Udhaifu wa viongozi unaua michezo
Ibrahim Mkamba Septemba 17, 2008
LEO natanguliza kwenu wasomaji wa safu hii ombi la msamaha kwa kuanza na maelezo yanayoonekana hayahusiani na michezo.Naomba uvumilivu wenu, tutaelewana tu.Viongozi wetu wengi wa sasa ni dhaifu wa kuzidi kiwango.Hebu tazama udhaifu wa mmoja wao.
Anatetemeshwa kidogo na maandamano ya vitoto vyetu vya shule ya msingi na sekondari kuhusu suala la ongezeko la nauli ya daladala toka shilingi 50/= kwenda 100/= anavipooza vitoto hivyo kwa kuvipa ukubwa wa kukaa kwenye viti vya mabasi vikishalipa hiyo shilingi 100/= vinavyopewa na watu wanaolingana na wale wanaovigomea viti kwenye mabasi!
Matokeo yake, zaidi ya uhasama wa makondakta wa daladala na wanafunzi, umezuka uhasama mwingine wa ndani kwa ndani baina ya wanafunzi hao na watu wazima unaodhihirishwa na wao (watu wazima) kuacha kuwa watetezi wa wanafunzi pale wanaponyanyaswa na makondakta, tofauti na ilivyokuwa wakati maadili ndani ya daladala yalipokuwa yanaheshimiwa kwa wakubwa pekee kukaa vitini.
Miongoni mwa watu wazima wanaonyimwa viti kwenye mabasi na vitoto ni wazee sana, kina mama wajawazito na wanaobeba watoto pamoja na wagonjwa.Watu kama hao wakiachiwa viti kwenye mabasi,wanaofanya hivyo ni wakubwa waliopata viti lakini si vitoto vyetu vinavyokaa,vilivyosababishwa na viongozi wetu dhaifu visiwe na adabu.Viongozi wetu hao wanaosahau hata maadili yetu kwa udhaifu wao huo uliopitiliza!
Sababu ya kuanza na maelezo hayo ni kuonyesha wazi kuwa, kwa aina ya viongozi dhaifu kama hawa, tusitegemee ikawekwa mikakati madhubuti ya kuinua michezo yetu na ikitokea mikakati hiyo ikawapo,viongozi dhaifu kama hawa hawawezi kusimamia na kuhimiza utekelezaji wake. Kama kiongozi anatishwa na vitoto, anagwaya na kuviambia vikae kwenye viti vya mabasi na wazazi wao wasimame,ataweza kweli kuchachamalia viongozi wa chini yake walioharibu mipango ya maendeleo ya michezo?
Hoja hii imenijia kichwani baada ya kusikia majibu ya jeuri ya walioiongoza timu yetu ya Olimpiki, Beijing, China, ya viongozi wa Kamati ya Olimpiki nchini(TOC) na ya viongozi wa Chama cha Riadha nchini (RT) kila walipohojiwa kuhusu matokeo mabovu mno kwenye mashindano hayo.
Viongozi hao walikuwa jeuri hivyo kwa kujua kuwa hakuna kiongozi yeyote wa Serikali juu yao angechachamalia madudu yao kwa kuutambua udhaifu wa viongozi wetu. Udhaifu huo katika suala hilo ulijionyesha katika kikao cha Bunge kilichopita, pale kiongozi mmoja wa serikali alipolieleza Bunge kuwa matokeo mabaya tuliyoyapata Beijing hayakuwa ya aibu kwa Taifa! Kama huyo anayetarajiwa kuwajia juu waliovurunda katika maandalizi na mipango mingine ya ushiriki huo anautangazia umma kwamba matokeo hayo hayakuwa ya aibu, haishangazi mahojiano kati ya wanahabari na wavurundaji hao yaonekana kama wanahabari ndio waliokuwa wanahojiwa kutokana na kiburi cha wavurundaji hao!
Mwanahabari atauliza,"kwa nini tumefanya vibaya namna hii?" Mvurundaji atasema,"Kwani ni Tanzania peke yake imekosa medali katika mashindano hayo?" Atajibiwa na Mwanahabari,"yapo mataifa mengine yamekosa medali lakini kuna yaliyopata,kwa nini nasi tusipate?" Mvurundaji huyo atasema "Sisi tulipeleka wanariadha wangapi na hao waliopata medali nyingi walipeleka wanariadha wangapi?"
Mwanahabari atapuuza swali hilo kwa kusema"lakini hayo ya wengine hayatuhusu, ninakuuliza kuhusu matokeo mabaya ya timu yetu inayotuhusu". Mvurundaji atasema zaidi,"Nani anasema matokeo hayo ni mabaya?" na mazungumzo ya swali-kwa-swali yanaendelea hivyo bila kujulikana anayetakiwa kujibu maswali ni nani kati ya Mwanahabari na Mvurundaji huyo anayeonekana kutojutia kuharibu kazi ya Watanzania! Jeuri.Kwa nini asifanye jeuri wakati anajua hakuna wa juu yake wa kumpa kashkash?
Ili nchi yoyote iendelee kimichezo inapaswa iwe na sera nzuri za kuwatengeneza wanamichezo wa michezo mbalimbali tangu wakiwa wadogo, ziwe za klabu au za kiserikali kutegemeana na tofauti za nchi kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.Vile vile,inapaswa itengeneze majukwaa ya kuvionyesha na kuviimarisha vipaji hivyo kama mashindano ya UMISHUMTA(baadaye UMITASHUMTA), UMISSETA, michezo ya majeshi na SHIMIWI yaliyokuwapo zamani.
Tuko chini sana kimichezo kwa sababu, kwa sasa, tumekosa yote hayo. Ninaposema viongozi imara ndiyo msingi mkuu wa mafanikio kimichezo ninamaanisha kwamba sera nzuri za kutengeneza wanamichezo zitatengenezwa na kutekelezwa kiuhakika chini ya uongozi imara. Majukwaa ya kuonyesha na kuinua vipaji, yatajengwa chini ya uongozi imara. Maaandalizi ya uhakika ya mashindano nayo yatafanikishwa chini ya uongozi imara na inapotokea waliopewa dhamana ya kusimamia ushiriki wa mashindano ya kimataifa wakavurunda, uongozi imara huchukua hatua kali kwa watu hao ili wao au wengine wasirudie kuboronga siku za usoni.
Kwa udhaifu wa viongozi wetu, nani ndani ya TOC na RT ametetemeshwa kutokana na matokeo mabaya ya Beijing na hivyo atazamiwe kujiweka sawa kuanzia sasa asivurunde tena London mwaka 2012? Kwani hata mwaka huo akiwa madarakani na akivurunda tena nani atamfanya nini cha kumtisha!
Wenzetu wanaojali hawafumbii macho ujinga ujinga.Kwa mfano,baada ya timu ya soka ya Express ya Uganda kufungwa na Yanga ya Tanzania magoli 4-0 kwenye mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na ya Kati, Zanzibar mwaka 1975, aliyekuwa Rais wa Uganda wakati huo, dikteta Idd Amin Dada, aliamuru msafara mzima wa timu hiyo ulioshiriki mashindano hayo, isipokuwa wachezaji ambao hawakucheza mechi hiyo,upewe adhabu ya viboko vinne kila mmoja, idadi ya magoli waliyofungwa na Yanga.Walichapwa idadi hiyo ya viboko hadharani! Hata kama Idd Amin alizidisha kiwango, lakini hivyo ndivyo anavyopaswa kutendewa aliyeharibu kazi ya nchi hata kama si viboko vya hadharani.
Kama viongozi wetu wasingekuwa dhaifu kiasi cha kuwagwaya watoto wetu na kuwaelekeza wawavunjie heshima wakubwa kwenye mabasi ya daladala,wangewasimamia vizuri Maafisa Utamaduni na Michezo katika kuwekwa kwa mikakati ya kuendeleza michezo kwenye maeneo yao ya uongozi badala ya kusubiri mafanikio yanayoletwa na wadau tofauti na kuwa mbele kwenye shamra shamra za kushangilia mafanikio hayo na kuyatangaza kuwa ni matokeo ya sera nzuri za michezo za serikali ya chama cha siasa kinachotawala. Si tuliona jinsi sera za CCM zilivyohusishwa na ushindi wa Big Brother Africa 2(BBA2) wa Mtanzania Richard Bezuidenhout mwaka jana mwishoni?
Ni vizuri viongozi wetu wa leo wangejifunza toka kwa Dk.Lawrence Gama na Abubakar Mgumia walioshughulikia sana maendeleo ya michezo katika kila mkoa walioongoza kama wakuu wa mikoa.Waliagiza utekelezaji,waliukagua na kukosoa utekelezaji huo,wakiwawajibisha wazembe na matokeo yake yakawa mazuri kimichezo kwenye mikoa hiyo iliyokuwa nyuma kimichezo kama Ruvuma na Tabora kwa Dk Gama na Lindi na Kigoma kwa Mgumia.
Wanachopaswa kufanya viongozi wetu wa sasa ni kuwabana kweli kweli Maafisa Utamaduni na Michezo,kama walivyofanya viongozi makini waliotajwa,wawape mipango yao ya kuendeleza michezo.Mipango hiyo iwe madhubuti na waonyeshwe utekelezaji wake.Wote wakifanya hivyo, si kwa kucheka cheka, lazima tutakwenda juu kimichezo.
Litakuwa jambo jema sana pia endapo viongozi wetu wa sasa watajifunza mbinu za uongozi za wenzao wa awamu ya kwanza ambao kila mmoja alikuwa imara katika kutimiza wajibu aliopewa ambapo kwenye michezo kina Jenerali Mirisho Sarakikya,Chediel Mgonja na wengine walisimamia vizuri na kwa nguvu maendeleo ya michezo na matokeo yake nchi yetu ilikuwa juu sana kimichezo. Ni katika awamu hiyo ndiyo kulikuwa na majukwaa ya UMISHUMTA, UMISSETA, Michezo ya Majeshi na kadhalika. Viongozi wetu wa leo wangekuwa na mipango mizuri kama wao,tungekuwa hata na mashindano ya michezo ya vyuo vya elimu ya juu,ikizingatiwa wingi wa vyuo hivyo kwa sasa na umri mdogo,wa kimichezo, wa wanaoingia vyuoni humo miaka hii.
Kutokana na mipango ya kisayansi ya viongozi wa zamani na usimamizi wao madhubuti,mwaka 1974 tulibeba makombe yote ya soka kwa ukanda wa Afrika Mashariki na ya Kati. Januari: Simba ya kina Abdallah "King" Kibaden, bingwa Afrika Mashariki, Dar es Salaam. Mei: Timu ya vijana, matunda ya UMISSETA, ya kina Mwinda Ramadhani "Maajabu", bingwa wa Afrika Mashariki, Kampala.
Oktoba: Timu ya Taifa ya wakubwa, chini ya kocha Marijan Shaaban,bingwa wa Challenge,Dar es Salaam. Kwa mipango mizuri iliyokuwapo,wengi wa wachezaji wa timu hiyo ya wakubwa iliyobeba kombe la Challenge walitoka timu ya vijana, matunda ya UMISSETA.
Baadhi ni Mwinda, Lucas Nkondola, Jellah Mtagwa, Godfrey Nguruko na wengine. Novemba: Simba ilifika nusu fainali ya klabu bingwa Afrika na kutolewa kwa vitisho na Mehalla el Kubra ya Misri kwa penelti.
Kwenye michezo mingine, mwaka huo Filbert Bayi alivunja rekodi ya mbio za meta 1500 kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola kule Christchurch, New Zealand na kuleta nchini medali ya dhahabu.
Rekodi hiyo ya mbio za meta 1500 ilikuwa ikishikiliwa na mwanariadha John Walker wa New Zealand kwa miaka saba! Kipindi hicho tulikuwa na wanariadha wa kujivunia kama Bayi,Suleiman Nyambui,Claever Kamanya, Juma Ikangaa, Gidamis Shahanga, Nzael Kyomo, Mwinga Mwanjala na wengineo.
Kulikuwa na wanamasumbwi wazuri kama Titus Simba na Habibu Kinyogoli.Hata michezo mingine inayopondwa sasa ilithaminiwa na ndiyo maana tulikuwa na wachezaji bora kama Zakayo Marekwa kwenye kutupa mkuki na Nancy Mtawali kwenye kutupa kisahani huku mpira wa pete ukawa na timu kali nyingi za kutosha kutengeneza ligi zenye msisimko mkubwa za madaraja hata matatu!
Litakuwa jambo jema pia endapo viongozi wetu wa sasa watajifunza mbinu za uongozi wa wenzao wa awamu ya kwanza ambao kila mmoja alikuwa imara katika kutimiza wajibu aliopewa kiasi cha nchi kuwa juu sana kimichezo kufikia hatua ya timu yetu ya soka kucheza fainali za mashindano ya mataifa huru (wakati huo) ya Afrika nchini Nigeria mwaka 1980.
Hayo yalikuwa ni matunda ya kuwa na viongozi imara na wakali kwenye kuhimiza utimizaji wa wajibu kwa kila aliyehusika na utekelezaji fulani wa kimichezo.Bila wengi wa viongozi wetu wa leo kuacha kuwa dhaifu kama walivyo,tusiote ndoto ya kupata maendeleo kimichezo.Sera nzuri za kuibua,kuinua na kutunza vipaji vya wanamichezo haziji zenyewe, ni kazi yetu chini ya viongozi wetu.
Jukwaa la kuonyeshea na kuimarishia vipaji halijijengi bali hujengwa na viongozi wetu.Maandalizi ya uhakika ya ushiriki wa mashindano hayaji yenyewe, ni kazi yetu chini ya viongozi wetu na kuwakaripia waliovurunda dhamana ya kuongoza timu za mashindano ni kazi ya viongozi wetu.
Kwa udhaifu wao, nani leo atathubutu kuwaambia TOC na RT "nataka maelezo ya kuridhisha kwa nini msichukuliwe hatua kwa kushindwa kutimiza wajibu wenu"? Kama yupo, afanye hivyo sasa kabla aibu hiyo haijapitwa na wakati.
Source:
raia mwema