Rostam apokewa `kitemi` kwao Igunga
[FONT=Verdana, Arial, Helvetica, sans-serif]Na Mwandishi Wetu, Igunga
WANANCHI wa Jimbo la Igunga, Tabora, wametuma salamu maalumu kwa mahasimu wa kisiasa na kibiashara wa Mbunge wao, Rostam Azizi, kwa kumpatia mapokezi makubwa.zito.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati Mbunge huyo alipotembelea jimbo hilo, na kupata mapokezi mazito yaliyowakusanya watembea kwa miguu wa rika zote, waendesha baiskeli, pikipiki, Bajaj, mikokoteni na magari makubwa na madogo.
Katika mapokezi hayo yaliyoanzia takriban kilomita tano kabla ya kuingia mjini Igunga, ambayo hajawahi kuyapata Mbunge huyo tangu achaguliwe kwa mara ya kwanza 1994, baadhi ya wananchi wa mji wa Igunga na vitongoji vyake walisema mapokezi hayo wameyafanya ili kutuma salamu kwa mahasimu wa kisiasa wa Mbunge wao, pamoja na kumpongeza kwa ujasiri aliouonyesha katika kujibu mapigo.
"Tulikuwa na shauku ya kumuona moja kwa moja ili tumpongeze kwa ujasiri aliouonyesha wakati akimjibu yule anayetaka kuwasemea Watanzania kwa kutumia magazeti, redio na televisheni zake na kuwatukana watu, wakati hajawahi kuchaguliwa na wananchi kuwa hata mjumbe wa nyumba 10, wala mwenyekiti wa kitongoji," alisikika akisema kijana mmoja mwendesha baiskeli.
Rostam alifanya ziara ya siku moja jimboni Igunga Ijumaa iliyopita, ziara ambayo pamoja na mambo mengine, ililenga kuhani misiba iliyotokea jimboni humo na kuwapa pole wagonjwa wenye maradhi mbalimbali katika kijiji cha Mwisi, ambako ndiko alikozaliwa pamoja na kijiji jirani cha Ndembesi ambako kuna wajomba zake.
Maandamano hayo ya mapokezi kwa Rostam baada ya kuingia mjini Igunga, yalielekea moja kwa moja katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na baadae yeye na wajumbe wenzake wa Halmashauri ya Wilaya, waliendelea na kikao cha ndani, ambacho kilifunguliwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Asha Kimengule.
Aidha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, Mbunge wa Urambo Mashariki, ambaye pia ni Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, na Mbunge wa Viti Maalumu na pia Mumbe wa NEC Taifa, Azuza Sleyum, walihudhuria kikao hicho kama wageni waalikwa.
Akijibu mapokezi hayo, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya kumbukumbu ya Sokoine jioni mara tu baada ya kikao hicho cha halmashauri ya wilaya, mbunge huyo alisema baada ya majibu yake kwa mmoja wa mahasimu hao, kwa sasa hana ‘time' (muda) nao tena na wala hawamnyimi usingizi.
"Sisi watu wa Igunga tunapendana na tunaishi kama ndugu wa baba na mama mmoja. Hatuna tabia ya kutuhumiana wala kuhukumiana. Watu kama hawa ni ‘kuwabebye', nashukuru nanyi kuniambia hapa kwamba ‘mmewabenye," alisema Rostam na kufuatiwa na makofi na vigelele kutoka kwa mama waliohudhuria.
‘Kubedye' ni neno la Kisukuma na Kinyamwezi, lenye maana ya kuwadharau. Kwamba wananchi wa Igunga, wamewadharau mahasimu wa Mbunge huyo.
Akizungumzia mahasimu wake hao bila kuwataja majina, Mbunge huyo alisema kipo kikundi cha watu wachache walioko Dar es Salaam na Dodoma, ambao wameamua kuchafua rekodi nzuri za watu. Alisema tayari watu hao wamepenya hadi ndani ya Mkoa wa Tabora kwa lengo la kuwafitinisha wabunge wa Mkoa huo ili wasielewane.
"Hawa ni mahasimu wa kisiasa na wengine ni mahasimu wa kibiashara. Hawa ni watu wanaotapatapa, wana agenda zao za kisiasa nje ya utaratibu wa chama na wengine wana chuki zao binafsi za kibiashara, mimi kama mjumbe wa NEC ninayewakilisha Mkoa wa Tabora, nitaendelea kushirikiana na wabunge wote wa mkoa huu kuleta maendeleo katika majimbo yote ya mkoa wetu," alisema Rostam.
Akiwakumbusha wananchi wake baadhi ya mambo waliyoshirikiana kuyatekeleza kwa ajili ya maendeleo yao, Rostam alisema Igunga ndio wilaya pekee nchini, si tu yenye zahanati katika kila kijiji, bali iliyoweka utaratibu wa bima ya afya kwa kila kaya, gari moja la wagonjwa lenye redio ya upepo (radio call) katika kila tarafa, pamoja na zahanati zisizokaukiwa dawa.
Alisema, Igunga ya 1994 wakati anapata ubunge, ilikuwa na shule za sekondari tatu, lakini leo ina sekondari 29, sawa na sekondari moja katika kila kata. Aidha, alisema aliikuta wilaya hiyo ikiwa haina umeme, lakini leo karibu vijiji vyote vimefikiwa na umeme, na vinapata mawasiliano ya simu kupitia mitandao yote ya simu nchini.
"Tuna kiwanda kikubwa cha kisasa na cha mfano hapa Igunga cha kuzalisha mafuta ya pamba, na mwakani kitaanza kusokota nyuzi za pamba.
"Tuna mabwawa 40 ya maji kwa ajili ya kilimo na mifugo yetu, kuna mradi mkubwa umeanza wa kuweka mtandao wa maji safi na salama hapa mjini na katika vijiji vyote vya wilaya hii, najua tuna safari bado ya kuelekea kwenye maisha bora, lakini nawahakikishieni Igunga tunapaa ikilinganishwa na wilaya nyingine nchini."
Kabla ya Mbunge huyo kupewa jukwaa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mgeja na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Kapuya, walipewa fursa ya kuwasalimia wananchi wa Igunga.
Katika salamu zake, Mgeja alisema Igunga anayoijua ya mwaka 1994 kabla ya Rostam kuwa Mbunge si Igunga hii ya sasa baada ya kushikwa na Mbunge huyo.
Alisema wote wanaomchokonoa Mbunge wao, wamejawa na wivu wa maendeleo, kwa hiyo akawataka wananchi hao kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao ili awaletee maendeleo zaidi.
Kwa upande wake, Profesa Kapuya katika salamu zake alizoziwasilisha kwa kutumia zaidi methali na hadithi za kale, alisema wahenga wa zamani, ingawa hawakuwa wamesoma wala kulijua darasa, waliweza kutoa maono ambayo hadi leo yanaendelea kutuongoza.
Alitolea mfano wa methali isemayo; "Asiyekujua hakuthamini' na ile ya ‘Ukiona vinaelea vimeundwa.' "Ndugu zangu, asiyekujua, anaweza akakupuuza, akakutukana na kukukejeli. Lakini, kwa unayemjua sivyo, nyie na sisi Urambo ndio tunaojua kwamba Rostam ni lulu kwetu, tusiipoteze," alisema Kapuya.[/FONT]