SoC02 Sababu saba (07) zinazopelekea mtoto wa Kitanzania ashindwe kupata elimu bora

SoC02 Sababu saba (07) zinazopelekea mtoto wa Kitanzania ashindwe kupata elimu bora

Stories of Change - 2022 Competition

MAKA Jr

JF-Expert Member
Joined
Nov 17, 2016
Posts
267
Reaction score
209
pic-ufundishaji-mtihan-data.jpg

Picha. Chanzo: Mwananchi (12/08/2022)

UTANGULIZI

Nchi masikini na zinazoendelea zina changamoto nyingi kama vile; changamoto za umasikini, utandawazi, na kielimu. Changamoto za upatikanaji wa elimu bora ndio kubwa zaidi. Tanzania kama moja ya nchi zinazoendelea pia ina changamoto kadhaa zinazotatiza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto.

Makala hii imejikita katika kujadili sababu saba (07) zinazopelekea mtoto wa Kitanzania ashindwe kupata elimu bora:

01. Lugha ya Kufundishia
Mtoto wa Kitanzania anakuzwa katika mfumo wa elimu unaokinzana juu ya lugha gani itumike katika kufundishia.
Mfumo wetu wa elimu nchini hauwezi kuepuka madhara yatokanayo na “mtaka vyote hukosa vyote”. Katika Elimu ya Sekondari, tunatumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, lakini ni ndani ya jamii inayotumia lugha ya Kiswahili muda wote. Matokeo yake tumekosa vyote. Tumekosa kuwa na Kiingereza kizuri, tumekosa kuwa na Kiswahili kizuri, na tumekosa maudhui ya masomo. Mifano mingi inadhihirisha hili. Wahitimu wengi wa Kidato cha Nne wanabangaiza Kiingereza na Kiswahili chao sio fasaha pia. Hata baadhi ya hotuba za viongozi zinadhihirisha tatizo hili. Leo, sio ajabu kumsikia Kiongozi akichanganya lugha mbili kwenye hotuba rasmi. Utasikia: "Tumeweka system sawa na …..tumeongeza bajeti kwenye dispensaries nyingi….". Hii ndio halisi tuliyonayo. Wasomi wamelisemea sana hili lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

02. Kufundishwa na Mtu Anayenung’unika
Mtoto wa Kitanzania anafundishwa na mtu anayenung’unika kila wakati. Mwalimu anayemfundisha mtoto ni mtu wa kunung’unika. Mwalimu huyu ana kinyongo kwa sababu hajatimiziwa haki na mahitaji mengine. Mwalimu huyu amekata tamaa na kuona kuwa maisha yake ndivyo alivyo. Mtoto wa Kitanzania anarithi kila kitu kutoka kwa Mwalimu na yeye atawarithisha wengine.

03. Kauli za Viongozi Zinazobeza Ualimu na Walimu
Mtoto wa Kitanzania amekuwa ni shuhuda wa kauli mbovu za kushusha na kubeza hadhi ya Ualimu kutoka kwa viongozi mbali mbali. Kauli hizi zimemfanya mwanafunzi aamini kuwa mwalimu ni mtu wa kubezwa na kunyimwa haki. Kauli hizi zinawafanya walimu waonekana si chochote mbele ya jamii. Kiongozi mmoja aliwahi kuwaambia walimu mbele ya wanafunzi kuwa kwenye ualimu hatutafuti utajiri.
Kauli hii haikupaswa kutolewa kwa Mwalimu. Mwanafunzi anapaswa asione mwalimu wake anadharauliwa kwa sababu anategemea kujifunza kutoka kwake. Hali hii pia inamuathiri mwanafunzi wa Kitanzania katika kujipatia elimu bora.

04. Kuishi Katika Mazingira Yasiyo Rafiki Katika Kujifunza
Mtoto wa Kitanzania anaishi katika mazingira ambayo hayajapangwa vizuri na hayamvutii kusoma. Hali ya kuwa na makazi ya watu karibu na baa, hoteli, nyumba ya kulala wageni, na kumbi za starehe kunaathiri upatikanaji wa elimu bora kwa mtoto. Kwa mfano, mtoto ambaye nyumba yao iko karibu na nyumba ya kulala wageni atakuwa na wakati mgumu wa kusoma. Kuna wengine wanaishi karibu na kumbi za disko. Mazingira haya yanatatiza upatikanaji wa elimu bora kwa mtoto.
Makazi yetu yanapaswa kuwa na sehemu za kucheza watoto, sehemu za starehe, sehemu za ofisi, soko, na sehemu za makazi pekee. Mazingira kama haya yanamfanya mtoto ajue na kuelewa kuwa kila eneo lina makusudi yake na hawezi kuyachanganya maeneo yote kwa wakati mmoja kirahisi.

05. Wazazi/Walezi Wamewaachia Walimu Peke Yao Kazi ya Kulea Watoto
Mtoto wa Kitanzania yuko katika mazingira ambayo hapati msukumo wa kusoma kutoka kwa mzazi au mlezi. Watoto wengi wa Kitanzania wanasukumwa na walimu wao pekee huku wazazi wao wakijiweka pembeni. Hali hii ya kuwepo kwa msukumo wa upande mmoja tu umewafanya watoto wengi wa Kitanzania kulegeza morali katika kusoma na hivyo kuwafanya wajiingize katika mambo mengine ya kidunia. Mazingira ya mtoto wa Kitanzania yanapaswa yapate msukumo mkubwa kutoka pande zote mbili, yaani kutoka kwa mwalimu na kwa mzazi au mlezi.

06. Ushawishi wa Vifaa vya Kidijitali kama vile Televisheni na Simu
Kuwepo kwa ushawishi mkubwa wa vifaa vya kidijitali kama vile televisheni, simu na michezo ya kompyuta (games) kumeathiri pia upatikanaji wa elimu bora kwa mtoto.
Mtoto wa Kitanzania amekuwa chini ya ushawishi mkubwa wa vitu hivi vya kisasa. Sio rahisi kuwatenga watoto na vitu hivi vinavyozidi kuenea kwa kasi. Lakini mzazi anaweza kuweka utaratibu mzuri juu ya vitu hivi ili mtoto aweze pia kufuatilia masomo. Kwa sisi watanzania tumekuwa na changamoto kubwa sana katika kuwadhibiti watoto juu ya vitu hivi. Ni wakati sasa mtoto akae akijua kuwa wakati gani aangalie TV na vipindi gani atazame pia. Michezo ya kompyuta pia inatakiwa kuwekewa ratiba. Pia umefika wakati ambapo mtoto awekewe taratibu za kutumia simu na hatakiwi kwenda kwenye kumbi za starehe kwa jinsi anavyojisikia. Haya yote yanatakiwa kupangwa na mzazi au mlezi. Pale tu mtoto akiwa mkubwa ndipo ataweza kuamua mambo yake mwenyewe japo si yote pia anaweza kujiamulia.

07. Masomo Yote Yanalenga Kuajiriwa au Kufanya Kazi Ofisini
Mwisho, mtoto wa Kitanzania anafundishwa ili siku moja aajiriwe au afanya kazi ofisini tu. Hali hii inatokana na mfumo wa elimu yetu ambapo hata mwanafunzi asiye na juhudi darasani anafikiria siku moja afanye kazi ofisini. Hasa ukizingatia kuwa kufanya kazi ofisini ni heshima, basi kila mtoto ana matarajio ya namna hiyo tu. Hakuna anayejisikia fahari kujiajiri kwenye kilimo kwa sababu elimu haijamuandaa kuwa hivyo. Mfumo wetu wa elimu unapigiwa sana kelele kwamba hauwaandai wanafunzi kujitegemea. Sio rahisi kuwa na jamii yenye wasomi tu, na inawezekana kabisa mwanafunzi asiyeweza kusoma akafanya kitu kingine tena kwa ufanisi mkubwa zaidi. Umefika wakati elimu yetu iwaandae wanafunzi kujitegemea. Umefika wakati mtoto afundishwe stadi za maisha ili asipoajiriwa ajiajiri au ajishughulishe na shughuli nyingine.

HITIMISHO
Kutokana na kutokuwepo kwa msukumo wa kila upande, mazingira yanayomzonga, na mfumo wa elimu usio rafiki na endelevu, mtoto wa Kitanzania atashindwa kujijengea tabia madhubuti za kisomi na za kujiajiri. Hata akifika Chuo Kikuu atakuwa ni mtu wa kusoma tu ili afaulu afanye kazi ofisini.
Wito unapaswa kutolewa kwa kila mdau wa elimu ili kuhakikisha kuwa Elimu bora inatolewa Tanzania ili baadae tuwe na kizazi chenye wabunifu waliojaa maofisini na waliojiajiri pia. Baada ya kufanikisha hili tutapata maendeleo binafsi na Taifa letu litasonga mbele zaidi.

Rejea:
[Picha] Ufundishaji wa mitihani unawadumaza wanafunzi (12/08/2022)
 
Upvote 1
Back
Top Bottom