SEHEMU YA NANE
“Sio kazi bure komredi…akaunti zetu zimenona…tuombe tunusurike tu hapa…” Imraan alimjibu.
“Kweli kaka…”
Safari yao iliendelea bila ya tukio lolote…
________________
Saa moja baadaye helikopta ilitua pembezoni mwa jiji la Islamabad, na mara baada ya Imraan na kundi lake kuteremka,rubani aliirusha tena ile helikopta na kutokomea angani.
Imraan aliwaongoza wenzake kimya kimya, wakikata mitaa kadhaa kabla ya kutokea kwenye kituo cha teksi. Walionekana kama wenyeji watatu tu waliokuwa na mgeni wao mmoja wa kiafrika wakitoka kwenye moja ya sehemu kadhaa za starehe, ambazo kwa mazingira ya nchi ile zilikuwa ni za siri sana.
"Okay makomredi...mimi naelekea kwangu sasa. Ninyi mtarudi kwenye mahoteli yenu na kukipambazuka mtoweke nchi hii...si tiketi na pasipoti zenu viko sawa?" Imraan aliwaambia na kuwauliza wenzake.
"Yah...tuko vizuri..."Mmoja alijibu.
"Okay..tutawanyike. Ikiwa kutatokea kazi nyingine ninajua nitawasiliana vipi na nyie..."
"Kuna kazi tena na dalali wako wa madili keshadunguliwa kule?" Mwenzake mmoja alimuuliza.
Imraan akafyatua kicheko kifupi, kisha akamjibu, "Kufa ndio sehemu kuu ya kazi yetu kaka…ndio maana hata kama mmoja wetu angeuawa leo hii, bado hela yake ingetumwa tu kwenye akaunti yake, familia yake ikanufaika. Kafa yeye...sio harakati, bwana. Atawekwa mwingine wa kusimamia mambo haya badala yake...na atanitafuta tu muda ukifika..." Alimjibu.
Kila mmoja akachukua teksi yake na kuelekea kwenye hoteli aliyofikia. Imraan alimuelekeza dereva wa teksi yake amrejeshe nyumbani kwake...ambako alipaacha kwa siku kadhaa alipokuwa ameenda kwenye misheni ile ya hatari.
________________
CNN ndio walikwa wa mwanzo kutangaza juu ya shambulizi lile kubwa kabisa la ndege zisizo na rubani dhidi ya ngome kuu ya wataleban iliyokuwa kilomita saba kutoka kwenye kile kijiji cha Dargah Mandi.
Kupitia taarifa ile, dunia ilihabarishwa kuwa kiongozi mkuu wa wataleban ndani ya Waziristan alikuwa ameuawa pamoja na wafuasi wake wengi wakiwemo wale wa Al-Qaida waliokuwa wamehifadhiwa kwenye ngome ile.
Aidha, CNN ilihabarisha kuwa katika kampeni ile ya mashambulizi iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya jeshi la marekani na lile la Pakistani, jeshi la shirikisho lilifanikiwa kumtia mbaroni gaidi muhimu aliyehusika katika ulipuaji mabomu ubalozi wa Marekani nchini Tanzania mwaka 98, aliyekuwa akisakwa sana, Nouman bin Fattawi...lakini helikopta aliyokuwa akisafirishwa nayo kutoka Pakistani ilidunguliwa na vikosi vya wapiganaji wasiojulikana na yeye pamoja na watu wengine saba waliuawa. Mpaka muda habari ile inarushwa hewani, hakukuwa na kundi lolote lilojinadi kuhusika na udunguliwaji wa helikopta ile. Habari hii ilidakwa na vyombo vingine vya habari na kusambaa dunia nzima.
Ni habari iliyoleta kizaazaa kikubwa nchini Tanzania...
___________________
Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam, Tanzania. Wiki moja baadaye:
Umma wa watu ulikuwa umefurika kwenye makaburi ya kisutu. Muda ulikuwa ni saa kumi za alasiri. Ufurikaji wa umma makaburini pale haukutokana na kwamba kulikuwa kuna mtu maarufu aliyekuwa akizikwa siku ile, La Hasha. Mfuriko ule ulitokana na ukweli kwamba kulikuwa kuna marehemua watano waliokuwa wakizikwa siku na wakati ule, na hivyo kulikuwa kuna makundi matano ya ukubwa tofauti kwenye makaburi matano yaliyochimbwa sehemu tofauti ndani ya uzio wa eneo lile la makaburi maarufu jijini.
Ni kutokana na ujumla wa makundi yale matano yenye ukubwa tofauti kuwa ndani ya eneo lile kwa wakati mmoja, ndipo taswira ya umma wa watu kufurika ilipopatikana makaburini pale.
Nje ya uzio wa makaburi yale magari mengi yalikuwa yameegeshwa pande zote za barabara finyu, kiasi kwamba ilikuwa ni shida kwa magari mengine kupita tu pale barabarani, wachilia mbali kupishana.
Kwenye kaburi lililochimbwa pembeni kabisa ya eneo lile la makaburi, upande wa kushoto mara baada ya kuingia kwenye geti la makaburi yale, kulikuwa kuna kundi la wastani la wanandugu waliokuwa wakimzika mpendwa wao, wakiongozwa na sheikh aliyekuwa mjuzi katika taratibu za kuendesha maziko. Lilikuwa ni kundi lenye huzuni kwa kuondokewa na ndugu na jamaa yao ambaye hata hivyo wamekuwa mbali naye kwa muda mrefu, siku zote hizo kabla ya umauti kumkuta mpendwa wao, wakiwa wamegubikwa mashaka mazito juu ya hatma yake…mpaka habari zilipowafika kuwa hatimaye mpendwa wao alikuwa ameuawa kwenye kifo kibaya kabisa, huko ughaibuni.
Walikuwa wamekusanyika kumzika Nouman Fattawi.
Kaka, mwana, mjomba, rafiki, mpenzi…na kwa wengine, ndugu yao katika imani.
Hata hivyo, hawa wote walikuwa ni sehemu moja tu ya wale waliokuwapo kwenye mazishi ya Nouman Fattawi siku ile.
Pamoja nao walikuwepo wana usalama wa taifa, ambao walikuwa pale kushuhudia maziko ya gaidi aliyekuwa akisakwa na wamarekani kwa udi na uvumba, akihusishwa na ulipuaji wa ubalozi wa marekani jijini Dar miaka kumi na minane iliyopita… na pia kuwatazama kwa makini wote waliokuwa wamefika kwenye mazishi ya mtu yule hatari sana kuwahi kutokea kwenye historia ya Tanzania tangu vita dhidi ya kile kilichokuja kunadiwa na kutambulika kama “ugaidi” inadiwe duniani. Na ni kutokana na kulijua au kulitarajia hilo ndio maana hata kundi lililokuwa kwenye maziko ya Nouman Fattawi jioni ile pale kisutu ndilo lilikuwa dogo kuliko yale mengine manne yaliyokuwa pale makaburini siku ile.
Ni nani anayetaka kuhusishwa na gaidi?
Hakuna…isipokuwa kama ni ndugu wa damu au wa karibu sana…au ambaye yuko bega kwa bega na harakati za marehemu kiasi kwamba hajali iwapo na yeye atahusishwa na harakati hizo.
Na ni hawa wa mwisho ndio ambao wanausalama waliojipenyeza kwenye maziko yale, wakiwa wamejivika kanzu na vibaraghashia ili kufanana na waombolezaji halisi wa tukio lile, ndio waliokuwa wakijaribu kuwabaini kwenye mkusanyiko ule. Walitaraji kupata cha kuwaongoza kwenye azma yao ile kutoka kwenye mawaidha ya mwisho yatakayotolewa na yule shekhe atakapomaliza kuongoza maziko yale.
Lakini pia walikuwepo watendaji wa shirika la ujasusi la marekani, C.I.A., ambao nao walikuwa ni weusi kama wengine pale kaburini, wakiwa wamejivika mavazi muafaka kwa tukio lile, na ambao pia walijua namna ya kuitikia dua zilizokuwa zikielekezwa na shekhe mazikoni pale. Lengo lao lilikuwa ni kujithibitishia kuwa kweli gaidi waliyekuwa wamemtamani kwa miaka mingi, hakika alikuwa amezamishwa ndani ya tumbo la ardhi jijini Dar…ili watakapopeleka ripoti huko kwenye makao yao makuu kule Langley, Virginia, wawe na ushahidi wa dhahiri kabisa kwa kile walichokishuhudia. Lakini vilevile, uwepo wao pale ulikuwa na lengo la kujaribu kuona iwapo kutakuwa kuna atakayepandwa na jazba pale makaburini na kubwabwaja kulipiza kisasi kwa wamarekani kwa kifo cha yule mshirika wao…au kuona yeyote ambaye angeelekea kuwa alikuwa akishirikiana na marehemu kwa namna moja au nyingine.
_________________
Maziko yaliendelea kama ilivyotakiwa. Kutokana na namna mwili wa marehemu ulivyoharibika, ulizikwa kwa shida sana, kilichozikwa kikiwa ni mabaki yaliyopatikana ya mwili wake. Baada ya mwili kuingizwa kaburini na kuzikwa, shekhe alitoa mawaidha kwa wafiwa kuwa wawe wastahamilivu, na kuwa Nouman Fattawi alikuwa ameshakunywa kifo chake kutoka kwenye gilasi ya umauti, ambayo sote hapa duniani tumeahidiwa kunyweshwa baada ya muda fulani…hivyo wote waliobakia pamoja na yeye mwenyewe walikuwa wana gilasi zao zinazowasubiri.
“Siku gani…saa ngapi…mahala gani na sisi tutaletewa gilasi zetu za umauti haijulikani. Mwenzetu kapelekewa gilasi yake Pakistani, lakini huenda kuna miongoni mwetu ambaye ya kwake inamsubiri hapo morogoro road akiwa njiani kutoka hapa mazikoni…basi na tushike ibada ndugu zangu, tumrejee mola wetu na tuchukulie kifo cha ndugu yetu, mpendwa wetu, mwana imani mwenzetu, raia mwezetu huyu…kuwa ni ukumbusho kwetu sisi tuliobaki…”
Shekhe alimalizia. Akapiga “Fat-ha”, kisha akaomba dua ndefu kwa lugha ya kiarabu. Watu wakaitikia dua. Alipomaliza akaruhusu watu kutawanyika kwa maelezo kuwa wanafamilia wamesema kuwa hakutakuwa na matanga nyumbani kwao. Hakuongelea hata neno moja kuhusu ugaidi wa Nouman Fattawi wala namna alivyokufa.
Maziko yakaisha.
Watu wakatawanyika.
Wanausalama wa taifa na wenzao wa C.I.A. wakaambulia kunufaika na mawaidha tu ya shekhe kwenye maziko yale.
Kutokea chini ya mti uliokuwa hatua kadhaa kutoka kwenye kaburi la jirani ambako napo maziko mengine yalikuwa yakiendelea, mtu mmoja mrefu aliyevaa suruali nyeupe ya kitambaa chepesi, viatu vyeusi vya ngozi bila ya soksi na shati jeupe la mikono mirefu ambalo hakulichomekea, wala hakuwa amelifunga vifungo kiasi cha kuionesha fulana nyepesi nyeusi aliyoivaa chini ya shati lile, alikuwa akifuatilia kwa makini sana kile kilichokuwa kikiendelea sio pale kwenye yale maziko aliyokuwa amesimama karibu nayo, bali kule kwenye maziko ya gaidi Nouman Fattawi.
Usoni alikuwa amevaa miwani ya jua iliyoficha macho yake, na kichwani alikuwa amevaa barghashia moja ghali sana. Kwa pale alipokuwa amesimama kando ya mti, uso wake ulikuwa umeelekea pale kwenye yale yaliyokuwa yakiendelea kwenye maziko yaliyokuwa jirani na ule mti aliokuwa amesimama chini yake, miongoni mwa wazikaji wengine, lakini macho yake yaliyokuwa nyuma ya miwani ile myeusi, na masikio yake vilikuwa kule kwenye kilichokuwa kikifanyika kwenye kaburi la Nouman Fattawi.
Na sasa alibaki pale pale chini ya mti wakati akiwatazama watu waliokwenda kumzika Nouman wakitawanyika, ilhali wale waliokuwa wakimzika marehemu wa kwenye kaburi alilokuwa amesimama kando yake, wakimalizia kumfukia yule marehemu wao pale kaburini.
Alibaki akiwa amesimama pale pale chini ya mti hata pale wale watu waliokuwa wakimzika yule marehemu mwingine walipomaliza na kutawanyika…
****Doh, katoka Nouman, kaja mzee wa chini ya mti...nini hii sasa?