MAMBO 20 MUHIMU YA WANANCHI YALIYOTUPWA NA KATIBA INAYOPENDEKEZWA.
UNATAKA KUUJUA UKWELI BASI SOMA HAPA NA MJULISHE MWENZIO.
Katiba Inayopendekezwa ina mapungufu makubwa na imeyatupilia mbali maoni muhimu ya wananchi kama yalivyotolewa na wananchi wenyewe kama ifuatavyo;-
1. Kupunguzwa kwa madaraka ya Rais Wananchi walipendekeza madaraka makubwa ya Rais hasa ya uteuzi yapunguzwe na ziundwe Taasisi za kikatiba za kumshauri Rais kabla hajafanya teuzi. Wananchi walipendekeza pia baada ya Rais kumteua kiongozi basi itabidi mteuliwa huyo Bunge limthibitishe. Katiba Inayopendekezwa imeyafuta haya yote na imemuongezea Rais Madaraka.
2. Kutenganisha Mamlaka ya Mihimili ya Dola Wananchi walipendekeza uhuru zaidi kwa Bunge na Mamlaka zaidi kwa Bunge kuisimamia, kuiwajibisha na kuishauri Serikali. Pendekezo hili linaenda sambamba na kutenganisha serikali na Bunge, hali ambayo iko sasa. Rasimu ya Warioba ililipa Bunge Mamlaka zaidi kuisimamia Serikali na hata pale ambapo Bunge lingekataa bajeti au muswada mbaya wa serikali mara kadhaa, Rais asingeliweza kulivunja Bunge. Wananchi walisema sana Mawaziri wasitokane na wabunge, ili wabunge wafanye kazi ya uwakilishi pekee na mawaziri watumie weledi wao kumsaidia Rais kazi za Serikali.
3. Kumwajibisha Mbunge Rasimu ya Warioba iliwapa wapiga kura uwezo wa kuwawajibisha Wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao wakati wowote (Recall Powers) kama wakienda kinyume na maslahi ya wananchi katika jimbo husika. Wananchi walijiuliza kama mbunge ni mtumishi wao, iweje hayuko katika kituo cha kazi kwa miezi kadhaa na wasiweze kumwajibisha mpaka miaka mitano?
4. Vyanzo vya Mapato vya kuaminika Kuwepo kwa vyanzo vya mapato vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakavyogharimia mambo ya Muungano ambayo yamepunguzwa kutoka 22 hadi 7 lilikuwa pendekezo ambalo hata taasisi za serikali zilipendekeza. Pendekezo la Katiba Inayopendekezwa imerudisha mapato ya Muungano kama Katiba ya Mwaka 1977, na kwa kufanya hivyo tumerudi kwenye mgogoro wa msingi, kuchukua kodi tatu, ushuru wa forodha, ushuru wa bidhaa na mapato kutoka Zanzibar ni kuiua Zanzibar na kuifanya ishindwe kumudu matumizi yake ya ndani kwa mambo yasiyo ya Muungano na vivyo hivyo kwa Tanganyika.
5. Muundo wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili Kwa miaka nenda rudi tumekuwa na kitendawili cha ni muundo gani wa Muungano Jamhuri yetu inao. Kitendawili hiki kimeelezwa na wengi akiwemo Baba wa Taifa Mw. J.K Nyerere. Rasimu ya Warioba iliweka kwa mara ya kwanza Muundo Jamhuri ya Muungano kuwa ni wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili na lenye Serikali 3.
6. Kupunguza ukubwa wa Serikali Wananchi walionesha kutofurahishwa na ukubwa wa serikali unaopelekea matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi. Walipendekeza uwepo wa serikali ya muungano iliyo imara, yenye ufanisi na ndogo. Rasimu ya Warioba ilisema idadi ya mawaziri isizidi 15, Katiba Inayopendekezwa inasema Mawaziri wasizidi 40
7. Tume ya Uhusiano na Uratibu Rasimu ya Warioba ililenga kuhakikisha kunakuwepo uhusiano mzuri, mawasiliano na uratibu wa serikali zote tatu chini ya Mamlaka ya Serikali ya Muungano na kupitia Tume ya Uhusiano na Uratibu. Bunge Maalum lilishindwa kuelewa mantiki ya pendekezo hili na Katiba Inayopendekezwa imelivuruga kabisa, kutoka pendekezo la Warioba la Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali hadi Tume ya Uratibu wa Mambo ya Muungano katika Katiba Inayopendekezwa.
8. Kupunguza ukubwa wa Bunge Wananchi walizungumzia pia ukubwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na gharama zinazoambatana nalo, na wakapendeza bunge dogo na lenye ufanisi mkubwa. Warioba alisema idadi ya wabunge isizidi 75, Bunge Maalum likasema Wabunge 390.
9. Ukomo wa vipindi vya ubunge Wananchi walizungumzia nafasi za ubunge kuhodhiwa na watu fulani kwa miaka nenda rudi na wakapendekeza ifike mahali kuwe na ukomo ili kuleta uwakilishi mpana na mabadiliko. Rasimu ya Warioba iliweka ukomo wa vipindi vya ubunge kuwa vitatu na kuwa na ukomo wa miaka 15 kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Bunge Maalum na Katiba Inayopendekezwa wamefuta pendekezo hili.
10. Kuwepo kwa Tunu za Taifa (Core Values) Wananchi walipendekeza uwepo wa tunu za Taifa (core values) katika katiba, tunu hizi ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa. Raia wa Tanzania walikuwa na wajibu wa kuheshimu tunu hizi lakini Katiba Inayopendekezwa imezifuta tunu hizi.
11. Maadili na Miiko ya Viongozi Wananchi walizungumza kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya jamii, watumishi na viongozi wa umma, wengi wakisema Katiba iainishe Maadili na miiko ya viongozi wa umma ambayo kwayo tutawawajibisha. Katiba Inayopendekezwa imesema Maadili na Miiko kwa viongozi (mathalani kutenganisha biashara na uongozi ili kuepusha mgongano wa maslahi), isiwemo kwenye Katiba bali ikawekwe kwenye Sheria.
12. Masharti yasiyoweza kubadilishwa na Bunge Rasimu ya Warioba iliweka masharti ya kuzuia Bunge kubadili baadhi ya masharti mahususi ya Katiba (entrenched provision) ibara ya 119 isipokuwa kwa ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni (mathalan Malengo Makuu ya Taifa, Haki za Binadamu n.k. Na bahati mbaya tulisahau kuweka na Sura ya 3 juu ya Maadili). Masharti yote ya Ibara hii yamefutwa isipokuwa Muundo wa Muungano na Uwepo wa Jamhuri ya Muungano.
13. Kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi Wananchi walizungumza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia chaguzi za Jamhuri ya Muungano. Ilisisitizwa juu ya umuhimu wa Tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kwamba Mwenyekiti wa Tume na Makamu wake wathibitishwe na Bunge ili kuwapa uhalali wa kitaifa, pendekezo hili limefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
14. Usawa wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume Kuwepo uwiano wa uwalikishi wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume ni lazima kwa mazingira ya sasa. Uwiano kati ya wanawake na wanaume katika vyombo mbalimbali vya dola hasa vile vya kutung sheria limeendelea kuwa tatizo nchini na lililokaa kwa muda mrefu. Wananchi na hasa wanawake na baadhi ya wanaume walipendekeza uwiano ulio sawa katika kufikia fursa hasa ukizingatia wanawake ndio wazalishaji wakubwa. Katiba Inayopendekezwa imefutilia mbali pendekezo hili muhimu.
15. Kuanzishwa kwa Mgombea Huru Haki ya wananchi kushiriki shughuli za umma imekuwa ikizuiwa siku nyingi na kwamba ushiriki katika shughuli za umma kama kiongozi wa kuchaguliwa inapaswa kuwa haki ya msingi ya mwananchi yeyote yule. Rasimu ilitoa haki ya mgombea huru bila vikwazo, Katiba Inayopendekezwa imeweka masharti magumu ambayo hakuna mtu anayeweza kuyatimiza kirahisi, kitendo hiki sio sawa.
16. Msaada wa Kisheria kwa Wananchi Wananchi walieleza kutokuridhishwa kwao na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji huo na wakapenda huduma ya msaada wa kisheria liwe suala la kikatiba kwa mwananchi yeyote yule na serikali iwajibike kutoa huduma hiyo. Katiba Inayopendekezwa imesema wananchi hawatakuwa na haki ya kudai huduma hii kokote nchini, hata mahakama hazitaweza kusikiliza mashauri ama Serikali imetoa haki hii au haikutoa haki hii rejea Ibara ya 21.
17. Uhuru wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Rasimu ya Warioba ilipendekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi atekeleze kazi zake kwa uhuru, bila woga, upendeleo wala chuki na kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na sheria za nchi. Masharti haya yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa
18. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Wananchi Tume ya Warioba ilipendekeza kuwepo kwa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania itakayokuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya utumishi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti haya licha ya wapiganaji kupendekeza utaratibu wa kusimamia maslahi yao Kikatiba.
19. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itakayokuwa na jukumu la kusimamia utumishi wa Jeshi la Polisi. Katika uajiri wa askari wa Jeshi la Polisi, Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itazingatia kanuni na misingi ya utumishi iliyoainishwa katika Katiba hii
20. Misingi ya utendaji wa Jeshi la Polisi Rasimu ya Warioba ilipendekeza kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano litazingatia (a) viwango vya juu vya kitaaluma na nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wake; (b) ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu; (c) kanuni za uwazi na uwajibikaji; na (d) kukuza mahusiano na jamii. Warioba akaendelea kusema, Jeshi la Polisi, katika kutekeleza majukumu yake, litashirikiana na vyombo vinavyohusika na kupambana na uhalifu vya Nchi Washirika katika kufanya uchunguzi na kushughulikia makosa ya rushwa na ufisadi. Misingi hii yote imefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
UKISOMA MPAKA HAPA HAKIKISHA NA MWENZAKO ANAPATA UJUMBE HUU
Daah..nimesoma visababu vyako....naona umedhamiria kupotosha nadhani kwa kutoona umuhimu wa wananchi kufaidika na yale yaliyomo ndani ya Katiba Inayopendekezwa na kudharau idadi kubwa ya wawakilishi wa makundi yaliyobaki kuwakilisha maeneo yao....nashangaa unaleta hoja za kufikirika na zisizomhusu mwananchi moja kwa moja zooote za kisiasa hii inaelekea kuna unachotaka kinachokufanya umsahau mwananchi wa kawaida...nitakuwekea baadhi ya majibu yatakazojibu huu ----- wako humu.....Hlafu mfikishie polepole taarifa mwambie anajiabisha kutoa hoja zinazomfanya aonekane he is not an intelectual mwambie MARAMLA anampenda sana
https://www.youtube.com/watch?v=R944hfzQX7A
https://www.youtube.com/watch?v=kNuZOO4Drzk
MAJIBU YA HOJA ZINAZODAI KATIBA INAYOPENDEKEZWA IPIGIWE KURA YA HAPANA
Hoja
Kupuuzwa kwa maoni ya wananchi kama yalivyoainishwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba. Rasimu hii ya Pili iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilizunguka nchi nzima ikakusanya maoni ya wananchi lakini maoni hayo yamepuuzwa.
Jibu
Katiba Inayopendekezwa imezingatia kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi moja kwa moja, hoja za makundi na taasisi mbalimbali pamoja na zile zilizotolewa na wabunge wa Bunge Maalum la Katiba. Ndani yake haki za makundi mengi zimetajwa na kulindwa, mifumo mbalimbali ya utawala na namna ya kuendesha nchi imeboreshwa na kero nyingi zimepewa ufumbuzi.
Watanzania waliotoa maoni yao moja kwa moja kwa Tume ni 684,303 kutoka Bara na 49,671 toka Zanzibar. Hawa ni watu wachache sana ukilinganisha na Watanzania wapatao 20,000,000 wenye umri na sifa za kupiga kura. Mawazo yao pekee hayawezi kuwa ndio mawazo ya Watanzania wote. Hivyo kudai haya yawe ndiyo mawazo pekee ya kuzingatia na kuachia wengine haingekuwa haki.
Rasimu ya pili ya Katiba ilipaswa kuzingatia maoni toka katika Mabaraza ya katiba ya wilaya na yote ya taasisi ambao wajumbe wake walichaguliwa na wananchi kuingia katika mabaraza haya. Maoni mengi sana toka kwenye Mabaraza haya hayakuzingatiwa na Tume kwenye Rasimu yake ya pili.
Ndani ya Bunge Maalum la Katiba Watanzania waliwakilishwa na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao waliwachagua wenyewe kuwawakilisha na ili hoja toka makundi mbalimbali kuzingatiwa walichaguliwa wajumbe 201 toka makundi mbalimbali ya kijamii kwenye hili Bunge Maalum. Hii yote ilikuwa ni kupanua na kuimarisha ushiriki wa wananchi.
Hoja
Muundo wa Bunge Maalum ulifanya Bunge lijae wanasiasa kwani lilikuwa na wabunge wote, wawakilishi wote hivyo kufanya idadi ya wanasiasa kuwa robotatu ya Bunge lote. Hata wajumbe 201 nao ndani yake kulikuwa na wanasiasa 40 wawakilishi wa vyama. Vilevile kulikuwa na wawakilishi wa AZAKI pia ni makada wakongwe wa vyama vya siasa. Suala hili lilipelekea majadiliano kufuata mrengo wa kisiasa.
Jibu
Bunge Maalum la Katiba liliundwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilisomwa, ikajadiliwa kwa kina Bungeni na kufanyiwa marekebisho kadhaa. Hakuna mtu wala kikundi au chama cha siasa kilicholeta hoja hii iangaliwe na ikibidi ijadiliwe. Kuileta hoja hii sasa ni wazo la baadae.(
An afterthought)
Majadiliano ya kupata katiba mpya ya nchi huhusisha mchakato wa kutengeneza muundo wa serikali, mfumo wa uongozi wa nchi, mfumo wa uchumi wa nchi na mfumo wa ulinzi na usalama wa nchi. Katika kuijadili hii miundo na mifumo haiyumkiniki mitazamo yenye mirengo tofauti ya kisiasa ikasikika katika majadiliano hayo.
Wabunge, wawakilishi na wawakilishi wa AZAKI wanawakilisha wananchi moja kwa moja au makundi mbalimbali ya jamii na wao pia ni sehemu ya wananchi hivyo kushiriki kwao katika kazi hii ni sawa, haki na muafaka.
Hoja
Bunge Maalum la Katiba lilikosa uhakika wa kisheria na kisiasa pale lilipoendelea na majadiliano ilhali baadhi ya wajumbe walikuwa wametoka nje ya ukumbi. Ingepaswa maridhiano yafanyike ndipo Bunge hilo liendelee.
Jibu
Bunge Maalum la Katiba lingeweza kukosa uhalali wa kisheria kama lingefanya shunguli zake kinyume na sheria iliyoliunda mfano kutozingatia akidi, kufanya maamuzi ambayo halina mamlaka nayo, kufanya kazi nje ya siku lilizopangiwa nk. Bunge Maalum la Katiba lilifanya shunguli zake zote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni zake hivyo lilikuwa halali kisheria na lilifanya kazi zake kwa uhalali.
Bunge Maalum la Katiba lingeweza kukosa uhalali wa kisiasa iwapo lingefanya mambo yake nje ya sheria au kwa ubaguzi wa namna yoyote, ubabe au kutozingatia kanuni lililojiwekea. Hili halikutokea kwani Sheria na Kanuni zilifuatwa kwa uwazi na usahihi.
Maridhiano ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kutafuta Katiba mpya. Lakini ni budi pande zinazotofautiana zikubaliane kukutana, kuongea bila masharti yenye kulenga kulazimisha upande mwingine na kila upande ukubali kuwa katika maridhiano kila upande upate na baadhi ya vitu utapoteza. Kundi lisilo rasmi lililojiita UKAWA lilitoka nje ya ukumbi wa Bunge na tofauti na matukio ya nyuma hawakutaka majadiliano ya aina yoyote wala kurudi Bungeni. Mwenyekiti wa Bunge Maalum aliitisha Kamati ya Maridhiano ikutane Dar Es Salaam UKAWA wakakataa, viongozi wa madhehebu yote ya dini waliowaomba warudi Bungeni na wakae kwenye kwenye meza ya mazungumzo wakakataa, Rais wa Jamhuri ya Muungano akawanasihi kufanya kurudi Bungeni wakakataa. Mwishowe Msajili wa Vyama vya Siasa akaitisha vikao vya kutafuta kiini cha tatizo lakini napo UKAWA wakagoma suluhu. Kama kutoka kwa UKAWA kungekuwa na athari ya kisheria na kisiasa kwa mustakabali wa nchi yetu lakini kwa bahati nzuri haiupo, basi lawama ni kwao.
Hoja
Kuweka kwa makusudi kura za wazi na siri ili kuwabana wanachama watakaokwenda kinyume na maslahi ya vyama husika.
Jibu
Bunge Maalum la Katiba lilikuwa linaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria ililoliunda na Kanuni iliyotunga na kupitishwa na wajumbe wake. Uendeshwaji wake ulikuwa hausimamiwi wala kuratibiwa na chama chochote cha siasa hivyo hapakuwa na namna ya kushawishi au kushinikiza aina ya upigaji kura.
Uamuzi wa wajumbe kuamua kupiga kura ya wazi au siri ulikuwa ni Bunge lote tena kwa maridhiano na kwa mujibu wa Kanuni hivyo hapakuwa na kulazimishana.
Wakati wa kupiga kura wajumbe walio wengi hata waliojiita UKAWA walipiga kwa hiari yao kura ya wazi. Hata katika kura ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa wapo wajumbe kwa hiari yao walipiga kura ya wazi kuikataa Katiba Inayopendekezwa.
Hoja
Kuweka kanuni ya kuruhusu upiganaji kura kwa watu waliokuwa hospitali, hijja na kwingine ili akidi itimie.
Jibu
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo iliyounda Bunge Maalum la Katiba ililipa uwezo Bunge hili kutunga kanuni juu ya namna ya kuendesha mambo yake. Bunge Maalum la Katiba lilipitisha kanuni inayompa mjumbe ambae hayuko kwenye eneo la Bunge na ana ruhusa ya Mwenyekiti kupiga kura yake atakapokuwa kwa kuwekewa utaratibu kama akiomba kwa maandishi kwa Mwenyekiti.
Kwa mujibu wa Kanuni iliyotajwa hapo juu wajumbe waliokuwa wamelazwa hospitalini, wako likizo ya uzazi au kwenye ibada ya hijja Saudia waliomba nafasi ya kupiga kura na utaratibu ukafuatwa na wakapiga kura. Hapakuwa na busara ya kuwanyima haki yao ya kupiga kura wakati walishiriki mchakato wote wa majadiliano hadi mwisho na walitaka kupiga kura. Kumnyima mjumbe kupiga kura kwa sababu kaenda kuhudhuria ibada ya hijja au ni mgonjwa hospitalini au kwenye uzazi ni kumnyima haki yake ya msingi.
Hoja
Kutokutimia kwa akidi za kamati mbalimbali walipokuwa wanajadili ndani ya Kamati Rasimu ya Katiba. Akidi ilikuwa haitimii kwani wengi wa Zanzibar walitoka na UKAWA.
Jibu
Hakuna ushahidi wa kitakwimu unaothibitisha kuwa akidi zilikuwa hazitimii hasa za Wabunge toka Zanzibar. Kamati nyingi akidi ilitimia.
Kanuni ziliweka wazi kuwa hata kama 2/3 ya upande wowote haitapatikana katika kupitisha vifungu hii haitazuia ripoti ya Kamati hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge kwa majadiliano na ndipo kura ya mwisho itapigwa na kupitishwa kwa kupata 2/3 toka kila upande wa Muungano.
Hoja
Kulikuwa na kura za maruhani na watu wasiokuwepo Bungeni.
Jibu
Kura zilizopitisha Katiba Inayopendekezwa ni zile zilizopigwa kwa wazi au siri Bungeni na kuhesabiwa chini ya mawakala na matokeo kusomwa. Hapakuwa na kura ya mtu toka nje. Madai kuwa marehemu Shida Salum aliyefariki mwezi Juni 2014 alihesabiwa amepiga kura ni ya uongo na yana sababu ovu kwani yanalenga kuamsha uchungu kwa familia yake kwani hayana ukweli wowote. Madai ya Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Zanzibar kuwa alihesabiwa kupiga kura hayana ukweli kwani utaratibu wa kupiga kura na kuhesabu ulikuwa ndani ya Bunge na hakuwa mmoja wa wapiga kura. Jina lake lilionekana kwenye orodha ya majina ya wajumbe kwenye nakala maalum za Katiba zilizotolewa kwa ajili ya uzinduzi kimakosa na Naibu Katibu wa Bunge alilitolea maelezo kuwa yalikuwa ni makosa ya kiuchapaji kuingiza jina lake.
Hoja
Baadhi ya Wabunge wa Bara kuonekana wamepiga kura Zanzibar na kinyume chake mf Zakhia Meghji.
Jibu
Orodha ya Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba ilionyeshwa kwenye orodha maalum zilizotolewa na Bunge zikionyesha wabunge toka pande zote za Muungano.
Mheshimiwa Zakhia Hamdani Meghji ni Mzanzibar kwa kuzaliwa, kukulia na kwa sehemu kubwa alisomea Zanzibar. Yeye ameolewa Bara na amekuwa kwenye utumishi Serikalini kwa miaka mingi. Kuolewa na kufanya kazi Bara hakuwezi kumwondolea Uzanzibar wake. Aliingia Bungeni kama Mbunge wa Bunge la Muungano kwa kuteuliwa na Rais. Wapo Wazanzibar walioolewa na kufanya kazi Bara na haki yao ya kufanya siasa Zanzibar haijawahi kuhojiwa mfano Mama Fatma Maghimbi na Anna Maulida Komu.
Hoja
Sheria ya mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalum kubadilishwa kila kukicha ili kukidhi mahitaji ya kisiasa katika kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Mfano Desemba 2013 sheria ilibadilishwa ili kufuta Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jibu
Katiba, sheria na Kanuni ni nyaraka hai ambazo kazi yake ni kuelekeza, kutoa mamlaka, kuratibu na kudhibiti mambo kulingana na mahitaji na hali ya walengwa na nyakati. Mabadiliko yeyote yanapotokea au mahitaji ya kufanya mambo fulani ni budi sheria au kanuni zifanyiwe mabadiliko ya kidemokrasia ili kukidhi mahitaji na hali hiyo mpya.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilifanyiwa marekebisho kadhaa na Bunge ili kukidhi mahitaji yaliyojitokeza mfano marekebisho ya mwisho yalihusu idadi ya wajumbe 201, mgawanyo wake kwa makundi na namna ya kuwapata. Haya yalikuwa ni marekebisho ya muhimu sana kuhakikisha uwakilishi mpana wa wananchi na si tu kukidhi mahitaji ya kisiasa.
Tume ya Marekebisho ya Katiba haikufutwa kama inavyodaiwa bali ili kutoa nafasi kwa kila chombo kilichoundwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuweka bayana hatua zote za mchakato ilionekana ni muafaka kwa Tume ikishakabidhi Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Muungano na Rais wa Zanzibar na hatimae kuiwasilisha Bungeni huo uwe ndio mwisho wake rasmi ili kupisha vyombo vingine viendelee na hatua zinazofuata. Rais kwa mamlaka aliyopewa na sheria aliivunja rasmi Tume mara baada ya kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba kwenye Bunge Maalum na haikufutwa.
Marekebisho mbalimbali yaliyofanywa kwenye Kanuni yalilenga kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa Bunge Maalum na yaliridhiwa kwa kura na Bunge lenyewe baada ya kujadiliwa kwa kina.
Hoja
Kufutwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulipelekea wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoelewa baadhi ya vifungu na kuvitafsili tofauti.
Jibu
Kama tulivyoeleza kwenye ibara ya 9 hapo juu Tume haikufutwa bali ilifikia ukomo wake kwa sababu na taratibu zilizoelezwa Rais aliivunja rasmi.
Bunge Maalum la Katiba lilikuwa na wajumbe 629 na wengi wao ni watu weledi na mabingwa wa masuala ya katiba, sheria, utawala, uchumi na nyanja zote ambazo elimu yake inahitajika katika utengenezaji wa Katiba pengine kuzidi hata wajumbe 33 wa Tume. Kusema wajumbe wa Bunge Maalum hawakuelewa baadhi ya vifungu na kuvitafsiri tofauti ni kuwatukana wao, Watanzania waliowachagua na Rais aliyewateua.
Hakuna uhusiano kati ya kuwepo au kutokuwepo kwa Tume na wajumbe wa Bunge Maalum kutoelewana au kutoa tafsiri tofauti ya vifungu vya Rasimu ya Pili. Hivi vilikuwa vyombo viwili tofauti vilivyokuwa na majukumu tofauti na Bunge Maalum kutokana na kuwa ni wawakilishi wa wananchi na idadi yake kuwa kubwa kimamlaka lilikuwa kubwa kuliko Tume ya watu 33 ya kukusanya maoni.
Hoja
Kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kutoka kwenye Kamati ya Uandishi. Hakueleza sababu zake lakini kuna maswali ya kujieleza.
Jibu
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alipojiuzulu toka kwenye Kamati ya Uandishi hakutoa sababu na kwa uzito wa nafasi yake alipaswa kutoa sababu. Kwa kuwa hakutoa sababu si busara na vyema kubuni sababu za kujiuzulu kwake
.
Hoja
Kufukuzwa kazi kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar bila sababu za msingi siku moja kabla ya kukabidhiwa kwa Rais Katiba Inayopendekezwa.
Jibu
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ni taasisi na mamlaka ya uteuzi huteua mtu mwenye sifa na vigezo kuongoza ofisi hii. Pale kwa sababu za msingi ikibainika mtu huyo amekosa sifa au kwenda kinyume na maadili ya kazi na hadhi ya ofisi ile ni wajibu na haki kwa mamlaka ya uteuzi kuchukua hatua stahiki. Hili ndilo alilofanya Rais wa Zanzibar.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ndiye mshauri mkuu wa Rais na serikali juu ya masuala yote ya sheria. Ni mtu aliye karibu sana kikazi na Rais hivyo haiwezekani Rais amfukuze kazi bila sababu za msingi.
Hoja
Kupindisha kwa Kanuni za Bunge la Katiba siku ambayo Rais alikuwa akifungua Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa Kanuni ilipaswa Rais afungue kwanza ndipo Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe Rasimu ya Pili lakini ilifanyika kinyume chake kitu ambacho ndio kiini cha matatizo kwani Rais alianza kutoa maoni yake kwenye Rasimu ya Pili badala ya kuzindua Bunge la Katiba.
Jibu
Tarehe iliyokuwa imepangwa kwa Rais kuzindua Bunge Maalum kwa bahati mbaya tarehe hiyo Rais kutokana na majukumu yake kama Mkuu wa Nchi alipata udhuru na kwa kuwa siku za Bunge kufanya kazi zake zilikuwa maalum na zilihesabiwa kisheria, Mwenyekiti wa Bunge Maalum aliwasiliana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kukubaliana Rasimu ya Pili ya Katiba iwalisishwe halafu Rais aje azindue Bunge Maalum baadaye.
Mabadiliko ya uwasillishaji Rasimu ya Pili ya Katiba na uzinduzi wa Bunge Maalum hayakuwa na athari yoyote kwa sababu yalikuwa hayategemeani na yalifanywa na mamlaka mbili tofauti kwa mujibu wa sheria na Kanuni.
Hoja ya kusema kuwa Rais wa nchi azindue Bunge Maalum halafu baadaye aje amsikilize Mwenyekiti wa Tume aliyemteua akiwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba Bungeni, kiitifaki haileti picha nzuri wala heshima.
Rais katika kuzindua Bunge Maalum lengo kuu lilikuwa kuwapa wabunge nasaha zake juu ya umakini katika kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ili kuipatia Tanzania katiba nzuri. Kiutaratibu ni lazima Rasimu hiyo iwe ilishawakilishwa rasmi Bungeni na Mwenyekiti wa Tume. Rais asingeweza kuongea Bungeni juu ya Rasimu ambayo ilikuwa haijawasilishwa rasmi Bungeni kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Rais kutoa maoni yake juu ya Rasimu ya Pili ya Katiba alikuwa na uwezo wa kuyatoa maoni hayo wakati wowote na popote na hakutegemea Mwenyekiti wa Tume awasilishe Rasimu Bungeni ndipo aongee.
Hoja
Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum kuongozwa na Mwenyekiti hana rekodi za uadilifu na uwajibikaji.
Jibu
Hizi ni tuhuma nzito dhidi ya haiba ya mtu hivyo zinapaswa kuungwa mkono na ushahidi mzito. Ni vyema kuonyesha kwa uthibitisho ni kwa vipi Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi alikosa uadilifu au uwajibikaji na jinsi ilivyoathiri Katiba Inayopendekezwa.
Kamati ya Uandishi ilikuwa ni kundi la wabunge wa Bunge Maalum waliokuwa na weledi wa kutosha ambao mbali na kushiriki kwenye mijadala ndani ya kamati na Bungeni, ndio waliokusanya mawazo, maoni na hoja za kitaaalam baada ya mijadala na kuandika Katiba Inayopendekezwa. Mwenyekiti alikuwa anaongoza vikao vya majadiliano na kutoa mchango wake.Hivyo Katiba Inayopendekezwa ni mkusanyiko wa mawazo ya wananchi, wabunge wa Bunge Maalum pamoja na mawazo na utaalamu wa kuandika katiba wa wajumbe wa Kamati ya Uandishi na si mawazo ya mtu mmoja.
Hoja
Bunge Maalum kutumia muda mwingi kutengeneza Kanuni na kudai posho ilhali wakitumia muda mfupi sana kutengeneza Katiba Inayopendekezwa.
Jibu
Upatikanaji wa Kanuni nzuri zinazofanya kazi kwa ajili ya Bunge Maalum la Katiba lilikuwa ni jambo muhimu na nyeti sana. Kanuni mbovu zingevuruga mjadala mzima au Katiba isingepatikana. Kanuni ndizo zilijenga msingi wa majadiliano mazuri, namna ya kufanya maamuzi na njia za kupata maridhiano pale tofauti zilipotokea.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa siku 70 kwa Bunge Maalum la Katiba kufanya kazi zake na ilipoonekana hazitoshi Rais kwa mamlaka aliyopewa na sheria aliongeza siku nyingine 60 jumla zikawa siku 130. Utungaji na upitishaji Kanuni ulitumia siku 40. Hii ni historia kwani kuna nchi zilitumia miezi 5 au 6 kupata Kanuni tu na nyingine pamoja na kutumia muda huo hawakuweza kupata Kanuni.
Hoja
Kupitisha vifungu vya Katiba Inayopendekezwa kwa mafungu yaani kupigia kura sura nzima badala ya kwenda kifungu hadi kifungu.
Jibu
Rasimu ya Mwisho iliyopigiwa kura ili kupata Katiba Inayopendekezwa ilikuwa na ibara 296 na ibara ndogo nyingi. Wastani wa mbunge mmoja kupiga kura ni dakika moja. Ukichukulia wabunge wapatao 450 kupigia ibara 296 kila ibara ingehitaji masaa saba na dakika thelathini ambayo ni siku moja ya kazi. Hii ina maana zingehitajika siku zaidi ya 296 ambayo ni miezi tisa na siku kadhaa kupiga kura kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Kamati ya Uongozi iliona ni busara kwa kuwa wabunge walishaijadili Rasimu ya Mwisho kwa undani, wapewe siku kadhaa za kujisomea wenyewe na ilipofika siku ya kupiga kura kila mbunge alipiga kura akiwa ameshasoma Rasimu ya Mwisho yote. Kudhihirisha hili baadhi ya wabunge walikubali baadhi ya ibara na kukataa baadhi. Hapakuwa na kura moja kwa sura moja nzima kam inavyodaiwa.
Hoja
Wajumbe wa Bunge la Katiba kutumia lugha chafu na zenye kuudhi mfano kuwatukana viongozi wadini na waandishi wa habari.
Jibu
Hakuna ushahidi unaoonyesha viongozi wa dini au wanahabari kutukanwa. Kulikuwa na ushirikiano na uhusiano mzuri na makundi haya ambayo yalikuwa na uwakilishi ndani ya Bunge na mbali na hilo wanahabari waliripoti yaliyokuwa yanaendelea Bungeni kwa uhuru mkubwa.
Kanuni ziliweka katazo la wazi dhidi ya matumizi ya lugha zenye kuudhi na pale hali hiyo ilipojitokeza aliyelengwa na maudhi alichukua hatua stahiki. Yaliweza kuwepo pale mwanzo mazungumzo ya baadhi ya wabunge kurushiana vijembe lakini hali hii ilikemewa wala haikuwahusu wabunge wote.
Hoja
Rasimu iliyopigiwa kura Bungeni ilikuwa tofauti na ile iliyokabidhiwa kwa Rais kimaudhui.
Jibu
Madai haya hayana chembe yoyote ya ukweli. Yalipaswa kuungwa mkono na ushahidi kuonyesha maeneo yenye tofauti kimaudhui.
Hoja
Kukosekana kwa ulinzi wa Haki za Binaadamu. Ibara 119 (a) ya Rasimu ya Pili iliweka ulinzi lakini ibara ya 134 ya Katiba Inayopendekezwa imeondoa ulinzi huo hivyo Haki za Binadamu zilizoko sura ya 4 zitaweza kuondolewa wakati wowote.
Jibu
Rasimu ya Pili ya Katiba ililenga kuwepo kwa serikali tatu yaani ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar. Rasimu ya Pili haikusema kuwa Katiba ya Muungano itakuwa juu ya Katiba za Tanganyika na Zanzibar. Hii ina maana serikali za Tanganyika na Zanzibar ambazo zingekuwepo na zenye watu zinaowaongoza moja kwa moja zingeweza kuwa na Katiba ambazo zingetoa uzito dhaifu kwa haki za binadamu na serikali ya Muungano chini ya Katiba yake isiweze kufanya lolote. Maana yake ni kuwa Rasimu ya Pili iliweka Haki za Binadamu ndani yake lakini zisingetekelezeka kwa sababu dola ya Muungano isingeweza kuingia na kukemea pale serikali za Tanganyika na Zanzibar, vyombo vyake na watendaji wake watakapokiuka haki za binadamu.
Uwepo wa haki za binadamu ndani ya Katiba ya nchi ni kitu kimoja na utashi wa kuziishi, kuziheshimu haki za binadamu ni jambo jingine. Jambo la msingi si kuziingiza tu ndani ya Katiba bali pia ni kwa namna gani utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu ulivyojijenga katika fikra na maisha ya wanajamii na wanavyoziishi.
Kwa mujibu wa ibara ya 134 ya Katiba Inayopendekezwa Bunge linaweza kubadilisha masharti ya Katiba hiyo kwa kufuata misingi maalum iliyowekwa kikatiba. Katika ibara ya 134(2) inasisitizwa kuwa kubadilisha masharti ya kubadilisha Katiba hii maana yake ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti haya au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo.
Hapa Katiba Inayopendekezwa imetambua bayana kuwa hali/ mazingira katika jamii, nchi na hata ulimwengu hubadilika kwa nyakati hivyo kuhitaji namna ya kukabiliana na mabadiliko na mahitaji mapya ya watu. Katika hali hiyo mabadiliko ya Katiba au sheria kwa njia ya kidemokrasia huwezesha mabadiliko hayo kupokelewa na kukabiliwa.
Hoja
Kuondolewa kwa kifungu kinachoipa nguvu mikataba iliyoridhiwa na Tanzania kuwa na nguvu katika mahakama.
Jibu
Hoja hii haijawekwa sawa. Mikataba iliyoridhiwa na Tanzania iwapo imetungiwa sheria za kuifanya itumike ndani ya nchi hakuna ibara ya Katiba Inayopendekezwa imezuia hilo kufanyika. Ibara ya 65 ya Katiba Inayopendekezwa imefafanua kwa mapana juu ya usimamizi wa haki za binadamu na mamlaka ya mahakama katika jambo hili.
Tanzania ni nchi ya Jumuiya ya Madola na mfuno wake wa Katiba, muundo na utendaji wa serikali kwa kiasi kikubwa unafuata mfumo wa Jumuiya ya Madola. Chini ya mfumo huu panapokuwa na mkataba wa kimataifa Bunge likiridhika serikali hutia saini mkataba huo kuonyesha kuridhishwa na mashart ya mkataba huo. Hatua inayofuata ni Bunge kuiagiza serikali kuridhia mkataba huo kuonyesha kuwa nchi imekubali kufungwa na masharti ya mkataba huo. Hatua ya tatu ni kwa Bunge kutunga sheria ya kuwezesha mkataba huo kuwa moja ya sheria za nchi. Njia hii ni shirikishi zaidi kwani wananchi kupitia wawakilishi wao hupata fursa kuipitia kwa makini mkataba hiyo na kama kuna chochote kinachokinzana na maslahi, maadili au utamaduni wetu wataweza kukibaini na kuchukua hatua.
Hoja
Haki ya kuishi sio thabiti kwani iko kwa mujibu wa sheria. Hii inalea kuendelea kuwepo kwa adhabu ya kifo kwa mujibu wa ibara ya 33 ya Katiba Inayopendekezwa.
Jibu
Hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa kupitia maoni ya wananchi au mijadala iliyofuata watu walio wengi walipendekeza adhabu ya kifo iondolewe moja kwa moja. Ibara ya 24 ya Rasimu ya Pili ya Katiba inasema;
(24) Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kutoka katika serikali na jamii kwa mujibu wa sheria za nchi,
Katika Randama ya Rasimu ya Pili ya Katiba, Tume imeeleza kuwa ibara inayoweka haki ya kuishi inaweka masharti ya kulinda na kuthamini uhai wa mwanadamu na isiondolewe kinyume na masharti ya kikatiba na sheria za nchi.
Bado kuna mjadala mkubwa sehemu nyingi duniani na hapa nchini juu ya kufutwa adhabu ya kifo. Walio wengi wanaonyesha haja ya adhabu hii kuendelea. Hoja zao zinaongezewa nguvu na matendo ya mauaji ya kikatili wanayofanyiwa watu wasio na hatia mfano katika milipuko ya kigaidi, mauaji ya albino na vikongwe wasio na hatia kwa imani za kishirikina yanayotokea hapa nchini na menginenyo kama kuua watu hadharani na hata kuwachoma moto kwa kisingizio cha kuwa ni wananchi wenye hasira kali.
Hoja
Kuwepo kwa vifungu vy urembo mfano haki ya Afya na maji safi zitakuwepo endapo rasilimali zitapatikana.
Jibu
Serikali iliyo makini popote duniani ni ile inayofanya jitihada za makusudi za kuhakikisha wananchi wake wanakua na afya na wanapata maji safi na salama. Katiba Inayopendekezwa imeamua kuzipa hizi haki kinga ya kikatiba kwa kutambua umuhimu wake. Ibara ya 51 ya Katiba Inayopendekezwa imeweka bayana jambo hili kama ifuatavyo;
(1) Kila mtu ana haki ya kupata huduma ya afya na maji safi na salama.
(2) Mamlaka ya nchi itahakikisha kwamba huduma zilizorejewa katika ibara ndogo ya (1) zinapatikana kwa urahisi kwa kuzingatia mahitaji ya nchi na rasilimali zilizopo.
Hakuna mahali panaposema haki hizi zitapatikana iwapo rasilimali zitakuwepo. Mantiki ya ibara iliyorejewa hapo juu ni kuwa jinsi rasilimali zinavyoongezeka ndivyo huduma zitakavyozidi kuwa bora na kupatikana kwa urahisi. Si sahihi wala haki kusema haki za afya na maji safi na salama ni haki za urembo.
Hoja
Kuondolewa kwa kifungu cha 50/50 uwakilishi wa wanawake katika ngazi za maamuzi na kuweka uwiano tu kijinsia.
Jibu
Dhana ya uwakilishi wa 50 kwa 50 ni dhana iliyojadiliwa kwa kina na kuingizwa katika Katiba Inayopendekezwa pamoja na uwiano wa kijinsia. Ibara ya 129 (2)(a) inasema;
(2) Kutakuwepo na aina zifuatazo za Wabunge,;
- Wabunge wa kuchaguliwa kupitia majimbo ya uchaguzi yatakayotangwazwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Ibara ya 129 (4) inasema
Bila kuathiri masharti ya Ibara hii, msingi wa uwakilishi katika ibara ndogo ya (2) (a) itazingazitia uwakilishi ulio sawa kati ya wabunge wanawake na wanaume.
Tafsiri yake hapa ni kuwa uwakilishi kwenye majimbo ya uchaguzi ni 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume.
Hoja
Kuchanganya Haki za makundi ambayo mahitaji yao hayafanani mfano haki za wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimba madini.
Jibu
Katiba ya nchi huweka misingi na miongozo mikuu Haipambanui na kuelekeza juu ya mahitaji ya makundi ya jamii kwani hili hufanywa na sheria na kanuni mbalimbali. Misingi ya haki za makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimba madini imewekwa vizuri na bayana zaidi bila muingiliano. Ibara ya 46 ya Katiba Inayopendekezwa inasema;
4.6 (1) Wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji madini watakuwa na haki ya;
- Kumiliki, kutumia na kuendeleza ardhi kwa ajili ya shughuli zake.
- Kupata taarifa na maarifa kwa lengo la kuboresha kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji madini.
- Kumiliki na kunufaika na rasilimali za kijenetiki za kilimo, mifugo na uvuvi .
- Kushirikishwa katika utungaji wa sera, sheria na mipango mbalimbali inayohusu shughuli zao.
Ili kuongeza ulinzi wa haki zao na kuepusha migongano na migogoro baina yao ibara ya 46(2) inasema;
(2
) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa kisheria kwa madhumuni ya kubainisha na kutenga maeneo ya ardhi kwa ajili ya matumizi ya kila kundi lilioaainishwa katika ibara ndogo ya (1) (yaani wakulima, wafugaji , wavuvi na wachimbaji madini).
Katika kuongeza mkazo haki kwa makundi haya ibara ya 23(2) (c) inasema.
(a) Haki ya kumiliki mali, kutumia kuendeleza na kuhifadhi ardhi kwa ajili ya mtu yeyote au makundi ya jamii yakiwemo wakulima , wavuvi, wafugaji, wachimbaji madini na makundi madogo itatambuliwa na kulindwa kwa mujibu wa Katiba hii.
Hoja
Kuondolewa kwa vifungu vingi vinavyoelekeza sheria kutungwa katika mambo muhimu mfano haki za wanawake, ibara ya 47 (2) ya Rasimu ya Pili.
Jibu
Haki za Binaadamu kama zilivyooanishwa katika Sura ya Tatu ya Katiba Inayopendekezwa zimepewa kinga na ulinzi wa kutosha kikatiba na maelezo ya kutosha ya kisheria ya namna ya kuzilinda, kuzifaidi na nini cha kufanya pindi ukitokea ukiukwaji. Ibara ya 67 inatoa maelekezo ya kisheria kwa haki, uhuru na wajibu kama ifuatavyo;
(67) Bila kuathiri masharti ya Sura hii Bunge litatunga sheria, ambayo pamoja na mambo mengine itasimamia matumizi na utekelezaji wa haki, uhuru na wajibu ulioainishwa katika surah ii.
Hoja
Kuondoa vifungu vyote vinavyohusu uwajibikaji
Jibu
Katiba Inayopendekezwa imeweka vizuri sana eneo hili la uwajibikaji kwa kuweka misingi ya utawala bora kwenye Katiba na uwajibikaji ukiwa ni msingi mmojawapo. Katika kuimarisha utawala bora ibara ya 6(1) ya Katiba inasema;
6(1) Katika kutekeleza mamlaka au shughuli zozote kwa mujibu wa Katiba hii au sheria za nchi, misingi ya utawala bora katika Ibara hii ni lazima izingatiwe na taasisi ya serikali, ofisa wa Serikali au mtu yeyote aliyepewa dhamana ya;
- Kutumia au kutafsiri Katiba hii.
- Kutunga, kutumia au kutafsiri sheria yoyote na,
- Kufanya au kutekeleza maamuzi ya sera za kitaifa.
Katika inayopendekezwa katika sura ya nne imeweka maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa umma. Chini yake maana ya dhamana ya uongozi wa umma imeelezwa na nini kizingatiwe, kadhalika zimewekwa kanuni za uongozi wa umma, utii wa miiko ya uongozi wa umma, marufuku kwa baadhi ya vitendo na imeelezwa mambo yatakayosimamiwa na sheria yanayowahusu viongozi wa umma.
Katiba Inayopendekezwa imeipandisha hadhi Secretariati ya Maadili ya Umma na kuifanya kuwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo ni Tume huru iliyopewa majukumu kuyatekeleza bila kuingiliwa uhuru wake.
Hoja
Kuondoa Tunu za Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu zilizokuwa kwenye Rasimu ya Pili.
Jibu
Tunu ni kitu ambacho mtu au taifa linakiona kama tunu au adimu kupatikana kirahisi ambacho tayari unacho na si matarajio au matamanio ya kuwa na hicho kitu. Kwa taifa tunu ni kitu cha thamani kilichopatikana katika jamii baada ya jitihada za muda ndipo likatunukiwa. Tunu (virtues) ni tofauti na maadili (values). Kwa msingi huu uwajibikaji, uwazi na uadilifu ni maadili na siyo tunu ndio maana wananchi na serikali zinajitahidi maadili hayo, yawepo kwa ukamilifu. Ni matamanio taifa lingependa kufanikisha na si kitu ambacho tayari kipo mikononi kama ilivyo mfano lugha ya Kiswahili.
Katika Rasimu ya Pili, Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu viliodhorodheshwa tu kama Tunu za Taifa. Kwa namna zilivyowekwa hazikuwa na maana yoyote kwa sababu haikusemwa nini kifanyike ili kuziimarisha au kuzilinda. Katika Katiba Inayopendekezwa Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu ni moja ya misingi ya utawala bora. Katiba imetoa maelekezo ya msisitizo katika ibara ya 6(1) umuhimu wa kuzingatia misingi ya utawala bora. Hili ina maana na manufaa zaidi kwa wananchi katika maisha yao ya kila siku.
Hoja
Kuondoa nguvu ya wananchi wapiga kura kuwawajibisha wabunge wao ambao hawawajibiki majimboni.
Jibu
Kazi za Mbunge mbali na kuhamisisha maendeleo katika eneo lake, kazi yake kubwa ni kuwawakilisha na kutetea wananchi wake Bungeni na kwenye vikao vinginge vinavyojadili na kupanga mipango yao ya maendeleo. Ushiriki thabiti wa Mbunge ni ili ahakikishe jimbo linaingizwa au kunufaika na mgao wa rasilimali utakaowezesha miradi mbalimbali ya maendeleo ya jimbo lake kama maji, hospital shule nk iweze kupata fedha. Kazi hii ni kwa wabunge wa nchi nzima na huchukua muda kufanikisha kwani kila mmoja ana mahitaji jimboni. Kuruhusu uhuru wa kumwondoa kwenye nafasi yake kwa kigezo cha kumwajibisha kinaweza kutumiwa vibaya na kutoa nafasi kwa mahasimu wake wa kisiasa aliowashinda kwenye kura za maoni ndani ya chama chake au wagombea toka vyama vingine au wagombea huru aliowashinda kujiandaa na kuhamisisha wafuasi wao kwa pamoja kumuondoa.
Ndani ya kupindi cha miaka mitano wananchi wanakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya utendaji wa Mbunge wao na kama hafai hawatamchagua tena. Hilo limeshatokea karibu sehemu zote nchini kwa wabunge kunyimwa kura kwa kutowajibika ipasavyo. Hii njia inafaa na ingeachwa iendelee kutumika.
Rasimu ya Pili ilipendekeza Bunge la Wabunge 75 ambapo 70 ndio wanaochaguliwa na wananchi. Wabunge hawa majimbo yao yangekuwa ni mikoa na kila mkoa ungekuwa na wabunge wawili tu. Mambo mengi yanayowagusa wananchi na kero kwao yasingeshughulikiwa na Bunge hili la watu 75 kwani mengi si ya Muungano. Hivyo Rasimu ya Pili haikuwa imetoa jawabu au suluhisho la kweli juu ya nini afanyiwe Mbunge anayewawakilisha wananchi jimboni kwake na hawajibiki. Wabunge wanaozungumziwa kwenye Rasimu ya Pili ni wale wawili wanaowakilisha kila mkoa kwa mambo machache na mengi yasiyowagusa moja kwa moja.
Hoja
Kuondoa ukomo wa wabunge katika Rasimu ya Pili kiliwekwa kikomo cha mihula miwili tu.
Jibu
Kama ilivyoelezwa hapo juu Bunge lililopendekezwa katika Rasimu ya Pilia ni dogo la watu 75 ambapo kila mkoa ungewakilishwa na wabunge wawili tu. Bunge linalopendekezwa katika Katiba Inayopendekezwa ni la wabunge kati ya 340 hadi 390 wakiwawakilisha wananchi moja kwa moja toka toka majimboni. Haya ni mabunge wawili tofauti yanayofanya kazi zinawagusa wananchi kwa viwango tofauti na ukaribu wake kwa wananchi ni tofauti. Wabunge wa mkoa wanaweza kuwa vigumu kubaini utendaji wao kutokana na ukubwa wa mkoa mfano mkoa wa Tabora tofauti na wa jimbo ambalo ni dogo na upatikanaji wake ni rahisi. Katika hali hii inaweza kuwa muafaka kumwekea Mbunge anayewakilisha mkoa ukomo kama mfumo huo ungepita na si yule wa jimbo. Huyu wananchi watamwekea ukomo wenyewe kutokana na utendaji wake.
Hoja
Kuongeza idadi ya wabunge waBunge la Jamhuri kutoka 75 mpaka 390.
Jibu
Bunge lililopendekezwa na Rasimu ya Pili ya Katiba ni Bunge dogo la wabunge 75 ambalo lingekuwa na mamlaka kwenye mambo 7 tu yalioainishwa kwenye Rasimu. Kila mkoa ungewakilishwa na wabunge wawili tu mwanamke na mwanamme. Bado Serikali za Tanganyika na Zanzibar zilizopendekezwa zingekuwa na mabunge yake ya wabunge wa majimbo haya yaliyopo kushughulikia huduma nyingi za kijamii ambazo Bunge la Wabunge 75 wasingeshughulikia. Ina maana wabunge wangeweza hata kuwa wengi zaidi kuliko idadi ya 390 inayotajwa.
Hoja
Kuongezwa kwa idadi ya mawaziri toka 15 iliyopendekezwa na Rasimu ya Pili mpaka 40.
Jibu
Rasimu ya Pili ilipendekeza kuwepo kwa Serikali ndogo ya Muungano inayoshughulikia mambo 7 tu. Serikali ya Tanganyika iliyopendekezwa nayo ingekuwa na Baraza lake la Mawaziri hivyo idadi ya mawaziri bado ingeweza kuwa kubwa zaidi.
Idadi ya mawaziri inayotajwa inahusisha pia manaibu waziri . Ibara ya 115 (2) inasema
(2) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1) idadi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano haitazidi arobaini.
Hoja
Kuongezwa kwa Makamu wa Rais kufikia watatu.
Jibu
Kwa mujibu wa makubaliano ya Muungano ya 1964 Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais. Sharti hili liliondolewa 1992 na kuletwa dhana ya mgombea mwenza. Baada ya muda hali hii ilianza kuonekana kero kwa upande wa Zanzibar kwa Rais wake kutokuwa mmoja wa viongozi wa Muungano. Marekebisho haya yamelenga kuondoa tatizo hilo. Dhana ya mgombea mwenza imeendelea kubaki ili kuhakikisha kuwa Rais na Makamu wa Kwanza wanatoka chama kimoja. Ikitokea bahati mbaya kwa sababu zozote Rais ameondoka madarakani Makamu wake wa kwanza wanaotaka chama kimoja atachukua nafasi yake ili kuendeleza ajenda ya chama chake. Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu wanaweza wakatoka vyama tofauti na Rais.
Hoja
Waziri ni lazima awe mbunge. Hii ni kuondoa dhana ya mgawanyo wa madaraka katika mihimili mitatu yaani Bunge, Mahakama na Serikali.
Jibu
Nchi yetu tangu tupate uhuru tumekuwa tukitumia mfumo wa utawala wa kibunge ambao ni wa Jumuiya ya Madola. Chini ya mfumo huu mawaziri hutokana na wabunge na huwajibika bungeni moja kwa moja. Kuwa bungeni hakufifishi au kuingilia mamlaka ya Bunge bali kunaongeza ufanisi na uwajibikaji katika utendaji kwani mawaziri na wabunge hufanya kazi pamoja bungeni.
Mfumo wetu wa siasa hapa nchini ni kwa vyama vya siasa kushindanisha ilani zao za uchaguzi na kile kinachoshinda ilani yake ndiyo inayotekelezwa na serikali. Mtu anapogombea ubunge hunadi ilani ya chama chake na akishinda na chama chake kikishinda pindi akiteuliwa kuwa waziri atakuwa anatekeleza ilani ya chama chake anayoifahamu vizuri tofauti na mtaalamu aliyeteuliwa toka kwenye taasisi au chuo kuwa waziri ambapo ilani anaiona siku ya kuapishwa.
Mtu anapoteuliwa kuwa waziri ambaye si mbunge na haiingii bungeni wakati wa vikao vya bunge hii inaweza kufifisha dhana ya utii na uwajibikaji kwa bunge na badala yake mawaziri wanaweza kuteuliwa kwa urafiki na utii wao wakaulekeza kwa aliyewateua tu. Kwa ajili ya uwazi na uwajibikaji wananchi wamezoea na wangependa kuona mawaziri wanajibu na kufafanua bungeni mambo yanayowahusu na inapobidi wanawajibishwa pale kwa waliyotenda.
Hoja
Sifa za Mbunge ni kujua kusoma na kuandika tu.
Jibu
Ubunge ni kazi ya utumishi kwa watu na kila mtu anayo haki ya kidemokrasia kuomba. Kwa kuwa kupiga kura na kupigiwa kura ni haki ya kila mwananchi kikatiba kikiwekwa kiwango cha elimu ili mtu agombee watakaokuwa hawana kiwango hicho watakuwa wamebaguliwa na kunyimwa haki yao.
Kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza ni kigezo cha msingi cha kuonyesha mtu huyo ana kiwango fulani cha elimu. Kujua kusoma na kuandika si kiwango cha elimu bali ni kigezo cha kuonyesha mhusika ana uelewa wa mambo kadhaa au anao uwezo wa kutafuta maarifa zaidi kwa kujisomea
Katiba Inayopendekezwa haikuweka kiwango cha elimu kwa anayegombea ubunge ili kuwaachia wananchi pamoja na vigezo vingine muhimu waangalie na kujiridhisha wenyewe na kigezo cha kiwango cha elimu ya mgombea. Historia inaonyesha kuwa wapo watu waliokuwa na shahada kadhaa lakini kutokana na kukosa vigezo vingine vya muhimu kama uadilifu, uwajibikaji, unyenyekevu nk walinyimwa kura na wakapewa wenye elimu ya kawaida na wakaweza kutumikia wananchi kwa umahiri wa kutosha.
Hoja
Kuweka masharti magumu kwa Mgombea Huru.
Jibu
Mgombea huru ni mtu anayegombea nafasi bila kuwa na chama cha siasa. Wanaotoka kwenye vyama kwa vyama vinavyoendesha siasa zake kidemokrasia hupatikana kwa mchujo ili kupata mwenye vigezo stahiki na ambaye anaishi na kufanya mambo katika misingi fulani ya maadili ndani ya chama chake kwa kuwa kuna mfumo wa kumdhibiti. Mgombea huru hachujwi wala hakuna namna ya kumdhibiti bali hujipangia mambo yake yeye mwenyewe na wapambe wake.
Masharti yaliyomo kwenye Katiba Inayopendekezwa ni ya msingi na ya muhimu hasa kwa mgombea huru anayetaka kugombea Urais kuongoza nchi yetu. Ibara ya 216(2) juu ya Mgombea Huru inasema;
(2
) Bunge litatunga sheria itakayoweka masharti mgombea huru kuhusu-
(a) Idadai ya wapiga kura wanaohitajika kumdhamini kwa nafasi anayogombea
Lengo la sharti hili ni kuhakikisha mgombea kama ni Urais anao wafuasi na ana ufuasi wenye sura ya kitaifa.
- Kipindi ambacho amekoma kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa kabla ya siku ya uchaguzi.
Lengo hapa ni kuhakikisha mgombea huru ni huru kweli ili isije ikawa mtu ana chama lakini akajifanya mgombea huru lakini akiingia madarakani anatekeleza sera za chama fulani. Hii pia itaepusha mtu aliyeangushwa katika mchujo wa ndani ya chama chake kujifanya mgombea huru ilhali ugombea huru ameutaka baada ya kuangushwa kwenye chama lakini akishinda fikra na falsafa zake ni kile chama kilichomwangusha kwenye kura ya maoni na wananchi hawakukichagua.
- Kutojiunga na chama cha siasa katika kipindi ambacho atakuwa kiongozi baada ya kuchaguliwa.
Mgombea huru anapochaguliwakama yeye ina maana sera zake zimeonekana ni bora kuliko za wale wa vyama aliowashinda. Yeye kujiunga na chama baada ya kushinda ni kuweka pembeni sera zake na kukumbatia sera za chama kimojawapo ambazo katika uchaguzi wananchi hawakukichagua. Pili inazuia vyama kuweza kufadhili kwa siri watu kusimama kama wagombea huru huku navyo vikiweka wagombea na kutoa mwanya kwa chama kuweza kuwa na wagombea wengi kwenye nafasi moja. Isipokatazwa mgombea huru aliyefadhiliwa na chama fulani akishinda ataweza kujiunga na chama kilichomfadhili na kukifanya chama hicho kuwa madaraka bila ridhaa ya wananchi.
- Utaratibu wa kuainisha vyanzo vya ndani na nje vya mapato ya kugharamia kampeni za uchaguzi.
Ni muhimu mgombea huru akaonyesha vyanzo vya mapato yake ili asijetokea mgombea akafadhiliwa na magenge ya wahalifu ya wauza madawa ya kulevya au vikundi vya kigaidi kwa ahadi ya kurudisha fadhila. Kadhalika itawezesha kujua kama mgombea ana madeni kiasi gani ili aweke bayana namna atakavyokuja kuyalipa pindi akiingia madarakani ili kuepusha matumizi mabaya ya ofisi kwa ajili ya kulipa madeni sugu binafsi.
- Utaratibu wa kuanisha vigezo ni sifa zitakazotumika kuwapata viongozi wa ngazi za juu kitaifa.
Lengo ni kuweka udhibiti mtu asiingie madarakani akawa anafanya uteuzi kwa vigezo vya ukabila, udini, ukanda wapambe nk.
- Kuweka wazi ilani ya uchaguzi inayoonyesha mipango ya uendeshaji wan chi.
Ni muhimu mgombea huru hasa katika nafasi ya urais kutoa ilani yake ya uchaguzi ili kutoa fursa kwa washindani wake nao kuelewa anachosimamia na kushindanisha na zao. Pili kuwezesha wananchi kufanya rejea ya kila anachokisimamia badala ya kuacha mawazo yanayotokea kichwani mwake tu ambayo yanaweza kubadilika kulingana na mahali alipo au mapokeo ya wananchi na mwisho akiwa madarakani wananchi wataweza kupima ufanisi wake kwa kuangalia alichotekeleza katika ilani yake ambayo ipo na inaonekana.
- Kuweka masharti yanayozuia sera zenye mrengo na kuligawa Taifa.
Lengo hapa ni kuzuia mtu atakayetaka kuleta sera kwa mfano za kuongoza sehemu moja tu ya Muungano, kutoa upendeleo usio na maana kwa makundi au maeneo ya watu kutokana na dini au kabila.
- Masharti mengine kwa kadri itakavyoonekana inafaa.
Hapa sheria itaweka masharti kulingana na mahitaji ya nyakati.
Masharti haya yanalenga kuonyesha kuwa kama ni nafasi ya Urais anayegombea atambue hii ni nchi moja, apate ridhaa ya wananchi kwa umoja wao nchi nzima na awaongoze wote kwa umoja wao kuelekea kwenye maendeleo.
Hoja
Kuweka muundo wa serikali mbili ilhali kimsingi ni serikali tatu kwani kuna Makamu wa Rais watatu.
Jibu
Idadi ya serikali mbili ni muundo wa serikali uliowekwa na idadi ya makamu wa rais ni mfumo wa namna ya kuendesha muundo wa serikali mbili kwa ufanisi zaidi. Idadi ya Makamu wa Rais haiamui idadi ya serikali ila inyume inawezekana.
Hoja
Kuongezeka kwa madaraka ya Rais kuliko hata ilivyokuwa kwenye katiba ya 1977. Ibara za 80-86 na 93-98.
Jibu
Hoja hii haina usahihi. Katiba Inayopendekezwa imeweka bayana zaidi madaraka ya Rais na si kuyaongeza. Kwa kuanzia, katika kuonyesha wananchi walivyopewa mamlaka makubwa ndani ya Katiba Inayopendekezwa ili mtu atangazwe kuwa Rais ni lazima ashinde zaidi ya 50% ya kura halali zilizopigwa na matokeo ya Urais yanaweza kupingwa mahakamani. Ibara ya 80 inaeleza juu ya uwepo wa Rais, kama Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, ibara ya 82 ni kuhusu utekelezaji wa madaraka ya Rais, ibara ya 83 ni juu ya Rais kuzingatia ushauri, ibara ya 84 inaelezea taratibu za kufuata pindi Rais akishindwa kumudu majukumu kwa sababu zozote zile, ibara ya 85 inaeleza utaratibu wa kujaza nafasi ya Rais kabla ya kumaliza muda wake na ibara ya 86 inaeleza utekelezaji wa majukumu ya Rais iwapo nafasi ya madaraka ya Rais ipo wazi. Haya ni mambo ya msingi na ya kawaida na ni maboresho ya masharti yaliyo katika Katiba ya 1977. Pia haya ni mambo ambayo yako katika Katiba zote za kidemokrasia duniani.
Ibara ya 93 inatoa madaraka kwa Rais kutangaza vita baada ya kupata idhini ya Bunge, ibara ya 94 inampa madaraka Rais ya kutangaza hali ya hatari baada ya kushauriana na Baraza la Usalama la Taifa, ibara ya 95 inampa Rais madaraka ya kutoa msamaha kwa wafungwa, ibara ya 96 inaelezea juu ya kinga ya mashtaka dhidi ya Rais, ibara ya 97 inatoa mamlaka na utaratibu wa Bunge kumshtaki Rais na ibara ya 98 inazungumzia maslahi ya Rais.
Haya masharti na madaraka kwa Rais ni ya msingi na ya kawaida popote katika ulimwengu wa demokrasia.
Hoja
Kuulinda Muungano na mfumo wake kupita kiasi. Nyongeza ya Pili na ya Tatu ya Katiba Inayopendekezwa zimelenga kulinda Muungano kwa maslihi ya watawala.
Jibu
Muungano wetu ni moja ya Tunu za Taifa na zipo kila sababu kuulinda na kuuimarisha zaidi. Muungano wetu ni wa watu na historia yake inajipambanua namna watu wa pande hizi walivyojenga mahusiano ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kidugu.
Nyongeza ya Pili ya Katiba Inayopendekezwa inalenga kuweka masharti ya kulinda mambo ya Muungano na pale inapotokea haja ya kuyafanyia marekebisho ni budi kuwe na uwakilishi mkubwa toka kila upande ili kuimarisha na kulinda zaidi maslahi ya pande zote. Ili uamuzi juu ya mambo ya Muungano ni budi yaungwe na 2/3 ya wabunge toka kila upande wa Muungano.
Nyongeza ya Tatu ya Katiba Inayopendekezwa imeweka masharti juu ya muundo au uwepo wa Jamhuri ya Muungano ambapo uamuzi ni budi ufikiwekwa kupiga kura ya maoni na hoja kuungwa mkono na zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wananchi kila upande wa Muungano.
Nyongeza zote mbili zimelenga kuimarisha zaidi madaraka na mamlaka ya umma katika kufanya maamuzi kwenye mambo ya msingi yanayowahusu. Maamuzi ya kura kwa 2/3 toka kila upande au kwa kura ya maoni kwa mshindi wa zaidi ya nusu kila upande si kwa manufaa ya watawala bali ni kuhamisha mamlaka ya maamuzi toka kwao na kuyarudisha kwa wananchi.
Hoja
Kuchanganya Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora kama ilivyokuwa kwenye Katiba ya 1977.
Jibu
Haki za Binadamu na Utawala Bora vina uhusiano wa karibu sana. Nchi inapoongozwa kwa kufuata misingi ya utawala bora na watu nao wakaishi katika misingi hiyo kiwango cha heshima kwa haki za binadamu huwa juu kwani mfumo wa utawala na maisha ya watu unakuwa unaendeshwa vizuri na kwa haki. Kuwa na Tume itakayofuatilia masuala ya haki za binadamu na utawala bora ni muundo mzuri hata kiutendaji.
Katiba Inayopendekezwa mbali na kuunda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeipa pia Tume hii mamlaka ya kuhamisisha, kulinda na kufuatilia utekelezaji wa usawa wa jinsia na ulinganifu kwa ujumla katika maendeleo ya Taifa. Hii ni hatua ya muhimu katika kuhakikisha usawa katika nchi yetu.
Katiba Inayopendekezwa imeweka misingi ya utawala bora ndani yake na kati ya misingi hiyo ni haki za binadamu na usawa wa jinsia. Katika kutilia mkazo Katiba imeelekeza taasisi za serikali, maofisa wake au mtu yeyote katika lolote analofanya katika nafasi aongozwe na misingi ya utawala bora.
Hoja
Kuongeza masuala ya Muungano toka 7 hadi 16. Wingi wa masuala ya Muungano imekuwa kero ya muda mrefu kwani inaongeza Tanganyika kuvaa koti la Muungano.
Jibu
Yanayosemwa kuwa yalikuwa mambo 7 ya Muungano kwenye Rasimu ya Pili ukiangalia maudhui ya Rasimu yenyewe utaona kulikuwa na mambo mengi zaidi ya Muungano ambayo hayakuorodheshwa kama mambo ya Muungano lakini yaliwekwa kwenye hiyo Rasimu mfano polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, mamlaka ya hali ya hatari, utumishi katika serikali ya Muungano nk. Kuongeza mambo ya Muungano toka 7 hadi 16 ni kuboresha na kuimarisha Muungano, kulinda maslahi ya pande zote za Muungano na kuimarisha mamlaka na utambulisho wa Zanzibar ndani ya Muungano.
Kero za Muungano hazitokani na idadi ya mambo ya Muungano bali namna ya kushughulikia mambo ya Muungano na utatuzi wa matatizo ya utekelezaji pale yalipojitokeza. Katiba Inayopendekezwa imepunguza kwa kiasi kikubwa sana kero halisi za Muungano kwa pande zote. Yanaweza yakawepo manungunika lakini manunguniko na kero ni vitu viwili tofauti .
Hoja
Kutoweka tafsiri ya makundi mengine ya haki ya binadamu kwa mfano vijana na wazee.
Jibu
Hapajawahi kuwepo na tatizo kwa makundi ya vijana na wazee ambalo chimbuko lake ni kukosekana kwa tafsiri ya nani ni kijana au mzee. Katiba Inayopendekezwa imetokea tafsiri ya mtoto ni nani kutokana na mtoto kutafsiriwa tofauti na sheria mbalimbali hali iliyosababisha athari kwa haki za mtoto. Hilo halijajitokeza kwa ukubwa huo kwa wazee na vijana.
Sheria mbalimbali zinazowahusu wazee na vijana zilizoko au zitakazotungwa zina nafasi ya kutoa tafsiri ya makundi haya pindi ikionekana haja ya kufanya hivyo.
Hoja
Kurudisha cheo cha Waziri Mkuu. Cheo hiki kilikuwa kimeondolewa na Rasimu ya Pili.
Jibu
Kuondolewa kwa cheo cha Waziri Mkuu lilikuwa ni pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katika kwenye Rasimu ya Pili ambayo ilikuwa ni Rasimu kwa ajili ya majadiliano zaidi na maamuzi na halikuwa ni agizo kwa wananchi. Bunge Maalum la Katiba kwa kutumia madaraka lililopewa chini ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba inayopendekezwa, lilijadili na kupitisha muundo wa serikali ambao mfumo wa kuiendesha unahitaji uwepo wa cheo cha Waziri Mkuu na huo ndio msingi wa kurudisha cheo cha Waziri Mkuu.