Sabaya alivyoshinda Rufaa yake

Sabaya alivyoshinda Rufaa yake

Mpinzire

JF-Expert Member
Joined
Jan 18, 2013
Posts
7,503
Reaction score
13,463
Someni mpate kujifunza jambo.

Sehemu ya 1
Kesi ya rufaa ya kupinga kifungo cha miaka 30 jela kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili imeanza kusikilizwa leo Februari 15 katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ambapo Wakili Majura Magafu ametoa hoja 14 akisema kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haikufanya uchambuzi wa kina wa ushahidi hadi kutoa hukumu hiyo.

Oktoba 15, 2021 Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Arusha ilimkuta na hatia Sabaya na wenzake wawili ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na hivyo kuwahukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 129, inayosikilizwa na Jaji Sedekia Kisanya, waleta rufaa wengine ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura.

Baada ya rufaa hiyo kutajwa mahakamani hapo, Wakili Magafu ameanza kutaja hoja nane, huku akisema hoja nyingine ataendelea nazo Wakili mwenzake Mosses Mahuna.

Amesema kama Hakimu angefanya uchambuzi wa kina angeweza kugundua mambo kadhaa ikiwemo hati ya mashitaka iliyopelekwa mbele yake haikukidhi matakwa ya kisheria na ushahidi uliotolewa ulikuwa hauendani na hati ya mashitaka.

"Mheshimiwa Jaji ground (hoja) ya nane inahusu mheshimwa aliyeendesha hii kesi kufanya uchambuzi wa kina na kuwatia hatiani waleta rufaa na kuwpa adhabu.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 312 cha CPA ni matakwa ya kisheria kwamba jaji anapoandika hukumu yake inabidi afanye mchanganuo wa kina juu ya ushahidi ulioletwa mbele yake asipofanya hibyo hiyo hukumu inakuwa ni batili," amesema Wakili Magafu.

Akirejea mashauri ya mahakama ya rufaa ikiamua juu ya suala hilo, Magafu amesema; "Kila hakimu au jaji anayo staili au utaratibu wake wa kuandika hukumu lakini kitu cha msingi anachotakiwa kuangalia ni kupitia viini vyote vya mashitaka na ushahidi kama ulivyotolewa na pande zote."

Wakili Magafu amesema tatizo la kwanza lilikuwa ni kuhusu majina ya washitakiwa mshitakiwa wa kwanza na wa tatu (Sabaya na Mbura) na kwamba, Julai 18, 2021 wakati shauri likiendelea Jamhuri iligundua jina la mshitakiwa wa kwanza lilikuwa limekosewa na wao wakasema ni ‘typping error’ ila wao wakasema hapana na kuhusu jina la mshitakiwa wa tatu ambaye yeye mwenyewe analikana limeendelea kuwepo kwenye hati ya mashitaka.

"Mheshimiwa Jaji wakati maelezo ya hoja ya awali, mshitakiwa wa tatu alikana hilo jina linaloonekana kwenye charge sheet (hati ya mashitaka) ushahidi wa kukana jina uko ukurasa wa nne wa nakala ya hukumu.

“Tatizo lingine ni mahali ambapo tukio lilitokea mashahidi wanasema tukio lilitokea mtaa wa Soko Kuu lakini charge sheet mpaka leo inaonyedha tukio liliyokea mtaa wa Bondeni Arusha," ameeleza Magafu.

Ameendelea; "Mheshimiwa ili charge sheet iweze kuitwa charge sheet lazima ionyeshe kinaga ubaga ni nani alikuwa mlalamikaji kwenye hilo tukio na lilitokea eneo gani na kifungu cha sheria anachoshitakiwa nacho.Baada ya upande wa mashitaka kuona kulikuwa na utata juu ya tukio lilipotokea walijaribu kumuita shahidi wa 11 ili awasaidie kutatua hilo tatizo.”

Wakili huyo amedai kuwa shahidi wa 11 DC James, ushahidi wake kuanzia ukurasa 168 ukiangalia aya ya mwisho anasema alipopewa faili kufanyia uchunguzi alienda Soko Kuu katika duka la Mohamed Saad akini wakati akihojiwa alisema tukio liliyokea Mtaa wa Bondeni Arusha.

Aliendelea kudai kuwa kwa mujibu wa sheria hati inataka itaje walalamikaji kwa majina na kwa mujibu wa hati ile inaonyesha walalamikaji walikuwa watatu ambao ni Bakari Msangi, Ramadhan Ayoub na Saad.

"Nataka nifafanue zaidi mpelelezi ambaye ni PW 11 yeye anasema kwamba mlalamikaji katika shauri hili aliyefika mbele ya polisi ni PW 6, tunashindwa kuelewa shahidi wa kwanza na wa tatu ambao hawajawahi kufika polisi wanakuwaje sehemu ya walalamikaji hii inaonekana kulikuwa na hola katika uandaaji wa mashitaka?

"Hakuna sehemu yoyote katika walalamikaji walioandika kutoka polisi PW 7, Gwakisa Minga hakusema kama aliwahi kuwaita mashahidi namba moja na tatu kwa ajili ya kuwahoji.

"Kwa hiyo tunasema mheshimiwa Hakimu angeweza kufanya upembuzi halali na umakini angegundua kasoro nyingine zote,tukio linadaiwa kutokea sehemu moja lakini katika kuhakikisha washitakiwa wanatiwa hatiani wakatenganisha hizo count zikawa tatu,"

Ameendelea kusenma kuwa upande wa mashitaka walileta kielelezo cha tatu na wakati walipokuwa wakifanya uchunguzi wao walimpiga picha Bakari Msangi wakasema waliipeleka forensic bureau kwa ajili ya kuihakiki.

"Kitu kinachotufanya tuone hicho ni cha kupika kielelezo P5 kinaunga mkono tunachokisema sasa hivi fomu ya polisi namba 27.

“Inaonyesha barua ya kupeleka hizo picha iliandikwa 24/7/2021 wakati kesi inakaribia kuisha hii haukuwa utaratibu sahihi kwani polisi hawawezi kuendelea kufanya upelelezi wakati kesi iko tayati mahakamani inasikilizwa,"alieleza

"Mheshimiwa Jaji kama inavyojua prosecution wanapomaliza upelelezi huiomba mahakama kesi ianze kusikilizwa, hawatakiwi kusikiliza ushahidi unaoendelea mahakamani kisha waende kufanya upelelezi wazibe mapengo. Baada ya kugundua wameshafanya makosa na wanataka wazitumie picha za PW6 ambaye ndiyo mlalamikaji wakaandika barua ya tarehe 26/6/2021 na majibu yakawaumbua," alisema.

Kuhusu wadaiwa PW 2 na 4, alisema licha ya kuwa walikuwa wamenyanyasika sana kwa kupigwa na mshitakiwa lakini waliwaomba wawanulie ndizi.

“Hapo ndiyo utaona kuna shida kwenye upelelezi wa hii kesi na uchambuzi wa ushahidi, mtu aliyekupiga sana huwezi kumuomba akununulie ndizi,” amesema.

"Sisi tunaona mheshimiwa Hakimu hakuweza kujielekeza vizuri katika uchambuzi wa ushahidi ulioletwa mbele yake.Mheshimiwa tuna submit vilevile angeweza kugundua PW 6 ambaye ndiye aliyekuwa chanzo cha hii kesi alikuwa na hila dhidi ya mleta rufaa wa kwanza," amesema.

Akizungumzia suala la upelelezi kutokufanyika vizuri alidai kuwa ameshatoa sababu baadhi ya wapelelezi hawakufanya upelelezi vizuri baada ya kupata malalamiko toka kwa PW 6 na kuwa haiwezekani kwa hali ya kawaida polisi wako kwenye eneo la tukio, haiwezi kusema Bondeni Street na Sokoni street ziko pamoja.

"Polisi wangechunguza vizuri wangejua ni uongo. Pw 6 anasema alipekuliwa akaibiwa 390,000 na simu lakini PW 4 anasema alishuhudia PW6 akipekuliwa alichoshuhudia aliona akinyang'anywa simu na wallet na kama wakati anapekuliwa hawa wengine waliona walipaswa kuona fedha zikichukuliwa hatupaswi kuweka watu hatiani kwa maneno ya kusikia bali ushahidi madhubuti,"

Aliendelea kueleza kuwa waleta rufaa walikanusha wizi wa Sh35,000 na PW 3 alisema alienda pale kwa ajili ya kununua bidhaa kwenda kuuza kwenye ushahidi wake anasema 35,000 alipewa kwa ajili ya kwenda kununua vitu vya nyumbani vya kula mheshimiwa tunajiuliza kwanini hakwenda polisi kulalamika.

Baada ya Wakili Magafu kutoa hoja hizo, Wakili Mahuna naye aliendelea kuwasilisha hoja ambapo alianza na hoja ya rufaa ya kwanza aliyodai kiwa ni Mahakama ya Hakimu Mkasi Arusha ilikosea kuwatia hatiani na kuwapa adhabu waleta rufaa kwani hati ya mashitaka ilikuwa batili.

Alieleza mahakama kuwa na mashitaka matatu yote unyang'anyi wa kutumia silaha yameonekana kuna tatizo bayana la ni wapi tukio hilo lilitendeka hiyo 9/2/2021 na kuwa katika ukurasa wa 112 wa uamuzi wa mahakama ilielezwa hoja za majumuisho za mawakili na mahakama ilisema shahidi wa saba na wa 11 wote wawili walisema duka hilo liko Bondeni street karibu na Soko Kuu.

"Tunajiuliza hilo ni sawa kwenye ukurasa wa 124 Gwakisa anasema kuwa alifahamishwa na mrufani wa kwanza bwana Sabaya kuwa aliwakamata PW2 na PW4 kwenye duka lao huo sokoni.

"Siku ya 12/2/2021 na 12 1 2021 alienda yeye PW 7, 2, 4 kwenye duka la PW 2 na 4 lililoko Bondeni Street lililoko karibu na Soko Kuu. Duka linalozungumziwa hapa ni la PS 1 lililopo bondeni street near market .PW 7 hakuwahi kuzungumzia duka la PW 1 ambalo ndilo lipo kwenye hati ya mashitaka na PW 11 anasema kosa lilitendeka Soko Kuu kwenye duka la PW 1 na hazungumzii chochote juu ya duka lililopo Bondeni," amesema.

Wakili Mahuna alidai tatizo lingine ni tarehe ambapo kwenye hati ya mashitaka inadaiwa 9/2/2021 washitakiwa hao waliiba Sh Milioni 2.769 lakini shahidi wa pili wa jamhuri anasema siku hiyo hakujua nini kiliibiwa dunkani hadi walipofungua duka 12/2/2021.

Baada ya kuwasikiliza mawakili hao, Jaji Kisanya ameahirisha rufaa hiyo hadi kesho mawakili hao watakapoendelea kuwasilisha hoja zao za rufaa.


Sehemu ya 2

Rufaa ya Sabaya na wenzake - 4​

Jana katika sehemu ya tatu ya mfululizo wa mapitio ya hukumu ya rufaa ya aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura tuliona jinsi Jaji Sanya alivyokubaliana na kubainisha dosari katika mwenendo wa kesi ya msingi wa kesi hiyo.

Hii ni katika hukumu ya rufaa ya Mahakama Kuu iliyotengua hukumu iliyowatia hatiani Sabaya na wenzake kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu na kuwahukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Baada ya kubaini na kukubaliana na dosari za ukiukwaji wa sheria katika mwenendo wa kesi ya msingi katika mahakama ya chini, ni hatua au amri gani Jaji Kisanya aliitoa? Kwa nini alifanya hivyo? Endelea

Kutokana na dosari hizo za ukiukwaji wa sheria katika mwenendo wa kesi alizozibainisha na kukubaliana nazo Jaji Kisanya, amri ambayo alipaswa kuitoa ni kuamuru kesi hiyo ikasikilizwe upya kuanzia mahali zilizoanzia dosari hizo, lakini akasema masilahi ya haki ndio jambo muhimu la kuzingatia.

Alisema pia kuwa amri ya kesi kusikilizwa upya haiwezi kutolewa katika mazingira ambayo ushahidi hautoshelezi au pale ambapo amri hiyo inaweza kuupa nafasi upande wa mashtaka kuziba mapengo katika ushahidi wake uliokwishakupokewa mahakamani.
Hivyo ili kuamua kama atoe amri ya kesi kusikilizwa upya au la, Jaji Kisanya ilibidi ajadili kwanza masuala machache yaliyoibuliwa katika baadhi ya sababu za rufaa hiyo kwa lengo la kuona kama ushahidi ulikuwa unatosheleza kama ulivyolalamikiwa na mawakili wa warufani. Kwanza aliangalia malalamiko katika sababu ya kwanza ya rufaa, kwamba hati ya mashtaka ilikuwa na dosari.

Mbali na madai kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na dosari kwa kujirudia kwa mashtaka, pia mawakili wa Sabaya, Moses Mahuna alidai kuwa mashtaka na ushahidi wa upande wa mashtaka vinakinzana, huku Majura Magafu akidai kuwa mahakama ilishindwa kuchanganua ushahidi uliotolewa wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Verdina Mlenza na mwenzake Baraka Mgaya kwa nyakati tofauti walidai kuwa hapakuwa na mkinzano kati ya mashtaka na ushahidi na kwamba kama kulikuwa na mkinzano wowote basi haukuwaathiri warufani.

Kuhusu hoja hiyo, Jaji Kisanya alisema kutokana na malumbano ya hoja ya pande zote, kifungu cha 234 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinataka hati ya mashtaka inayotofautiana na ushahidi kufanyiwa marekebisho.

Alisema kuna hukumu nyingi za kesi za Mahakama ya Rufani zinazoeleza kwamba kushindwa kurekebisha hati ya mashtaka kunaifanya kuwa mbovu na zaidi kunaufanya upande wa mashtaka kuchukuliwa kuwa umeshindwa kuthibitisha mashtaka.

Jaji Kisanya alitamka kuwa katika kesi hiyo alibaini kuwa hati ya mashtaka inahitilafiana na ushahidi, hususan kuhusu mali inayodaiwa kuibwa (dukani kwa mlalamikaji- shahidi wa kwanza).

Alisema shtaka la kwanza linaonyesha kuwa Sh2,769,000 ziliibwa kutoka dukani kwa shahidi wa kwanza (Mohamed Saad), lakini ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka unaonesha kuwa sarafu na mashine ya risiti ya kielektroniki (EFD) pia viliibwa dukani humo.

Katika shtaka la pili mali iliyotajwa kuibwa ni Sh390,000, wakati shahidi wa sita katika ushahidi wake anaeleza kuwa leso yake pia ilichukuliwa. Shahidi wa nne katika ushahidi wake alieleza kuwa pochi ya shahidi wa sita pia ilichukuliwa.

Jaji Kisanya alieleza kuwa maelezo kwamba pochi ya shahidi wa sita nayo ilichukuliwa yanaonekana katika maelezo yake ya maandishi, ambayo yalipokewa mahakamani na kuwa kielelezo cha kwanza cha upande wa utetezi.

Mawakili wa Serikali hawakupinga kuwa sarafu, EFD na leso au pochi havikujumuishwa kwenye hati ya mashtaka. Hata hivyo, kwa mtazamo wao, dosari hiyo haikuwaathiri warufani.

Hivyo wakili Mgaya aliiomba mahakama kupuuza malalamiko hayo ya warufani kwa kutumia kanuni ya kutokuzingatia ukiukwaji sheria usiokuwa na athari (overriding objective).

Lakini Jaji Kisanya alisisitiza kuwa msimamo wa kisheria ni kwamba kushindwa kufanya marekebisho ya hati ya mashtaka (kwa hati yenye dosari kama hizo) ni dosari isiyoweza kutibika.

Hivyo hakubaliani na mawakili wa Serikali na hakimu aliyesikiliza na kuamua kesi hiyo, aliyekuwa na mtazamo kuwa kutokufanya hayo (marekebisho ya hati), hakukuwaathiri warufani.

“Kwa hayo ni dhahiri kuwa kutokufanya marekebisho ya hati ya mashtaka hakuwezi kutibiwa kwa kutumia kanuni ya kutokuzingatia ukiukwaji wa sheria usio na athari. Ni dosari isiyotibika ambayo huifanya hati ya mashtaka husika kutokuthibitishwa,” alisisitiza Jaji Kisanya.

Jaji Kisanya alibainisha mkinzano mwingine wa hati ya mashtaka na ushahidi kuwa ni katika jina la mrufani wa tatu (Mbura).
Alibainisha kuwa wakati hati ya mashtaka inaonyesha kuwa jina la mrufani huyo ni Daniel Gabriel Mbura, lakini katika ushahidi wa shahidi wa sita anamtaja kama Daniel Bura, wakati katika kielelezo cha pili cha upande wa mashtaka anatajwa kuwa ni Daniel Laurent Bura.

“Mkanganyiko kama huo unakwenda kwenye mzizi wa kesi kwa sababu mrufani wa tatu alisisitiza kuwa yeye siyo Daniel Gabriel Mbura,” alisema Jaji Kisanya na kuongeza:

“Hata kama ikizingatiwa kwamba mrufani wa tatu alikubali katika hatua ya usikilizwaji wa awali kuwa jina lake ni Daniel Gabriel Mbura, upande wa mashtaka ulipaswa kuhakikisha kuwa jina Daniel Bura na Daniel Laurent Bura yanaingizwa kwenye hati ya mashtaka.”
Amesema kuwa kwa hali ilivyo, hakuna kitu kinachoonyesha kuwa Daniel Gabriel Mbura, Daniel Bura na Daniel Laurent Bura ni mtu mmoja yuleyule na kwamba pia haikuwa dhahiri kama majina hayo yanamhusu mrufani wa tatu ambaye alijitambulisha kama Daniel Laurent Mbura.

Jaji Kisanya anaendelea kuchambua katika hukumu hiyo kuwa jambo la pili la kuzingatia ni sababu ya saba ya rufaa kwamba warufani walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu (kifungo jela miaka 30) licha ya mkanganyiko wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Alisema kuwa Mahakama ya Rufani katika kesi mbalimbali imebainisha kanuni kwamba mkanganyiko katika ushahidi wa shahidi mmoja au miongoni mwa mashahidi haziwezi kuepukika katika kesi yoyote, kwa sababu shahidi hatarajiwi kukumbuka na kuelezea kila kitu kuhusiana na tukio husika.

Hata hivyo, mkanganyiko unatakiwa kutathminiwa katika muktadha wake wa kawaida ili kubaini uzito wake na kwamba undani wake ni kama mkanganyiko huo unakwenda kwenye mzizi wa shauri au la.

Ushahidi picha jongefu (video) za kamera za usalama (CCTV), nao ulitajwa kuhusika katika kesi hii. Je, nini alichokisema Jaji Kisanya kuhusiana na ushahidi huo? Kwa nini alihitimisha kwa amri ya kuwaondolea hatia kina Sabaya? Usikose sehemu ya tano na ya mwisho kesho.


Chanzo: Mwananchi

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Rufaa ya Sabaya na wenzake - 5

Mkanganyiko wa ushahidi kuhusu picha za CCTV zilizorekodiwa wawabeba Sabaya na wenzake

Katika sehemu ya nne tuliona jinsi Jaji Kisanya alivyojadili na mambo ya kuzingatia kabla ya hukumu baada ya kubaini ukiukwaji wa sheria katika mwenendo wa kesi ya msingi.

Moja ya mambo aliyoyabainisha ni dosari katika hati ya mashtaka jinsi ilivyokinzana na ushahidi pamoja na mkanganyiko wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hususan ushahidi wa picha za CCTV. Fuatilia sehemu hii ya tano na ya mwisho.

Jaji Kisanya alibainisha kuwa moja ya mikanganyiko katika ushahidi ilijitokeza katika picha za usalama (CCTV) za dukani kwa mlalamikaji na shahidi wa kwanza wa mashtaka, Mohamed Saad.

Alisema kama ilivyobainishwa na mmoja wa mawakili wa Sabaya, Moses Mahuna, shahidi wa kwanza upande wa mashtaka katika ushahidi aliieleza mahakama kuwa matukio yote yalirekodiwa kamera ya CCTV.

Lakini vilevile katika ushahidi wake alisema “sikuwepo dukani wakati Sh2,769,000 zilipoibwa, sijui nani miongoni mwa washtakiwa aliniamuru kufika dukani ndani ya dakika tano. Yote yaliyotokea dukani niliyaona kwenye kamera ya CCTV.”

Wakati akihojiwa zaidi na mmoja wa mawakili wa utetezi, Olawa kuhusu CCTV kurekodi tukio, shahidi huyo alieleza kuwa, “nilielezwa na Numas (Justine Numas, mmoja wa wasimazi wa duka) kuwa washtakiwa waliiba Sh2,769,000. Kadhalika kamera ya CCTV inawaonesha hao waliochukua pesa.”

Jaji Kisanya baada ya kurejea sehemu za ushahidi huo anasema unakinzana na wa shahidi wa saba na wa 11.

Amebainisha kuwa wapelelezi hao katika ushahidi wao unaonyesha kuwa kamera za CCTV zilikuwa zimehujumiwa na kugeuziwa sehemu nyingine.

“Duka lilikuwa na kamera za CCTV, lakini kwa makusudi ili kwamba tukio lisiweze kurekodiwa, kamera nne zilikuwa zimegeuzwa kuelekea ukutani.”

Advertisement
Baada ya kurejea sehemu ya ushahidi wa mashahidi hao, Jaji Kisanya alisema ni dhahiri kwamba shahidi wa kwanza kwa upande mmoja na shahidi wa saba na wa 11 kwa upande mwingine walikinzana kuhusu iwapo tukio la wizi lilirekodiwa na kamera za CCTV.

Wakijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga na wakili wa Serikali Baraka Mgaya walimuomba Jaji Kisanya asizingatie ushahidi wa shahidi wa saba kuwa kamera za CCTV zilikuwa zimeelekezwa katika kona nyingine tofauti.

“Inaonekana wakili Mwandamizi ananialika kuuona ushahidi wa footage za CCTV haukuwa na manufaa katika upelelezi,” alisema Jaji Kisanya.

Alisema kuwa kwa kuzingatia mazingira ya kesi hiyo ni mtazamo wake kwamba mkanganyiko huo hauwezi kuchukuliwa kwa wepesi kwa kuwa unakwenda kwenye mzizi wa kesi.

Amesema kuwa hata kama ikizingatiwa kwamba mrufani wa kwanza (Sabaya) alikiri kwenda dukani kwa shahidi wa kwanza, lakini alikana kutenda kosa na kwamba
katika hali hiyo ushahidi uliochukuliwa kutoka kwenye picha za CCTV ungeweza kutoa mwanga zaidi kuhusu nini kilitokea dukani.
“Ni mtazamo wangu kwamba mkanganyiko katika suala la CCTV unaibua shaka katika kujenga kesi,” amesema Jaji Kisanya.

Mkanganyiko mwingine ni kuhusu muda na kiasi cha pesa na mali nyingine zinazodaiwa kuibwa dukani humh

Katika hilo Jaji Kisanya amebainisha kuwa shahidi wa pili katika ushahidi wake alidai kuwa pesa, mashine ya EFD na simu vilichukuliwa wakati mtu mwingine ambaye alikuwa kwa amri ya Sabaya alipokuwa ameondoka dukani humo.
Anamnukuu shahidi huyo kuwa “kiongozi alirudi dukani baada ya hapo, na alimwachia Abu Mansur, Anas, Mzee Salim, Bakari Msangi na mwanamke. Kiongozi baada ya kuwa amerudi aliamuru pingu iliyokuwa mikononi mwa Abuu Mansur na Bakari kufunguliwa, kwa kuwa walikuwa wamefungwa pingu moja.

“Walichukua nyaraka, mashine ya EFD, simu za mkononi vilivyokuwa mikononi mwa wale waliokuwa wamekamatwa.
“Sikuona walichokichukua kutoka kwenye kaunta bali vilivyokuwa mezani. Kwenye kaunta kulikuwa na droo mbili. Ya juu ilikuwa kwa ajili ya kutunza nyaraka na sarafu na ya chini ilitumika kuhifadhi pesa. Kwa siku hiyo droo ya chini ilikuwa na Sh2,769,000.”
Jaji Kisanya amesema hata hivyo shahidi wa sita na wa nne walitoa ushahidi unaoashiria kwamba mali ziliibwa wakati shahidi wa sita akiwemo dukani.
Ananukuu: “Wakati tulipobaki tu watu wanne, mbali na Jeneral (Sabaya) na watu wake. Harijini (shahidi wa nne, wa pili na mwanamke) na mimi.
Rufaa ya Sabaya na wenzake – 5


Halafu Jeneral aliamuru vitu vyote vilivyokuwa juu ya kaunta vikusanywe. Niliona watu wa Jeneral wakichukua mali zetu kwenye kaunta na wakaviweka kwenye bahasha, wakachukua mashine ya EFD na karatasi zake (risiti). Simu zetu ziliwekwa kwenye bahasha.”

Akiamua hoja hiyo, Jaji Kisanya amesema kuwa anakubaliana na kanuni kuwa hitilafu za kawaida haziwezi kuepukika na kwamba anakubaliana na wakili wa Serikali kuwa mazingira ya kesi hiyo yanaashiria kuwa mashahidi walikuwa katika hali ya vurugu.

Hata hivyo, amesema mkanganyiko huo unakwenda kwenye mzizi wa kesi na kwamba unaibua mashaka kama shahidi wa sita wa upande wa mashtaka aliwashuhudia warufani wakikusanya au wakichukua vitu kutoka katika kaunta ya duka la shahidi wa kwanza (Saad).

Jaji Kisanya amesisitiza kuwa mkanganyiko huo unatia mashaka kuaminika kwa shahidi wa pili, wa nne na wa sita ambao wanakanganyana kama shahidi wa sita alikuwepo wakati warufani wakichukua mali hizo.

Kuhusiana na kiasi cha pesa kilichoibwa, Jaji alisema kulingana na kumbukumbu za kesi hiyo, shahidi wa kwanza na wa pili walipishana, kama zilikuwa ni Sh2,769,000 kinachoonekana kwenye hati ya mashtaka kilikuwa kinajumuisha Sh1 milioni zilizodaiwa kubakia dukani siku ya tukio.

Akijibu malalamiko hayo, wakili wa Serikali, Mtenga alisema shahidi wa kwanza na wa pili hawakukinzana huku akirejea kumbukumbu za rufaa hiyo na kudai kuwa Sh2,769,000 zinajumuisha na Sh1 milioni.

Hata hivyo, Jaji Kisanya alisema alichunguza kumbukumbu za rufaa kuwa kiasi cha pesa zilizoibwa ni Sh2,769,000.

Alisema kuwa shahidi huyo alikuwa imara kwamba alikijua kiasi hicho kwa kuwa tukio hilo lilitokea mara tu baada ya kumaliza kuhesabu mapato ya mauzo.

“Hivyo shahidi wa pili aliendelea kutoa ushahidi kwamba mapato ya mauzo (Sh2,769,000) yalijumuisha Sh1 milioni zilizoachwa na shahidi wa kwanza.”

Anarejea sehemu ya ushahidi wa shahidi huyo wa pili ambapo Jaji Kisanya anamnukuu:

“Tarehe 17/02/2021, nilimuita Saad (shahidi wa kwanza) aliyenieleza kuwa aliacha Sh1 milioni dukani, kiasi ambacho alikichukulia kama mapato ya mauzo. Katika Sh2,769,000 kiasi hicho kilijumuishwa.”

Jaji Kisanya alifafanua zaidi kuwa kwa upande mwingine ingawa shahidi wa kwanza (Saad), alitoa ushahidi kwamba aliacha pesa dukani, alieleza akiwa chini ya kiapo kuwa hakujua jumla yake.

“Wakati naondoka dukani kwenda msikitini, niliacha kiasi cha pesa ambacho sikujua jumla yake halisi.”

Jaji Kisanya anaendelea kusisitiza kuwa mkanganyiko huo si mdogo na kwamba unakwenda kwenye mzizi wa kesi, yaani kama Sh2,769,000 ziliibwa kutoka dukani kwa Saad, kama ilivyoelezwa kwenye shtaka la kwanza.

Mkanganyiko mwingine kuhusu kuwatambua washtakiwa wakati wa gwaride la utambuzi.

Shahidi alieleza kwamba wakati wa gwaride hilo aliwatambua watu wawili, aliowataja kuwa ni Deogratias Peter na Daniel Bura.

Hata hivyo, katika ushahidi wa shahidi wa tisa na kielelezo cha pili, ilionyeshwa kwamba mtuhumiwa aliyetambuliwa na shahidi wa sita ni Daniel Laurent Bura na Deogratias Peter haonekani kwenye ushahidi wa shahidi wa tisa na kielelezo cha pili. “Kutokana na uchambuzi huo, ninakubaliana na rufaa hii kwa namna ambavyo imeonyesha hapa. Hatimaye mwenendo wa kesi ya msingi unabatilishwa, hatia dhidi ya warufani inatenguliwa na adhabu iliyotolewa kwao inatupiliwa mbali.

“Inaamuriwa kwamba Lengai Ole Sabaya, Sylvester Wenceslaus Nyegu na Daniel Gabriel Mbura waachiliwe kutoka gerezani isipokuwa kama wataendelea kushikiliwa kwa sababu nyinginezo halali.”
 
Back
Top Bottom