1.
Ubeti huu wa kwanza, hoja yako kuchangia,
Safari uliyoianza, siku bado kutimia,
Pasi mwalimu kufunza, kitanda ukarukia,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
2.
Safari yako ya hima, tena isiyo na shari,
Wadhani huwezi kwama, hata wakati wa hari,
Hilo laweza simama, bila kutoa hadhari,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
3.
Nimekurushia fataki, ili uanze fikara,
Wala siyo kuhamaki, bali ukune kipara,
Kama mpara samaki, Yule asiye na dira,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
4.
Anza sasa tafakuri, juu ya yako kauli,
Ati unayo safari, kabla ya hiyo nauli,
Utavukaje bahari, nawe wapanda bakuli,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
5.
Mapenzi uloanza , hakika siyo asali,
Japo watoka uvinza, shurti kwanza usali,
Tena bila kuviza, wale wasafiri kweli,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
6.
Uzoefu waonesha, mwisho wa pendo udhia,
Busu zikali nyesha, mengine yaja tibua,
Japo waweza kesha, bila pendo kuokoa,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
7.
Utamu uliolamba, ndiyo wenyewe utamu,
ukikinai mtamba, koo hakidhi hamu,
Utakimbilia kamba, hima kujihukumu,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
8.
Shukuru ulicholamba, zaidi yake hakuna,
Uache huko kutamba, demu lisije kununa,
Utatamtmani komba, demu huyo akiguna,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia
9.
Mwisho nakupongeza, kwa penzi kuweka wazi,
Japo si wa kwanza, kupiga mwenzi kwa jozi,
Sasa ule machenza, pasi toa machozi,
Safari bado kuanza, japo ndiyo yaishia.