Lugha ya Kichina inaendelea kupata umaarufu katika nchi na sehemu mbalimbali duniani, na vijana wengi wanapenda kujifunza lugha hii kwani imekuwa ni daraja la kuunganisha tamaduni za nchi mbalimbali.
Miriam Wambui, binti wa miaka 13, anazungumza lugha hii ya Kichina kwa kujiamini sana kama mtaalamu wa lugha, licha ya kwamba amejifunza lugha hii kwa miaka miwili tu.
Kipaji cha Miriam kiko wazi, kwani alikuwa mshindi wa shindano la kitaifa la Daraja la Kichina nchini Kenya, na kushika nafasi ya sita katika bara la Afrika, na kuwa miongoni mwa wanafunzi 30 wa juu katika Shindano la Kimataifa la Daraja la Kichina kwa Wanafunzi wa Kigeni wa Shule za Sekondari lililofanyika Tianjin, China, mwezi Oktoba mwaka jana. Miriam anasema alifurahi sana alipotangazwa mshindi wa shindano la Daraja la Kichina nchini Kenya, kwa kuwa alikuwa na wiki mbili tu za kujiandaa baada ya kujiandikisha katika mashindano hayo.
Safari ya Miriam kujifunza lugha ya Kichina ilianza kwa kupitia kaka yake mkubwa, ambaye alikwenda China mwaka 2015 kuendelea na masomo ya shahada ya uzamili katika Lugha ya Kichina. Aliporejea nchini Kenya kutembelea familia yake katika eneo la kahawa Sukari jijini Nairobi mwaka 2019, Miriam alivutiwa sana na uzungumzaji wake wa ufanisi wa lugha ya Kichina na kuvutiwa na uwezo wa uzalishaji wa kampuni za China.
Miaka miwili iliyopita, Miriam alijiandikisha kwenye darasa la Kichina katika Shule ya Sekondari ya Awali ya Presbyterian Sukari. Mwezi Mei mwaka jana, alitoa ombi la kijasiri kwa mwalimu wake wa Kichina, kwamba anataka kujiunga na timu inayowakilisha shule yake katika shindano la Daraja la Kichina, kauli iliyomshangaza sana mwalimu wake wa Kichina. Anasema muda wote kabla ya hapo alikuwa anasubiri kuchaguliwa, lakini alipoona wazi kwamba hatachaguliwa, aliamua kuomba kushiriki katika shindano hilo kwa kuwa alikuwa anajiamini kwamba anaweza.
Imani yake ilizaa matunda, kwani aliwavutia sana majaji kwa uzungumzaji wake wa lugha ya Kichina, uandishi wa insha na maonyesho kwenye shindano hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, na alipata zawadi ya laptop, kombe na kulipiwa safari ya wiki mbili nchini China.
Miriam, ambaye amepata ufadhili wa miezi sita nchini China, anasema, baadaye anataka kuwa balozi na kujifunza zaidi kuhusu lugha na utamaduni wa China.
Mafanikio ya Miriam yamewatia moyo wanafunzi wengine katika shule yake kujifunza lugha ya Kichina. Kwa mujibu wa mwalimu wake, Charity Atunga, lugha ya Kichina kwa sasa ni maarufu zaidi kati ya lugha tatu za kigeni zinazofundishwa, ikiwa na wanafunzi 90 kati ya 200 waliochagua kujifunza lugha hiyo.
Mwalimu Atuga anasema, hivi sasa umaarufu wa lugha ya Kichina unaongezeka kwa kasi katika shule za nchini Kenya, na wazazi pamoja na utawala wa shule wanaunga mkono hatua hiyo, na kufanya kujifunza Kichina kuwa na uzoefu chanya. Mwalimu Atunga, ambaye amekuwa akifundisha lugha ya Kichina kwa miaka minne sasa, naye amefaidika sana na ifadhili unaotokana na lugha ya Kichina, kwani baada ya kusoma nchini China, alifanya kazi katika kampuni kadhaa za Kichina na taasisi za elimu kabla ya kuwa mwalimu wa lugha hiyo.
Chuo Kikuu cha Kenyatta, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ualimu cha Shandong, huandaa shindano la Daraja la Kichina kwa wanafunzi wa sekondari nchini Kenya, na kupitia ushirikiao huu, zaidi ya wanafunzi 300 wa Kenya wametembelea China.