Nakumbuja kusoma stori hii kitambo,sina kumbukumbu sana kwani nilikuwa darasa la tano au la sita.Nachokumbuka,its a very good story to the end!
I will try to find the book n write to you when I can!
Katika chumba kimoja cha ghorofa ya pili katika jengo linalotizamana na Tupetupe Hotel vijana watatu waliketi wakimung'unya kuku wa kuoka na chipsi na kuteremshia kwa vinywaji.
Chox aliketi kando ya dirisha, mara kwa mara akichungulia nje, hasa kwenye uwanja wa kuegesha magari na mlango wa mbele wa Tupetupe Hotel. Fensy aliketi mezani kando ya chupa za vinywaji na vifurushi vya kuku na chipsi. Chiko yeye aliketi kitandani, kando yake pakiwa na darubini.
Chiko akasema, "Kwa hiyo tumeelewana, Chox?"
"Manta hofu." Alijibu Chox, akivunja mifupa. Mbele yake palikuwa na kichuguu cha mifupa cha kudhibitisha aliwaacha mbali wenzie. Na alikuwa na mwili kuliko wenzake. Akasema, "Hata ukitaka niwe Profesa nitakuwa Profesa. Na utashangaa."
"Hapana, nataka uwe daktari wa kawaida tu."
"No sweat." Akatema mifupa na kuzidi kukikuza kichuguu chake. Akachungulia nje, akisema, "Lakini una hakika yule kijana atarudi tena hapa Tupetupe?"
"Sina hakika, nnasikia tu." Alijibu Chiko. Hatufahamu ni nini Dikwe ameloloma. Alikuwa anafahamu kuwa mimi na Fensy tuna vyumba Tupetupe."
"Kama atarudi kwa nia hiyo, atataka kuvipekua vyumba vyenu."
"Hataambulia kitu. Nimempigia simu Osiga na kumwambia avisafishe. Amenihakikishia vitapakwa na rangi upya."
Chox akatoa guno la kuridhika na kuchukua paja jingine. Chiko akamuuliza, "Lakini ukimwona utamtambua?"
"Hapana shaka." Chox alijibu, Akachungulia nje na kustuka. "Yulee! Gari lake lilee!"
Chiko na Fensy wakakurupuka na kukimbilia dirishani. Wakaliona Bentley likiegeshwa. Chiko akaipeleka darubini usoni. Akawaona waziwazi Denny na Bessy wakitoka garini. Akauliza, "Ndiye?"
"Ndiye." Alijibu Chox baada ya kuwatazama kwa darubini. "Yuko na yule msichana nuksi, Kachero Inspekta Bessy."
Chiko akaichukua tena darubini. Akasema, "Ni mtoto mdogo kabisa. Wote wawili ni watoto wadogo kabisa. Natamani hata niwadungue hapo hapo walipo." Alisema Fensy.
"Acha uchizi, hapa noma." Chiko akadakia.
"Nafahamu hapa hapafai. Naifurahisha nafsi yangu tu. Lakini ingekuwa rahisi kabisa,"
"Umbali huu ungehitaji kitu kikubwa zaidi kuliko .36 yako."
"Nafahamu, Chi, nafahamu." Alisema Fensy, akiirudisha bastola yake kwenye soksi. "Nilikuwa naifurahisha nafsi yangu tu."
"Naam," Alisema Chox, akiwaangalia Denny na Bessy wakiingia Tupetupe. "Dikwe ameimba kama chiriku."
*************************************
Mchana Tupetupe Hotel ilikuwa na sura tofauti kabisa na ile ya usiku. Palikuwa kimya na pamepooza. Bessy akiongoza, yeye na Denny walienda moja kwa moja kwenye mlago ulioandikwa MENEJA. Bila ya kubisha, Bessy akaufungua wakaingia ndani. Ilikuwa ofisi finyu yenye meza ndogo na viti viwili mbele yake. Mezani palikuwa na simu na kibao chenye jina la mwenye ofisi hiyo - Konga Osiga.
Mwenyewe alikuwa ameketi nyuma ya meza, akisoma gezeti. Alikuwa mtu mwembamba, mwenye sura ya kitumbili, aliyevaa suti iliyohitaji kupigwa pasi. Akainuka haraka, akisema, "Karibu Inspekta Bessy." Huku akichanua tabasamu la kizandiki.
Bila kuketi wala kusalimu, Bessy akasema, "Tunawataka Chiko na Fensy. Wako vyumba gani?"
"Bahati mbaya Inspekta, wameshahama." Alisema Osiga kama mwenye masikitiko ya kweli.
"Tangu lini?" Denny aliuliza.
"Jana afande. Jana mchana."
"Wamehamia wapi?"
"Ntajuaje, afande? Sikuwa na uhusiano wowote nao zaidi ya kuwa wapangaji wangu."
Bessy akasema, "Unajua Osiga, utasababisha hoteli ifungwe."
"Kwa nini Inspekta? Hatuna kosa lolote. Hatudaiwi chochote na serikali. Tunalipa kodi zetu kama kawaida."
"Unadhani kuhifadhi wakora wauaji si makosa?"
"Huo ni uonezi Inspekta. Tutamjuaje mtu kama ni mkora au padri? Hawana alama usoni."
"Unataka kuniambia kuwa hukujua kuwa Chiko na Fensy ni wakora?"
"Naapa Inspekta, sikujua. Nipe Biblia nishike kama huniamini."
"Kama vile hukujua kuwa Hoza alikuwa mkora na pusha!"
"Sikujua, Inspekta, naapa. Nipe msahafu..." Denny akamkatiza. "Nitapenda kuviona vyumba vyao."
"Twende mkavione kama itasaidia. Vinapakwa rangi."
"Kitu gani?" Bessy alimaka.
"Vinapakwa rangi, Inspekta. Tunaikarabati hoteli yetu."
"Kwa kuanzia kwenye vyumba vya hao wakora?"
"Ndivyo vitupu, afande. Hatuwezi kupaka rangi vyumba vyenye watu, eti, tunaweza?"
Kengele ya simu ikalia. Osiga akaomba radhi, Akasema, "Tupetupe Hotel hapa." Akasikiliza kidogo kisha akasema, "Ndiyo, Inspekta Bessy yupo hapa. Ndiyo, pamoja na mwenzake. Nasikitika jina lake silijui. Naam, unataka kuzungumza naye? Sawa."
Osiga akamtazama Denny, akasema, "Ni yako afande." Denny akamtupia Bessy jicho la mshangao kisha akaupokea mkono wa simu. Akasema,"Hallo!" Sauti nzito tulivu ikamwambia, "Hujambo, School Boy?"
"Ni nani wewe!" Denny akauliza.
"Chiko." Denny akamtupia tena jicho Bessy ambaye alibetua kichwa, ishara iliashiria aliweza kusikia anazungumza na nani.
Chiko akaendelea, "Nasikia unanitafuta. Ni nani wewe?"
"Komandoo Luteni Dennis Raymond Makete."
"Oh, ni komandoo!" Chiko alibeza. "Na inaelekea una uhusiano na yule mzee aliyegongwa na gari jana asubuhi."
"Ni babangu mzazi mliyemgonga, na mnayetaka kumuua kule hospitalini."
"Sikiza, babako amegongwa kwa bahati mbaya. Aliyemgonga anasikitika na yuko tayari kulipa fidia."
"Kiasi gani?"
"Tamka mwenyewe. Huyo bwana ni tajiri sana. Hana tatizo la pesa."
"Nataka kichwa chake."
"Kitu gani?"
"Nataka kichwa chake. Hiyo ndiyo bei yangu.Nipatie kichwa cha Kassim Hashir na ugomvi unakuwa umekwisha."
"Ndiye nani huyo Kassim Hashir?"
"Ndiye aliyemgonga babangu."
"Umekosea, School Boy. Huyo bwana haitwi hivyo."
"Anaitwaje?"
"Potelea mbali anaitwaje. Wewe sema bei yako."
"Nimekutajia bei yangu. Ni kichwa chake."
"Wewe mtoto chizi nini? Kichwa chake kwa sababu ya kumgonga babako kwa bahati mbaya? Tena hakuafa!"
"Kwa manufaa yako, hakumgonga kwa bahati mbaya. Isitoshe, hilo ni dogo sana , silo hasa ninalomtakia."
"Kumbe unamtakia nini?"
"Analijua yeye."
"Sikiza School Boy. Wewe ni mdoga sana kwa kufa. Mimi si Dikwe au Hoza."
"Unadhani mimi ndiye Kikoti au Bob?"
"Shauri yako, umeshaonywa."
"Unataka tuteue kilingo?"
"Ukiwa peke yako au na nusu ya jeshi la polisi likiwa nyuma yako."
"Peke yangu. Wewe ukiwa na mwenzako Fensy."
"Yaelekea fal@ Dikwe kakupakia upuuzi wa kutosha."
"Wa kutosha, tena kilingo na muda mchague wenyewe."
"Kiwanda cha zamani sukari, leo saa kumi na moja jioni."
*******************************************
Wakinywa chai ya saa kumi nyumbani kwa Bessy, msichana huyo akasema, "Hivi kweli Denny hutaki kuniambia Chiko amesema nini?"
"Nakwambia hakusema lolote la maana." Alijibu Denny. "Kazungumza upuuzi mtupu."
"Nataka kuusikia huo upuuzi."
"Kwamba Kassim Hashir yuko tayari kunilipa fidia kubwa kwa kumgonga babangu."
"Kiasi gani?"
"Nitakacho."
"Ukamwambiaje?"
"Nataka kichwa chake."
"Upuuzi mwingine?"
"Akatishia kuwa ataniua, akajigamba kuwa yeye si Hoza au Dikwe."
"Na kuhusu kilingo?"
Dennis akasita kujibu. Bessy akakaza sauti. "Denny mmepatana kukabiliana!"
"Ndiyo."
"Wapi na saa ngapi?"
"Mahali fulani muda fulani."
"Denny lazima nifahamu."
"Aakk. Siwezi kukwambia hilo. Si sasa hivi, anyway. Utavuruga kila kitu. Utataka kulipeleka jeshi zima mahali hapo."
"Lakini Denny hatuwezi kwenda peke yetu. Wanaweza wakawa wengi."
"Hatuendi sote. Nakwenda peke yangu."
"Una wazimu wewe, Denny! Je, wakiwa watano? Je, wakiwa kumi?"
"Shauri yao, watajijua."
"Unadhani nitakuacha ukawe bango la shabaha? Una wazimu! Akina Chiko ni wehu, ni watu hatari. Na wewe huna silaha yoyote. Huna hata manati!" Denny hakujibu.
Bessy akakiweka kikombe chake mezani akainuka. Akazunguka nyuma ya Denny na kumshika bega. Baada ya kumkanda kidogo, akainama na kumbusu shavuni. Akasema kwa sauti tulivu sana. "Denny tafadhali nisikilize."
"Bessy, hakuna njia nyingine." Denny alisema kwa uchungu. "Nimemwaidi Chiko kwenda peke yangu." Msichana akazunguka na kumtizama Denny usoni kwa macho makali. "Ahadi kwa jambazi? Ina thamani gani? You can bet bloody ass yeye hatakuwa peke yake."
"Hatakuwa peke yake. Nimemwambia awe pamoja na Fensy."
"Na bado unataka kuhatarisha maisha yako? Na pengine wasiwe wawili tu. Pengine wawe kumi! Pengine wawe wakora wote wa jiji hili lote lililolaaniwa!"
Dennis akabaki kimya.
Bessy akapumua na kusema kwa sauti yake ya kawaida, "Kama ungekuwa na busara, Denny wala usiingeenda wewe mwenyewe. Wewe umeshamaliza kazi yako. Ungewaachia polisi wakapambane na hao wehu."
"Lakini kwa nini hutaki niende?" Denny aliuliza kwa karaha, "Huna imani na mimi?"
"Hapana."
"Kumbe?"
"Sitaki uumie."
"Kwa nini? Mimi ni mwanajeshi."
"Kwa sababu... kwa sababu... ooh, mpaka nigeuze wimbo niimbe?"
"Ndiyo geuza wimbo uimbe."
"Aah, haya! Kwa sababu umeshaanza kuniingia moyoni kharamu we!"
Taratibu Denny akakiweka chini kikombe cha chai. Taratibu akainuka, akasimama wakatizamana, hakuna aliye pepesa jicho. Hatimaye Denny akauliza, "Bessy , unasema kweli au unanitania?"
"You idiot! Jambo kama hilo ni la kudhihaki?"
Kufumba na kufumbua wakajikuta wamevaana.