Safari ya Rais KIkwete Sunderland huenda ikawa mwisho wa kiu ya mpira Tanzania

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363

Freddy Macha


KWA UFUPI
Ingawa msafara huo ulihusu michezo na mpira, uliwakutanisha pia baadhi ya Watanzania wakazi wa Jiji la Sunderland na wale wasomao Chuo Kikuu cha New Castle, Kaskazini Mashariki ya Uingereza


Jumapili iliyopita nilibahatika kuwa ndani ya msafara mahususi uliozunguka na mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete.

Ingawa msafara huo ulihusu michezo na mpira, uliwakutanisha pia baadhi ya Watanzania wakazi wa Jiji la Sunderland na wale wasomao Chuo Kikuu cha New Castle, Kaskazini Mashariki ya Uingereza

Rais Kikwete alipotua jijini Sunderland jua lilikuwa liking'ara, saa za adhuhuri...Mwezi wa sita huwa kiangazi ndiyo kinaanza anza Ulaya hivyo siyo lazima kuvaa makoti mazito. Mkuu wa nchi alikuwa nadhifu na wasaizidi wake kama kawaida, akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara, Balozi wetu hapa Peter Kallaghe na maofisa wengine husika walichangamkia shughuli hii muhimu na ya kihistoria, kama tutakavyoona.

Upande wa wenyeji je?

Mmiliki klabu ya Sunderland ni tajiri wa Kimarekani, Ellis Short kipato chake kinakisiwa kuwa Dola za Marekani 3.5 bbilioni, ndiye alimwalika Rais Jakaya Kikwete na Paul Hinks, Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi Umeme ya Symbion Power, yenye makao Marekani. Pande hizi mbili ndizo zitashirikiana, moja kujenga Symbion chuo cha kufundishia watoto mpira, mwingine kutoa mafunzo hayo Sunderland AFC.

Kwa vipi klabu iliyochukua nafasi ya 17 mwaka huu ndani ya Ligi ya Uingereza kati ya timu 20, ichaguliwe kutufariji, aliulizwa Rais Kikwete baadaye na wanahabari? Kwa nini wasiwe Arsenal, Chelsea, Liverpool au watemi wa Manchester United?

Rais Kikwete akajibu ilitokana na Ellis Short mwenyewe kuitembelea Tanzania kwa shughuli zake nyingine; Hapo msosi ukatayarishwa. Sunderland inasifika kwa kituo chake bora kufunzia watoto kiitwacho "Academy of Light." Ukichunguza sana maendeleo ya wachezaji wote wakubwa duniani, huanzia vilabu vidogo ndiyo wakanunuliwa na hatimaye kutamba na timu zenye fedha na uwezo zaidi. Mfano mzuri ni wanasoka maarufu wa ligi ya Uingereza Theo Walcott (Arsenal) Oxlade Chamberlain( Arsenal ) na Gareth Bale wa Tottenham walioanzia mpira utotoni Southampton Football Academy.

Sidhani ni wengi tunaoijua au kuisikia, Southampton, barani Afrika. Lakini huu ni ushahidi wa namna klabu ndogo zisizojulikana zinavyoivisha na kumeng'enya wachezaji chipukizi. Gareth Bale sasa hivi anapiganiwa na kila klabu na inasemekana Real Madrid wanamtamani kwa mate na udenda. Hata kwetu Bongo wachezaji wengi huanzia klabu ndogo za mikoani kabla ya kununuliwa Simba na Yanga.

Hivyo Sunderland inaweza isiwe kubwa, lakini uwezo wake wa kiufundi utaikidhi sana Tanzania. Msafara wa Rais ulionyeshwa eneo hili kubwa lililokamilika miaka kumi iliyopita. Humo mna sehemu za kuogelea, viwanja vyenye majani safi ndani na nje, Gym za mazoezi, madarasa na vyombo mbalimbali vya mafunzo. Mbali na chuo, Rais Kikwete alitembezwa uwanja wa "Stadium of Light" ambao hujaza watazamaji 49,000. Huu ni uwanja wa tano kwa ukubwa Uingereza nzima. Hapa huwepo vilevile maonyesho siyo madogo ya muziki, kama lile la mwimbaji nguli Rihanna toka Barbados aliyetumbuiza juzi Alhamisi.

Kuna hilo la kiufundi, halafu historia.

Si wengi wanaofahamu historia za vilabu vyetu.

Rais alipowaeleza wanahabari wa Kizungu kuwa zamani Simba ilipoanzishwa mwaka 1936 iliitwa Dar Sunderland, alikuwa akikumbusha tulikotoka.Tujue kwamba kihistoria Sunderland AFC ya Uingereza iliyoasisiwa mwaka 1879 ilikua timu kali na iliwahi kushinda kombe la FA Uingereza 1937 na 1973. Kati ya mwaka 1892 na 1936 (wakati Simba inaanzishwa) jamaa hawa wa Kizungu walishinda ligi mara sita. Jina la Dar Sunderland lilikaa hadi mwaka 1971, neno Simba lilipojizatiti hadi leo. Mtangazaji aliyebobea Charles Hillary wa BBC- Swahili alitaka kujua msaada wa ujenzi wa kituo cha kufundishia vijana wetu utaifaidiaje Tanzania yetu?
Rais akajibu bila kupepesa: "Mimi ni mpenzi wa michezo. Hapohapo ni Rais wa Tanzania. Mimi mwenyewe mchezo wangu ni mpira wa kikapu. Lakini ningependa sana kuona mchezo wa soka unaendelea. Hasa kwa sababu ndiyo mchezo unaopendwa kuliko yote. Ni mchezo ambao unawaletea raha Watanzania. Watanzania wangependa kuona soka inakua. Lakini ukiwaangalia wale wote wenzetu waliofanikiwa wamewekeza katika kufundisha watoto toka wakiwa wadogo wanawalea; ndiyo historia ya wachezaji wote maarufu akina Messi, Beckham , Ronaldo, wote wameanza hivyo. Naamini kama tunataka soka ikue lazima tuwekeze katika watoto."

Ellis Short aliikaribisha Tanzania, Sunderland; akasema ujenzi wa chuo cha mafunzo ya mpira utakaonza mara moja Dar es Salaam utawafaidi sana watoto wanaoanza na kuendeleza mpira nchini.

Ujenzi huo utakaofanywa na kampuni ya umeme ya Symbion toka Marekani unaungana na mradi wa kuwekeza Afrika (Invest In Africa) ambao umeendelea toka mwaka jana. Mradi huu anasema msemaji wa Sunderland una azma ya "kuondoa dhana kwamba Afrika ni bara lenye mambo mabovu tu."

Sasa hivi mpira ni chombo kikubwa cha kuwekeza na sukari ya ajira kwa vijana. Wachezaji maarufu wastaafu wa Afrika wamekuwa wakisaidia jamii zao kwa hali na mali. Mfano mzuri ni Didier Drogba (Ivory Coast), Jay Jay Okocha na Nwanko Kanu. Licha ya Kanu wa Nigeria kuwa na maradhi ya moyo akiwa mtoto alitibiwa na hatimaye kuipatia sifa si tu nchi yake bali klabu kali alizochezea kama Arsenal (enzi zile Arsenal ikitamba kati ya 1999-2004). Leo anaendesha kazi nyingi za fadhila ikiwemo kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo.

Kwetu hatujawahi kuwa na mchezaji maarufu kiasi hicho.

Iangalie timu ya Hispania, miaka 10 iliyopita haikuzungumziwa. Leo inao wachezaji wazuri waliotokana na matayarisho ya watoto wadogo chuo cha" La Masia" kama Andrew Iniesta, Xavi Hernandez (na mwenzao Lionel Messi) wameifanya Barcelona kuwika.

Tangu mwaka 1980 hatujaambulia chochote kikubwa katika riadha au mpira. Miaka 30 ya njaa hii imetokana na matayarisho mabaya ya vilabu, kutojipanga na kutowekeza.

Wenzetu waliopitia vita kama Rwanda, Angola na Afrika Kusini wametuzidi na wanaendelea kutuzidi. Tofauti yao na sisi nini? Bila shaka kitendo cha kuwekeza katika mafunzo ya vidudu hadi vijana wa miaka 18 kama wanavyofanya wenzetu Sunderland utakuwa mwanzo wa kukata kiu na kujenga ari na jazba ya matumaini ambayo huhamasisha sana wazalendo na wananchi wa mataifa mengi duniani.

Barua pepe: kilimanjaro1967@hotmail.com

Tovuti: Freddy Macha


Safari ya Rais KIkwete Sunderland huenda ikawa mwisho wa kiu ya mpira Tanzania - Jicho La Msafiri - mwananchi.co.tz


 
kumbe hakuenda kuomba suti kama kawaida yake...
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…