SoC02 Sadaka

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Aug 30, 2022
Posts
5
Reaction score
3
Sadaka
Je, ni sawa kuwa wanufaika wa jasho na sadaka za wengi waliokuwepo kabla yetu ikiwa hatuko tayari kuwa wa manufaa kwa watakaokuwepo baada yetu? Asilimia kubwa ya tulio hai leo hii, hatukuhusika katika jitihada za kujishindia uhuru dhidi ya ukoloni, bali ni wanufaika wa jitihada hizo. Japo ilikuwa wazi kwa wengi waliojitoa sadaka kwa ajili ya uhuru (na si kwa nchi yetu pekee) kwamba ingewagharimu hata maisha yao, hawakurudi nyuma katika yale waliyojitolea kufanikisha.

Kama Tanzania isivyo mali ya mtu yeyote leo hii, haikuwa mali ya mtu yeyote wakati huo. Waliopambania na kufanikisha uhuru wa nchi yetu hawakufanya hivyo kwa maslahi binafsi, bali kwa manufaa ya wananchi wote, waliokuwepo wakati huo na watakaofuata, sisi tukiwa katika kundi hili la pili. Licha ya changamoto na magumu tupitiayo leo hii, ni mengi ya kuumiza tumeepushwa kutokana na sadaka na jitihada za waliotutangulia.

Huwa ninawaza jinsi ambavyo maisha yangekuwa endapo uhuru walioupigania ungekuwa na kikomo (expiry date) ambapo baada ya miaka kadhaa ingebidi kuupambania tena kama ulivyopambaniwa kabla. Fikiria uhuru kama tuzo ipatikanayo baada ya ushindi katika kila msimu/awamu ya kuupambania. Pengine kizazi chetu kingeangukia katika msimu mwingine wa kuupambania, ambapo tusingekuwa wanufaika wa uhuru uliopatikana kabla yetu bali ingetupasa kujitoa sadaka kwa ajili ya uhuru wetu na watakaofuata mpaka kikomo cha uhuru huo, uwadiapo msimu mwingine wa kujishindia uhuru kwa mara nyingine tena. Hili ni swala la fikra tu, dhamira ikiwa ni kukumbusha kwamba wapo waliojitoa sadaka kwa ajili ya mengi tunayonufaika nayo leo hii, mengi tusiyotambua labda mpaka pale yakitoweka.

Uhuru tuliupata, ndio, lakini haimaanishi hakuna mengine ya kupambania, ya kujitoa sadaka.

Baada ya wakoloni kutambua kwamba isingewezekana kuendelea kututawala kwa njia walizotumia kipindi hicho, tulipatiwa uhuru wetu, japo mabadiliko hayo hayakupelekea mataifa yetu kuwa na nguvu sawa, au uzito sawa wa kauli. Maisha yalivyo leo hii, badala ya mataifa imara kutumia nguvu kunyenyekesha mataifa dhaifu, mataifa imara huelekeza rasilimali zake katika kujiendeleza yenyewe ili mataifa yanayoshindwa kujiendeleza yenyewe, yajilete kwa haya mataifa imara na kujinyenyekesha kwa ajili ya misaada na fadhila ambayo ni nadra sana kutoambatanishwa na mategemeo au masharti kandamizi.

Je, ubaya ni kwa mataifa haya makubwa? Je, haya mataifa yanayojinyenyekesha yastahili kuhurumiwa? Ni wazi kuwa mataifa yetu yapo katika ushindani usiokuwa na mwisho, bali ubadilikao kuendana na wakati. Mataifa imara hayakutokea hivihivi tu— yalitengenezwa na yaendelezwa zaidi. Muda ambao wananchi wake hutumia kuendeleza nchi hizo, twapaswa kutumia kuendeleza nchi yetu, tofauti na hapo tutabaki kuwa wa kutazama wengine wakiendelea, tuje tujinyenyekeshe kwao ili kupata misaada na fadhila.

Achana na misaada, asilimia kubwa ya bidhaa tunazoagiza kutoka nje, vitu kama mavazi, samani, hadi bidhaa kama magari, sio kwamba hatuna mali ghafi kwa ajili yake. Ni mali ghafi chache ambazo ingebidi kuagiza kutoka nje ya bara la Afrika, endapo tungeamua kuzalisha bidhaa hizo sisi wenyewe. Badala yake, tunauza mali ghafi kwa bei ya kutuumiza, na baada ya bidhaa hizo kutengenezwa nje, tunaziagiza tukilipia utaalamu uliotumika, maradufu ya gharama tuliyowalipisha kwa ajili ya mali ghafi.

Sio kwamba hatuwezi kuwa na utaalamu wa kujitengenezea yale tunayohitaji. La hasha! Ni mara ngapi tumesikia Mtanzania, wakati mwingine asiye msomi mwenye vyeti, ameunda kitu ambacho tusingetegemea Mtanzania au Mwafrika kuweza kuunda? Watu hawa hupotelea wapi? Inashangaza pale tunapotegemea mapinduzi katika nyanja za sayansi na teknolojia kutoka kwa wasomi pekee huku tukiwapuuza wabunifu ambao tayari wamedhihirisha uwezo wa kipekee katika maeneo hayohayo licha ya kutotambulika kama wasomi. Tukiamua kufuatilia historia ya teknolojia nyingi, hakika tutakutana na wasomi na wabunifu wasio ‘wasomi’ walioamua kuwa na mchango chanya katika jamii kupitia uwezo wao, na leo hii twanufaika kutokana na waliyofanikisha.

Labda tayari tulipaswa kuwa kati ya nchi zinazoongoza katika maswala ya teknolojia kwa nchi za Afrika, lakini kila aliyeonesha uwezo wa kipekee, tulimdogoesha. Kuwa taifa linaloongoza katika maswala ya teknolojia (hili ni eneo mfano) haitatokea kupitia kichwa kizuri kimoja bali, agharabu, vichwa vingi, kila mmoja akichangia kadri ya uwezo na upekee wake. Yale tunayoweza kuchangia binafsi yaweza kuonekana madogo, lakini mataifa imara hayajawa hivyo kutokana na mchango wa mtu mmoja, bali wengi kwa mengi madogo yao yaliyounganika kuwa kitu/vitu vikubwa.

Ila yote hayo ni bure ikiwa hatutotambua ni katika yapi twaweza kuwa wa manufaa kwa nchi yetu, au watu wenye uwezo wa kipekee kupuuza yale waliyonayo kutokana na hofu ya kutofanikiwa. Labda tumechoshwa kuwa wa kuburuza mkia katika michezo, lakini wanamichezo wenye vipaji vya kipekee, kwa hofu ya kutofanikiwa kupitia hivyo vipaji vyao, wameamua kupuuza vipaji hivyo wakilenga fursa za maofisini. Ikiwa huo ndio uhalisia basi watakuwa hawajavitendea haki vipaji hivyo na taifa. Kwani, ni kitu gani waliopambania uhuru wetu walijiona nacho kijihakikishia kuwa wangefanikiwa katika jitihada zao?

Ni lazima ufike wakati tufanye maamuzi kwamba yapo mambo inabidi yabadilike katika maisha yetu. Pengine ni wazi kuwa hatutoshi kufanikisha mabadiliko au maendeleo, lakini wengine wanapoona uthubutu wetu, ndipo watakaponyoosha mikono ya ushirika.

Wakati mwingine ukakasi huwa katika familia zetu. Julius Kambarage Nyerere alikuwa na familia pia. Kama familia yake ingekuwa kikwazo kwake katika kupambania uhuru wa nchi yetu, hakika wangekuwa na maswali ya kujibu badala ya kumiminiwa sifa. Julius Nyerere hakuwa kwa ajili yao tu bali kwa ajili ya wengi zaidi. Vivyo hivyo, familia zetu, kama wanufaika wa sadaka za familia nyingine kabla, hazina budi kuwa tayari kwa sadaka ikiwa miongoni yupo au wapo walio kwa ajili ya manufaa kwa wengi zaidi.

Ikiwa twatambua yale inayobidi tunufaike kutoka kwa nchi yetu, basi yatupasa kutambua ni katika yapi twaweza kuwa wa manufaa kwa nchi yetu, na ufike wakati wa kuacha fikra za kibinafsi na tuwafikirie wengi wanaopaswa kunufaika kwa yale tuliyonayo. Hatuna budi kupuuza hofu juu ya yale tunayoweza kupoteza binafsi ikiwa tupambaniayo ni kwa manufaa ya wengi zaidi. Hio ndio sadaka. Kama wewe ni mnufaika wa sadaka za wengine— na hakika sisi wote ni wanufaika— hatuna budi kusimama katika nafasi zetu pale tunapopaswa kuwa wa manufaa kwa wengi zaidi. Tufanye kitu kwa ajili ya Tanzania.

Mwandishi: Julianus Julius
Email: julianusjuliusjj@gmail.com
 
Upvote 2
Muandishi wa sadaka ametulia sana sana kuandaa makala hii limezungumziwa swala la kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine kitu ambacho karne hii ni kama kinapotea...
 
Muandishi wa sadaka ametulia sana sana kuandaa makala hii limezungumziwa swala la kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine kitu ambacho karne hii ni kama kinapotea...
Hakika Mkuu! Naamini tunapokumbushana sadaka za waliotutangulia hali ya kujitolea kwa manufaa ya wengi itajengeka zaidi. Asante kwa kura na reply/comment yako!
 
Hakika tufanye kitu kwa ajili ya Tanzania. Inspired!!!!!Asante mwandishi Kura yangu umeistahili.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…