile chumba cha lifti. Halaiki ya mashuhuda waliokuwa
wakiongezeka eneo lile ikazidi kuongeza uzito wa tukio lile tofauti na mimi nilivyokuwa
nikilichukulia. Hata hivyo roho yangu ilikuwa ni kitu cha thamani zaidi.
Kile kitendo cha mimi na yule mateka wangu kutoka nje ya kile chumba cha lifti
kikawapelekea wale makachero wazidi kujipanga. Nikaikamata vizuri bastola yangu
kiganjani huku yule mateka wangu akiwa ameenea vyema kwenye kabari yangu
matata ya shingo na hapo tukaanza kutoka nje. Tulipotoka nje kile chumba cha lifti
mara nikasikia tangazo kutoka kwenye spika ya kirushia matangazo iliyokuwa juu ya
Landcruiser moja iliyokuwa eneo lile.
“Tafadhali! tupa silaha yako chini na nyoosha mikono juu. Hii ni amri kutoka
kwa polisi vinginevyo tuna haki ya kukupiga risasi endapo utakaidi” ile sauti kutoka
kwenye ile spika ikahanikiza eneo lile na sikuwa na wasiwasi kuwa mimi ndiye
niliyekuwa mlengwa. Hata hivyo sikusalimu amri kwani ule ulikuwa ni mchezo wa
kufa na kupona.
“Tupa silaha yako chini na nyoosha mikono yako juu tafadhali!” ile sauti ikaendelea
kunionya wakati nikiendelea kutembea taratibu na mateka wangu huku ile bastola
yangu mkononi nikiwa nimeielekeza kichwani kwa yule mateka wangu.
Nilipoyatembeza macho yangu tena eneo lile nikagundua kuwa wafanyakazi
waliokuwa kwenye lile jengo na watu wengine waliokuwa katika majengo ya ghorofa
yaliyokuwa jirani na pale walikuwa wametoka nje ya ofisi zao kushuhudia tukio lile
la aina yake. Akili yangu ikafanya kazi haraka kwani nilifahamu fika kuwa ukimya
usingenifaa kitu hivyo ile amri walionipa wale makechero nikaigeuzia kwao.
“Wekeni silaha zenu chini na mrudi hatua tano nyuma vinginevyo uhai wa huyu
mtu utadaiwa kwenu” nikafoka kwa hasira nikiwaambia wale watu.
“Nitahesabu mpaka tatu na mkiendelea kukaidi amri yangu msinilaumu”
nikaongea kwa sauti huku nikiwa na hakika kuwa mtu yoyote ambaye angekuwa eneo
lile angenisikia vizuri.
“Moja…” nikaanza kuhesabu “Mbili…” nilipokuwa mbioni kumaliza kuhesabu
mara nikasikia sauti nzito kutoka upande wa kushoto.
“Okay!…Okay! vijana wangu wekeni silaha zenu chini huwenda huyu mwehu ana
jambo zuri la kutuambia”
Nikageuka na kutazama upande ule ile sauti alipokuwa ikitokea na mara hii
nikamuona mwanaume mwenye umri wa kukadirika kati ya miaka arobaini hadi
arobaini na tano. Mwanaume mrefu na mweusi lakini mwenye umbo imara lililojificha
ndani ya suti yake ya rangi ya samawati. Macho makubwa na makali ya mwanaume
yule yakanitazama katika uso wake mrefu kiasi wenye pua ndefu na pana huku mdomo
wake ukizungukwa kwa ndevu zilizokatiwa vizuri kuuzunguka.
Misuli iliyokaza usoni kwa mwanaume yule ilikuwa ni ishara tosha kuwa yule mtu
alikuwa amekasirishwa sana na tulio lile. Nikamtazama yule mtu kwa makini na hapo
nikagundua kuwa mkono wake mmoja alikuwa ameutia kwenye mfuko wa suruali
yake na ule mwingine alikuwa ameshika bastola na hivyo kuyapelekea mabega yake
yanye umbo la mraba yazidi kutuna kama bondia.
“Wehu ni nyinyi mnaosababisha shughuli za watu zisiendelea kwa tukio lisilo na
maana” nikafoka kwa sauti huku taratibu nikisogea na yule mateka wangu kuelekea
kule nilipokuwa nimeegesha gari langu chini ya lile jengo.
“Okay! muachie basi huyo mateka sisi tumeshaweka silaha zetu chini” yule mtu
akafoka.
“Tupa chini bastola yako!” nikamwambia yule kachero aliyeonekana kuwa ndiye
kiongozi wao.
“Hivi mnadhani nyinyi ni watu wa kuaminika kirahisirahisi?. Nimesema wekeni
silaha zenu chini na mrudi hatua tano nyuma. Hii ni amri na siyo ombi na yeyote
atakayejaribu kuleta hila basi mjue kuwa nyinyi ndiyo mtakaowajibika na akifo cha
huyu mtu” nikawaonya wale makachero huku macho yamenitoka kwa msisitizo
katika hali ya kuhakikisha kuwa amri yangu inatekelezwa.
“Okay!...” yule kachero kuona vile akasalimu amri huku akiiweka bastola yake
chini na kitendo cha yeye kurudi nyuma baada ya kuiweka bastola yake chini na kurudi
hatua tano nyuma kikawapelekea na wale makachero wengine watii amri na kuanza
kurudi nyuma.
“Good!” nikaongea kwa msisitizo huku nikiwa napiga mahesabu ya kawaacha
wale makachero kwenye mataa. Hivyo nikayatembeza macho yangu taratibu na kwa
makini nikitazama eneo lile na kwa kufanya vile nikagundua kuwa umati wa watu eneo
lile ulikuwa umeongezeka mara mbili zaidi ya pale awali na hali ile ikanivutia sana.
Nikayapeleka macho yangu kutazama tena kule lilipokuwa gari langu na hapo
wasiwasi ukaniingia baada ya kuliona gari langu kuwa lilikuwa limetengwa kwani
yale magari mengine yaliyokuwa jirani na gari langu hapo awali hayakuwepo. Nilihisi
kuwa kulikuwa na hila fulani iliyokuwa ikitaka kuchwezwa eneo lile hata hivyo sikusita
kuendelea mbele na safari yangu huku yule mateka wangu nikiwa nimemdhibiti
kikamilifu mkononi mwangu. Nikageuka tena na kumtazama yule kachero mkubwa
na kumwambia
“Naondoka na huyu mateka wangu na asijaribu mtu yoyote kunifuata!”
nikafoka kwa sauti nikitaka kuhakikisha kuwa mtu aliyekuwa eneo lile ananisikia
vizuri. Yule kachero akanisikiliza kwa makini huku akiumba tabasamu jepesi usoni
mwake. Nilipomtazama usoni kwa haraka nikagundua kuwa kulikuwa na kitu hatari
kilichokuwa kimejificha nyuma ya tabasamu lake. Hata hivyo ule haukuwa muda wa
kuendelea kutafakari.
Muda mfupi baadaye nikawa nimelifikia gari langu kwenye yale maegesho ya magari
ya lile jengo huku kijasho chepesi kikiwa kinanitoka kwenye sehemu mbalimbali za
mwili wangu. Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakienda mbio sana kila nilipokuwa
nikitafakari kitu ambacho kingefuatia baada ya pale. Hata ule mkono wangu ulioshika
bastola nao kwa mbali niliuhisi kuwa ulikuwa mbioni kulowana kwa jasho la hofu.
Wakati nilipokuwa nikijiandaa kufungua mlango wa gari hisia zangu
zikanitahadharisha kuwa kabla ya kufungua mlango ule nilipaswa kugeuke na kutazama
kwanza kule kwenye kile chumba cha lifti alichokuwa mdunguaji. Hivyo nikayapeleka
macho yangu haraka kutazama upande wa lile jengo la ghorofa kulipokuwa na kile
chumba cha lifti. Kwa kufanya vile macho yangu yakakutana na macho ya mdunguaji
huku akiwa amevua miwani yake na kuishika mkononi na hapo nikaweza kukiona
kilichokuwa kimefichika ndani ya macho yale. Jambo la hatari! hisia zangu zikaniambia
na hapo akili yangu ikaanza kufanya kazi haraka.
Hivyo kufumba na kufumbua kwa nguvu zangu zote nikamsukuma yule mateka
wangu mbali na lile gari langu huku nikijirusha upande wa pili. Muda uleule sauti ya
kishindo kikubwa cha mlipuko ikazizima eneo lile. Nililiona lile gari langu likirushwa
hewani kama kiberiti na likiwa kule angani mlipuko mwingine mkubwa ukasikika
huku lile gari likichanguka vipandevipande. Vipande vile vitakawanyika angani na kwa
kuwa madhara yake nilikuwa nikiyafahamu vizuri hivyo nikawahi kujiviringisha na
kupotelea chini ya gari moja lililokuwa jirani na eneo lile. Nilichokisikia baada ya pale
ni kelele za hofu zikihanikiza kutoka kwa umati mkubwa wa watu waliokuwa eneo lile
kushuhudia hatima yangu.
Nikiwa chini ya lile gari niliweza kuiona miguu ya watu wengi waliokuwa wakitimua
mbio huku kila mtu akishika uelekeo wake katika hali ya kujihakikisha usalama wa
maisha yake. Sikumuhurumia mtu yeyote kwani tatizo moja la watanzania wengi ni
kupenda kushuhudia hatari hata kama mazingira ya kufanya hivyo hayaruhusu.
“Ile ilikuwa nafasi yangu pekee ya kutoweka eneo lile” niliwaza kisha nikajiviringisha
na kutokea upande wa pili wa uvungu wa lile gari. Nikiwa pale chini nilitazama kule
kwenye kile chumba cha lifti kwenye lile jengo la ghorofa lililokuwa upande wa pili
wa ile barabara. Kile chumba cha lifti kilikuwa tupu na yule mdunguaji hakuwepo.
Tukio lile likanishangaza sana na sikutaka kuendelea kujilaza pale chini na kutafakari
hivyo haraka nikasimama na kuanza kutimua mbio nikijichanganya kwenye lile kundi
la watu waliokuwa wakilikimbia eneo lile.
Kachero mmoja alikuwa ameniona wakati nikitimua mbio kulitoroka eneo lakini
hakuweza kunifikia kwani mwendo wangu ulikuwa siyo wa masihara.
Kitu kilichozidi kunifurahisha zaidi ni kuwa hata watu waliokuwa wamepanda
kwenye mabasi ya daladala yaliyokuwa yakikatisha kwenye barabara ya eneo lile nao
walivyoona vile wakaingiwa na hofu na kuanza kushuka chini wakitimua mbio huku
wengine wakitokea milangoni na wengine madirishani. Baadhi ya watu walianguka
chini wakati wakitoka kwenye daladala za eneo lile hususan akina mama na watoto.
Wakati nikiwapita wale watu na kuendelea kutimua mbio kulitoroka eneo lile
bastola yangu nilikuwa tayari nimeichimbia mafichoni. Bado nilikuwa salama na kazindiyo kwanza ilikuwa imeanza. NILIKUWA NAJIDANGANYA
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…