Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir katika nasaha zake
amesema historia ya Saigon Club iandikwe kwani kiandikwacho
hudumu.
Mufti akaendelea kusema kuwa Saigon Club ni kielelezo cha
historia ya mji wa Dar es Salaam, Tanzania na wazee wake
waliotangulia mbele ya haki ambao walifanya makubwa kwa
taifa hili.
Saigon Club imeutwisha mzigo huu wa kuiandika historia ya
Saigon kwa Abdallah Tambaza na Mohamed Said.
Naweka hapo chini picha ya Saigon Club ya miaka ya 1970
wakati Saigon bado vijana na wanacheza mpira.
Picha kwa hisani ya Aziz wa Azam
Kulia ni Hassan (Gilbert Mahinya), Said Ali Abbas, Yakub Mbamba,
Ahmada Digila (Danny Blanchflower) (marehemu) na
Atika Kombo
Picha hii nimeipunguza kuifanya ndogo ili nimuonyeshe rafiki yangu
Ahmada Digila tukimwita Danny Blanchflower jina la mchezaji wa
Uingereza katika miaka ya 1960.
Danny Blanchflower alikuwa mmoja wa wachezaji wazuri sana katika
Ligi ya Uingereza.
Wakati ule kulikuwa hakuna TV lakini tukifuatilia Ligi hii kupitia gazeti la
''Shoot.''
Ahmada tulimpa jina hilo kwa uchezaji wake katika nafasi ya kiungo.
Namkumbuka Ahmada uchezaji wake na jinsi alivyokuwa hodari wa
kuhamasisha timu.
Alikuwapo midfielder mwenzake Khalid Fadhili na yeye ni marehemu
pia.
Khalid tukimwita George Young mchezaji mwingine wa katika Ligi ya
Uingereza.
Saigon kulikuwa na Okasha akicheza kama striker na jina lake
lilikuwa Mazola katika wachezaji ambao Italy haitaweza kumsahau.
Okasha na yeye katangulia mbele ya haki na hawa wote wamekufa
katika umri mdogo sana.
Hassan (GIlbert Mahinya) yeye ni mstaafu akiwa afisa mkubwa Idara
ya IT NPF.
Hassan yeye hakuchukua jina la mchezaji kutoka Ulaya.
Yeye alichukua jina la kiungo hatari sana aliyekuwa Simba kisha akaenda
Yanga, Gilbert Mahinya.
Hadi leo tumekuwa watu wazima Hassan bado tunamwita Hassan Gilbert.
Hivi niandikapo ni kama niko Mnazi Mmoja ambao ndiyo ulikuwa kiwanja chetu
toka tulipokuwa tunajiita Everton hadi tulipokuja kujulikana kama Saigon.
Hii ilikuwa miaka ya katikati 1960 na umri wetu ulikuwa wastani wa miaka 15.
Katika utoto huu wengi wetu tukiwa shule za msingi na wachache sekondari
kama Said Ali Abbas hatukujua kama hii club yetu itakuja kuwa club kubwa
na maarufu sana.
Nilitaka kueleza historia ya Saigon kwa mukhtasari tu kupitia maisha ya wenzetu
wachache waliotangulia.
Mola awasamehe dhambi zao hawa wenzetu wana Saigon Club waitangulia
mbele ya haki na awatie peponi.
Amin