Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Mchoro wa moyo unaoonyesha madhara ya ghafla yanayoweza kusababisha kifo.
KWA UFUPI
Matukio ya waliokufa ghafla Tanzania
-Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba
-Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Ditopile Mzuzuri
-Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa
Ni jambo la kushtua inapotokea habari kuwa mtu wa karibu, ndugu, rafiki au mtu maarufu ambaye ulishiriki naye jambo fulani muda mfupi uliopita, amekufa ghafla.
Taarifa za kifo chake ambacho kimetokea ghafla kabla ya kupita saa 24 tangu mlipoachana naye, hushangaa.
Kifo hiki cha ghafla ni cha kiasili na cha kawaida kinachoweza kumpata mtu yoyote pasipo kuwapo na ugonjwa unaojulikana au kuwa na dalili za muda mrefu.
Kitaalamu inaelezwa kuwa kifo cha namna hii hutokea baada ya mgonjwa kudondoka au kupoteza fahamu saa moja baada ya kujitokeza dalili wakati akiwa usingizini.
Mara nyingi, vifo vya ghafla huambatana na matatizo au magonjwa ya moyo na tatizo hili huwapata zaidi watu walio na umri wa miaka 30 au zaidi.
Yapo matatizo mengine ya kiafya yasiyohusiana na moyo lakini yanayoweza kusababisha kifo cha aina hii.
Kila mwaka duniani kote watu wengi hufariki ghafla hasa katika nchi ambazo zimepiga hatua kiuchumi kutokana na maradhi ya moyo.
Wataalamu wa afya hufanya uchunguzi wa kina kila inapobidi ili kubaini sababu za kifo cha aina hiyo. Baadaye taarifa hizo husaidia katika utafiti kujua mambo gani katika jamii ambayo ni hatarishi au nini kilidhurika kwenye mwili wa mtu aliyekufa ghafla. Ni vyema ifahamike kuwa kuna tofauti kati ya kifo cha ghafla na mshtuko wa moyo.
Mshtuko wa moyo ni pale misuli ya moyo inaposhindwa kufanya kazi na kusimama ghafla na baada ya kupewa huduma ya kwanza kwa kutomasa moyo, huweza kuisha na moyo huendelea kufanya kazi yake.
Sababu za vifo vya ghafla
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk. Meshack Shimwela anasema zipo sababu tofauti zinazosababisha vifo vya ghafla, baadhi ikiwa ni maradhi ya moyo, mapafu, ubongo, mfumo wa upumuaji na wakati mwingine sumu.
Dk. Shimwela alisema moyo inasababisha vifo kwa asilimia kubwa kwa sababu mishipa au milango ya moyo inaweza kupasuka; athari za dawa kwenye moyo; moyo kukosa hewa safi au kiungo kimoja kukosa usambazaji wa damu. Tatizo la Watanzania wengi ni kuwa hatuchunguzi afya zetu mara kwa mara. Watu wengi wanatembea na maradhi bila kufahamu na hicho ndicho chanzo cha vifo vya ghafla, anasema Dk. Shimwela
Anasema inawezekana kabisa kuwa mtu aliyefariki ghafla alikuwa akiugua kwa muda mrefu bila kuchukua tahadhari au kudharau hali yake na wakati mwingine alikuwa akiumwa lakini hakufuata masharti ya ugonjwa wake.
Kikubwa baada ya vifo vya ghafla ni kufanya uchunguzi wa sababu ya kifo hicho (postmortem) badala ya kuhisi tu, anasema
Mara nyingi sababu kuu huwa ni matatizo katika mishipa inayopeleka damu katika misuli ya moyo. Mishipa hiyo huathirika kutokana na urundikaji wa lehemu mwilini hivyo kusababisha mishipa hiyo kunyauka na kukakamaa hivyo kuifanya ishindwe kutanuka na kuwa myembamba.
Urundikaji wa lehemu katika mishipa hii pia husababisha kutokea kwa vichuguu katika mishipa midogo inapeleka damu katika moyo hivyo kuwa kama kizuizi cha damu kupita.
Vilevile, damu iliyoganda nakuwa kama vibuja vya ugali huweza kutoka sehemu yoyote ya mwili kupitia mzunguko wa damu hufika katika mishipa inayopeleka damu safi katika misuli ya moyo na kuwa kizuizi cha damu kupita, hivyo basi mambo haya matatu yakitokea husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa ua kupata kiasi kidogo sana.
Dk. Jennifer Ndosi, bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Mount Meru, Arusha anasema misuli ya moyo ikikosa damu, huharibika na kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kwa ufanisi wa kawaida.
Misuli ya moyo huharibika na kuifanya misuli ya moyo kupiga bila mpangilio na ndipo ghafla moyo husimama kudunda.
Anaeleza kuwa sababu ya pili ni misuli ya chumba cha upande wa kushoto wa moyo kuongezeka ukubwa na mara nyingi huwapata wenye shinikizo la damu la muda mrefu hii ni kutokana na kujibadili kwa misuli ya moyo na kuongezeka ukubwa na kufanya kazi ya ziada ya kusukuma damu.
Kuongezeka huku kwa misuli ya moyo husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo ya kupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu.
Sababu nyingine ni ya magonjwa mengine ya moyo ni kama vile moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo ya kawaida ya mishipa ya damu, uambukizi wa valvu za moyo na hivyo valvu kushindwa kufanya kazi.
Nyingine ni matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, usafirishaji taarifa katika moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, kuwa na wingi wa mafuta mabaya mwilini. Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo yanayoweza kuwa chanzo cha vifo vya ghafla ni sumu, au mrundikano wa taka mwili zenye sumu, matatizo ya mfumo wa hewa, kupaliwa na kitu katika mfumo wa hewa, kuvuta hewa chafu na ajali.
Pia, hali ya kifo hiki huweza kutokea na sababu isijulikane.
Dalili kabla ya vifo vya ghafla
Mtandao wa Habari za Afya (WebMed) unaeleza kuwa mara nyingi kabla ya tukio la kifo cha ghafla kutokea, watu walio kuwa karibu nao hutoa historia ya watu hawa waliokufa ghafla ya kuwa na maumivu ya ghafla ya kifua, ambayo hutawanyika katika taya na mkono wa kushoto.
Wengine husikia kichefuchefu, kutapika, kuona giza, kichwa kuuma ghafla, kukatika kwa pumzi na kushindwa kupumua baaada ya dalili hizi kutokea ndipo hali yakupoteza fahamu hutokea, wengi huthibitika kufariki baada ya saa moja tu tangu kujitokeza kwa dalili.
Na wengi wa wagonjwa hawa hufariki njiani wakati wakipelekwa kupata huduma za afya au wakiwa wanapatiwa huduma za dharura.
Nini kifanyike kuepuka vifo vya ghafla?
Ni vyema kuchukua tahadhari mapema kuepukana na maradhi hasa ya moyo. Jambo la msingi ni kubadili mienendo yetu kwa kuzangatia mlo bora kiafya na mazoezi ya mara kwa mara angalau hata kutembea muda wa dakika 15 kwa siku.
Epuka mambo kama ya ulaji holela wa vyakula vya mafuta hasa vyakula vitokanavyo na wanyama, ulaji wa vyakula vya wanga, sukari na chumvi nyingi.
Zingatia ulaji wa mboga kwa wingi, matunda na maji mengi.
Fanya uchunguzi wa mara kwa mara wa mwili wako, fika mapema katika huduma za afya pale unapoona dalili. chanzo. Sababu, dalili na udhibiti wa vifo vya ghafla - mwanzo - mwananchi.co.tz