Riwaya: Mteule

magnifico

JF-Expert Member
Joined
Jan 14, 2013
Posts
11,075
Reaction score
24,634
MTEULE

UTANGULIZI

Mfalme Efroni alikuwa mtawala wa nchi ya Nahori. Mfalme huyu alimuoa binti wa mfugaji aliyeitwa Raheli na kujaaliwa kupata watoto kumi na wawili. Wote wa kike. Aliipenda sana familia yake. Mfalme huyu alikuwa mtawala mwenye huruma, hekima, busara na upendo. Uso wake ukitawaliwa na tabasamu wakati wote. Wakazi wote wa Nahori wakampenda.

Nahori ilipatikana ulimwengu wa mbali kabisa kutoka ule wa kibinadamu. Japo wakazi wake walifanana kila kitu na binadamu wa kawaida lakini wao walikuwa na kitu cha ziada. Kila mmoja alizaliwa akiwa na kipawa chake, wakiwa na uwezo na maarifa makubwa kupita wanadamu wa kawaida. Nahori ilizungukwa na milima mikubwa kwa midogo yenye ukijani wa kuvutia.

Na iliinasemekana pia ni katika ufalme huu kuna njia za siri za kuelekea ulimwengu mwingine. Njia hizi ziliitwa Njia za Mashimo ya giza. Hakuna aliyekuwa na uhakika wa jambo hili wala kuthibitisha habari hizi, sio vijana sio wazee. Nazo zikabaki kuwa hadithi za usiku wajukuu wakiwa wameuzunguka moto na babu akisimulia kwa utuo hadithi hizi kwa kadri atavyoona inavutia. Hakika ilipendeza.

Mashariki ya mbali mwa ufalme huu wa Nahori ilipatikana nchi ya Shekemu. Wamekuwa mahasibu wakubwa kwa miongo mingi sana. Na Inasadikika ni katika ufalme huu wa mbali kilipatikana kisima cha Shetani. Ukiyanywa maji ya kisima hiki utu hukutoka na nguvu za kishetani zinaishi ndani yako. Na hapo utajazwa tamaa ya kupata mali hata madaraka makubwa, huku ukitamani kubwaga damu pasi na sababu ya msingi. Nazo kama zilivyo habari za Njia za mashimo ya giza ndivyo hata habari hii ilivyokuwa. Hadithi njoo, utamu kolea.

Basi safari moja watu wa ufalme wa Shekemu huko inakosadikiwa kinapatikana kisima cha shetani walifanya uvamizi katika ardhi ya ufalme wa Nahori. Huu ulikuwa ni uvamizi wa pili kufanywa na watu wa Shekemu. Uvamizi wa kwanza waliufanya wakati Mfalme Efroni anarithi ufalme kutoka kwa baba yake. Na inasemekana lengo ilikuwa wapate kuteka kisima cha maji ya Maajabu.

Kisima hiki kilipatikana katika ufalme huu wa Nahori kikilindwa usiku na mchana na mashujaa waliofunzwa mafunzo ya kimapigano ya kivita ya hali ya juu kabisa pamoja na nguvu zao za asili. Hata sisimizi hakuthubutu kakatiza eneo lile. Maji haya hupewa mteule wa kiti cha ufalme tu, hii humpa uwezo na nguvu zaidi ya kiumbe chochote kile katika ulimwengu wao wote. Na ambaye sio mteule akijitia kiherehere kuthubutu kuyagusa maji yale huunguzwa vibaya mno hata akageuka majivu. Naam, kibali kilitoka kwa Wahenga wa Nahori.

Mara hii hapakuwa na budi kuupiga ufalme ule hata kwenye ardhi yao ya Shekemu. Mfalme Efroni aliongoza jeshi lake kwa kushirikiana na Jemedari wake mtiifu aliyeitwa Bethueli. Walishinda vita vile huku mashujaa wote wa ufalme ule wa Shekemu wakiuwawa sambamba na mfalme wao.

Na ndipo Jemedari Bethueli alijaribu kumshawishi mfalme kuhusu uwepo wa kisima cha shetani katika nchi ile. Lakini mfalme alikemea vikali kuhusu jambo lile na kumtaka asije akajaribu kuliongelea tena jambo hilo. Akatii amri.

Hapo Mfalme akaamuru tena hakuna kuua raia yoyote yule maana kisasi chao kilikuwa juu ya wale mashujaa na mfalme wao ambao wameuwawa tayari. Wakatii amri wote. Wakaianza safari kurudi Nahori.
********

Wiki kadhaa mbele Mfalme Efroni alipata taarifa kutoka kwa Jemedari Bethueli kuwa watu wa ufalme ule wa Shekemu wameuwawa wote kinyama. Hakuna kiumbe chenye uhai kimebaki hata miti yote imekauka kana kwamba eneo lile ni jangwa wakati ni masika. Mfalme akashtuka sana akasema, “kuna mmoja wa wale watu wa Shekemu katumia maji ya kisima cha shetani, hii ni hatari.”.

Jemedari alishtuka sana hata akauliza kwa kiwewe, “Sasa itakuaje? Vipi tukivamiwa?”, aliuliza mfululizo huku macho yakiwa yamemtoka pima. “Hatuwezi kuvamiwa, yoyote aliyokunywa maji yale anaijua nguvu yangu vyema kabisa, maji ya maajabu yapo ndani yangu.”, aliongea Mfalme Efroni kwa kujiamini kabisa hata ile hofu iliyokuwa machoni pa Jemedari Bethueli ikayeyuka huku akishusha pumzi za matumaini.
***************

Miaka mingi ikapita na mfalme Efroni umri ukazidi kumtupa mkono. Naye hakujiweza tena akawa mtu wa kulazwa kitandani siku nzima usiku hata mchana. Hata nguvu zake za maji ya maajabu hazikufua dafu mbele ya uzee ule.

Mkewe, Malkia Raheli alikuwa na ujauzito mkubwa kabisa lakini hakutaka mumewe ahudumiwe chochote kile na mtumishi. Aliyafanya yote kama mke pekee wa Mfalme Efroni huku akisaidiwa na mabinti zake kumi na wawili. Waliyafanya haya kwa mapenzi yote hata mfalme hakuwahi kujihisi upweke. Hakika walimpenda. Na katika siku zake za mwisho bado uso wake ulitawaliwa una tabasamu. Hakika tabasamu la mfalme, tabasamu la ufalme.

Jemedari Bethueli alitumika kufanya shughuli zote za kiuongozi wakati huu mfalme yupo kitandani. Alipokea maelekezo kutoka kwa mfalme na kuyatekeleza vyema kabisa hata pengo la mfalme lisiwepo tena mbele ya wakazi wa Nahori.

Mfalme Efroni alimuamini sana Bethueli, aliwachukua kuwalea tangu wakiwa watoto yeye na mdogo wake Rafaeli. Hii ni baada ya Baba na Mama yao kuuwawa baada ya uvamizi wa kwanza uliofanywa na jeshi la mashujaa wa Shekemu.

Jemedari Bethueli aliyatenda majukumu hayo kwa furaha na moyo wake wote akitambua fika yeye ni mrithi halali wa ufalme ule kwa kuwa mfalme hakubahatika kupata mtoto wa kiume. Kwa upande wa mdogo wake Rafaeli yeye hakutaka kujishughulisha na shughuli jeshi, alichagua kuwa tabibu, akirithi kazi ya marehemu mama yao. Mama yao alikuwa ni tabibu aliheshimika sana hata mfalme akampa hadhi ya tabibu mkuu wa Nahori akitibu mamia kwa maelfu ya watu. Kila homa ilisalimu amri mbele ya dawa zake. Mti gani wa dawa mama yule asiujue?.

Sheria za Nahori ziliamuru kama mfalme aliyekaa kwenye kiti cha ufalme atafariki na hakuna mtoto wa kiume wa kurithi kiti hicho basi ufalme ungehamia kwenye familia ya Jemedari mkuu wa wakati huo. Jemedari Bethueli alikuwa MTEULE ikitokea mfalme amefariki. Naye akazihesabu siku hizo kama mtoto mdogo anavyohesabu vidole vya mikono yake ili apate jawabu la hesabu ya kuongeza.

La, angalikkuwa makini, asingalipuuzia jambo lile linalokaribia kutokea. Ama kweli jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Ndiyo, walisema wahenga.
 
SEHEMU YA KWANZA
Akiwa amejilaza kitandani asubuhi hii na matumaini ya kuukwaa ufalme baada ya mfalme kufariki yakizidi kuwa juu maana sheria za nchi hii zinavyoamuru mfalme akifariki na hana mtoto wa kiume basi ufalme utahama utaenda kwenye ukoo wa Jemedari. “Kuna Jemedari mwingine zaidi yangu?”, akauliza kichwani mwake asijali kamuuliza nani, hakujali.

Hapo akarudisha kumbukumbu miaka mingi iliyopita walipopigana vita na watu wa Shekemu na kuibuka washindi. Akalikumbuka katazo la Mfalme Efroni kuhusu kisima cha shetani. Hapa akacheka kwa dharau akisindikiza na maneno kwa sauti sio kuwaza tena, “Sasa nisingefanya vile ningewezaje kulipa kisasi changu?, Kwa mapigo yasiyo na idadi nimeufuta Ufalme wa Shekemu ndani ya usiku moja. Siku moja tu.”, Hapo akacheka tena kwa dharau lakini hakumaliza vizuri kicheko chake safari hii.

Ghafla kibaraka wake akaibuka kwenye chumba kile asikumbuke kubisha hodi. ”Kamanda.. Kamanda..Malkia, Malkia, ame..ame…”, alikuwa anongea huku ameinamia magoti mikono yake miwili ikiyakamata vyema magoti yale kana kwamba anajikinga asianguke huku anahema kwa kasi. “Ukishindwa kujidhibiti ukaongea kitu kinachoeleweka nakulipua sasa hivi.”, Jemedari Bethueli alitoa onyo katika sauti nzito ya kutisha ya yenye kila viashiria vya ushetani ndani yake. Kibaraka akagwaya, hapo akazikamata pumzi zake vyema na sasa akaongea kama mwanaume rijali, “Malkia kajifungua.”.
“Sasa tatizo lipo wapi?”, aliuliza Jemedari katika sauti ya kibinadmu iliyojazwa furushi la dharau. “Kajifungua mtoto wa kiume.”, Kibaraka akanyoosha maelezo.

Jemedari aliunguruma kama Simba huku akiruka kitandani kana kwamba palikua na kaa la moto kwenye godoro lile laini la sufi, tetemeko dogo likapita. Ushetani mtupu. Kibaraka akaona hapamfai tena, akapotelea mlangoni kwa mwendo wa kujikwaa katika sakafu tambarare iliyopambwa na zulia la kuvutia akiwa haeleweki anaruka au anakimbia.

Jemedari alijiona mpuuzi wa mwisho kwa kutoutilia maanani ujauzito wa Malkia Rahel, labda aliishi kwa mazoea. Malkia Raheli ambaye hakuufikia uzee bado japo alikuwa kwenye hatua za karibu kabisa kubisha hodi kwenye lango la uzee. Malkia huyu alikuwa na watoto kumi na mbili na wote ni mabinti wazuri kabisa. Jambo hili labda ndio lilifanya Jemedari Bethueli asiwe na mashaka na ujauzito ule.

“Lakini mfalme hana nguvu tena za kunizuia atakufa kinyama kama walivyokufa wale watu wa Shekemu. Ndio wakufa wakufa tu.”, aliufariji moyo wake na tazama tabasamu la kifedhuli likaupamba uso wake. Hapo teke la nguvu likatua kwenye mlango ule usio na hatia. Ukarushwa umbali ambao macho ya kibinadamu yasingeweza kuuona tena. Ukapotea kama alivyopotea Kibaraka yule. Lo!


******

Furaha ya Mfalme Efroni kupata mrithi iliingia shubiri baada ya kuletewa taarifa na Rafaeli kuwa kaka yake Bethueli ameasi yeye na mashujaa wengine. Yoyote anaekaidi amri yake anauwawa kikatili kwa kulipuliwa na nguvu ya kishetani. Uchungu mkuu ukamshika Mfalme Efroni .

“Anayatenda haya kwakuwa anajua sina nguvu tena, na kama ana nguvu za shetani basi hakuna kiumbe chochote miongoni mwenu kinachoweza kupambana nae kikamshinda. Ni mteule pekee wa kiti cha ufalme aliyekunywa maji ya maajabu.”, aliongea kwa taabu Mfalme yule akionekana kukata tamaa.

Hapo akamgeukia Rafaeli akamwambia, “Kaka yako nilimpa vyeo vikubwa sana lakini wewe nilikuamini, hata sasa nakuamini. Umekua msiri wangu miaka yote hii. Unaujua ukweli wote kuhusu njia za mashimo ya giza, naamini kaka yako angezijua pia angeshafanya jambo kuzuia hadi wakati huu.”, akaweka kituo akimeza fundo la mate kwa shida, nae akaendelea, “Tafadhali sogeza sikio lako karibu yangu unisikilize kwa makini.”,

Akasogea Rafaeli huku machozi yakimlengalenga. Mtu yule aliyelala kitandani pale alikuwa kama baba kwake, alimlea kama mtoto wake. Hakika alimlaani Kaka yake Bethueli kutokana na madhila aliyoleta. Muda haukuwa rafiki tena wakasikia lango la kuingilia kwenye ngome ile ya mfalme likianguka na kufuatiwa na kishindo kikuu kilichoambata na vilio vya uchungu za mashujaa waliobaki kupambana. Hakika zilikuwa dakika za mwisho za utawala wa Mfalme Efroni. Mfalme kipenzi wa Wanahori wote. Kiza kikatanda, kurasa za utawala wa Mfalme Efroni zikafungwa rasmi na kurasa za kitabu cha utawala wa kishetani zikafunguliwa. Miaka mingi ikapita.


*******************
 
SEHEMU YA TATU


WIMBI LA MAPENZI



Wanakijiji walishangilia sana kuuwawa kwa yule Chui aliyekuwa anasumbua kijiji kile kwa kuua watu pamoja na mifugo yao. Chifu Harani akatangaza zawadi nono kwa yoyote alifanya jambo lile la kishujaa. Hakuna aliyejitokeza kujitwalia zawaida hiyo iliyosemekana kuwa nono. Uvumi ukawa mkubwa na uvumi ukahalalishwa kuwa ile ni kazi ya mizimu. Japo wengine wakahoji imekuaje msitu wa Milomo ukawa na mizimu wema. Likawa fumbo.



Sara naye mwenye mawazo mengi akimfikiria shujaa yule aliyeokoa maisha yake. “Au atakuwa Abunaye?, maana ana maguvu sana yule kaka. Lakini yule ni mbinafsi na katili sana kwa wasichana. Atakayeolewa na yule kaka kazi anayo jamani mmhuu.”, aliwaza Sara huku akimalizia kupiga vikofi kama ananawa vinavyoashiria ‘kazi ipo’ ama ‘inipitie mbali’ huku kichwa kakieleza upande tofauti na ule anaopiga vikofi vile.



“Wewe mtoto maji yako wapi, au hujui tuna ugeni leo na unakuhusu wewe?”, alishtuliwa na Mama yake akiongea kutoka upande ule aliompa mgongo. “Samahani mama”, aliongea kwa kusihi tayari ameushika mtungi wake na anaishika njia ya kisimani huku nyuma akisindikizwa na maneno makali ya kulaani kutoka kwa mama yake. Yakizidi kupungua kadri anavyozidi kuiacha nyumba ile.



Sara alikaribia kisimani na kwa mbali aliweza kumuona kijana wa kiume akiteka maji. Akazidi kusogea na kujisemea, “Kaka huyu angekuwa kaka yangu ningenenepa mimi. Yaani kazi zote nafanya mimi, kuni mimi, kufua mimi, kupika mimi,kuosha vyombo mimi, kuteka maji mimi. Ati wenyewe mashujaa, mashujaa wa nini na Wabondo wakija hapa hakuna hata mmoja anayethubutu kurusha hata fimbo, mfyuuuuuuu”, alimalizia kusonya asijue amesonya kwa sauti na ameshakifikia kisima tayari.



Uso wa yule kaka uliingiwa na huzuni, alishazoea kuzomewa kukejeliwa na kusonywa kama hivi haikuwa mara ya kwanza. Akajitahidi kupuuza hali ile akaendelea na zozi la kuteka maji aujaze mtungi wake. Sara akatambua ule msonyo wake umeleta maana tofauti kwa yule kaka ambaye sasa alimtambua ni Taji.



“Samahani… samahani sana Taji sikumaanisha hivyo.”, aliongea kwa kubabaika Sara wakati huo mtungi wa Taji unakaribia kujaa maji. Taji akamuangalia akahisi bado anamkejeli. Akainuka na mtungi wake aondoke Sara akamsihi sana asiondoke hata imani ikamuingia Taji kwamba yawezekana huyu binti yupo tofauti na mabinti wengine pale kijijini.



“Unajua siku nzima ya leo ni kazi tupu na sijapata nafasi ya kupumzika hata kidogo. Tafadhali Taji nisaidie kuujaza maji mtungi huu”, Sara aliongea kwa sauti ya kudeka. Tai alimuangalia Sara usoni akiwa makini sana lakini Sara hakuwa na chembe ya hofu wala kubabaika kwenye kile alichosema. Akautua mtungi chini huku akirejea tena kisimani asitie neno lolote.



Sara hakuwahi kuyatilia maanani maneno ya familia yake tangu anakuwa hadi sasa kwamba Taji ni mtoto wa mazimu asithubutu kumkaribia. Hakuwahi kuwa na ukaribu na pia hakuwahi kumuita jina lile lilopendwa na wanakijiji, Mzimu. Sara alikua binti wa tofauti sana. Na leo yupo karibu na Taji anamsesha hajibu chochote, Taji na vitendo, vitendo na Taji.



“Hivi Taji huwa unaongea kweli?”, Sara aliendeleza ngonjera zake za maswali ili mradi zoezi lile la kutekewa maji lisiende kimya kimya. “Huwa naongea na Wazazi wangu na Moha pia”, kwa mara ya kwanza akaisikia sauti ya Taji. Hakutarajia hali ile huku Taji amemkazia macho kana kwamba anauliza ‘una linguine?’.



“Na leo umeongea na Sara, Sara mwenye bahati zake.”, aliongea Sara katika nanamna ya’kishambenga’. Sasa Taji akatabasamu huku akisitisha zoezi lile la kuteka maji, akamtazama usoni na wote wakashindwa kuzuia kicheko, wakacheka.



Mtungi ukajaa maji na Taji alipotaka kumtwika wakatizwa na sauti ya Sai akifoka ambaye haikueleweka ametokea wapi. Sara akaogopa sana alishujua kitachofuata huko nyumbani.

“Wewe mpumbavu na huyo mpumbavu mwenzako mnafanya nini hapo?”, alifoka Sai huku akimuelekea mdogo wake, usoni amefura kwa hasira mithili ya mbogo aliyejeruhiwa na kumchapa kibao kikali kilichompeleka chini.



“Kaka nisamehe!”, aliomba msamaha Sara katika sauti ya kusihi. “Nikusamehe?, utaenda kumueleza baba ulikuwa wapi hadi mchumba wako na wazazi wake wameondoka.”, Sara alishtushwa na taarifa zile. Hakutarajia baba yake, Mzee Sango angemtafutia mchumba. Japo kwa mila na desturi zao mtoto hutafutiwa mchumba na wazazi wake na hana haki ya kupingana na maamuzi yale. Sara alijawa na wasiwasi asijue huyo mchumba ni nani.



“Yaani hii ni bahati kwetu maana baba yake na Abunaye ana maelfu ya ng’ombe, tusingekuwa na wasiwasi tena wakuchuliwa utumwa na Wabondo.”, alibwabwaja Sai huku akirusha mikono huku na huku. Uchu wa mali ukionekana dhairi shairi machoni pake. Sara akawa kama amepigwa mkuki moyoni na habari ile.



Abunaye katili huyu ambaye kila msichana kijijini hapo hataki kumsikia kutokana na ubabe wake usio na maana. Ni wiki iliyopita tu alimpiga hadi kuzirai rafiki kipenzi Sipora kisa tu alikataa kwenda alipomuita waongee.



“Baba huyu baba, kwanini lakini”, alinung’unika moyoni mwake hata asimakinike na kaka yake ambaye safari hii alimkwinda Taji akimfokea. “Nikikuona tena na mdogo wangu, hesabu kifo. Sitajali Chifu kasema nini, wewe ni wakufa wakufa tu.”, sasa povu lilimtoka bado kamkwinda Taji aliyeonesha kuzoea hali ile hata asiwe na chembe ya wasiwasi kwenye uso wake.



“Kwa hiyo kaka, akina Abunaye hawatarudi tena, si eti eeh?”, aliuliza Sara akijizoazoa pale chini. “Ati nini?”, alihamaki Sai na Taji akashindwa kujizuia. Kicheko cha chinichini kikamtoka kwa lile swali lake.

Sara akabaki kinywa wazi akimshangaa Taji, kana kwamba sio yeye aliyeuliza swali lile la kipuuzi.



“Unacheka sio, unaona mazuri sio?”, aliuliza Sai kwa sauti nzito ya kibabe akimsukuma mbali kabisa Taji. “Siku zako za kilio zinakaribia. Na wewe mpumbavu inuka twende ukamueleze baba upuuzi uliofanya.”

Sai na mdogo wake wakaongozana kurudi nyumbani huku Taji akijaza tena maji kwenye mtungi wake uliopigwa teke na Sai wakati wa purukushani zile. Kwa mbali Sara akaupunga mkono wake na Taji asiuone. Naam, mawimbi yalianza kujitengeneza yakielekea kuwazoa vijana wale nao wasijue. Mawimbi ya Mapenzi. Ndiyo, MAWIMBI YA MAPENZI.
 
SEHEMU YA NNE


UNAHITAJIKA NYUMBANI MTEULE!



NAHORI,



Nahori haina mfalme tena, wakazi wote waliombeleza kwa siri kifo cha mfalme na familia yake. Jemedari Bethueli anatawala ufalme huu kwa mkono w chuma. Hataki kusikia jina la mfalme Efroni likitajwa popote pale. Wazee wote waliopinga ufalme kwa hoja kwamba hawezi kutawala wakati MTEULE halali wa kiti cha ufalme bado hajulikani kama anaishi au la waliuwawa kinyama hadharani. Kwa mkono wake mwenyewe. Mkono wa shetani.



Miaka ikapita wakazi wengi wakizidi kufa kwa njaa kutokana na maghala yao ya vyakula kuporwa na mashujaa wa Jemedari Bethueli na vyakula hivyo kupelekwa jeshini ambako walipiga vita visivyoisha miaka yote hii. Hakika walidhoofu. Na wakazi wengine wakapotea wasijulikane wapo wapi. Uvumi ukaenea wanapelekwa kutolewa kafara kwenye kisima cha shetani. Hali ilikua inatisha na matumaini ya kuiona kesho kwa wakazi waliowengi ni kama hayakwepo.



*************



“Mpwa wangu unajua hutakiwi kuwa mahali hapa, ni hatari sana”, aliongea Mzee mwenye mvi nyingi kwenye kila moja ya unywele wake. Uzee ulibisha hodi. “Najua mjomba Uzieli, lakini kama unavyoona mambo yanazidi kuwa mabaya. Kama tutakaa kimya hapatakuwa na ufalme tena wa Nahori. Nahori inaingia gizani taratibu.”, aliongea kwa hisia kali mtu huyu ambaye sio kijana tena yupo kwenye utu uzima. Wakiwa kwenye nyumba hii ambayo ndiyo makazi ya mpiga ramli mkuu wa Naholi aliyejulikana kama Uzieli. Mtiifu kwa mfalme Efroni. Marehemu sasa.



“Sikiliza kwa makini mpwa wangu Rafaeli, nguvu za kaka yako Bethueli nadhani unazijua vizuri hakuna kiumbe chochote kinaweza kupambana nae isipokuwa mteule wa kiti cha ufalme ambae hata sasa hatujui kama ni mzima au amekufa…” aliongea kwa kirefu Mjomba Uzieli.



“Ni mzima.”, Rafaeli alisema kwa kifupi. “Una uhakika gani?, ramli zangu zote zimeshindwa kumuona kabisa!”, alihoji Mjomba Uzieli safari hii akimakinika na uso wa Rafaeli. “Ramli zako zinashindwa kumuona kwa kuwa hayupo ulimwengu huu. Bado anaishi ndio maana Bethueli anashindwa kuingia kwenye kisima cha maji ya maajabu. Kama unavyojua ukiwa sio mteule ukaingia huko utaunguzwa vibaya sana na maji hayo yanayochemka.”, alifafanunua kwa kirefu Rafaeli.



“Sasa huo ulimwengu mwingine alifikaje tena?”, aliuliza mjomba huku matumaini yakianza kurejea tena usoni mwake. “Mashimo ya giza mjomba, Mashimo ya giza.”, aliweka msisitizo Rafaeli. Sasa Mjomba aliinuka pale alipokaa na kupayuka, “Nilijua, nilijua mimi. Haya mashimo yapo, nilijua mfalme Efroni hakuniamini katika jambo hili.”. Ikabidi Rafaeli amtulize maana sauti yake ilikuwa kubwa.



“Nafikiri Bethueli anajua yalipo pia na ameweka walinzi eneo hilo asipite mtu.”, alisema mjomba Uzieli huku akiwa na hamu ya kusikia Rafaeli ana usemi gani kuhusu jambo lile. “Ndiyo, ile siku namtorosha yule mtoto nahisi nilionekana wakati wa kurudi. Ilikuwa nikawachukue Malkia na mabinti zake na hapo ndipo nlipokumbana na upinzani. Nilikuta eneo lile likiwa tulivu lakini wakati tunataka kuingia pangoni tukavamiwa. Tuliingia kwenye mtego. Nguvu zangu za kupotea katika hali yoyote ndio ziliniokoa lakini…..”, sasa Rafaeli alishindwa kuongea machozi yakaanza kumtoka na kilio cha kwikwi kwa mbali. Raphaeli alikuwa kwenye majuto makuu.



“Mimi sio shujaa mjomba, sikuweza kuilinda familia ya mfalme. Niliwaingiza kwenye mtego malkia na mabinti zake wote wakaangamia. Nikamteleza mtoto kichanga katika ulimwengu wa watu huko nisijue ni mzima ama la?”, sasa alishindwa kuzuia kilio, kikatoka kama kilivyo. Mjomba akamsogelea karibu zaidi akampigapiga mgongoni katika namna kumfariji akamwambimbia, “Ni mzima.”. Rafaeli akamgeukia mjomba wake akaikumbuka kauli ile. Kilio kikakoma, machozi yakafutwa.



“Kwa hiyo kama Bethueli ameyagundua hayo mashimo hayo kwanini ameshindwa kumfuata huko huko aliko Mteule na kumuua.”, alihoji mjomba.

“Mashimo yale ni mengi sana idadi yake haijulikani, na kila moja linakupeleka kwenye ulimwengu wake na sayari yake. Hakuna namna atajua alipo mana sayari zenye binadamu kama sisi ni nyingi sana.”, alitoa ufafanuzi Rafaeli.



“Nimeelewa kwanini msako wa kukutafuta ni mkubwa hivi, Bethueli ameahidi kutoa hata robo ya ufalme wake kwa atakayefanikisha kupatikana kwako. Anajua wewe ndio ufunguo wa kumfikisha kwenye ulimwengu alipo Mteule.”, alitoa mawazo yake Mjomba Uzieli.



“Sasa huyu mteule inabidi arudi nyumbani haraka iwezekanavyo.”, aliongeza Mjomba Uzieli kwa msisitizo mkuu. “Na ndio maana niko hapa, nakusikiliza tunafanyaje?”, aliongea Rafaeli huku akimsukumia fumbo lile mjomba alitatue. “Alaa!, kumbe una wazimu we mtoto. Nimekuambia ramli zangu hazimuoni.”, aling’aka Uzieli.



**********************



Katika makazi ya mfalme, Jemedari Bethueli alikuwa amekalia kiti cha mfalme akiwa na mawazo tele. Alimtafuta Mteule karibu kila shimo aliloingia asimpate. Mpango wake wa kuingia kwenye kisima cha maajabu aliona wazi ukielekea kukwama.



“Rapfaeli”, alilitaja jina la mdogo wake kwa hasira hata akapigiza ngumi juu ya mkono wa kile kiti. “Msaliti mkubwza wewe, nitakutia mikononi na utakufa kinyama na nguvu zako za kupotea potea hazitakuwa na msaada tena.”, aliongea kwa sauti sasa hata mtetemo ukahisiwa vizuri tu na walinzi waliosimama pembeni yake. Nao wakatetemeka.



“Niitie Kibaraka wangu.”, alimtuma mmoja wa wale walinzi amuite Kibaraka wake mtiifu wa tangu na tangu. Akatii amri haukupita muda akarudi nae. “Ewe, mtukufu mfalme.”, Kibaraka alitoa heshima huku akipiga goti kichwa ameinamisha chini. “Kelele! Funga bakuli lako, mfalme mfalme, unamjua mfalme wewe?”, alifoka Jemedari akiona kama amekejiliwa na yule Kibaraka kumuita mfalme wakati bado anahangaika na Mteule.



“Sikiliza kwa makini, sasa msako wa Rafaeli tunauelekeza kwa Mjomba Uzieli. Chunguza mienendo yake yote, chunguza wote wanaoingia na kutoka kwenye makazi yale. “Sawa mkuu.”, alijibu Kibaraka.

“Tokaaaaa! Mkuu mkuu, unamjua mkuu wewe?”, alifoka Jemedari Bethueli na Kibaraka akapotea eneo lile. Ama kweli Mteule alimpeleka puta. Lo!



“Nawewe niandalie watu watatu wa kafara, tunaelekea kisima cha shetani. Nina ombi.”, aliongea Jemedari Bethueli pasi na chembe ya huruma.



************************



Kipindi Jemedari Bethueli anatoa maagizo yale kwa Kibaraka ndio kipindi ambacho Rafaeli alikuwa anaagana na Mjomba wakiwa wamefashanya la kutakiwa kufanya kumrejesha MTEULE nyumbani.
 
SEHEMU YA TANO


ANANIPENDA, ANANIPENDA TOKA ZAMANI!



Sara alikua amejiliza kitandani akijiuguza majeraha ya mikwaju ile isiyo na idadi aliyoipokea kutoka kwa baba yake, Mzee Sango. Ajabu maumivu haya hayakufanya ashindwe kuikumbuka nyakati ile alipokuwa na Taji. Naam, Taji aliyeitwa mtoto wa mizimu kutokana na macho yake ya buluu bahari.


Mawazo yalimrudisha nyuma na akakumbuka kitu alichokiona. Akainuka kitandani wasiwasi ukamuingia hata asiyahisi tena maumivu ya mikwaju ile. “Jambo hili ni Sipora pekee anaweza kunishauri.”. aliwaza huku akiwa anaiacha nyumba taratibu muda huu wa mchana.


*************


Jana yake kisimani.


“Taji nimekukuta tena, leo hayo maji nakutekea mimi, nikujazie mtungi wako huo.”, Taji aliisikia sauti laini ikiongea kwa pozi ikielekea pale alipokuwepo.
“Hapana, nitaujaza mwenyewe.”, alijibu Taji akionekana kutoifurahia upendeleo ule.
“Ha, Taji usiniambie unamuogopa kaka Sai, achana nae yule hana lolote.”, Sara alisema kana kwamba sio yeye alyekuwa anabembeleza asamehewe na kaka yake yule.

“Kwanini unaniita Taji?”, aliuliza Taji akiwa amemakinika na uso wa binti yule mrembo aliyesimama mbele yake. “Ah! Kwa sababu ndio jina lako, afu sio wote tuna mawazo potofu.”, Sara aliongea harakaharaka akiwa ameelewa fika msingi wa swali lile na huku akipeleka mikono yake achukue ile kata ya iliyo mikononi mwa Taji.


Taji akaikwepesha akiileta nyuma ya mwili wake, kiunoni na huku akisema, “Hapana Sara, mwenzako nina kibali, siruhusiwi kupigwa na mtu yoyote hapa kijiji. Nakuonea huruma wewe. Na isitoshe wewe ni mchumba wa mtu.”.
Uso wa Sara ukabadilika ghafla, ni kama hakupendezwa na kauli ile ya kwamba yeye ni mchumba wa mtu. “Mtu gani, Abunaye? Mfyuuuuu”, aliuliza Sara huku akisindikizia na msonyo.


“Sasa nasema na hiyo kata utatoa na maji nakutekea utake usitake, umeshaniudhi.”, aliongeza Sara uso ukionesha hauna chembechembde za utani, alionekana kumaanisha anachokisema.
“Binti huyu ana wazimu.”, aliwaza Taji kichwani mwake huku akijibidiisha kuikwepesha ile kata.
Sasa ikawa kama mchezo Taji akirudi nyuma Sara anasogea, akienda kushoto anakuja, kulia anakuja.


Ukawa mchezo sasa wakikimbiza kukizunguka kisima kile, wanakimbizana wanacheka. Ama kweli mapenzi kikohozi, ukiyaficha utabanja.
Hatimaye Sara anafanikiwa kumpata Taji, kata haipo nyuma tena, imekimbiziwa mbele. Ikawa amemkumbatia toka nyuma mikono yake ikilazimisha kuifikia ile kata hata asiipate.


“Aisee leo naua mtu…...”, alikuwa Sai. Safari hii hayupo peke yake tena bali ameongozana na Mshami, mdogo wake. “Huu ndio mzimu unaokuzuzua hadi unamkataa Abunaye sio?, ngoja leo tumfunze adabu”, aliongea Mshami akijiandaa kumvaa Taji.
“Mumfunze adabu nani?”, iliuliza sauti tokea nyuma yenye chembechembe zote za mamlaka.


Wote wakageukia kule inakotokea ile sauti yenye mamlaka. Moha. Ndiyo alikuwa rafiki kipenzi wa Taji akijongea eneo lile taratibu kana kwamba hakuna kibaya alichoshuhudia pale. “Tulikua tuna….”, alitaka kubwabwaja Mshami, akakatizwa na ishara ya mkono kutoka kwa Moha ikiashiria ‘basi inatosha.’ “Taji uko sawa? “ aliuliza Moha a asipate jibu zaidi ya tabasamu usoni pake.


Moha akawageukia Sai na mdogo wake Mshami akawaambia, “Mashujaa wenzangu neno la Chifu ni sheria na adhabu ya kutupwa kwenye maporomoko yenye majabali sio utani kuweni makini.” Akaweka kituo huku ndugu wale wakiwa wameinamisha vichwa vyao kwa utii.


“Mama yako aliniambia umefika huku kisimani ndio nikaamua kukufuata.”, alizungumza Moha huku kamgeukia Taji ambaye hakusema chochote. Moha alimuelewa rafiki yake. Hakuwa mzungumzaji kabisa hasa pakiwa na watu ambao hajawazoea.


“Na nyie mbona mitungi yenu siioni, mnasubiri nini hapa?”, aliuliza Moha akiwalenga Sai na Mshami nao wakaelewa msingi wa swali wakapotea eneo lile. Sara akaendelea kuijaza mitungi ile huku tayari akijua kuna kizaazaa kinamsubiri ataporudi nyumbani.


“Wabondo wanatarajiwa kuja wiki ijayo hapa kijijini kwetu. Karibu kila nyumba imeandaa cha kuwapa wasije vijana wao wakachukuliwa utumwa.”, Moha aliongea na kuweka kituo, kisha akaendelea, “ Je, rafiki yangu mnachochote cha kuwapa watu hawa watakapofika katika kaya yenu?, Nisingependa kusikia rafiki yangu umechuliwa utumwa.”, aliongea kwa hisia Moha huku Sara akiwa amemakinika na ile mitungi akijifanya hasikii mazungumzo yale.


“Baba ana mbuzi watatu, tutawapa hao.”, alijibu Taji na Moha akaishia kutabasamu. Akazipiga hatua kuondoka huku akisema, “Na huyo binti ukajitambulishe kwao umuoe utanichosha kukukingia kifua kila siku.”. Taji na Sara wakaangaliana vinywa vyao vikiwa wazi kana kwamba wanauliza, “sisi?, akha!”. Hawakutarajia shambulizi kutoka kwa Moha.


********************************************


Sara alishafika nyumbani kwa rafiki yake Sipora, alimkuta rafiki yake huyo akiwa anachambua mboga. Maandalizi ya chakula cha jioni. “Mbona una tabasamu hivyo, kuna nini?”, aliuliza Sara baada ya kuona mwenyeji wake huyo kamkaribisha na tabasamu lisilo la kawaida. “Hamna shoga yangu, nimefurahi tu ujio wako.”, aliongea Sipora katika namna ya kujitetea na kuhalalisha tabasamu lake lile. Ajabu tabasamu halikukauka kwenye uso wa binti yule, Sara akapuuzia akaeleza kilichomleta kwa msiri wake huyu.


“Unajua jana nlikua na Taji kule kisimani….”, alianza kueleza Sara kabla hajakatishwa. “Niliwaona sana, mlipendezana wenyewe.”, aliongea Sipora huku viganja vya mikono yake akiwa amevitega kwenye kidevu chake huku tabasamu lake likiimarika maradufu usoni pake. “Hiiiii! Mwanamke mbeya ka nini!”, alisema Sara katika namna ya kusuta. Sipora akafungulia kicheko na wote wakacheka.


“Hivi humuogopi yule kaka nani sijui?”, aliuliza Sipora akijitahidi asilitumie jina la Mzimu mbele ya shoga yake yule. Mara kadhaa ameshuhudia Sara akigombana na mabinti wenzake pale kijijini waliomuita Taji kwa jina la Mzimu. Hata wengine wakmtuhumu ana mahusano naye ya siri. Hakujali.


“Nimuogopee nini mimi?, yule ni mtu kama watu mengine. Halafu hujui tu alivyo mcheshi.”, alijibu Sara katika namna ya ‘kushushua’ . “Eh na kuongea anaongea kumbe?!”, Sipora alionesha kushangazwa. “Sasa!, ila anaongea na Wazazi wake, Moha na mimi hapa.”, aliongea Sara huku akijitikisatikisa katika namna ya ‘kujifagilia’.


“Tuachane na hayo shoga yangu, unajua jana wakati tunagombaniana ile kata na Taji, niliona alama za mikwaruzo mikononi mwake.”, aliongea Sara akiwa hana chembe ya utani kabisa.
“Shoga yangu naye, sasa mikwaruzo kwenye mikono kwa mtoto wa kiume si jambo la kawaida?”, aliuliza Sipora akitegemea Sara akubaliane na hoja yake.


“Ni kweli, lakini ile mikwaruzo ni mikubwa, ni kama ameparazwa kucha na mnyama mkali.”, alisema Sara katika sauti yenye mashaka na wasiwasi mkubwa.
“Mmmmh!, naona unakoelekea. Unafikiri Taji ndiye aliyekuoa kutoka kwenye makucha ya yule.”, aliuliza Sipora safari hii akiwa makini sana.
Sara akabetua mabega kuashiria hana uhakika. “Lazima atakuwa yeye tu.”, Sipora aliongea kwa sauti pasi na kutarajia hata Sara akashtushwa na kauli ile.


***********************************************************************


SIPORA ANASIMULIA MIAKA KUMI NA SABA ILIYOPITA.


Siku hii ilianza kwa mvua za rasha rasha, wakujiandaa kwenda shamba walifanya hivyo lakini hawakufanikiwa kutoka maana mvua kubwa ilishuka. Mvua kubwa iliyonyesha zaidi ya masaa sita. Ikakata, anga lililofunga kwa wingu jeusi likaanza kufunguka tena. Ikawa ahueni kwa wale wenye majiko nje. Wakatoka kupika.


Hata majiko hayajawashwa, vikasikika vilio na sauti ya mwanamke akipiga kelele zilizotokea mabondeni, “Jamaniii mwananguu uwiiiii, mwanangu anasombwa na maji huku, uwiiiiiiii,”


Mto Medadi ni mto mkubwa uliopita katika kijiji cha Mporosai. Mto huo ni mdogo sana kwa upana na kina katika vijiji vinne vya mwanzo. Ni kwenye kijiji hiki mto umetanuka na maji yake yana nguvu sana.Hali imesababishwa na maporomoko makubwa yaliyojitengeneza mwishoni mwa kijiji hiki.


Maporomoko haya yana urefu sawa na kiwanja cha mchezo wa kandanda.Maji haya yanayoporomoka huanza kupiga miamba mikubwa iliyojitokeza kwenye ardhi mithili ya majabali na ndipo huendelee na safari yake kuvitafuta vijiji vingine. Mara kadhaa wachungaji wamepoteza mifugo yao baadaya kupelekwa na mkondo huu wa maji na mwisho kutupwa kwenye majabali.


Hali hii ikapele Chifu wa miaka hiyo kuweka katazo la watoto kutocheza maeneo ya mabondeni unakopita mto huo. Katazo ambalo lilidumishwa hadi miaka hii. Lakini mtoto ni mtoto, safari hii haikuwa bahati kwake labda sababu ya mvua kubwa iliyokuwa inanyesha tokea asubuhi ya siku hiyo.


Nasasa mtoto huyu anapelekwa na maji huku na huko naye akitii bila kipingamizi chochote. Wanakijiji wanakimbia kandokando ya mto huyo huku matumaini ya kumuokoa mtoto huyo yakizidi kuyayuka maana tayari maji yalianza kuchanganya kasi na maporomoko yakionekana. “Jamani binti wa Sango anakufa..”,aliongea kwa huzuni kijana mmoja na kuwagutusha wengine wakatambua kumbe mtoto anayepelekwa na maji ni Sara, mtoto pekee wa kike wa Sango.


Hawakuweza kumuona tena mbele ya upeo wa macho yao. Tayari alishaingia kwenye maporomoko.
Sango alifika eneo lile akiwa ameambatana na Chifu Harani pamoja na wazee wa kijiji kile. Wakateuliwa vijana kadhaa washuke kule chini ili wakautoe mwili wa mtoto Sara kwenye majabali. Zoezi likaanza mara moja. Walipita njia za kandokando ya mto zenye mteremko mkali.


Mama Sara alikuwa hajiwezi kwa kilio, alimpenda sana binti yake yule. Wanawake wenzake wakawa wanamfariji. Haikusaidia kitu, kilio kilikuwa kikuu. Sango yeye alionekana kujikaza japo uso wake ulionesha majonzi tele.


Baada ya kitambo kidogo vijana waliopewa jukumu la kuutoa mwili wa Sara huko kwenye majabali hawakurudi na mwili bali habari za kushangaza.
“Vijana nini tatizo?”, aliuliza Chifu Harani.
“Hatukuweza kuuona mwili wake wala mabaki yake, sidhani kama alitupwa kule chini.”, Alijibu mmoja wa vijana wale.
“Inawezekana vipi na sote kwa macho yetu tumeona akipotelea kwenye mkondo wa maporomoko?”, aliuliza mmoja wa wanakijiji wale ambaye ni miongoni mwa waliokimbia kandokando ya mto.


“Mama, Mamaa!! Ilisikika sauti ikitokea kwenye moja vichaka vya matete vilivyo pembezoni mwa mto ule hatua kadhaa kutoka yanapoanza maporomoko.


Wakwanza kukurupuka alikuwa Mama Sara, Sango akafuata. waliitambua vyema sauti ya binti yao yao, huenda kupita mtu yoyote. Naam, uchungu wa mwana.


**********************************
“Sijaelewa Sipora japo ni kweli nakumbuka maafa yalivyonipata na namna nilivyopona katika namna ya ajabu.”, aliongea Sara akimkazia macho Sipora apate ufafanuzi zaidi.
“Shoga unakumbuka pale walipokukuta kwenye kichaka cha matete zilionekana nyayo za mtoto kwenye tope la mfinyanzi zilioenda kupotelewa huko kwenye nyasi ndefu?”, aliuza Sipora akiwa na lengo la kupata uhakika kama wapo pamoja kabla hajafika kwenye kile anachotaka kuhitimisha nacho. Sara akathitisha lile jambo kwa kutikisa kichwa chini juu, juu chini akiwa na hamu Sipora aendelee na ile habari.


“Sasa mama yangu aliniambia nibaki nyumbani nisitoke anaenda kushirikiana na wanakijiji wengine kukutafuta wewe. Kwa kweli sikuweza kuvumilia shoga yangu ninavyokupenda, mama alipotoka na mimi nikatoka kuekekea huko mtoni.”, akaweka kituo Sipora hata asijue anampa kimuhemuhe shoga yake yule.
“Wakati nakunja kona mojawapo ya zile njia za kuelekea mtoni ghafla nilikutana na Taji ameoga tope la mfinyanzi kama kinyago. Alitisha sana na yale macho yake ya buluu. Lakini yeye alinitazama akatabasamu asiseme chochote huyo akakimbia kushika njia ya wapi sijui.”, alihitimisha Sipora asijue shoga yake amesimama akiwa kaingiwa na ubaridi ghafla. “Mama yangu, ni yeye!”, Sipora ni yeye.”, aliongea Sara pasi na utulivu. “Kwanini hukuambia mapema Sipora.”, aliuliza Sara katika namna ya kutaka kulaumu.


“Ningejuaje mimi?, Mi nilijua katoka kucheza na watoto wenzake huko.”, Sipora alijitoa lawamani.
“Kwa hiyo kama ni hivyo atakuwa nani huyu, maana kipindi naanza kuteremshwa na maporomoko kuelelekea kule chini kwenye majabali, kuna kitu kilinipita kama upepo kikanibeba na kunitupa pale kwenye matete.”, aliongea Sara akionekana kuwa mwingi wa mawazo na maswali.


“Bibi eeh! Unataka niseme nini mimi?, niseme ni Mzimu unicharuane kama ulivyomcharuana Zuwena kule kwenye kuni.”, alisema Sipora asijue amesesema kitu ambacho hata yeye Sara anaanza kukubaliana nacho kabisa. “Ananipenda, anapenda tangu zamani.”, akijua anawaza kichwani kumbe hata Sipora kayasikia vyema tu. ANANIPENDA, ANANIPENDA TOKA ZAMANI.


********************************
 
SEHEMU YA SITA


KIKAO CHA FAMILIA.



Ndani ya nyumba ya Mzee Mombo, baba wa Taji kuna kikao kidogo kilikuwa kinaendelea kati ya baba na mama. Ndiyo, Baba Taji na Mama Taji.
“Unajua huyu mtoto jana hajalala kabisa alikuwa anaweweseka tu karibu usiku wote.”, alisema Baba Taji akiwa mwenye wingi wa wasiwasi. “Kuweweseka?!”, aliuliza kwa mshangao Mama Taji.


“Ndio, alikuwa analia akisema msiwaue baba na mama, usiwaue dada zangu,. Akasema pia sawa Rafaeli, Mteule mteule, nimekuelewa nitakuona asubuhi na mpema.”, Baba alieleza alichokisia usiku ule kwa kirefu. Mama Taji akaingiwa na ubaridi mkali hata akakumbuka miaka mingi nyuma.

******************************************


Mwanamke alionekana shambani akifanya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo. Alionekana akijaribu kukimbizana na wingu zito lililoanza kutanda kote angani likiashiria wakati wowote mvua kubwa itadondoka. Hata hivyo hakuweza tena kuvumilia kitisho kile cha mvua, akaelekea chini ya mti wa mwembe alipoweka mzigo wake mdogo wa kuni akiadhimia kurudi nyumbani ili asije kuisifu mvua. Naam, Wahenga walisema aisifuye mvua imemnyeshea.


Ghalfa akasikia sauti ya kilio cha mtoto kichanga kutokea ndani msitu uliopo hatua kadhaa mbele kutoka lilipo shamba lake. Mwanamke huyu aliyeitwa Malika hakuwahi kulipenda shamba hili kutokana na kuwa karibu na msitu huu wa kutisha wenye masimulizi ya kuogofya.


Hakuna mwanakijiji anayethubutu kuingia kwenye msitu huu pasipo kufanyiwa kwanza mambo ya kijadi na wazee wa kijiji hicho. Na sasa anajiuliza ni nani huyo mwenye ujasiri wa kuingia na kitoto kwenye msitu huu wa Milomo?


Akajishauri kupuuzia aondoke lakini sauti ya kilio ikawa kubwa, huruma ikamwingia hata akasahau habari zile za kutisha kuhusu msitu huu. Akaanza kupiga hatua taratibu zenye chembechembe zote za hofu kuelekea kule anakoisikia sauti.


Manyunyu ya mvua nayo hayakuwa na subiri yakaanza kudondoka moja baada ya jingine huku ngurumo za radi zikimweka kwenye wasiwasi. Hakwenda mbali sana kabla hajaona kikapu kilichoundwa kwa miti ambao hajawahi kuona popote pale kijijini pale. Akakifikia kikapu kile na kilio cha kitoto kile kikakoma huku tabasamu la kitoto likichanua, akinyosha mikono kumuelekea kana kwamba kanaashiria ‘mama,mama nichukue…’.


Akiwa haelewi afanye nini na huku mvua inaanza kuchanganya, likamjia wazo ajaribu kuita kwa sauti labda kuna mtu yupo karibu anahusika na kile kichanga. Lakini alichoambulia ni majibu ya ngurumo za radi. Sasa hakuweza kuvumilia kilio cha kichanga kile baada ya kushindwa kuhimili matone makubwa ya mvua. Malika akakinyakua kitoto kile na kikapu chake. Naye akakifunika vizuri kwenye moja ya vazi zito alilojifunga. Hata mzigo wa kuni hakuukumbuka tena.


*********************************************************************
Malika alipata wakati mgumu sana kumuelewesha mumewe Bwana Mombo namna upatikanaji wa kale kachanganga ulivyokuwa. Akiwa hana uwezo wa kushika ujauzito Malika aliamini hii ni zawadi aliyopewa kutoka kwa Mizimu.


Mumewe akajawa na mashaka tangu lini Msitu wa Milomo ukatoa kitu kizuri. La angefanya nini na alimpenda mke wake hakutaka lile jambo lile lilete mgogoro. Basi wakakubaliana aondoke kwa muda akakae kwao halafu atarudi tena na yule mtoto ili wanakijiji waamini alikuwa mjamzito.


Ikawa hivyo.


******************************


“Mama Taji”, Mzee Mombo alimgutusha, Mama Taji kutoka kwenye lindi la mawazo. “Nafikiri ni wakati sahihi wa kumueleza ukweli.”, alizungumza kwa hisia kali Mama Taji, ikawa amezungumza kile kilichokuwepo kwenye kichwa cha Mzee Mombo.
“Yuko wapi sasa?”, aliendelea na swali Mama Taji.
“Ameelekea msitu wa Milomo kule ulikomuokota.”, alijibu swali lile Mzee Mombo akiwa na uhakika wote.
“Kwa sababu ile haikuwa ndoto, yalikuwa maelekezo.”, alikazia maelezo yake Mzee Mombo.


“Maskini mwanangu hata hakutaka kuniaga ameondoka. Alinifichia aibu huyu mtoto”, kilio cha kwikwiki kilimtoka Mama Taji. Mzee Mombo alimuangalia mke wake kwa huzuni hata asiwe na neno la kutia kwenye masononeko yale.


“Baba, Mama analia nini?”, waligutushwa na sauti ya Taji kutokea mlangoni akiwa ameshikilia kifurushi kidogo. Mama Taji akashindwa kujuzuia akainuka na kumkimbilia mwanae akamkumbatia machozi yakimtoka, sio ya uchungu tena bali ya faraha. Wakamuomba wakae chini kuna kikao. KIKAO CHA FAMILIA.


Taji akatabasamu kama ilivyo kawaida yake. Wakaketi chini na kwa maajabu yeye ndio akawa mtoa historia wa namna alivyopatikana, akawasimulia kuhusu nguvu zake, familia yake ilivyouwawa na yeye kuokolewa. Pia akawaambia namna Ufalme wake unavyomuhitaji akamalize utawala wa kishetani wa Jemedari Bethueli. Naam, ni taji MTEULE wa kiti cha ufalme wa Nahori.


“Umeyajuaje yote haya mwanangu?”, aliuliza kwa makini Mama Taji.


“Kwasababu Rafaeli alinitumia maono na kunipa maelekezo leo asubuhi sana tukutane katika msitu wa Milomo.”, alijibu Taji na hapo Mzee Mombo alimuangalia mke wake kwa jicho la ‘si nilikuambia’.


“Nahitaji kikapu ulichonikuta nacho, kina dawa za kifalme na kibinadamu.”, aliomba Taji.


Mama Taji alipinga vikali kuwa hajawahi kuona dawa zozote kwenye kikapu kile, lakini Taji alisisitiza. Kikapu kikaletwa. Taji akakigeuza kikapu, akauweka mkono kwenye uvungu wake, akafumba macho, nywele zake zikatoa mng’aro wa dhahabu hata wazazi wake wakashtuka sana.


Akawasihi wasiogope zile nguvu ni za kawaida kwa watu wa Nahori. Uvungu wakikapu ukafunguka na vyupa vingi vikaonekana.Akachagua kimoja kilichokuwa na rangi ya dhahabu na maji ya kumetameta.


“Haya ni maji kutoka Kisima cha maji ya maajabu, marehemu baba yangu aliyahifadhi baada ya ujauzito wa mwisho wa Malkia ambao nilizaliwa mimi. Aliamini angepata mtoto wa kiume na ikawa hivyo.”, alizungumza mambo yale huku akisindikizia na kuyanywa maji yale yote.


“Sasa nimekuwa na nguvu za kifalme rasmi.”, alisema Taji huku akiwaangalia wazazi wake usoni, ambao bado wanaelewa nusunusu.


Kisha akatoa kichupa kingine akampa mama yake akamsihi anywe. Ndani yake ilikuwa dawa iliyotengenezwa na yule tabibu nguli wa Nahori, Rafaeli.
Naye kwa imani akainywa asijue anatibu nini.


*********************************************************
 
SEHEMU YA SABA
MWISHO WA UBAYA NI AIBU.



Hatimaye ile siku ikafika. Ni mwishoni mwa mwaka, wakati huu Wabondo hukusanya jeshi zima pamoja na Chifu wao, Chifu Mshali. Chifu katili kupata kutokea, ambaye kwake kutoa roho ya mtu ni jambo la kawaida sana. Naam, ni kama ‘kunywa maji’. Wangefika kijiji muda wowote.


Jaribio la Wazazi waa Taji kumshawishi Mteule Taji aondoke kijijini hapo kabla Chifu Mishali na mashujaa wake hawajawasili lilionekana kugonga mwamba. Taji alilisisitiza ni lazima deni lilipwe. Deni gani? Hakuna aliyejibiwa. Walipombana sana wakajikuta wanaongea na Taji yule ambaye wanakijiji wamemzoea. Taji anayetabasamu.

“Unaenda wapi sasa?”, aliuliza Mzee Mombo akiwa na wasiwasi tele kwenye swali lake.


“Naenda kwa rafiki yangu Moha.”, angalau safari hii aliongeakitu kinachoeleweka, akaurudisha mlango ule wa nyasi kavu akiwaacha wazazi wake wakiwa na nusu amani nusu wasiwasi.


******************************************************

Abunaye alijiona kudharauliwa sana na Sara. Taarifa za Sara kuonekana na Taji wakiwa na dalili zote za kuwa wapenzi zilisambaa kama moto wa kif na hata kumfikia Abunaye. Abunaye msaidizi wa Moha katika Jeshi la mashujaa la Mporisai. Aliaminika kuwa na nguvu kuliko kijana yoyote pale kijijini. Akiwa na haiba ya ukatili, huku roho ya huruma ikiwa imempa likizo, aliogopeka sana sio kwa waume sio wakike.


Utotoni amekuwa akimsumbua sana Taji kwa vitisho vingi akitishia kumuua kama hataondoka kijijini hapo. Maisha ya utotoni ya Taji yalikumbana na upinzani mkali sana kutoka kwa Abunaye. Ni katika kipindi hiki ndipo Moha aliposimama na kuwa upande wa Taji akiapa kumlinda katika jina la baba yake, Chifu Harani. Taji akapata ahueni.


Moha kijana mwenye huruma na hekima kama alivyo baba yake. Aliheshimika sana kijijini hapo na vijana wenzake, akiwa na sifa kuu ya kusimamia anachokiamini na akishafanya maamuzi huwa harudi nyuma tena. Inawezekana ndio sababu Sai na Mshami hawakumsumbua tena Taji tangu alipowaonya kule kisimani ile siku.Na ndio sababu Chifu Harani alimsikiliza sana kijana wake huyu.


Moha hakuwa na mwili mkubwa kama Abunaye, na mwili wake mdogo alikuwa mjuvi wa kutumia kila silaha inayopatikana kijijini hapo. Hata upiganaji wake ulikuwa wa kutumia akili zaidi, haikushangaza siku moja walipomkuta amemkaba shingo Abunaye aliyekuwa anarusha miguu yake huku na huko katika hali ya kutapatapa. Hata mashuhuda wa lile jambo hawakuelewa imekuaje Abunaye mwenye misuli iliyoshiba ashindwe kujitoa kwenye mikono ya kijana yule mdogo. Naam, ilikua ile siku aliyoapa kumlinda Taji.


Kichwani mwa Abunaye bado aliamini yeye ni ndoto ya kutisha ya Taji. Asijue kijana yule ni mzaliwa wa Nahori iliyosifika kwa watu wake kuwa na uwezo mkubwa wa kiakili na kimwili. Taji hakuwahi kuzionesha nguvu zake mbele yake akiwa na hofu kubwa ya kuitwa Mzimu na kutimuliwa pale kijijini. Aliamini angewaponza Wazazi wake pia, wangetimuliwa wote. Na sasa amekutana na Rafaeli, amejitambua yeye ni nani na kwanini yupo pale.


******************************************


Abunaye na upanga wake mkononi aliendelea kupiga hatua za harakaharaka huku akiwa amefura kwa hasira. Hakuwa katika akili yake ya kawaida tena. “Nitamuua yeye na familia yake yote.”, aliyasema haya kichwani mwake huku akizidi kuzipita. Njia ile ilikua inakatiza karibu na maskani ya Sipora na ni katika eneo lile ndipo Abunaye alipogumiana uso kwa uso na kiumbe alichodhani kitakua kimestarehe nyumbani mwake huku kikipata kifungua kinywa asubuhi ile. Abunaye akagwaya, akafunga breki ya ghafla. Taji kasimama mbele yake na tabasamu tele usoni pake.


Sipora aliyekuwa anajishughulisha na kutwanga mihogo kwenu kinu kilichokuwa upenuni hapo, aliweza kushuhudia vizuri lile tukio. Naye akajiona ana mkosi mkubwa kuwaona watu wale kwenye makazi yake. Huyu mmoja alimpiga hadi akazirai, huyu mwingine ni juzi tu wamemtilia shaka ni Mzimu. Mzimu unaompenda shoga yake Sara.


“Aah we!”, akapayuka huku akiuacha mwichi na kinu chake palepale upenuni akakimbilia ndani kwa mwendo wa kujikwaa. Hakuna aliyekuwa na mpango naye kati ya wale mafahari wawili.


“Leo unakufa.”, aliongea Abunaye huku akimsogelea Taji, kauandaa upanga wake vyema kwa ajili ya kucharanga. Taji bado katabasamu.


“Dharau, ananidharau huyu!”, Abunaye alipatwa na jazba maradufu sasa. Akashusha upanga uliokusudiwa utue kwenye utosi wa Taji na kwa ajabu akaambulia patupu. Taji ambaye hakuonesha dalili za kukwepa pigo lile alikua amesogea upande wa kushoto kidogo kama hatua moja. Abunaye asielelewe kilichotendeka pale, akajaribu bahati yake tena. Majibu yakawa yaleyale. Patupu.


“Je, haijakujia akilini huyu unayepambana naye sio wa uwezo wako?”, aliuliza Taji kwa sauti ya upole kabisa, huku lile tabasamu lake zuri likianza kuyeyuka taratibu. Yawezekana uvumilivu ulianza kumuishia. Abunaye ni kama hakujali yale maneno akiwa anahema kwa kasi alishusha tena upanga wake, safari hii shingo ya Taji ikiwa ndio mlengwa.


Sio tu hakuwa na bahati safari hii bali pia aliweza kusikia sauti ya kitu kizito ikiwa imekita kwenye kifua chake kipana kilichojazia na kujikuta yupo hewani hadi alipokita kwenye kinu cha Sipora. Nguvu alizobakiza Abunaye zilikuwa za kukohoa, sio kikohozi cha kawaida. Kikohozi cha damu.


Taji akamfuata pale chini huku tabasamu lake likiwa llimerejea usoni pake. Akamuinua kama anamuinua rafiki yake na mkono mmoja wa Abunaye akauupitisha begani pake kana kwamba anamkokota majeruhi wa mchezo wa mpira wa miguu.


“Sipora, sisi tunaondoka na tabia yako mbaya hiyo, ukashindwa hata kutupikia chai.”, aliongea Taji kwa sauti ya juu akiwa na uhakika Sipora anamsikia kutoka moja ya kidirisha cha mbele alipokua anachungulia mchuano ule. “Ameongea na mimi leo.”, Sipora naye akawaza japo hofu bado anayo.


***********************************************


“Taji vipi tena.”, aliuliza Moha kwa wahka baada ya kumuona Taji anakaribia eneo la makazi ya Chifu akiwa anamkokota Moh aliyeonekana wazi hajiwezi. “Twende naye ndani ataeleza kila kitu,tafadhali.”, alisihi Taji na Moha akawaamuru walinzi wamruhusu kupita. Baadae kidogo Abunaye akapata nafuu, aibu na majuto yamemjaa usoni.


Naye Chifu Harani akasogea eneo lile na kupewa mkasa wote uliotokea. “Nimekuwa nikiwaonya kuhusu huyu kijana lakini hamkusikia, sasa wewe Abunaye utakuwa wa mfano, utatupwa kwenye maporomoko upasuke vipand vipande.”, aliongea Chifu Harani akiwa amefurwa na hasira. Abunaye macho yalimtoka pima, alikiona kifo hiki hapa. AMA KWELI MWISHO UBAYA NI AIBU.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…