RIWAYA YA ANGAMIZO 5

Joined
Feb 5, 2016
Posts
16
Reaction score
4
RIWAYA: ANGAMIZO
MTUNZI: HALFANI SUDY
SIMU: 0674 395733
WHATSAPP: 0757 633010
SEHEMU YA TANO

ILIPOISHIA JANA.....
Walimaliza kuongea na Mayasa saa nne usiku. Walikodi gari iliyowarejesha Arusha mjini. Sasa Abdul alihamia himaya mpya. Himaya ya Mayasa, alimkabidhi kila kitu Mayasa kuhusu maisha yake, kasoro moyo tu. Alipunguza mawasiliano na Raiya na kuongeza mawasiliano na Mayasa.

SASA ENDELEA.....
Ilikuwa siku ya jumatano jioni ya wiki ya pili tangu waanze chuo. Abdul alikuwa na Mayasa wanajisomea darasani muda wa jioni. Simu ya Abdul iliita. Alikuwa Raiya anapiga.
"Wewe unajifanya kiburi. Mimi nimekusomesha umefika Chuo unajifanya mjanja. Sasa kesho nakuja huko huko Arusha nione kinachokuzuzua. Ole wako nisikie una mwanamke. Ole wako!"
Bila salamu Raiya aliwaka kwenye simu. Abdul hakumjibu. Alikata simu na kuizima kabisa. Hamu ya kusoma ilimuisha. Mayasa alisikia kila kitu alichosema Raiya. Raiya alimkaripia kama mtoto Abdul na kwa nguvu.Halafu walikuwa karibu na Mayasa. Alimuonea sana huruma. Hamu ya kusoma ilimuisha. Alimuaga Mayasa na kurudi hosteli. Alifika kitandani na kulala chali. Alifikiria mustakabari wa maisha yake. Alijiona ni mtu mwenye mikosi. Aliulaumu umaskini wake. Aliulaumu umaskini wa wazazi wake. Machozi yalitoka yenyewe taratibu.
Akauhisi mkono laini ukimfuta machozi. Alifumbua macho yake na kuangalia. Alikuwa Mayasa..
"Acha kulia Abdul. Nimejitoa kukusaidia kwa lolote kaka yangu. Naamini tutaushinda mtihani huu.Tutamshinda Raiya. Sitokubali ulie tena."
Mayasa alimbembeleza sana Abdul. Mwishowe akamwelewa. Akanyamaza.
Ilipita wiki moja tangu Raiya ampe vitisho vyake Abdul. Hakutokea Arusha wala hakumpigia simu. Akajua labda amekata tamaa. Akawa anaishi maisha yake kama kawaida. Furaha ikarejea tena.Huku akimtegemea Mayasa kwa kila kitu. Naye hakuchoka. Alimsaidia Abdul.
Upande wa darasani alikuwa anafanya vizuri sana katika masomo. Alikuwa na uwelewa mkubwa sana. Mayasa hakuwa VIzuri sana darasani. Alijitahidi kumsaidia kila alipopata nafasi. Alielewana sana na Mayasa. Walifatana muda wote. Walijisomea pamoja. Walikuwa mithili ya chanda na pete. Kila mwishoni mwa wiki walikuwa wanatoka nje ya jiji la Arusha kutembea na Mayasa.
Siku moja jumamosi Abdul na Mayasa iliwakuta Same. Sasa walikuwa marafiki walioshibana. Abdul alikuwa anafahamu sasa baadhi ya vitu vya Mayasa. Kumbe baba yake Mayasa alikuwa, Ally Hamisi. Makamu wa raisi wa Zanzibar. Baba yake alikuwa mtu mkubwa sana Serikalini lakini hakuna hata siku moja aliyemtamkia mdomoni Abdul. Alisikia tu kutoka kwa watu wa pembeni.
Siku waliyoenda Same, walirudi chuoni saa kumi na mbili jioni kutoka. Same Ilikuwa mbali kidogo na Jiji la Arusha. Mayasa alimrudisha kwanza Abdul hosteli ili na yeye arudi kwao. Walienda Same na gari Mayasa. Walipofika karibu na chumba cha Abdul, nje walikutana na Justus. Kijana aliyekuwa wanakaa chumba kimoja pale hosteli.
"Daah afadhali umerudi Abdul, kuna mgeni wako ndani"
"Nani ?" "Simfahamu, ila amefika zamani sana"
"Sawa kaka" Waliingia ndani na Mayasa. Wakiwa hawana wasiwasi hata kidogo. Walipofungua mlango na kuingia ndani walimwona msichana amelala kitandani kwa Abdul. Wote walistuka sana! Walipomwangalia kwa makini, Abdul alimgundua msichana yule. Alikuwa Raiya .
"Naitwa Raiya Mohamedi" Aliongea huku akimwangalia Mayasa usoni.
"Naitwa Mayasa Ally" Mayasa nae alijibu kwa kujiamini.
"Wewe ndiye unajifanya unajua kutembea na wanaume wa watu ?"
"Sema kilichokuleta "
"Kilichonileta ndio hiki ninachoongea "
"Usione vyaelea dada......"
"Sina muda wa kuongea na wewe"
"Abdul ?" Raiya aliita.
Hakuitika.
"Umenisaliti kwa sababu ya hiki kikaragosi ?" Abdul alikaa kimya anamwangalia tu.
" Kumbuka nilipokutoa Abdul, Kumbuka Siku ile pale Mwenge, ningekuacha ungekutana na hiki kikaragosi leo ? " Raiya aliongea maneno yaliyomuingia kidogo Abdul. Pamoja na madhaifu yake kadhaa lakini Raiya alikuwa na mchango mkubwa sana katika maisha ya Abdul hadi alipofikia sasa.
"Sasa chagua moja Abdul. Utakuwa na mimi au huyu ?" Raiya aliongea kwa jazba. Abdul alibaki njia panda. Raiya na Mayasa wote walikuwa na mchango mkubwa katika maisha yake. Na wote walimwangalia yeye kusubiri jibu langu.
" Mayasa siyo mpenzi wangu" Alijua ametamka kwa sauti kumbe sauti haikutoka nje. Mdomo ulikuwa unatetemeka tu.
"Chagua Abdul"
"Achague nini, mimi Abdul siyo mpenzi wangu "
"Ni nani yako sasa ?"
"Rafiki yangu tu "
"Hahaha siku zote mapenzi yanaanzia kwenye urafiki, "OK marafiki. Basi mimi ni mke wa Abdul. Nasema naomba muvuunje kabisa huo urafiki wenu. Siutaki, siutaki, siutaki hata kuusikia. Mkewe nimesema !"
"Raiya wewe ni mke wa Abdul ?"
"Hilo jibu uliza swali "
"Una hakika Raiya ?"
"Ndio"
"Na Salehe je, unamwitaje Raiya ?" Swali hilo allouliza Mayasa lili mstua sana Raiya. Hali sasa ilibadilika mle ndani!
"Mimi ni Mayasa Ally Hamisi, unanikumbuka ?" Mumeo Salehe ni kaka yangu. Mtoto wa mama mdogo Fatma. Au nimpigie Salehe nimuulize kama kakuacha ?" Mayasa aliongea huku akitafuta namba za Salehe katika simu yake.
Raiya sasa alikuwa amechoka hoi. Hajui lipi aseme, lipi aache. Alikosa kauli kabisa. Ghafla alitoka nje ya hostel kwa ghadhabu mithili ya roketi, bila ya kuaga.
Abdul aligundua kitu kimoja kuhusu Mayasa. Mayasa alikuwa msichana msiri sana. Alimficha cheo cha baba yake hadi sasa. Pia kumbe alikuwa anamficha kama Raiya ni wifi yake, hakumwambia kabla. Alianza kumwangalia Mayasa kwa jicho la kumuogopa sasa.
"Usijari Abdul. Raiya ni wifi yangu lakini yeye hakuwa ananijua. Tulionana na Raiya siku moja tu. Tena siku ya harusi yake na kaka Salehe. Hata wewe ulivyonisimulia historia ya maisha yako. Ulipotaja jina la Raiya sikujua kama Raiya wifi yangu, sikufikiria kabisa. Leo nilivyomwona hapa ndio nimemkumbuka ". Mayasa alimjibu kitu ambacho alikuwa akifikiria.
"Sawa Mayasa nimekuelewa" Walitoka nje ili kumwangalia Raiya ameenda wapi ?
Hawakumuona.
Hawakujua ameelekea wapi? Aliyeyuka mithili ya upepo. Baadae Mayasa aliaga na kuondoka kwao huku Abdul akibaki na wingi wa mawazo. Abdul alisinzia akiwa na mawazo mengi. Lakini kutokana na uchovu wa kutoka Same na ukijumlisha mawazo aliyomletea Raiya ndio yalimchosha kabisa, alilala fofofo.
Saa kumi usiku simu yake ilitoa mlio wa sauti alioutega Kwa ajiri ya mwitikio wa ujumbe mfupi. Ikimaanisha kuna meseji mpya iliingia.
'Umeuchokoza moto. Niliacha zamani ukatili. Wewe unajitahidi kunirudisha huko. Nilikuwa katili sana zamani. Kama hupendi nirudie tabia zangu za zamani nakuomba achana na kikaragosi. Nitakuuwa, nitamuuwa pia!.Nakupa siku tatu za kufikiria juu ya suala hili. Mimi bado nipo Arusha. Namaanisha!"
Abdul alikaa kitandani na kuurudia kuusoma ujumbe ule mara tano. Jasho lilikuwa linamtiririka kama maji. Akamtumia ule ujumbe na Mayasa.
Hakuujibu.
Hajaujibu mpaka leo!
Asubuhi na mapema watu wanne walienda katika chumba cha Abdul. Walikuwa wamefuatana na kiongozi wa hosteli, Mshauri wa wanafunzi, na Raisi wa Chuo. Walimuita pembeni na kumwambia.
"Sisi ni askari wa kituo kikuu cha Polisi Arusha. Unahitajika kituo cha Polisi kwa mahojiano kidogo "
"Nimefanya nini jamani ?"
"Utajua hukohuko kituoni!
Askari mmoja alimnyanyua kwa nyuma suruali yake na kupelekwa kituoni. Alikuwa anatembelea vidole sasa. Wanafunzi wenzie walimuonea huruma pale chuoni .
Hakujua amefanya nini ?
Hawakujua amefanya nini?
Baada ya kufika kituoni ndipo alipoambiwa kosa lake. Eti alituhumiwa kwa kumuua Mayasa! Na ujumbe wake wa vitisho kutoka kwanye simu yake yake ulikutwa katika simu yake.
Na ulitumika kama ushahidi
.
INAITWA ANGAMIZO...LIKE, SHARE NA TOA USHAURI WAKO KUHUSU RIWAYA HII....ILA NAKUSHAURI USITHUBUTU KUIKOSA SEHEMU YA SITA...JIBU HILI BASI, JE KWELI MAYASA KAFA NA KAMA KWELI NI NANI ITAKUWA KAMUUA MAYASA UNAFIKIRI?
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…